Mjengwa ajibu: Tumejipanga upya,Tunakuja!

magoma

New Member
Mar 2, 2009
4
0
Kuhusiana na kuacha kuandikia raia mwema Mjengwa katoa ufafanuzi huu kwenye blogu yake ( mjengwa.blogspot.com)

Taarifa nilizotoa humu bloguni kuhusu kupumzika kwangu kuandikia ' Raia Mwema' na kuondoka kwa gazeti la ' Gozi Spoti' mitaani zimepokewa na baadhi kwa mitazamo tofauti. Na ibaki kuwa ni mitazamo tu. Kila mtu ana haki ya kutoa mtazamo wake.

Hata hivyo, sisi tuliofanya kazi ya kuandaa Gozi Spoti tumetiwa moyo na waliotupongeza, kutukosoa kwa kujenga, kutushauri na kututia shime. Si hivyo tu, tumetiwa moyo na kujengewa nguvu zaidi na hata wale waliokuja na mitazamo ya kutuvunja nguvu. Wote kwa pamoja tunawashukuru.

Kwa baadhi yetu, mimi nikiwa mmojawapo, Gozi Spoti ilikuwa ni sehemu ya maisha yetu. Tungependa Gozi Spoti liishi daima. Ni uzoefu wa Gozi Spoti uliotusaidia kutujenga ujasiri wa kuja na mawazo ya kuanzisha gazeti la uchambuzi wa masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Ili tufanikishe hilo niliona ni busara nipumzike kuandikia Raia Mwema ili niongeze nguvu katika hilo tulilolipanga; kuanzisha gazeti la uchambuzi.

Ndio, tulifikia uamuzi huo wa kuanzisha gazeti jipya. Hata hivyo, gharama kubwa zitokanazo na usajili wa gazeti la namna hiyo ulitupelekea tuchukue uamuzi wa kubadili jina na sera za Gozi Spoti. Hilo la mwisho lilikuwa na gharama za chini mno. Kuua Gozi Spoti ilikuwa ni moja ya maamuzi machungu niliyopata kuyaidhinisha katika uzoefu wangu wa uongozi. Lakini wakati mwingine ni lazima tutumie kanuni ile ya ' kumwua mpenzio!' ( Kill your darling!). Tusingefanya hivyo tungelazimika kuanza kupita kwa 'wajomba' kuomba senti za kusajili gazeti. Hatukutaka hilo.

Naam. Gozi Spoti limekufa. Kama ni mechi ya kandanda tuliamua kuingia uwanjani tukiwa pekupeku ( bila viatu). Hatukutaka kusubiri turushiwe viatu ndipo tuingie uwanjani. Tuliingia kwenye ushindani na kweli tuliumizwa sana na wenye 'njumu' kwa maana ya waliocheza na 'adidas' miguuni. Hatukukata tamaa. Tumejifunza mengi ikiwamo mbinu za kupambana katika uwanja huo mgumu. Tumejipanga upya, tunarudi uwanjani tukiwa tumevalia 'raba' miguuni.

Naam. Tumesajili gazeti jipya chini ya Kampuni yangu ya Ikolo Investiment Co. Ltd. Hivyo basi, mmiliki wa gazeti ni mimi. Ngome yetu kwa maana ya ofisi zetu zitabaki pale pale Kijijini Kinondoni Biafra ( Pichani ingawa hiyo kamera si ya ofisi yetu bali ni ya watu wa CNN waliopata kufika kwenye 'kaofisi ketu'). Na milango ya ushirikiano iko wazi kwa yeyote mwenye mapenzi mema na nchi yetu.

Hakika tunahitajiana katika kuijenga nchi yetu. Mimi naamini hivyo. Hata nilipokwenda kwa watani zangu Wasukuma na Wanyamwezi hivi karibuni niliukuta kwao usemi wa ' Kupandula na kuboda' kwa maana kutengeneza tuta kunahitaji wawili; wa kutifua na kupanga tuta. Ndivyo inavyotakiwa iwe katika juhudi tuzifanyazo za kuijenga nchi yetu. Ndivyo inavyotakiwa iwe katika maisha yetu ya kila siku.

Kwa ufupi sana nimejaribu kulifafanua hili la kupotea kwa Gozi Spoti na mimi kupumzika kuandikia Raia Mwema. Nafahamu fika, kuwa mara tu ninapoandika juu ya habari ya kuanzisha gazeti jipya, basi, muda huo huo, nitakuwa nimejipatia maadui wapya ( Ningependa wawe wapinzani wa kifikra na kibiashara na siyo maadui wenye kumtakia mtu mabaya).
Nafahamu, kuwa mara habari hii ikifahamika, itanipotezea baadhi ya niliodhani ni marafiki zangu. Nafahamu fika , kuwa habari hii itanipatia pia marafiki wapya , nitafurahi kuwa na marafiki hao.

Katika kuyaandika haya sina maana ya kutotaka kusoma mitazamo tofauti. La hasha, hilo ni jambo zuri kabisa.

Mwisho kabisa, gazeti jipya linaitwaje? Sera ni ipi? Lini litatoka? Kina nani watakaoandika humo? Bila shaka ni baadhi ya maswali mnayojiuliza baadhi yenu.

Kikosi nimeshakipanga. Kimekamilika kwa kuanza mapambano. Kuna wengine wanaonyesha moyo wa kujiunga nacho. Katika siku za karibuni, na kupitia blogu hii, nitajibu maswali hayo ikiwamo kuwatajia jina la gazeti, na baadhi ya waliomo katika kikosi hicho.

Naam. Tumejipanga upya, tayari kushiriki ngwe nyingine ya mapambano. Mwanzo utakuwa mgumu. Hatutokata tamaa. Tutapambana hadi risasi ya mwisho, hadi pumzi ya mwisho.

/Maggid

Mwenyekiti Mtendaji
Ikolo Investiment Co. Ltd
 
mmhh...yet macho, ila tunakutakia kila la heri. kama litakuwa ni la uchambuzi usio na dalili za kudhaminiwa kwa malengo binafsi (tunajua 2010 ndo hiyo) tutaukaribisha kwa mikono miwili
 
Ina furahisha sana kijana mzawa anapojishughulisha kuanzisha mradi utakaosaidia kuajiri ndugu zetu. Heshima Mkuu Mjengwa, tunasubiri utakayokuja nayo katika kuhabarisha na kuelimisha jamii.
 
Kaka Mjengwa hongera,rafiki yangu mmoja alikuwa fundi mjenzi mzuri sana ila hakuwa na jina,akafanyakazi yake vizuri kwa uaminifu sana.Siku moja fundi mkuu akamtuma kufanya kazi peke yake sehemu,aliifanya kwa ustadi,kwa muda mfupi na kwa viwango. Tajiri akampeleka mkoani,siku hizi ana ofisi yake na kazi zikimzidi humwita fundi wake aliyemtangaza. Kwa pamoja hufanya kazi na sasa ni marafiki wakubwa. Please go ahead bro.
 
Back
Top Bottom