Mjengwa katika kampeni za Kikwete 2010?

maggid

nadhani umerudia yale yale ya wiki mbili zilizopita na hakuna jipya japo una uhuru wa ku-recyle mawazo yako kila wakati.

Kigezo chako cha uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi wa 2005 ni weak mno kwa sasa. Kuna mambo mengi yamebadilika ikiwamo chemistry ya siasa za uchaguzi. Fikiria haya:
-jk kudai miaka 5 ya kwanza alikuwa anajifunza kazi, sasa anaomba ili afanye kazi ni tamko la hatari. Watu walichagua rais kufanya kazi si kufanya mazoezi.
-ccm ilikuwa moja na imara wakati wa uchaguzi wa 2005 kuliko ilivyo sasa. Kuna wana ccm wengi watakaopigia upinzani kuliko idadi ya wapinzani wenyewe. Ushindi wa kikwete 2005 ulichangiwa na kura za wapinzani kuliko unavyoweza kutegemea sasa.
-jk aliridhi uchumi mzuri kutoka ben kuliko hali ya uchumi tuliyo nayo sasa.
-kampeini za uchaguzi wa 2005 zilifanywa na mtandao plus chama - hizi za sasa zinafanywa na familia -jk, salma, ridhiwani na miraji. Jioni hii jk amemuita makamba kulalamika kuwa kuna maeneo hayana mabango na anahitaji maelezo. Hii si kazi ya mgombea wa chama kikubwa!

Chemistry ya namna hii, haina nafasi katika matundu ya uchambuzi wako uliolalia "mazoea" na theory iitwayo "makambaism".

ukweli unauma na ni mchungu kama shubiri!!!
 
hi majid!
kwanza sikatai kwamba ccm itashinda ila naomba upanue ubongo wako kidogo

1. Kwanini ukazanie tathmini ya lipumba mikoa ya pwani huku ukiacha tathmini ya slaa mikoa ya kaskazini?

2. Kwa nini huongelei tathmini ya chadema kuongoza halmashauri nne na unang'ang'ania nafasi ya pili ya lipumba uchaguzi uliopita?

3. Kwa nini huangalii mvuto kwa wananchi kati ya lipumba na slaa?

kuna mambo umeyasema ya ukweli kuhusu mtandao mpana wa ccm lakini hujagusia mtandao wa wapuuzi kama tendwa na usalama wa taifa ambao kwa aibu zao wenyewe wameamua kuwa makada wa ccm?

4. Umeongelea uchumi wa vyama pinzani ni sawa, lakini si unajua ccm wana nafasi ya kuchukua wanachotaka kwa wakati wanaotaka na mahali wanapotaka?
mimi naamini ushindi huwa unaanza moyoni.

Uchaguzi utakapoisha nina ujasiri wa kuwauliza ccm kama wangeachia uwanja sawa kwa wote je wangeshinda? Lakini pia hujadokeza juu ya rais mtarajiwa kutokuwa na uoga wa kuwa mnafiki na muongo mbele ya watanzania, kwamba leo nawashtaki mafisadi na kesho mafisadi walionewa!!! Kwa hakika jk atashinda ila kwa mara ya kwanza tutakuwa na rais aliyelaaaniwa!!!

 
you have to wake-up man,do not describe some topic according to your interest.
Go back n let them teach you again on how to influence people.

 
Magid

Umepanga hoja za kwenye wigo mfinyu ambao wewe mwenyewe umekuwa mkweli kwa kutanguliza msingi wa maneno "ni tathmini yangu kutokana na uzoefu wangu wa chaguzi zetu na hali halisi ninayoiona".

Kwa maneno yako mimi nakuelewa kuwa umEfikia hitimisho kupitia msingi dhaifu wa chaguzi zilizotangulia za dola kuamua matokeo badala ya wapiga kura. Mimi sitatoa uzoefu wangu kama shuhuda wa huo mchezo mchafu, lakini tupo wengi tulioshuhudia kwa mshangao hujuma hizo mfano kuzima taa wakati wa kuhesabu kura, kuwahonga mawakala, kutangaza matokeo kinyume, matumizi ya fedha na rasilimali za umma kufanyia kampeni na matumizi ya vyombo vyote vyadola kufanikisha uchafu huo.

