Mpira sasa uko kwa Kikwete, Karume na CCM

Mzee wa Kale

Member
Feb 7, 2009
44
0
Zanzibar
Na Ally Saleh

NILIKUWA sehemu ya historia mwishoni mwa wiki nilipokuwa katika uwanja wa Kibanda Maiti na kushuhudia Chama cha Upinzani CUF kikitangaza kuwa kimemtambua Rais wa Zanzibar Amani Karume.

Ni moja ya siku ambazo uwanja huo ulijaa sana maana wananchi, wapenzi na wanachama wa CUF walikuwa wakitarajia kusikia kitu kufuatia taarifa kuwa Seif Sharif Hamad na Amani Karume wamekutana.

Kama kuna mkutano wa hadhara niliowahi kuhudhuria ambapo watu walitulia kusikiliza hotuba basi ulikuwa ni huo. Maalim Seif, taratibu alielezea msururu wa mivutano ya kisiasa ya Zanzibar kwa zaidi ya dahari na ukimya uliokuwapo hata ingeanguka sindano basi mlio wake ungesikika.

Lakini ghafla mambo yalibadilika pale Maalim Seif aliposema kuwa Baraza Kuu la Chama hicho katika mkutano wake uliofanyika siku hiyo limeamua kumtambua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume.

Kwa dakika sita hivi Maalim alibaki jukwaani lakini hakuna aliyetaka kumsikiliza. Ghafla zilisikika sauti za wananchi, wapenzi au wanachama wa CUF wakisema; “Hatutaki! Hatutaki!”. Maalim Seif akadhani ni maskhara. Lakini jinsi hali ilivyokuwa, ikamlazimu ashuke jukwaani na naamini hiyo ilikuwa ni moja ya siku ya unyonge sana kisiasa kwake.

Na kweli huo ulikuwa ni uamuzi mkubwa, mgumu, wenye athari hasi kufanywa na chama hicho lakini Waswahili wanasema inaonekana kuwa CUF imefikia hatua kwamba lazima walitafune jongoo kwa meno! Haina haja ya kukazia zaidi kuwa CUF kwa muda itakuwa imegawika mapande mawili -wanaoafiki na wasioafiki.

Na hiyo ndiyo hasara ambayo CUF itaipata hivi sasa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 ambapo tokea hapo inaeleweka upinzani na ukinzani uliopo baina yake na CCM na jinsi ambavyo chati yake kwa muda itashuka kutokana na maamuzi hayo, ambapo wengi wa wanachama wake wanaona kuwa hayakujali mateso, madhila, manyanyaso na masusuiko ambayo wanachama wa CUF wanapitia.

Na hata hivi sasa ambapo Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) linaendelea kupita mitaani, wanachama wa CUF wameendelea kubaguliwa kwa kunyimwa kwa makusudi Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (Zan ID) na hivyo kutoweza kuingia katika daftari hilo na hivyo kukosa haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Daftari lenyewe kwa hali nyingi limedoda kwa sababu baada ya majimbo 18 na siku 100 za kazi watu walioandikishwa ni 90,000 na hivyo kudhihirisha umuhimu wa CUF katika siasa za Zanzibar. Japokuwa Tume ya Uchaguzi inajidai imefanikiwa.

Wanachama wengi waliopinga kauli ya chama chao wanasema ni kwa sababu Katibu Mkuu Hamad hakuwaeleza wao watafaidi nini kwa uamuzi huo au pia wengine wakisema kuwa uamuzi huo ulikuwa ni mkubwa sana kutangazwa hadharani moja kwa moja na badala yake kwanza ingefanywa kazi ya kisiasa kabla ya kuushusha katika mkutano wa hadhara.

Kwa hivyo ina maana kuna wanachokosoa ni mbinu iliyotumika na wakati kwamba haukuwa muafaka. Kwa fikra zangu wote wako sahihi na hakuna haja ya kuendeleza malumbano katika hilo. Lakini bado hoja inabaki kuwa je, ni mbinu ipi ingeridhisha wote na ni wakati gani ungekuwa ni muwafaka kwa watu wote?

Kitu ambacho wapenzi na wanachama wa CUF walipaswa kukielewa ni kwamba kwa kawaida maamuzi hufanywa na viongozi na kwa kuwa viongozi wanatokana na wanachama basi itoshe kufahamu kwamba mawazo ya wananchi yanawakilishwa katika maamuzi anuai yanayofanywa na chama.

