Mtoto aibwa katika mazingira ya kutatanisha

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MWANAMKE mkazi wa Mtaa wa Maili 18 eneo la Mkundi, Kata ya Lukombe katika Manispaa ya Morogoro, Bahati Emmanuel (28), ameibiwa mwanawe mchanga wa kike na msichana asiyemfahamu vyema katika mazingira ya kutatanisha baada ya kumwomba amchukue na kwenda naye dukani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Adolfina Chialo, alisema jana mjini hapa, wakati akitoa taarifa ya matukio yaliyojitokeza kuanzia mkesha wa sikukuu ya Krismasi na hadi
jana, mkoani hapa.

Kamanda Chialo alisema mbali na mkoa kutokuwa na matukio ya kutisha yakiwemo ya uhalifu wa ujambazi ama ajali mbaya, tukio la wizi wa mtoto mchanga wa miezi mitatu ndiyo lililotoa sura mpya juu ya jambo hilo kwa mwanamke asiyefahamika kumwiba mtoto huyo.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, tukio hilo lilitokea Desemba 25, mwaka huu asubuhi katika eneo hilo ambapo msichana aliyemwiba mtoto huyo, alikuwa karibu na nyumbani anakoishi mwenye mtoto, hivyo alimwomba achukue ili aweze kwenda naye duka lililo karibu na eneo hilo.

Hata hivyo, Kamanda huyo alisema baada ya mwenye mtoto kumwona msichana huyo ni muungwana na utamaduni wa Kitanzania haumnyimi mtu anayemwomba kushika mtoto, aliamua kumpatia ili aende naye dukani, naye akiendelea na shughuli zake nyumbani hapo.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, baada ya kitambo, mwenye mtoto aliona dalili za kuchelewa kurudi kwa msichana huyo na alipomfuatilia dukani hapo, hakumwona pamoja na mwanawe huyo.

Hivyo kutokana na kuingiwa na wasiwasi huo, alilazimika kufikisha taarifa ya kuibiwa mwanawe katika Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro, ambapo Polisi inaendelea kufanya
uchunguzi juu ya wizi huo.

Kutokana na hilo, Kamanda huyo amewatahadharisha wananchi hasa kinamama wenye watoto wachanga kuondokana na desturi ya kuwa wakarimu kwa watu wasiowafahamu kuwakabidhi watoto wao.

“Hizi mila za mtoto ni wote akihitaji kuchukua apewe bila kujali kama mtu huyo anafahamika vyema tuiondoe, tusimwamini kila mtu kuwaachia watoto ….huyu mwizi hafahamiki kwa jina wala eneo anakotoka,” alieleza Kamanda Chialo.

Tukio hilo la wizi wa watoto katika Wilaya ya Morogoro ni la tatu katika miaka ya karibuni, kwani mtoto mwingine aliibwa na mwanamke asiyefahamika ndani ya wadi ya wanawake wanaojifungua kwenye Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.
 
Back
Top Bottom