Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye maeneo machache ambayo nayafahamu vizuri ili niweze kuboresha Bajeti hii.
Kwanza nije kwenye mchango wa madini kwenye Pato la Taifa. Naungana na wenzangu kwamba mchango wake ni kidogo sana na matatizo ni Mikataba tuliyonayo. Kwanza labda nisahihishe neno moja tu ambalo linatumiwa hapa ndani ya Bunge, hakuna neno mrahaba kwenye Kiswahili, Kiswahili sanifu ni mrabaha, naomba mwangalie kwenye Kamusi zenu. Watu wote naona wanasema mrahaba, mrahaba nadhani hicho ni Kisukuma.
(Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mrabaha au royalty ya asilimia tatu ni ndogo sana. Namshauri Waziri wa Madini na Waziri wa Fedha, kaeni mpange royalty mpya, mrahaba mpya. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mbona wewe mwenyewe unasema mrahaba?
MHE. YETE S. MWALYEGO: Mrabaha mpya. Unajua mazoea tena. Napendekeza asilimia kumi ili tuweze kuongeza pato la Taifa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia limezungumzwa suala la lugha ya Kiswahili kwamba, tusiishie kutoa nyaraka na maelekezo bali tuchukue hatua madhubuti za kuhakikisha kwamba kauli za Serikali zinatekelezwa. Nataka niliahidi Bunge lako Tukufu kwamba sisi katika Wizara tumejiandaa kauli ile imepelekwa kwa Waziri wa TAMISEMI na yeye amepeleka kwa Halmashauri zote zilizopo chini ya TAMISEMI, tumepeleka kwa Waziri wa Utumishi na yeye pia ameshatoa maagizo kwa Ofisi zote za Serikali kuhakikisha kwamba zinatekelezwa lakini ushauri uliotolewa na Bunge tutaufuatilia na tutajitahidi kuhakikisha kwamba maelekezo haya yanatekelezwa ikiwa ni pamoja na kuona kwamba, tunatumia Kiswahili sanifu, saa kumi badala ya masaa kumi, mrabaha badala ya mrahaba na kadhalika. (Makofi)