Mtemi Mazengo ndiye aliyempa Nyerere kifimbo?

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
JINA la Mazengo Chalula si geni masikioni mwa watu hasa wale wa Kanda ya Kati. Ni la Mtemi wa Wagogo, moja ya makabila ya wenyeji wa Mkoa wa Dodoma ulioko katikati mwa Tanzania.

Mtemi Mazengo au Daudi Salomona Chalula kama alivyojulikana katika siku za mwisho za uhai wake baada ya kubatizwa, ameacha historia ndefu iliyotukuka kutokana na ukweli kuwa katika utawala wake hakufikiria kupata haki kwa mapigano na badala yake alipenda haki ipatikane kwa njia ya mazungumzo.

Historia inaonyesha kuwa Mtemi huyo alitumia muda mwingi kusuluhisha migogoro kabla ya kutumia nafasi yake kutoa hukumu kali ambayo hata aliyehukumiwa aliridhika.

Aliiongoza vyema jamii ya Wagogo na kuunganisha utawala wa Watemi wanne akiwemo Bilingi ambaye alikuwa Mtemi katika eneo la kati la Dodoma Mjini. Huyo ndiye aliyekuwa akistahili kuwa kiongozi wa watemi wenzake lakini alikubali kutoa madaraka hayo kwa Mazengo kutokana na busara zake.

Mazengo ambaye aliishi miaka 106, alikuwa na makazi yake katika katika Kijiji cha Mvumi Makulu, kilometa 50 kutoka Dodoma Mjini upande wa kusini. Alifariki dunia Januari 17,1967.

Jambo kubwa ambalo limekuwa likisifiwa na wazee wa Mvumi ni jinsi alivyotumia madaraka na mali zake kuwasomesha watoto wa maskini kiasi cha kuwasahau wa kwake ambao kwa wakati huo wakubwa walikuwa ni wasichana.

Moja kati ya watoto watano wa Mtemi huyo ambaye anaishi kwenye nyumba aliyoiacha Baba yake, Edina Mazengo anasema kuwa hakuna mtu anayeijali familia ya kiongozi huyo tangu siku walipomzika baba yao licha ya kuwa wapo waliosomeshwa na wengine kuachiwa maagizo mbalimbali juu ya familia yake.

Edina (56) anasema hawakutegemea hata siku moja kwamba wangeweza kuachwa kama watu wasiokuwa na kwao kutokana na ukweli kuwa baba yao aliwasaidia watu wengi ambao baadhi yao walifikia kuwa viongozi wakubwa nchini.

Anasema kuwa hata kauli ya baba yao ya kuifanya Mvumi Makulu kuwa ni sehemu muhimu katika historia haipo tena na kwamba wale aliowasaidia waliamua kuhamishia umuhimu huo katika Kijiji cha Mvumi Mission.

“Sisi tulibaki hivi kama unavyotuona ni moja ya familia ambayo ni maskini tena wa kutupwa. Hakuna hata mtu mmoja ambaye anajua kuwa sisi tulikuwa ni watoto wa Mtemi ambaye aliwasaidia na kuwaondoa katika umaskini. Tumeachwa bila ya kuwa na mbele wala nyuma.” anasema Edina na kuongeza:

“Kama ilivyo kwa watemi wengine baba alibahatika kuona wanawake wanne kati ya hao, watatu ndiyo alioishi nao katika kipindi chote na kubahatika kuzaa nao watoto kadhaa na huyu mmoja waliachana muda mfupi baada ya kumuoa na hawakuzaa naye watoto.”

Mtoto huyo ambaye ni maarufu kama Mwana Mtemi (mtoto wa mtemi) anasema hadi sasa ni watoto saba wa marehemu Mazengi walio hai, wanawake watano na wanaume wawili.

Kati ya watoto hao wote ni mmoja tu, Joyce Mazengo aliye na ajira. Anafundisha Shule ya Msingi Mvumi Makulu, wengine ni wakulima wadogo ambao kipato chao anasema ni cha chini mno.

Anatamani kama familia yao ingekuwa kama ile ya Mkwawa wa Iringa lakini wote waliachwa bila ya kusoma akisema kuwa hata mmoja ambaye alibahatika kuishia darasa la nane, Meshack naye ameishia kuwa mtu wa mitaani.

Mbali na kuwa baba yake alifariki wakati akiwa na umri wa miaka 13, Edina anasema alibahatika kuwa karibu naye kwa muda mwingi na kusikiliza mambo mengi ambayo alikuwa akiwaeleza wengine pamoja na kusisitiza namna alivyotaka watu waishi.

Moja ya mambo anayokumbuka ni kusisitiza kwake suala la amani na upendo kati ya jamii pamoja na kuwaasa wanafamilia kukaa katika hali ya upendo na amani wakati wote.

Anasema kuwa yapo mambo mengine ambayo anaamini kuwa Balozi Mstaafu Job Lusinde atakuwa na kumbukumbu nayo kwani mara aliporudi kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda alikuwa makalimani wa Mtemi Mazengo na hivyo alipata muda mwingi wa kukaa naye pamoja na kumweleza mambo mengi.

Anasema Lusinde ndiye aliyemtambulisha Baba wa Taifa, MWalimu Julius Nyerere kwa mtemi huyo huko Mvumi na tangu hapo viongozi hao walikuwa watu waliokuwa karibu.

Anasema mara baada ya Uhuru, Mtemi huyo alikuwa mmoja wa wazee wawili waliomuweka Mwalimu Nyerere katika kigoda kuashiria kubariki utawala wake kwa kufuata mila na desturi za Mwafrika.

Anasema pamoja na yote hayo, hata mambo ya msingi ya kumbukumbu ya kiongozi huyo yametelekezwa, akitlea mfano wa ambalo Mtemi Mazengo alikuwa akilitumia kutolea hukumu ambalo serikali iliahidi kulikarabati bila ya kutekeleza.

Vingine vilivyotelekezwa kwa kukosa hifadhi muafaka ni baiskeli ya kitemi aliyokuwa akiitumia pamoja na kiti alichokuwa akikalia wakati wa kutoa hukumu zake.

Anasema wanavyo vitu vingi vya marehemu baba yao ambavyo ni kumbukumbu nzuri kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho ambavyo kama vingetunzwa katika sehemu nzuri kwa umma, vingekuwa na manufaa makubwa katika historia ya nchi. Lakini anasema hawawezi kuvionyesha kwa mtu yeyote kwa kuwa vinaweza kupotea au kutelekezwa kama ilivyo hata kwa kaburi la baba yao.

Jambo kubwa analokumbuka ni kitendo cha baba yake kumweleza mama mzazi wa Edina ambaye ni mkewe wa tatu kuwa Nyerere ni miongoni mwa watoto wa familia yake akisema amemkabidhi fimbo ndogo nyeusi (ndogina) ambayo kwa Kabila la Wagogo ina maana kubwa sana na kumuasa kuwa kila atakakopita asithubutu kuiacha.

"Kwa kabila wa wagogo fimbo hiyo hupewa mtu anayetawazwa kuwa mkuu wa familia. Huambatana na upinde, kisu, shoka na ng’ombe jike au mtu anayetarajia kwenda kuposa na au ametokewa na jambo."

“Siwezi kuthibitisha moja kwa moja kuwa fimbo ile aliichukua kwa baba, lakini nina ushahidi wa kutosha kuwa baba alituita watoto wake na akasema kuwa ameamua kumfanya Julius (Nyerere) kuwa ni miongoni mwa watoto wake na akampa fimbo kama ilivyo kwa Kabila la Wagogo kuwa mtoto akikua anapewa fimbo na upinde.”

Anasema Mtemi huyo alijenga utamaduni wa kutoa zawadi kwa kila aliyefika kwake na hata watu kutoka nje ya nchi. Zawadi hizo zilikuwa ushanga na vitu vingine vidogo vilivyokuwa rahisi kubeba.
 
Sasa ndio iweje kama kapewa na Mizengo au Mwingine? Kwani kifimbo kina nini zaidi? Hata mimi nna kifimbo milichozaliwa nacho.

Wacheni kutuletea ushirikina wenu.
 
Back
Top Bottom