Mnyika bado alia na Dowans, Rex na Serikali

Paparazi Muwazi

JF-Expert Member
Dec 23, 2007
310
79
MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) ameitaka serikali kutotumia kisingizio cha maamuzi ya mahakama kuharakisha mpango wa kuilipa Dowans kwa fedha za Watanzania au kubebesha mzigo huo kwa wateja wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana Mnyika alisema iwapo serikali inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete imezidiwa na Dowans kwa sababu ya kujiingiza katika mikataba mibovu inapaswa kuwabebesha deni hilo mafisadi na wahujumu uchumi waliosababisha hali hiyo.

Hatua hiyo ya Mnyika imekuja siku moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupitia Jaji Fauz Twaibu, kutupilia mbali ombi la TANESCO lililotaka mahakama kuwaruhusu kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyoruhusu tuzo ya kampuni ya Dowans iliyopewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya Kibiashara (ICC) isajiliwe hapa nchini.

Tuzo hiyo ya dola za Marekani milioni 65 (takriban sh bilioni 94) ilitolewa Novemba 15 mwaka 2010 na ICC ikiamuru TANESCO iilipe Dowans kiasi hicho cha fedha kwa kosa la kuvunja mkataba kinyume cha sheria.

Mnyika ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini alisema mahakama ilichotupilia mbali ni ombi la ridhaa ya kukata rufaa kutoka mahakama kuu; hata hivyo mahakama imeeleza bayana kwamba TANESCO wana njia nyingine ya kufika mahakama kuu tofauti na njia waliyopitia.

Alisema hata hivyo uamuzi huo wa mahakama unaibua mjadala mwingine kuhusu uwezo na dhamira ya wanasheria wa Serikali na TANESCO katika kesi hizo kwa kuzingatia mtiririko mzima wa masuala na matukio katika majadiliano ya mkataba wa Richmond na hatimaye Dowans kati ya mwaka 2006 mpaka 2012.

Alieleza kwamba mashaka zaidi yanaongezeka kutokana na mgogoro wa kimasilahi dhidi ya Kampuni ya Uwakili ya Rex Attorney ambayo pamoja na kupoteza uhalali wa kimaadili katika kesi zinazoihusu TANESCO na Dowans kuhojiwa.
“Katika mazingira haya namtaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kueleza kwa umma mabilioni mangapi yamelipwa na TANESCO mpaka hivi sasa kwa kampuni hiyo na sababu za kuendelea kuilipa kampuni hiyo pamoja na kuwepo kwa uzembe wa wazi wenye kulisababishia hasara taifa.

“Umma uzingatie kwamba gharama kama hizi za Dowans na mikataba mingine mibovu ndizo zinazoongeza mzigo wa gharama za uendeshaji za TANESCO na kuchangia katika ongezeko la bei ya umeme na ongezeko la gharama za maisha kwa ujumla,” alisema Mnyika.

Alieleza kuwa maelezo hayo ni muhimu yakatolewa na serikali kwa kina badala ya kuendelea kueleza dhamira ya kukata rufaa bila kuchukua hatua za kusafisha safu yake ya kisheria ambayo imeiingiza TANESCO katika mikataba mibovu na madeni makubwa.

Alisema iwapo hoja binafsi aliyoiwasilisha Ofisi ya Bunge kutaka utekelezaji wa maazimio yote yaliyobaki kuhusu utekelezaji wa mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC ingejadiliwa bungeni, hatua zaidi zingechukuliwa kwa mafisadi na wahujumu uchumi waliohusika na Richmond, Dowans na masuala mengine ya kisheria yanayosababisha mzigo mkubwa kwa TANESCO na wananchi

Kutoka:Mnyika bado alia na Dowans
 
Back
Top Bottom