Indume Yene
Platinum Member
- Mar 17, 2008
- 2,948
- 710
Habari katika Mtanzania Daima zinadai kuna uwezekano Msekwa, Lowassa, Kisumo na wengine wakaonja Ukonga kwa kukaidi mahakama. Habari zaidi soma hapa chini:
Lowassa, Msekwa kortini
Wadaiwa kukiuka amri ya Mahakama Kuu
Lowassa, Msekwa kortini
Wadaiwa kukiuka amri ya Mahakama Kuu
na Happiness Katabazi
WASIWASI wa kuongezeka kwa idadi ya viongozi waandamizi, walio madarakani na waliongatuka wanaoweza kufikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali sasa umetawala Jiji la Dar es Salaam.
Kuibuka kwa wasiwasi huo, kunatokana na hatua ya Kampuni ya Uwakili ya Marando & Mnyele ya Dar es Salaam kuwasilisha ombi katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kutaka kukamatwa na kutupwa gerezani kwa vigogo kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kosa la kukiuka amri ya mahakama.
Ombi hilo lililowasilishwa na kampuni hiyo ya uwakili kwa niaba ya mteja wake, Ibrahim G. Alibhai, linaiomba mahakama hiyo itoe amri ya kukamatwa Baraza la Wadhamini wa CCM na viongozi wengine kadhaa wa chama hicho kwa kosa hilo.
Linaeleza kuwa, Alibhai ambaye ni mlalamikaji katika kesi ya msingi ya ardhi namba 81 ya mwaka huu, anawashtaki wajumbe wa Baraza la Wadhamini wa CCM, Mwenyekiti wa CCM Tawi la Gerezani, Ismail Idrisa, katibu wa chama wa tawi hilo na mtu mwingine anayetajwa kwa jina la Abdulrahman Twalibu.
Kwamba mlalamikaji anataka alipwe sh milioni 500 na CCM ambayo ilivamia nyumba yake, namba 107, kitalu namba 11, block 53, iliyoko Mtaa wa Sikukuu, Dar es Salaam, bila kujali kama yeye ni mmiliki halali wa nyumba hiyo.
Hati ya ombi hilo, inawataja wadhamini wa CCM ambao mahakama inaombwa iamuru wakamatwe kuwa ni pamoja na waziri wakuu wastaafu wawili, Rashid Mfaume Kawawa, Jaji Joseph Warioba na Edward Lowassa, ambaye alijiuzulu wadhifa huo mapema mwaka huu.
Wengine wanaotajwa kuwa wajumbe wa baraza hilo ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Pius Msekwa, Ahmed Ameir Ally, Khadija Jabiri, Peter Kisumo, Job Lusinde, Khamisi Juma Mkandara na Juma Ame Juma.
Hati ya maombi hayo ya mlalamikaji mahakamani, inaeleza kuwa aliwasilisha maombi hayo juzi, Desemba 22 mwaka huu. Inaeleza Mei 8 mwaka huu, Jaji wa mahakama hiyo, Alice Chinguwile, alitoa amri ya zuio dhidi ya wadaiwa wote, mawakala, wafanyakazi na watumishi kuacha kuendelea na ujenzi hadi shauri la msingi lililopo mahakamani hapo litakapomalizika.
Hati ilieleza Desemba 12 mwaka huu, mlalamikaji alitembelea eneo husika na kukuta wadaiwa wakiendelea na ujenzi, kinyume cha amri hiyo ya mahakama na kwamba wadaiwa wana mpango wa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo, ili waweze kulipangisha.
Mlalamikaji alidai alipata taarifa za kuendelea kwa ujenzi huo kutoka kwa wakili wake, Mabere Marando, aliyeeleza kuwa kitendo hicho cha kukaidi zuio la amri ya mahakama ni kukiuka amri halali ya mahakama iliyotolewa Mei 8, mwaka huu.
Mlalamikaji aliiomba mahakama kuwakamata na kuwatupa gerezani wadaiwa wote bila kutoa adhabu mbadala ya faini kwa kukiuka amri hiyo.
Alibhai alifungua kesi ya msingi chini ya kampuni ya mawakili hao katika mahakama hiyo, Aprili 14 mwaka huu dhidi ya wadhamini wa CCM na viongozi wa chama hicho, akitaka alipwe sh milioni 500 kwa kuwa waliingia katika eneo hilo bila idhini yake.
Kampuni ya mawakili hao ilieleza kuwa anayedharau amri halali ya mahakama kwa mujibu ya sheria ya mwenendo wa kesi za madai, sura ya 33 ya mwaka 1966, anapaswa kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani au kukamatwa kwa mali zake.