Mufti: Kikwete ni mti uliosheheni embe mbivu

MaxShimba

JF-Expert Member
Apr 11, 2008
35,772
4,054
Salim Said

SHEIKH mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba amemfananisha Rais Jakaya Kikwete na mti uliosheheni embe mbivu, hivyo wabaya wake hawataacha kumpopoa kwa mawe.


Katika siku za hivi karibuni, makada wa CCM na viongozi wa zamani wamepata ujasiri wa kumkosoa Rais Kikwete hadharani, wakidai kuwa ameshindwa kufanya maamuzi mazito juu ya mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi.


Hoja zilizostua wengi ni zile zilizotolewa na mawaziri wawili wa zamani, Matheo Qares na Mussa Nkangaa kwenye kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, huku Qares akieleza bayana kuwa iwapo mkuu huyo wa nchi atashindwa kuchukua maamuzi hadi 2010, basi CCM isimteue kugombea urais na kutafuta mwanachama mwingine.


Wengine waliokosoa serikali ya awamu ya nne ni waziri mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba na mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, lakini Kikwete alijibu kwa kifupi kuwa angeshangaa kama watu hao wasingetoa shutuma hizo na kuahidi kwenda kukaa na wenzake ambao hakuwataja kuandaa majibu.


Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, Mufti Simba alisema kiongozi yeyote mzuri ni kama mwembe uliojaa embe mbivu ambao daima hupopolewa kwa mawe ili kutungua matunda yaliyomo.


Alisema kila kiongozi ana wema na wabaya wake na kwamba wale wote wanaompopoa Rais Kikwete kwa kubeza juhudi zake ni wabaya wake.

"Kiongozi yeyote mzuri ni sawa na mwembe uliojaa maembe mabivu, ambapo kila mtu anataka kuupopoa kwa mawe. Historia ya uongozi inaonyesha hivyo tangu enzi za mitume hadi sasa," alisema Mufti Simba.

"Historia inaonyesha kwamba kila kiongozi ana wema na wabaya wake, hata kuanzia baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, walikuwa na maadui wao ambao walikuwa wakiwapopoa kwa mawe na kuona kwamba hawakufanya lolote."


Mufti Simba alisema kwamba, ikiwa kiongozi akiwa madarakani kunakuwa na ukosoaji na lawama ujue hiyo, ni ishara ya kiongozi bora na imara katika jamii yoyote duniani.


"Lakini kinyume chake ukiona kiongozi anasifiwa kwa kila analofanya na hana upinzani wowote, ujuwe hapo kuna tatizo la uongozi lakini ukuiona kuna ukosoaji ni ishara ya uongozi bora," alisema Mufti Simba.


"Kuna mambo mengi mazuri yanayofanywa na serikali ya rais Kikwete kwa maslahi ya watanzania lakini kuna baadhi ya watu hayawaridhishi na hiyo ndio sababu ya kumpopoa kwa mawe," alisema Mufti Simba.


Wakati Mufti Simba akisema hayo, kuna mjadala mzito unaoendelea kati ya jopo la wataalamu na wanasheria wa serikali na lile la waislaam kuhusu urudishwaji wa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara.


Akizungumzia mjadala huo, Mufti, ambaye ni mwenyeketi wa jopo la Masheikh na wanasheria wa Kiislaam katika mazungumzo hayo yaliyoanza takriban miezi mitatu iliyopita, alisema yanaendelea vizuri.


"Mazungumzo yetu yanaendelea vizuri na secretarieti iliyoundwa kwa ajili ya kuratibu mazungumzo hayo kwa kuzingatia kazi na hadidu za rejea walizopewa. inaendelea na kazi zake," alisema Mufti Simba.


Alisema kwa sasa anakusudia kulitafuta jopo hilo la masheikh na wanasheria wa kiislaam ili kukutana na kujua hatua ya mazungumzo ilipofikia.

Mufti Simba aliwataka waislaam wote nchini wanaotaka kujua maendeleo ya mazungumzo hayo wafike ofisi za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ili watapatiwe taarifa hizo.

From Mwananchi Gazeti
 
Back
Top Bottom