Uzoefu uliopatikana umezaa maazimio ya kulinda kura kwa namana yo yote. Haya tayari yamefanya taasisi nyingi za serikali kutahari kwa kuwa mipango yao inakabiliwa na mikakati ya wapiga kura wenyewe kulinda kura zao. Sababu ya ufujaji wa madaraka na rasilimali za umma zimebadilisha dhamira ya wapiga kura wote wa kambi zote kwa kujiimarisha, au kubadilisha mahali pa kuweka kura.

Ni kweli kuna uimara wa hoja katika nyanja tofauti za vyama zinazochora msitari wa mpaka wa uchaguzi. Mfano walionufaika na mfumo wa chama tawala watakipigia chama tawala; lakini kwenye chama hicho hicho wapo walioshuhudia usaliti ambao unaweza kutumiwa kwenye kubadilisha kura zao. Pili kuna kuimarika uelewa wa kudhihirisha udhaifu wa chama tawala, migawanyiko, ongezeko la hali mbaya ya maisha, (Nakuomba usisahau kuwa wote tunanunua nyama kwa bei hiyo hiyo ingawaje vipato vyetu vinaamuliwa kivyake vyake na waamuzi)

Mwisho takwimu zako pamoja na kwamba ni za kweli sababu za vyanzo za takwimu hizo hukutueleza. Kama nilivyo sema hapo juu takwimu hizo zinatokana na uchakachuaji wa mchakato wote wa uchaguzi. Kwa uchaguzi wa mwaka huu matayarisho ya kukabiliana na uchakachuaji huo yamefanywa hadi kuwepo kauli kali kama NGUVU YA UMMA, HATUDANGANYIKI, MPAKA KIELEWEKE. Chimbua undani wa kauli hizo utagundua kuwa kuna sababu ya msingi hadi zimeibuka. Kikubwa zaidi kauri hizi zimekwisha sababisha taharuki kwa wachakachuaji.

Nahitimisha kwa kusema matokeo yo yote yale (siyo ya uzoefu) yatakuwa na mabadiliko makubwa tofauti na uzoefu wako uliotuanikia hapa jamvini. Mimi binafsi naamini kwenye mazingira ya haki, na uwanja tambarare wa kisiasa MABADILIKO NI LAZIMA. Ujumbe wangu ni kuwa dhamira za maisha bora kwa wote si usanii bali inawezekana bila CCM tuuu!!!
 
Majidi kaolewe na Kikwete uwe mke wa tatu....Mjengwa si yule wa Global kila siku?Wale wale Wanaotafuta kujikomba kwa Kikwete kama MICHUZI....Viherehere wakubwa...tired of CCM...eti tathmni yako pwani...what about Arusha and other regions?
 
WENYE kupanga mikakati ya kivita wanajua, kuwa matokeo ya ushindi wa kivita hufahamika kabla risasi ya kwanza kupigwa. Inahusu matayarisho, malengo, mbinu na mikakati.

Ninapoandika haya, zimebaki siku 30 kabla ya Watanzania wenye sifa za kupiga kura hawajapanga foleni ya kwenda kupiga kura, nchi nzima. Kuchagua madiwani, wabunge na Rais.

Zilipobaki siku 45 kabla ya Oktoba 31, 2010 nikaandika; “ Kama Uchaguzi Mkuu Ungefanyika leo…” . Ilikuwa ni tathmini yangu kutokana na uzoefu wangu wa chaguzi zetu na hali halisi ninayoiona. Nikathubutu kuandika, kuwa mgombea wa kiti cha Urais kutoka Chama Cha Mapinduzi, Bw. Mrisho Jakaya Kikwete, angeibuka kuwa mshindi, na kwamba CCM ingepata wabunge wengi na madiwani. Kwamba Dr Wilbrod Slaa, mgombea urais kutoka CHADEMA angechukua nafasi ya pili.

Kwamba Chadema ingekuwa ya pili pia kwa idadi ya wabunge na madiwani kutoka bara. Nikabainisha, kuwa Profesa Ibrahim Lipumba, mgombea Urais kutoka CUF angechukua nafasi ya tatu.

Leo, zikiwa zimebaki wiki nne kabla ya siku ya uchaguzi naiona hali iliyobadilika katika uwanja huu wa mapambano ya kisiasa. Naiona hali ifuatayo kama uchaguzi ungefanyika kesho.

Mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete angeibuka kuwa mshindi. Profesa Ibrahim Lipumba angeshika nafasi ya pili na huku Dr Wilbroad Slaa angetoka akiwa mshindi wa tatu. Vivyo hivyo, CCM ingetoa wabunge na madiwani wengi ikifuatiwa na CUF na CHADEMA. Kwamba CUF ndio ingekuwa chama kikubwa cha upinzani bungeni na hivyo basi, kutoa kiongozi wa upinzani bungeni kama ilivyokuwa katika bunge lililopita.

Nafahamu kuwa hii ni tathmini itakayowakera baadhi humu mtandaoni, lakini najisikia huru na kuona umuhimu wa kuandika tathmini yangu hii kwa madhumuni ya kuchochea mjadala na kujifunza pia. Ni ukweli, kuwa ukweli mwingine unahuzunisha, lakini ni lazima usemwe. Maana, ukweli ni uhuru pia.

Ni nini basi tafsiri ya nilichokiandika? Kama tungekuwa na uchaguzi mkuu kesho, Jakaya Mrisho Kikwete angeunda Serikali huku yeye na chama chake wakikabiliwa na changamoto kama nilizozielezea katika makala yangu yaliyopita. Kwamba changamoto kubwa itatokana na upinzani utakaokuwa umeongezeka nguvu ndani na nje ya bunge kutokana na ujio wa Dr Slaa kama mgombea Urais katika uchaguzi wa mwaka huu. Na ziada hapo, ni kuibuka kwa CUF bara kama chama chenye wabunge kati ya 10 na 15 na idadi ya kutia moyo ya madiwani.

Huko nyuma nilibainisha, kuwa viashria vya jamii inayotaka mabadiliko vimeshaonekana. CCM itakuwa na mawili ya kuchagua; kuchukua jukumu la kuyaongoza mabadiliko hayo au kusubiri kuzamishwa na mkondo wa maji ya mabadiliko hayo.

Historia ni mwalimu mzuri. Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 na uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Oktoba mwaka jana yanaiweka CCM na mgombea wake Urais mahali pazuri zaidi kiushindi kulinganisha na CUF na Chadema. Angalia taarifa hii; Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Oktoba mwaka jana ulimalizika kwa kukipa ushindi mnono Chama Cha Mapinduzi. Chama hicho kilipata ushindi wa asilimia 91.71 za kura, kikifuatiwa kwa mbali na CUF iliyopata asilimia 3.94 na Chadema asilimia 2.76.

Katika Mkoa wa Dar es Salaam pekee, Chama hicho tawala kiliibuka na ushindi mnono kwa kupata viti 402 kati ya 448, sawa na asilimia 91, huku wapinzani wakiambulia viti 40, sawa na asilimia tisa tu. Katika mkoa wa Iringa ninakoishi, CHADEMA, ilifanikiwa kushinda mtaa mmoja wa Kihesa Kilolo “B”,. Ni kwenye Kata ya Mtwivila Manispaa ya Iringa.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. CCM na mgombea wake Urais waliibuka washindi. Jakaya Kikwete alipata zaidi ya kura milioni 9.2 . Alifuatiwa na Profesa Lipumba aliyepata kura milioni 1.3 na huku mgombea wa CHADEMA , Freeman Mbowe akiambulia kura laki 7.
Pamoja na Profesa Lipumba na chama chake cha CUF kuwa cha pili, hakikupata mbunge wa kuchaguliwa huku CHADEMA ikipata nafasi hiyo ya kuwa na wabunge wa kuchaguliwa zaidi ya watano katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Kwa hali ilivyo kwa sasa, CCM bado wanajivunia:
Kuwa ni chama kikongwe, kikubwa na kilichotawala kwa muda mrefu. Na nilibainisha huko nyuma, kuwa kuna hata wanaokipigia kura chama hicho ‘ Kwa mazoea tu’. Na katika nchi zetu hizi; kukiondoa chama kilicho madarakani, Chama kilichopigania uhuru au kinachotokana na chama kilichopigania uhuru ni kazi ngumu sana. Kwa anayetaka kufanikiwa katika hilo, anahitaji kwenda ilipo mizizi ya chama hicho. Ni vijijini. Na huko vijijini kwa leo hii chama wanachokijua ni CCM. Naam. Ndio ‘ Zimwi’ wanalolijua.

Mwanakijiji atatembea kwa miguu kilomita kumi kwenda kuhudhuria mkutano wa CCM. Atakwambia amepewa taarifa ya mkutano na Balozi wake wa Nyumba Kumi. Hivyo basi, CCM wanajivunia mtandao wao wa kichama kuanzia ngazi ya Balozi wa Nyumba Kumi, shina, tawi na kuendelea. Na hata mtandao wa Kiserikali.

Nyongeza ya Udhaifu wa CCM:
Kwamba CCM inajivunia ‘K’ zake tatu; Chama Kikongwe, Kikubwa na Kinachotawala, basi, kuna baadhi ya watendaji ndani ya Chama hicho walioshindwa kusoma alama za nyakati. Wanafanya kazi zao kwa mazoea. Jambo hilo limeigharimu CCM muda na rasilimali katika jitihada za kuziba mashimo. Matokeo ya Uchaguzi wa Oktoba 31 hayataiacha CCM na mfumo mzima wa uendeshaji nchi katika hali iliyozoeleka. Subirini, mtaona.

Mama Salma Kikwete na Ridhiwani Kikwete:
Wawili hawa wamekuwa kiini cha mijadala itakayoendelea huenda hata baada ya uchaguzi kwisha. Tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 uliomwingiza madarakani Jakaya Kikwete, Tanzania imeshuhudia aina mpya ya harakati na kampeni za kisiasa zenye kuhusisha mke wa mgombea na hata wana familia ya karibu kama hili la mke na mwana wa Rais, Ridhiwani Kikwete.

Inaonekana sasa, kuwa zama za ‘ First Lady’ kuwa ‘ Mama wa nyumbani’ Ikulu zimepita. Ni dhahiri, kuwa kwa mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, amenufaika sana na ushiriki wa karibu wa mkewe na mwanawe Ridhiwani. Na si kwa Jakaya Kikwete tu, CCM kama chama, wagombea ubunge wake wananufaika kwa kiasi kikubwa na uwepo wa Mama Salma Kikwete na Ridhiwani kwenye kampeni.

Wote wawili, Salma Kikwete na Ridhiwani Kikwete wana mvuto wa kisiasa unaoongezewa nguvu na wao kuwa wanafamilia ya Rais aliye madarakani na ambaye bado, kiukweli, ana mvuto kwa Watanzania walio wengi.

Katika mazingira ya sasa, Salma Kikwete na Ridhiwani Kikwete wanafanya kile ambacho Jakaya Kikwete hawezi kukifanya kwa urahisi kwenye kampeni kutokana na kubanwa na itifaki. Mama Salma Kikwete anaweza kufanya mikutano ya ndani Lindi, Mtwara na kwingineko akiongea na kundi kubwa la wapiga kura, wanawake, kwa lugha yao. Amefanya hivyo 2005 na sasa ana uzoefu zaidi. Anaongeza kura za JK.

Vivyo hivyo kwa Ridhiwani Kikwete, naye ana ametokea kwenye Chipukizi wa CCM na kuingia kwenye Umoja wa Vijana wa Chama hicho na kushika nafasi za uongozi. Ridhiwani ana mtandao mpana wa kichama ndani ya jumuiya hiyo na hata nje. Ni karata muhimu kisiasa. Ingekuwa ajabu kama asingezunguka kumtafutia kura zaidi mgombea wa chama chao ambaye pia ni baba yake.

CHADEMA:
Ujio wa Dr Slaa:
Niliandika, kuwa ujio wa Slaa, sio tu umewashangaza CCM na mgombea wake urais, bali pia unaonekana kuwashangaza CHADEMA wenyewe wanaoonekana kutokujiandaa na namna Dr Slaa alivyopokewa na wananchi. Dr Slaa ameongeza msisimko kwenye siasa za nchi yetu. Watu wengi wana shauku ya kumsikiliza, kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa 1995 uliomwibua Augustino Mrema. Akijipanga vema, hata baada ya uchaguzi huu. Akafanya kazi ya CHADEMA nje ya Bunge na kutembea nchi nzima, basi, Dr Slaa anaweza kuwa tishio kwa ye yote ndani ya CCM atakayekuja kupambana nae.

Udhaifu wa CHADEMA
Unajidhihirisha kwenye eneo la oganaizesheni na kifedha. Hilo nililibainisha katika makala yangu yaliyopita. Bado CHADEMA haina uwakilishi mpana katika ngazi za mashina na matawi. Niliandika, kuwa Dr Slaa anaweza kutua na helikopta Pawaga Iringa, lakini mara ile akiruka, huku nyuma hakuna watendaji wa CHADEMA wa kufanya kazi ya CHADEMA. Kuna taarifa pia za wagombea wake ubunge na udiwani kukosa nguvu za kifedha kuendesha kampeni .

Zitto Kabwe bado ni kitendawili:
Niliandika, kuwa Zitto Kabwe n i kada nyota ndani ya CHADEMA, lakini ‘sarakasi’ zake za kisiasa huenda zinachangia kukidhohofisha chama chake kuliko kukipa nguvu. Alipata kulipotiwa na magazeti kutamka hadharani kuwa anajiandaa kugombea urais 2015. Zitto Kabwe alituachia maswali; Kulikoni ndani ya CHADEMA? Je, Dr Slaa ni mgombea wa ‘msimu’ tu? Au ndio sababu Zitto Kabwe hakuhudhuria Mkutano wa ufunguzi wa kampeni za CHADEMA? Niliandika, kuwa kuna watakaouliza. Na maswali yanaongezeka.

Inachojivunia CHADEMA:
Bado ni chama kinachoonyesha kuwa na mvuto kama kitajipanga vema. Kuna vijana wengi na hususan wasomi wenye kuvutiwa na CHADEMA. Hizi ni dalili njema kwa CHADEMA kwa siku zijazo, endapo zitabaini mtaji huo , kuuwekeza na kuutumia vema mbele ya safari.

CUF: CHAMA CHA WANANCHI
Leo naweza kukiri, kuwa nilikosea, nilipoandika, kuwa CUF ( Bara) safari hii kinaonekana zaidi kuwa ‘ jokeli’ katika karata za kisiasa. Kwa hali ilivyo sasa, CUF bado ni chama chenye nguvu na kilicho na mizizi kwenye baadhi ya maeneo ya nchi. Na kwa hakika, Profesa Ibrahim Lipumba bado anaonekana kuwa na nguvu katika kanda ya pwani na mikoa ya kusini.

Mathalan, kama Uchaguzi Mkuu utafanyika kesho, CUF ina hakika ya kunyakua kati ya viti 8 hadi 10 kutoka mikoa ya Kusini pekee; Lindi, Mtwara na Ruvuma. CUF ina nafasi ya kushinda viti vingi vya madiwani kutoka mikoa hiyo na hata kuweza kuongoza halmashauri moja au mbili. Tunduru ni moja ya majimbo ambayo CUF ina nafasi kubwa ya kutoa mbunge na madiwani.

Ndio, Profesa Ibrahim Lipumba bado ni tishio. Ana uzoefu na anautumia. Na siku ile CHADEMA na CUF watakapokubaliana kuunganisha nguvu na kutoa mgombea mmoja wa Urais, basi, CCM itakuwa shakani. Lakini si kwa sasa, zikiwa zimebaki siku 30 kabla ya Oktoba 31. Ninapoandika fikra hizi huru.
Maggid
 
Magid Mjengwa,
Pole kaka na kazi.
Makala yako ni nzuri kutegemea ni nani anasoma, wala huna sababu ya kusema utaudhi wengi, hii ni jamiiforums.
Mimi nashindwa kukuelewa baada ya kusoma na kuona ni makala zile zile za siku zote. Nilitegemea wewe kama mwandishi wa habari kama sijakosea, ungekuja na tathimini yakinifu ya uchaguzi wa 2010 badala ya kutumia takwimu za zamani ambazo zinaweza zisifanyekazi mwaka huu. Dr Slaa alishinda ubunge Karatu 1995 bila ya kuwa na madiwani kama sio mmoja vilevile Dr walid amani kaburu, Lyatonga mrema Temeke, Makongoro nyerere Arusha nk.

Nilitegemea kwa kuwa wewe unabahati ya kukutana na wapiga kura katika pita pita zako ungeleta takwimu hata kama sio rasmi. Mfano ungewauliza wapiga kura kila unapopita usingekosa kumi au ishirini kwa jimbo moja na kuweka viswali virahisi angalau mmbunge na raisi ukaweka vyama, ungeweza kuja na picha ambayo tusingeweza kuweka walakini na kazi yako ya uandishi.

Nikijaribu kufuatilia makala zako, naona kama vile unaogopa kitu fulani kwahiyo huna jinsi ila kuna wakati unakuwa wewe kuna wakati inabidi uridhishe upande. Inaniwia vigumu kama Synavote wameminya matokeo ya utafiti ulioonyesha Dr.Slaa anashinda. Vilevile matokeao ya maoni kwenye majimbo mbali mbali yanaonyesha jinsi wapinzani wanavyokubalika sio Chadema pekee kuna baadhi Chadema, CUF. Kizazi hiki tunatakiwa kuwa tofauti kidogo badala ya kuandika ukiwa chumbani twendeni kwenye maeneo ya tukio na tuandike habari inayotokea.

Sina chanzo za habari zako, ila nanona umetumia uchaguzi wa mwaka 2005. Mapinduzi ya demokrasia duniani huwa yanashangaza wengi, watawala wengi wanashtukizwa ndio maana wengi wanaishia kuleta vita, kama Mugabe, nk. Wamarekani waliamini Obama hawezi kuwa Raisi kwani ni mweusi na kazaliwa na baba mwafrika. Walishangaa sana walipomkuta Ikulu, mpaka hivi leo wapo amabao hawaamini.

Sikulazimishi uandike habari ambayo unaona si ya kweli, lakini habari yako haina mshiko wowote. Tukiangalia mwamko wa wananchi mwaka huu tunaona uko juu, elimu ya uraia na uchaguzi na watu kujua haki zao imepanda, watu wa kada mbali mbali wameanza kuamini kuwa wapinzani nao wanaweza kuleta mabadiliko. Majimbo mengi wamesimama wagombea ambao wanaeleweka na wananchi tofauti na miaka mingi, wachangiaji wamaeongezeka wanakisaidia chama hii ikiwa ishara ya kukubalika.

Ni wabunge wangapi Chadema inaweza kupata, Tendwa alisema 80-100, wewe mjengwa unasema wachache kuliko wa CUF, Chadema wanasema zaidi ya 100. Na sisi tunasema tutawapata wengi kwani mori upo juu. Sisi tuliopo kwenye uhamasishaji kuanzia ngazi za matawi tunapata matumaini makubwa, tunaona tofauti yawananchi wa leo na 1995.

Ndugu Mjengwa Duniani hakuna kampuni ya poll ya chumbani, zote zinakwenda kufanya kazi na kuuliza wapiga kura waliojindikisha, na sayansi hiyo inafanya kampuni hizo zisitofautiane kwenye majibu yao kwa asilimia nyingi. Mara nyingi wanasema ukweli kutokana na hali halisi. Sasa wewe kuja na takwimu za chumbani sio za kisayansi kwenye dunia ya leo ukiwa mwandishi unakuwa umeshindwa kazi yako. Takwimu za ukweli hakuna wa kuziogopa wala kuchukia labda mwehu kama wananchi watasema tunamchagua Mjengwa huwezi kataa. Ila kutumia kalamu kuwa mtabiri kama shekhe Yahaya ni usaliti wa elimu ya uandishi wa habari. Kazi kubwa ya waandishi ni kuelimisha umma kwa kutumia vyanzo vya ukweli na habri zilizotafitiwa.

Unapima mwendo wa uchaguzi kwa kuuliza wapiga kura kwa wakati huo. Siasa za Tanzania zinabadilishwa na nani anagombea wakati huo, bado hatuna siasa za kichama sana, watu wanaswing na mgombea na rushwa wakati mwingine inahamisha wapiga kura. Sasa badala ya kutuletea matokeo ya maruhani anza kujadili jimbo kwa jimbo au mgombea kwa mgombea.
 
Unajua, tumekunywa sana maji ya bendera kiasi hatuwezi kufikiria out of the box. Kushindwa kwa CCM kutakuwa revolutionary nchini Tanzania na hili linawapa hofu watu wengi sana. Ukiangalia hasira za editorial ya juzi ya Daily News na maoni ya wengi waliokuzwa na bendera si jambo la kushangaza kuwepo wishful thinking kuwa Lipumba atashika nafasi ya pili na Slaa ya tatu. Kwa wengi haiwezi kuingia akilini kuwa Kikwete is beatable licha ya usanii mwingi aliowatendea Watanzania.
 
Kwa hiyo una maana kuwa sisi tunaotaka kumpigia kura Slaa maksusi kusudi awe President tuache tuache tu, tusihangaike.
 
Unajua, tumekunywa sana maji ya bendera kiasi hatuwezi kufikiria out of the box. Kushindwa kwa CCM kutakuwa revolutionary nchini Tanzania na hili linawapa hofu watu wengi sana. Ukiangalia hasira za editorial ya juzi ya Daily News na maoni ya wengi waliokuzwa na bendera si jambo la kushangaza kuwepo wishful thinking kuwa Lipumba atashika nafasi ya pili na Slaa ya tatu. Kwa wengi haiwezi kuingia akilini kuwa Kikwete is beatable licha ya usanii mwingi aliowatendea Watanzania.

halafu wengi wetu hatujui/hatuamini kuwa kura yangu/zetu inaweza kubadilisha uongozi iwapo unataka kuleta mabadiliko............kwa hiyo wandugu bado tuna kazi kubwa ya kuelimisha wananchi juu ya mabadiliko tunayotaka.......................

inabidi tuwaondoe wananchi wasiwasi kuwa CCM isiporudi madarakani maisha yatakuwa bomba tu na tena yatakuw amazuri zaidi kwani UFISADI tutaushughulikia 100%..............na huduma muhimu za kijamii i.e elimu, afya na miundombinu zitapatikana kutokana na major savings ambazo zitatokana na kufuta matumizi yasiyo ya lazima yanyofanywa na majambazi (yaliyopo) CCM.................
 
Mjengwa bwana anajulikana huyu katika mambo makuu mawili (kwa mtazamo wangu); ukichunguza sana kwa makini machapisho yake, ninashawishika kuamini ama ni kada wa kile chama kikongwe (japo hataki kuweka bayana); ama pia ni mfurukutwa wa zile siasa zinazoleta shida kati ya watu (za kiimani). Anyway, huu ni mtazamo wangu lakini nina uhakika siku moja nitakuja kuwa proved right. Ni sawa na usanii niliuona 2005 na kutokutoa kura yangu kwa "tumaini jipya". Madudu yalivyoanza moyoni nilipata amani maana nilijua kuwa nilikuwa sahihi kwa wakti ule (japo kwa hisia tu). Kuhusu Mjengwa.... tusubiri tuone... ndio wakuu wa wilaya wateule hawa wanaokuja...time will tell
 
Na sababu ya Dr Slaa kuondoka nafasi ya Pili kufikia ya Tatu ni nini?
 
Huyu mjengwa anapotosha umma,vijiji gani anaongelea,cuf ipo visiwani co bara,wakati chadema imeongoza halmashauri 3 bara cuf hata moja,mjengwa unakaa mjini mambo ya vijijini tuulize cc
 
Kama hamjui baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 niliacha kabisa kusoma makala zake.
amebakia kuupamba uchafu kuuita uzoefu.
Lakini kwa kuwa ni mtanzania ana uhuru wa kutoa maoni yake. na kwa kuwa anaijua media vyema sana na ni rafiki mzuri wa mr. Mkumbwa anajua kilichopangwa na kupangika. na kwa kuwa bado ni mfuasi mwema wa Muungwana anajua how to play salva's tricks. Huwa anafanya trips nyingi sana mikoani na alizidisha sana hivi karibuni kabla ya kampeni. Mnajua alikuwa anafuata nini huko mikoani? nani aligharimia safari zake? Namhurumia Jenerali Ulimwengu kwa kuzungukwa na mamluki wanaomchunguza kila move yake wakisaka weak link yake.

Ametoa maoni na sisi ndo wapiga kura. je tulazimishwe kupiga kura kwa mtazamo wake? Ina maana yeye hataki chadema ishinde? amefanya nini kupromote demokrasia na elimu ya uraia kamammdau zaidi ya makala za kuzungumzia watu na soka?
 
Ndugu zangu,

Mijadala kama hii inatusaidia kufahamu tunavyofikiri. Napenda sana kuona nchi yetu inapata mabadiliko ya kimsingi na kupiga hatua za maana za kimaendeleo. Demokrasia yetu bado changa. Tumeanza kupiga hatua, na Roma haikujengwa kwa siku moja.

Napenda kuona siku moja tunaanza rasmi mchakato wa kutengeneza KATIBA mpya ya nchi yetu, maana naamini tutakuwa tumeanza kupiga hatua za dhati katika kuifanya nchi yetu kuwa ya kisasa zaidi.

Bahati mbaya, mijadala hii wakati mwingine baadhi yetu tunaitumia kushambuliana badala ya kujibu hoja zilizowasilishwa, ni udhaifu wetu wa jumla.

Na kuna linganishi tunazotoa zisizo na uhalisia, mfano wa mwenzetu Kinepi anayesema; "Wamarekani waliamini Obama hawezi kuwa Raisi kwani ni mweusi na kazaliwa na baba mwafrika. Walishangaa sana walipomkuta Ikulu, mpaka hivi leo wapo amabao hawaamini."

Mimi sikushangaa, na wengi Marekani na duniani hawakushangaa. Maana, Obama na timu walikuwa na ajenda ya mabadiliko iliyokuwa wazi na waliomudu kuieleza ikaeleweka kwa Wamarekani wengi. Na Obama na timu yake alishatengeneza mtandao mpana uliomwezesha kuingia Ikulu ya Marekani. Ni kuanzia kwa vijana wa Vyuo Vikuu mpaka wazee.

Ingawa wengine humu ni mashabiki zaidi wa vyama na wagombea, lakini, nadhani ni vema tukaendelea kuwa huru zaidi katika kuchangia fikra kwa ustawi wa demokrasia ya nchi yetu.
 
Kama hamjui baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 niliacha kabisa kusoma makala zake.
amebakia kuupamba uchafu kuuita uzoefu.
Lakini kwa kuwa ni mtanzania ana uhuru wa kutoa maoni yake. na kwa kuwa anaijua media vyema sana na ni rafiki mzuri wa mr. Mkumbwa anajua kilichopangwa na kupangika. na kwa kuwa bado ni mfuasi mwema wa Muungwana anajua how to play salva's tricks. Huwa anafanya trips nyingi sana mikoani na alizidisha sana hivi karibuni kabla ya kampeni. Mnajua alikuwa anafuata nini huko mikoani? nani aligharimia safari zake? Namhurumia Jenerali Ulimwengu kwa kuzungukwa na mamluki wanaomchunguza kila move yake wakisaka weak link yake.

Ametoa maoni na sisi ndo wapiga kura. je tulazimishwe kupiga kura kwa mtazamo wake? Ina maana yeye hataki chadema ishinde? amefanya nini kupromote demokrasia na elimu ya uraia kamammdau zaidi ya makala za kuzungumzia watu na soka?
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom