Mko wapi wanaharakati?

Offish

Senior Member
Aug 14, 2008
170
2
Hakuna ubishi kuwa Tanzania inayumba kwa kukosa uongozi makini. Nyufa zimetapakaa kila pembe ya nchi na ufisadi unazidi kuzifumua. Mchango wa wanaharakati unahitajika sasa kuliko wakati wowote ule ili kuinusuru Tanzania ilyofumwa vema isifumuliwe kupita kiasi na mafisadi.

Hakuna ubishi kuwa bunge letu limepoteza mwelekeo kwani halina watetezi wa watu tena bali limejaa wapenda uheshimiwa na maslahi binafsi. Angalia walivyomshambulia Dr Slaa ati kwa kusema ukweli kuwa wabunge wanapata mishahara mikubwa isiyokatwa kodi wakati mishahara ya wafanyakazi iko pale pale na inakatwa kodi hata baada ya tume iliyoundwa na serikali miaka mitatu iliyopita kushauri kima cha chini kwa watumishi wa serikali kiwe angalau Shs350, 000.

Si wabunge wa chama twawala wala wale wa upinzani wanatetea ufisadi kwa mgongo wa kutunza siri za serikali. Bila aibu wanamzomea mtetezi wa wanyonge (Dr Slaa) Bungeni kwa juhudi zake za kuweka wazi njama za mafisadi. Bado tunawahitaji waheshimiwa hawa?

La hasha, tunawahitaji wanaharakati watusadie kuanzisha vuguvugu la kulikataa bunge la sasa na kuanzisha mfumo mwingine wa uwakilishi. Tunahitaji sheria ya mgombea binafsi ipitishwe kwani ni haki yetu kikatiba kama mahakama kuu ilivyoamua katika kesi iliyofunguliwa na Mtikila.

Tunahitaji wabunge wa kujitolea badala ya waheshimiwa hawa maslahi ambao hawaguswi na umasikini na matatizo mengine lukuki yanayotukabili watanzania tulio wengi.

Waheshimiwa hawa wanadiriki kutetea njiwa wawezeshwe ili wazaliane kwa wingi. Wanaazima hata hoja za nchi jirani za kulazimisha tohara ati kwa kuwa utafiti umebaini kuwa tohara kwa wanaume inasadia kupunguza maambukizi ya ukimwi.

Bila kutumwa na wanaowawakilisha Bungeni, wanajadili hoja hizi hadi mapovu yanawatoka midomoni. Ati bila haya hatimaye wanaomba waongezewe mishahara isiyokatwa kodi kwa kujadili pumba hizi masikioni mwa watanzania wawapo bungeni! Inasikitisha sana kumsikia Waziri Mkuu, mtoto wa mkulima, pia anatetea wabunge maslahi!

Wametukatisha tamaa watanzania, hatuwahitaji wao wala mfumo uliowapeleka Bungeni. Tunahitaji mfumo mpya wa kupata wawakilishi wenye uchungu na nchi hii na watu wake pia, hao wapo wa kumwaga ila mfumo uliopo unawatupa nje ya milango ya Bunge.

Mfumo unaoweka mbele maslahi ya vyama vya kisiasa kuliko ya Taifa hili hautufai tena, unapofusha hata mbongo za maprofesa wetu wanaolazimika kufuata bendera za vyama badala ya kusimimia mising ya taaluma zao. Mfumo huo unawakatisha tamaa wataalamu, wanadiriki hata kupindisha 'naked scientific facts' ili wapate fadhila toka kwa wanasiasa wanaoshikilia mpini wa nchi hii.

Wako wapi wanaharakati wainusuru nchi kutoka katika giza nene linalotanda katika nchi hii ili wapiga kura wengi walioko vijijini hususan kanda ya ziwa waelewe mustakabali wa nchi yao na kufanya maamuzi ya kuziba nyufa zilizofumuka kila siku badala ya kuendelea kuburuzwa na mazingaombwe ya vijisent, T-shirts, khanga na baiskeli toka kwa mafisadi.

Wanaharakati wawaelimishe waqpiga kura ili wasikatae vijisenti na mazingaombwe yote hayo kwani ni haki yao iliyoporwa na kurudishwa kwa mlango wa nyuma. Wapiga kura wasileweshwe kwa mazingaombwe hayo bali wafanye maamuzi kwa kuzingatia maslahi ya nchi.

Nawasilisha kwenu wana JF kwa uchungu mkubwa nikitegemea ujumbe utafika na kufanyiwa kazi ili watoto wetu wasijeyachapa viboko makaburi yetu kwa kukodolea macho maradhi yanayoitafuna nchi hii bila kuchukua hatua angalau ya kuchangia katika safu hii. Wasalaam....
 
Back
Top Bottom