Mkanganyiko katika Gharama za Vocha za Simu

serikali imetoa tamko kuwa haijapandisha bei za vocha na hao wafanya biashara wanaopandisha wanawahujumu wateja. bei ni kama ilivyochapishwa kwenye vocha yenyewe. ukichajiwa zaidi peleka huyo mhujumu kituo cha polisi

Hii habari nikiwa kama mmoja wa wauzaji wa rejareja wa Vocha za simu, yawezekana ni kweli serikali haijapandisha bei ya vocha za simu. Waliopandisha bei ni mawakala wa makampuni hayo na hao ndio wanaosababisha sisi wauzaji wa rejareja kuuza kwa bei ya juu.

Kinachotakiwa hapa makampuni hayo ya simu pamoja na mawakala wao ndio waliweke sawa hili suala.

Na kusema wauzaji wanaouza kwa bei ya juu wakamatwe ni kuwaonea tu. Labda hao mawakala ndio wakamatwe kwa kutuuzia vocha hizo kwa bei ya juu. Kwa sisi wauzaji wa rejareja hatuna tatizo japokuwa ndio kuna baadhi wana matatizo.

Ukifuatilia kwa makini habari hizi kwa vyombo vya habari kama vile magazeti hakuna hata mwandishi mmoja aliyeondea na mawakala wa makampuni hayo pamoja na wauzaji wenyewe wa vocha.

Jamani tuwe makini.
 
Nafikiri kama kweli gharama za vocha zimepanda, kitu sahihi cha kufanya ni kubadilisha hizo gharama hata kwenye vocha zenyewe, tatizo la wafanyabiashara wa kibongo ni kupenda kukamua wenzao pale wanapopata kisingizio cha kufanya hivyo. Nakumbuka nyakati fulani huko nyuma tulitangaziwaga kwamba gharama za mafuta zimeshuka lakini wauza mafuta wakagoma kushusha bei kwa kisingizio kuwa mafuta wanayouza kwa wakati huo ni stock ya yale waliyokuwa wamenunua kabla ya bei kushuka hivyo wakishusha bei watapata hasara.

Kama gharama za vocha kwenye vocha zenyewe hazijapanda na wauzaji wanawapandishia wateja kwa kisingizio cha bajeti mpya, huo ni wizi wa wazi wazi even in the face of law. Wamiliki wa makampuni ya simu wanatakiwa ku-respond to this for it to be justified, otherwise ni wizi mtupu!
 
jamani huu ni uhujumu uchumi kwa kiasi kikubwa haiwezekani serikali iseme watanzania tulipe kodi kuendeleza taifa letu kisha hawa wenye kushika au kumiliki haya makampuni kutolipa kodi kabisa nasema hivi kwa sababu wao kupandisha bei ya vocha ni wizi maana hizi 100tsh tunazotozwa zinatozwa kodi gani kama sio 0%
pia makato ya % yapo kwenye fedha halisi iliyopo kwenye vocha kama 1000 na sio 1100.
imekuwa ni jambo la kawaida watu au wafanyabiashara kuweka stoku kubwa kwenye bidhaa zao wakijua bajeti yetu itapanda hivyo kuendelea na stoku ya zamani na kuuza kwa bei mpya HUU NI WIZI na UFISADI
ushauri kama itawezekana:
kuwepo na lebo ambayo itakuwa kwen ye kiwango cha TBS itakayoonesha ni stock ya mwaka uliopita ili watu wasiumizwe kiasi hichi.
pili: TRA waanze kazi mapema kwa hawa wadogo katika maduka; sasa takribani wanaotumia simu tz ni 13mi sasa zidisha mara 100 utaona fedha inayoibiwa ndipo utajua ni kiasi gani tunaibiwa.
 
Sasa nyie watu wa Jamiiforum, mbona hamfuatilii mkatupa feedback juu ya kupanda kwa vocha?
 
Kwani tatizo la kuchapishwa 1000 ni nini? Wateja tunajua kuwa tunapata credit ya 1000, tunajua kuwa bei ni 1100. Sio kwamba tunanunua na matumaini ya kukuta credit ya 1100. Yaani hatujadanganywa kuzinunua tunafanya maamuzi wenyewe, na tunatoe hela huku tukijua tunachopata.

Sio rahisi wakakubali kuingia hasara ya mabilioni ya shiling huku wakisubiri vocha mpya.

tatizo lipo mkuu, kama vocha imeandikwa kuwa ni tsh 1000 hiyo ndio bei yake na sio 1100, mimi naona mteja anadanganywa na siku zote tanzania yetu mlaji (mnunuzi) ndio wa kupata hasara, kwa maana hata kama kupanda kwa kodi imepanda lini na bei wamepandisha lini, je zingekuwa kodi zimeshuka si tungeambiwa kushuka kwa bei ya vocha hadi zitoke nyingine ila kwa kuwa ni kupanda basi kufumba na kufumbua!

sidhani kama hayo ni maamuzi ya wateja bali ni kwa kuwa hakuna namna unahitaji mawasiliano huna namna lazima ununue vocha ukwelu inawauma wananchi, na inwaumiza mno, achilia mbali gharama za juu za simu ambazo wananchi wamekuwa wakilia siku zote!
nadhani unazungumza toka dunia nyingine ila kama ni tanzania yetu watu walivyochoshwa na gharama za simu sidhani kama hayo ni sahihi!
 
Jamani, hebu kwanza tusome habari hii kutoka gazeti la Mtanzania la leo kama ifuatavyo:::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::


ZAIN: Msipandishe bei vocha zetu, ziuzwe kama zamani

Penina Malundo na Hussein Issa

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Zain imewataka watu wanaouza vocha za kampuni hiyo kwa bei ya juu tofauti na zilivyoandikwa kuacha mara moja ili wateja wa simu waendelee kujimwaga nchini.


Imesema kampuni haijaongeza bei ya vocha zake na wateja wake wanapaswa kununua kwa bei ya zamani iliyozoeleka.


Wakati kampuni ya Zain ikiwapoza wateja wake, kampuni zingine za simu hususan Vodacom, Tigo na Zantel hazijatoa taarifa yoyote kupinga kuongezeka kwa bei hiyo, jambo ambalo linajenga hisia kwamba huendakampuni hizo zimepandisha bei.


Meneja Mawasiliano wa Zain Tanzania Beatrice Mallya alisema katika taarifa iliyotolewa na Zain Jijini Dar es Salaam kwamba wateja wa Zain wanapaswa kununua vocha za Zain kwa bei ya kawaida ya Sh 5000, 2000, 1000, 500 si vinginevyo.


"Hatujapandisha bei kwa mawakala wetu wanaonunua kwa bei ya jumla na pia tuna makubaliano nao wauze kwa bei tuliyokubaliana, hivyo bei ya vocha zetu kwa mtumiaji wa mwisho haijapanda na inabaki vile vile," alisema Beatrice.


Aidha alisema wauzaji wanaowauzia wateja wa mwisho ikiwemo wale wa Zain Chap Chap nao wanapaswa kuuza kwa bei iliyozoeleka.


"Napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha wateja wetu kwamba wanaweza pia kutumia akaunti zao za Zap kununua muda wa maongezi kupitia simu zao za mkononi," alisema .


Wakati huohuo wafanyabiashara wa vocha za simu bado wanaendelea kuuza vocha hizo kwa kuongeza bei kwa kisingizio cha kupanda kwa ushuru kama ilivyotangazwa katika bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2009/2010.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi baadhi ya wafanyabiashara hao waliopo jijini Dar es Salaam wanaouza vocha hizo kwa bei za reja reja, walisema kuwa upandaji huo umelazimishwa na wauzaji wa jumla kwa kupandisha bei.


"Sisi hatuwezi kupunguza wakati tunaingia hasara kwani tunauziwa kwa jumla 950 badala ya 940, sasa hapo faida yake inakuwa ni ndogo, tutaua biashara zetu,"alisema Pendo John anayeuza vocha zake maeneo ya Mabibo


Mwananchi ilishuhudia watu wakilalamikia bei hizo mpya za vocha huku wakisema utekelezaji wa bajeti bado, sasa inakuwaje hawa watuuzie kwa bei wanazotaka wenyewe? alihoji mteja wa vocha huyo ambaye jina lake halifahamika.


Kutokana na uchunguzi uliofanywa jana na Mwananchi maeneo mbalimbali jijini, ilibainika kuwa aina zote za vocha zimepanda bei.


Gharama za vocha zilivyopanda ukilinganisha na bei ya kwenye mabano ni pamoja na ile ya Sh 500 (550), 1,000 (1,100), 2,000 (2,200), 5,000 (5,500), 10,000 (11,000), pia imebainika bei hizi zimeleta usumbufu kwa watuamiaji wa simu za mikononi.
:::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::::


Sasa hapa tunaona kuwa ni Kampuni moja tu ya ZAIN ndiyo pekee haijapandisha bei ya vocha lakini hebu soma aya hii
(Wakati kampuni ya Zain ikiwapoza wateja wake, kampuni zingine za simu hususan Vodacom, Tigo na Zantel hazijatoa taarifa yoyote kupinga kuongezeka kwa bei hiyo, jambo ambalo linajenga hisia kwamba huendakampuni hizo zimepandisha bei.)

Haya makampuni mengine ndio tatizo, jiulize kwanini hawataki kutoa tamko lolote kuhusu vocha za simu kama walivyofanya ZAIN?

Mteja wa mwisho ataendelea kulalamika kuhusu bei hizo lakini hakuna atakayeshusha bei hizo vinginevyo akose mawasiliano au ahame mtandao.
 
Samani kidogo habari hiyo imetoka gazeti la Mwananchi. I'm sorry for error typing
 
Nimenunua Vocha za 50,000 mbili leo za Voda kutoka Shivacom pale. Total price 97,000/= so nimeokoa buku 3! Hela ya Bia ishapatikana!
 
hivi nini kinaendelea..jana nmemskia beatrice singano akikana wao zain kupandisha bei..na yeye kama msemaji wa zain tunamwamini...lakini mitaani bado twanunua kwa bei kubwa sana vouchers..hii haijakaa vizuri kwakweli.
 
Bosi wa Uhusiano wa Vodacom Tanzania Mwamvita Makamba akiongea leo na wanahabari juu ya libeneke la bei za vocha za simu za mkononi ambapo ghafla tu wauzaji walianza kupandisha bei kwa kuongeza shilingi 100 kwa kisingizio cha kodi
Bei ya Vocha za muda
wa maongezi za Voda wala hazijapanda

Dar es Salaam July 6, 2009:
Kampuni ya simu za mkononi, Vodacom Tanzania, haijapandisha bei za vocha za muda wa maongezi kwa wateja wa jumla na hivyo bei sokoni haitakiwi kupanda.

Akuzingumza Jijini mchana huu, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha Vodacom Tanzania, Mwamvita Makamba alisema kilichotokea ni kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imebadilisha mfumo wa wa ukusanyaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ambao umesababisha badiliko dogo katika gharama za usambazaji kwa wateja wa jumla.

Alisema mabadiliko hayo ya mfumo wa ukusanyaji wa kodi hayatakiwi kuleta mabadiliko katika bei ya uuzajiwa vocha sokoni.

Mwanvita alitoa ufafanuzi huo kufuatia hatua ya baadhi ya wauzaji wa rejareja wa vocha za muda wa maongezi kupandisha bei ya vocha hizo kwa kati ya shilingi 100 na 200, mathalani vocha ya Sh,1000 inauzwa kwa bei ya shilingi 1200, Sh.2000 inauzwa kwa Sh.2200. Sh.5000, inauzwa kwa Sh.5200 au zaidi.

"Kubadilika kwa mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya ongezeko la thamani hakupaswi kubadilisha bei kwa wauzaji wa rejareja, natoa wito kwa wauzaji hao kuacha kupandisha bei ya vocha hizo kwani mabadiliko madogo ya kodi yaliyofanywa hayana madhara kwao," alisema.


Mwanvita.Alifafanua kwamba Vodacom hivi sasa inakutakana na wauzaji wa jumla wa vocha ili kuhakikisha kwamba bei za vocha zinabaki na thamani kama zinavyotakiwa sokoni, yaani vocha ya 1,000 inauzwa kwa 1,000 na si vinginevyo.
Baadhi ya wateja wa Vodacom wamekuwa wakilalamika kufuatia kupanda huko kwa bei kwa madai kwamba hakuna tangazo lolote la Vodacom lilowataarifu mabadiliko hayo ya bei na kwamba kupanda huko kunawaumiza.
Vodacom Tanzania ndiyo mtandao unaoongoza hapa Tanzania ukiwa na wateja zaidi ya milioni 6 na ukiwa umesambaa nchini nzima.
Imetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano
Mwamvita Makamba
Kwa niaba ya Vodacom Tanzania

SOURCE: issa michuzi
 
Bosi wa Uhusiano wa Vodacom Tanzania Mwamvita Makamba akiongea leo na wanahabari juu ya libeneke la bei za vocha za simu za mkononi ambapo ghafla tu wauzaji walianza kupandisha bei kwa kuongeza shilingi 100 kwa kisingizio cha kodi
Bei ya Vocha za muda
wa maongezi za Voda wala hazijapanda

Dar es Salaam July 6, 2009:
Kampuni ya simu za mkononi, Vodacom Tanzania, haijapandisha bei za vocha za muda wa maongezi kwa wateja wa jumla na hivyo bei sokoni haitakiwi kupanda.

Akuzingumza Jijini mchana huu, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha Vodacom Tanzania, Mwamvita Makamba alisema kilichotokea ni kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imebadilisha mfumo wa wa ukusanyaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ambao umesababisha badiliko dogo katika gharama za usambazaji kwa wateja wa jumla.

Alisema mabadiliko hayo ya mfumo wa ukusanyaji wa kodi hayatakiwi kuleta mabadiliko katika bei ya uuzajiwa vocha sokoni.

Mwanvita alitoa ufafanuzi huo kufuatia hatua ya baadhi ya wauzaji wa rejareja wa vocha za muda wa maongezi kupandisha bei ya vocha hizo kwa kati ya shilingi 100 na 200, mathalani vocha ya Sh,1000 inauzwa kwa bei ya shilingi 1200, Sh.2000 inauzwa kwa Sh.2200. Sh.5000, inauzwa kwa Sh.5200 au zaidi.

"Kubadilika kwa mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya ongezeko la thamani hakupaswi kubadilisha bei kwa wauzaji wa rejareja, natoa wito kwa wauzaji hao kuacha kupandisha bei ya vocha hizo kwani mabadiliko madogo ya kodi yaliyofanywa hayana madhara kwao," alisema.


Mwanvita.Alifafanua kwamba Vodacom hivi sasa inakutakana na wauzaji wa jumla wa vocha ili kuhakikisha kwamba bei za vocha zinabaki na thamani kama zinavyotakiwa sokoni, yaani vocha ya 1,000 inauzwa kwa 1,000 na si vinginevyo.
Baadhi ya wateja wa Vodacom wamekuwa wakilalamika kufuatia kupanda huko kwa bei kwa madai kwamba hakuna tangazo lolote la Vodacom lilowataarifu mabadiliko hayo ya bei na kwamba kupanda huko kunawaumiza.
Vodacom Tanzania ndiyo mtandao unaoongoza hapa Tanzania ukiwa na wateja zaidi ya milioni 6 na ukiwa umesambaa nchini nzima.
Imetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano
Mwamvita Makamba
Kwa niaba ya Vodacom Tanzania

SOURCE: Issa michuzi
 
Kuhusu aya hii:
------------------------------------------------------------
Kampuni ya simu za mkononi, Vodacom Tanzania, haijapandisha bei za vocha za muda wa maongezi kwa wateja wa jumla na hivyo bei sokoni haitakiwi kupanda.
------------------------------------------------------------

Si kweli maana leo nimewahoji wauzaji wa jumla kama Simbatelecom kuhusu kupanda kwa bei ya vocha za Vodacom. Walinijibu kuwa Vodacom wenyewe ndio waliotupandishia bei hivyo na sisi yatupasa kupandisha.

Kwa hiyo kinachotakiwa kufanyika hapa ni hawa mabosi wa Vodacom kuongea na mawakala wao. Au kweli wamepandisha wanatuficha?
 
Mkanganyiko wa Mauzo ya Vocha za Simu kwa Bei ya Rejareja
Serikali inastahili lawama

Na Mwana wa Haki

NILIPOKUWA masomoni nchini Marekani, kwa masomo ya Stashahada (ya kwanza) ya Uchumi, huku nikiwa nimeongeza “nondo ndogo” (wenyewe wanaita Minors) za Uandishi wa Habari na Sayansi ya Tarakinishi, sikuwahi hata siku moja kufikiria kwamba ningeweza kunufaika na taaluma hii ya uchumi, haswa katika uchambuzi wa mkanganyiko ambao umejitokeza kwenye Bajeti ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2009-2010.

Serikali, kupitia Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango, imepitisha bajeti ambayo inaathiri mwenendo mzima wa kiutendaji wa biashara ya mawasiliano kwa simu za mkononi, yaani, Mobile Cellular Telephony, kama ifuatavyo:

Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2009-2010 imeainisha kwamba, mabadiliko yaliyofanyika kwenye Sheria ya Ongezeko la Thamani, hususan kwenye sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi, ni kama ifuatavyo:

“72. (x) Kutoza kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye muda wa maongezi kwenye simu kwa kutumia bei halisi inayoonyeshwa kwenye vocha badala ya bei nafuu anayotozwa muuzaji wa jumla. Lengo ni kuhuisha mapato yatokanayo na chanzo hiki cha kodi na kuziba mwanya wa ukwepaji kodi;”

Kidonda hiki kinaleta maumivu makubwa kwa wauzaji wa jumla wa vocha za matumizi ya simu za mkononi, lakini, kana kwamba kidonda hiki hakikutosha, Serikali yetu “tukufu” ikaongeza kingine, kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa:

“74. (i) Kutoza Ushuru wa Bidhaa katika huduma za simu za mkononi pale vocha au muda wa maongezi unapouzwa badala ya kusubiri hadi muda wa maongezi utumike; na”

(ii) Kurekebisha kwa sailimia 7.5 viwango maalum vya Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa zinazotozwa ushuru huu, isipokuwa zile za mafuta ya petroli. …”

Sipendi, narudia, sipendi kuonekana kwamba mimi ni “mtoto mtukutu”, lakini nauliza: Aliyefanya marekebisho haya yasiyo na kichwa wala miguu, alikuwa anatumia dawa aina gani za matatizo ya akili?

Hii haingii akilini hata kidogo. Hata kidogo!

Tuanzie kwenye suala la kodi ya Ongezeko la Thamani, au Value Added Tax (VAT). Hapo awali, ina maana kwamba VAT ilikuwa inatozwa KABLA au BAADA ya gharama inayooneshwa kwenye vocha? Kwa mfano, hapo awali – kabla ya mkanganyiko huu wa kiwendawazimu – vocha ya thamani (iliyochapishwa) ya Shilingi Elfu Moja (TZS 1,000/=) ilijumuisha yafuatayo:

Gharama halisi ya muda wa maongezi, bei ya jumla TShs. 750/=
(ikijumuisha kodi nyinginezo)

Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT 20%) TShs. 150/=
(hii imejumuishwa kutoka kwenye thamani
halisi ya vocha)

Jumla ya Thamani (pamoja na VAT, bei ya jumla) TShs. 800/=

Kwa wale wataalam wa masuala ya kodi, naomba mnikosoe, lakini hivi ndivyo mimi nilikuwa nimeelewa, kwamba, VAT ilikuwa inatozwa kwa kuzingatia gharama halisi ya vocha, kwa bei ya jumla.

Kwa kuwa tayari mwuzaji wa jumla amelipa VAT, mwuzaji wa rejareja anauza vocha hiyo kwa thamani ya TShs. 1,000/=, na kujipatia faida ya TShs. 200/=.

Kilichobadilika hapa ni VAT kutozwa kwa gharama halisi ya vocha, yaani, TShs. 1,000/=! Hapo, ukifanya hesabu, kwa kiwango kipya cha asilimia 18, unapata TShs. 180/=, na kuifanya bei mpya ya hiyo vocha kuwa TShs. 1,180/=!

Ninauliza, toka lini thamani ya Shilingi Elfu Moja ikawa Shilingi Elfu Moja na Mia Moja na Themanini? Huu wi wizi wa mchana huu?

Hiyo tofauti, ya nyongeza ya TShs. 180/=, nani anatozwa? Ni mteja, mtumiaji wa mwisho. Bei ya jumla iko pale pale, na mwuzaji wa rejareja bado ananunua (labda?) kwa bei ile ile, ila anakuuzia wewe na mimi kwa bei mpya, ambayo bado ina utata… bei mpya isiyo rasmi ikaja kuwa TShs. 1,100/= (kwa vocha ya TShs. 1,000/=), TShs. 2,200/= (kwa vocha ya TShs. 2,000/=), TShs. 5,500/= (kwa vocha ya TShs. 5,000/= na TShs. 11,000/= (kwa vocha ya TShs. 10,000/=)!

Astghafirullah!

Wizi mtupu!

Suala la pili – la Ushuru wa Bidhaa – wala sitaligusia, maana hili la kwanza bado halijakaa vizuri. Bado sana! Pamoja na usomi wangu wote, tena wa “nondo” ya nguvu ya Marekani, hii haijaniingia akilini. Nawaomba wanazuoni wenzangu wanisaidie hapa, maana “imekaa vibaya” mno hapa!

Nikiangalia kwa upande wa sheria, hususan kwa kuwalinda watumiaji wa mwisho, walaji, mimi na wewe, Serikali, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA), iliunda Kamati ya Mashauriano ya Walaji ya TCRA, yaani, TCRA-Consumer Consultative Council, ambayo jukumu lake kuu ni kuhakisha kwamba haki za walaji zinalindwa KILA WAKATI!

Cha ajabu ni kwamba, mitaani tunauziwa vocha kwa “bei ya kuruka” na TCRA-CCC wamekaa kimya! Kimya kabisa! Tuli, kama vile mtu anayenyolewa kichwa kwa maji na wembe, asijiguse wembe ukamkata kichwani! Lahaula! Mambo gani tena haya? Ina maana huko TCRA-CCC hawakuliona hili? Mbona hawajatoa tamko haraka na kuitisha Mkutano wa Dharura na watoa huduma (au ni hujuma) wa mawasiliano ya simu za mkononi, ili ufumbuzi upatikane? Kwa nini mlaji anapuuzwa “kihuni huni” wakati ni yeye ndiye anayetoa fedha mkononi mwake, kuwalipa wenye mitandao hii ambayo sasa inaonekana kuwa “dili” la aina yake? Nadhani mnanielewa nikisema “dili” sihitaji kuongezea.

Mimi napenda kutoa ushauri wangu, kama ifuatavyo, katika hitimisho la makala “tete” hii:

1. Ili kuonesha hasira zetu, sisi, kama walaji, tuendeshe mgomo baridi wa saa 24, wa kutopiga simu au kutuma ujumbe mfupi, kuwapa somo watu hawa kwamba kimya chetu kisitambulike kama unyonge wetu, sisi si wanyonge katu!
2. Baada ya mgomo huu, tuanzishe Chama Cha Watumiaji wa Mitandao ya Simu za Mkononi (Tanzania Cellular Subscribers Association), ili kuhakikisha kwamba Chama hiki kinakuwa mstari wa mbele daima kuwalinda watumiaji wa teknolojia hii, ikiwa ni pamoja na kufuatilia kila tukio la, (a) mtumiaji kutopata thamani halisi ya fedha zake anazotumia kwenye mtandao, (b) mtumiaji kukatwa fedha kwa makosa na kutorejeshewa fedha hizo, (c) mtumiaji kupoteza fedha wakati wa kuhamisha salio kutoka namba moja hadi nyingine, na kadhalika.

Watanzania tunaaminika kwamba ni watu “wapole” na hivyo, kutokana na “upole” wetu huu tunaweza kufanyiwa hujuma au ubabe wa aina yoyote ile pasi na sisi “kujibu mapigo”.

Ndugu zangu, nawaombeni mtafakari haya yafuatayo:

1. Leo tumepandishiwa bei ya vocha za simu za mkononi kiholela, kinyume cha sheria, tumeibiwa. Hatujatoa tamko.
2. Mimi – sijui wewe mwenzangu – ninavipata vijisenti vyangu kwa shida; kama wanavyosema wenzangu kule Eldoret, “Ninahenya sana!” Huoni uchungu kuibiwa mchana kweupe fedha zako, kwa madai kwamba “bei imepanda”?
3. Kama wameweza kutupandishia bei kiholela, leo, kutubia mchana kweupe, kesho watafanya nini cha ziada ili tuamke usingizini, na kuanza kudai haki zetu? Tutalala usingizini MPAKA LINI?

Natumai tutalifanyia kazi suala hili, hususan lile la mgomo… ni suala la kuamua tu, kwamba TUMECHUKIA na TUTAWANYIMA MAPATO hawa wenye mitandao ya simu pamoja na maswahiba zao, kwa muda wa saa 24! Nadhani ni adhabu tosha.

Lini mkakati huu ufanyike? Napendekeza siku ya Ijumaa, Julai 31, 2009, ili wote tupate fursa nzuri ya kujiandaa “kuwa kimya” kwa siku hiyo, kuanzia saa 6 za usiku wa kuamkia Ijumaa, Julai 31, 2009, hadi saa 6 usiku, wa kuamkia Agosti 1, 2009! Jina rasmi la siku hiyo litakuwa “Siku ya Ukimya Mkuu”, kwani, hata kwenye UKIMYA kuna SAUTI KUBWA!

Tuongee kwa SAUTI KUBWA kwa KUKAA KIMYA na kutozungumza kwa simu wala kutuma ujumbe mfupi, tutoe fundisho kwamba, HATUTACHEZEWA TENA, SASA BASI, IMETOSHA!

Watanzania, mpo? Mna uchungu na nchi yenu? Haitatokea fursa nyingine tena ya kuwaambia hawa wafanyabiashara waliokuja kuchuma kwenye migongo yetu, kwamba, ENOUGH IS ENOUGH! Kazi kwenu!
 
sasa wana JF siku hizi hawataki kabisa kuchangia hoja kama hizi, kwani nadhani wengi wao sio tena MA great Thinkers, bali ni wanasiasa za uchwara
, ni mchanganuo mzuri tu na vichwa kama hicho chako Tanzania ni jehanamu, yaani kwa kifupi huitajiki kabisa, na wala Serikali haitakusikiliza wanachotaka wao ni kauli za wanasiasa, mara Joka la mdimu nk, kwa kweli tunaitaji mapinduzi makubwqa sana katika nchi hii ya kumfanya msoimi ndio awe na kauli ya manufaaa kwa Taifa hili Kongwe lakini changa
 
Sawa sawa, nashaangaa wata wanayalaumu makampuni ya simu, wakati serikali yatu ndo inafanya madudu.
Nadhani kuna kosa kidogo hapo mwanzo 750+150 =900 not 800.
 
Sawa sawa, nashaangaa wata wanayalaumu makampuni ya simu, wakati serikali yatu ndo inafanya madudu.
Nadhani kuna kosa kidogo hapo mwanzo 750+150 =900 not 800.

Ya, nimeona... niliteleza kidogo.... hahahaha
 
Siku za karibuni kumetokea tabia chafu kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wa vocha za simu za mikononi kujipandishia bei kiholela kwa kisingizio cha ongezeko la kodi.
Vyombo vya habari vinajitahidi kukemea ubaradhuli huo wa wafanyabiashara wamero wenye uchu na tamaa ya utajiri wa harakaharaka.
Sasa ni wakati wa makampuni kutangaza kwenye mabango yao kuwa vocha ziuzwe kwa gharama ileile iliyoandikwa.
Kwa kufanya hivyo, wateja watajenga imani zaidi na hayo makampuni yao ya simu, watajiona kuwa wao ni sehemu ya umiliki wa kampuni hizo za simu za mikononi.
Au wenzangu mnaonaje??
 
Back
Top Bottom