Kwa maneno mepesi; yale ya kumtambua Rais Karume hayakuwa maamuzi ya Baraza Kuu la Chama hicho kama Baraza, bali ni maamuzi ya wanachama kwa sababu wametoa mamlaka kwa Baraza lao ambalo limeona kwa wakati uliopo hiyo ndio njia bora ya kukipeleka chama mbele. Lakini kwa kulipigia kelele hilo pia ni muhimu kujua kuwa sauti ya umma pengine haikusikilizwa vyema.

Lakini pia maamuzi magumu kama hayo yameshafanywa karibuni katika nchi ya Kenya na Zimbabwe ambapo hata baada ya Wapinzani kuibiwa waziwazi katika uchaguzi, lakini hatimaye walitambua ushindi wa waliotangazwa na walikubali kuunda nao Serikali.

Itakumbukwa kuwa yalipokwama mazungumzo ya Mwafaka ni kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilishindikana kwa kipengele cha CUF kutomtambua Karume. Ila kazi ya CUF sasa imemalizika, wamefanya kitendo cha kiungwana na kukomaa kisiasa.

Sijui kama CCM imeshaamka kujua kuwa matamshi ya CUF ya juzi yamefanya mpira sasa uwe upande wao. Kwamba sasa macho ya kila mtu yanakitizama chama hicho na wahusika wake wakuu Rais Jakaya Kikwete na Rais Karume mwenyewe.

Kwanza litakuwa ni kosa kubwa kwa CCM kujaribu kulitumia tamko la CUF kumtambua Karume kuwa ni udhaifu. Njia yoyote ya kujejea, kukebehi naamini litajenga ukuta wa chuki badala ya upendo. Pili, itakuwa ni uungwana wa kisiasa kwa CCM kuwapa fursa CUF kupita katika kipindi hiki kigumu kwa mtizamo wa kuwarudishia mpira baada ya kujeruhiwa yaani.

Tatu, ni kuwa CCM, JK na Karume wahakikishe kuwa kila linaloweza kutekelezwa wakati huu katika suala la Mwafaka basi litekelezwe. Japo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliobaki, kwa mfano kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutarudisha sana imani. Pia Karume atekeleze kwa haraka wajibu wake wa Kikatiba wa kuteua wajumbe wawili wa Baraza la Wawakilishi kutoka Chama cha CUF.

Tano, mchakato wa kutengeza Katiba imara zaidi ya kuwapo kwa Serikali ya Pamoja baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 uanze haraka na tabaan uwe shirikishi. Dhana ya kwamba Katiba ni mamlaka ya chama tawala na Serikali imepitwa na wakati.

Sita, ni suala la DKWK. Daftari hilo halijafika mbali na CUF wana wasiwasi mkubwa na uandishi wake.

Na kama hivyo ndivyo basi Serikali ijenge mazingira ya kufanya uhakiki kwa vile daftari hilo ni kama kwamba ndio limeshikilia amani ya nchi kwa sasa.

Saba, suala la Zan ID hapana shaka limezusha zogo kubwa. Na mbali ya sababu za Masheha kuwakatalia wenye haki, lakini pia watu wengi wamekosa kuandikishwa kwa sababu ya kukosa vyeti vya kuzaliwa na baadhi ya walivyonavyo wamekuwa wakiambiwa kuwa havitambuliwi.

Binafsi katika eneo la Mji Mkongwe nimekusanya majina 80 ya watu wasio na Zan ID lakini wana vyeti vya kuzaliwa na wamekataliwa na Masheha.

Lakini kuna majina mengine 220 ya watu wasio na Zan ID na hawataweza kupata vitambulisho hivyo kwa sababu hawana vyeti vya kuzaliwa. Kwa nia njema ya kutambuliwa Karume lazima Serikali ichukue hatua ya kutangaza utaratibu maalum wa watu kupata Zan ID.

Bila ya shaka baada ya muda vumbi la kishindo cha CUF kumtambua Karume litasita. Lakini wakati vumbi linatua CCM, Kikwete na Karume wajue mpira tayari uko kwao na ijapokuwa watatamani kutumia tukio hilo kwa faida ya kisiasa lakini pia naamini wanajua kuwa siasa ni mbinu za nipe nikupe na ukijifanya khiyana na bakhili upokee wewe tu, iko siku utaumbuka, maana kutakuwa hakuna tena cha kukupa isipokuwa damu na roho za watu. CCM, Kikwete na Karume wasisubiri kufikia hatua hiyo.

+255 777 4300 22

www.eternaltourszanzibar.net

jumbamaro.blogspot.com
 
Back
Top Bottom