Mtwara wabuni ndoa za palizi, talaka za mavuno

Andindile

JF-Expert Member
Mar 18, 2009
304
16
Wakati jamii ya kimataifa leo inasherehekea Siku ya Mama Duniani, hapa mkoani Mtwara katika wilaya za Tandahimba na Newala, baadhi ya wanaume wamedaiwa kuanzisha tabia ya kuoa wakati wa msimu wa palizi wa zao la korosho na kuacha wake zao muda mfupi baada ya mavuno.

Licha ya ndoa hizo za muda mfupi, talaka hizo za msimu wa mavuno zilizopewa jina la ‘safisha ghala', zimesababisha kuongezeka kwa maambukizi ya virusi wa Ukimwi na ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Tabia hiyo ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wanawake wilayani humo, imekuwa ikihatarisha mustakabali wa maisha yao na kuwafanya waendelee kuwa masikini mwaka hadi mwaka wakati wenza wao katika uzalishaji wa zao hilo wakinufaika kiuchumi.

Ndoa hizo zinadaiwa kufungwa mwezi Aprili kwa lengo la kuwatumikisha katika mashamba ya korosho na kuwataliki mara baada ya msimu wa mauzo ya zao hilo kuanza. "Mimi niliolewa na nikafanikiwa kuishi na mume wangu kwa miaka miwili…lakini labda kwa vile mwaka wa kwanza hatukupata mazao mengi ndio maana hakunitaliki.

"Mwaka wa pili tulivuna sana na alipouza tu, na kupata fedha nyingi akanitaliki… najuta kwa nini korosho zilizaa," alisema Hadija Hassan mkazi wa Kijiji cha Mitondi Wilaya ya Tandahimba. Naye Katibu wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake wilayani Tandahimba (TAWORO), Mwanahamisi Salimu alisema wanaume wamewafanya wanawake watumwa katika mashamba yao ya korosho.

"Wanajifanya kuoa lakini kumbe si hivyo, dhamira ya wanaume hawa ni kututumikisha katika mashamba ya mikorosho na ndiyo sababu wakipata fedha wanatutaliki na hatugaiwi mali yoyote. Tatizo hili linatuumiza wanawake wengi," alisema Salimu.

Naye Mwenyekiti wa Barala la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wa Wilaya ya Tandahimba, Abubakari Salama, amesema waumini wa dini hiyo wanatumia vibaya haki ya kuoa na kuacha kwani wengi wao wamekuwa wakiwataliki wake zao bila sababu za msingi.

"Hii ni changamoto kwetu viongozi wa dini…talaka za msimu wa mauzo ya korosho zimekuwa nyingi, tumekuwa tukiwahimiza waumini wetu kuondokana na tafsiri potofu ya mafunzo ya dini yetu," alisema Abubakar.

Kwa upande wa Ofisa ustawi wa jamii wa Wilaya ya Tandahimba, Jacqueline Manyanya amesema kuwa talaka za msimu wa mauzo ya korosho maarufu kama ‘safisha ghala', zimesababisha wilaya hiyo kuwa na ongezeko kubwa la watoto waishio katika mazingira hatarishi wapatao 5,000.

Alisema talaka hizo pia zimesababisha ongezeko la maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi ambapo kwa sasa maambukizi ni wastani wa asilimia 30. "Kimsingi hali ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi inaongezeka, hili la talaka holela linachangia kwa kiasi kikubwa sana. "Huu ni mzizi wa matatizo mengi yanayoikumba jamii ya Tandahimba, familia nyingi zimesambaratika," alisema Dk. Elias Nangosongo, Mratibu wa Ukimwi Kitengo cha Tiba wa Wilaya ya Tandahimba.

Tuwasaidieje wenzetu wa Tandahimba?

Source:Habarileo by Hassan Simba, Tandahimba; Tarehe: 10th May 2009
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom