Misamaha ya kodi imezidi, ipunguzwe

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Mwanzoni mwa miaka ya 90 kati ya mambo ambayo yalisababisha wafadhili mbalimbali wanaosaidia bajeti ya serikali kusitisha misaada yao ni uzembe wa kutokukusanya kodi, lakini pia kukithiri kwa misamaha ya kodi.
Serikali zote duniani hujiendesha kutokana na kodi za wananchi wake, yaani shughuli za kiuchumi za wananchi ndizo huipa serikali jeuri ya kutekeleza majukumu yake, kama kulipa mishahara ya watumishi wa umma; kuwa na jeshi lenye vifaa vya kisasa na wanajeshi/askari wanaolipwa na kutunzwa vizuri.
Kubwa zaidi ni kupitia kodi hizi ndipo serikali hupata uwezo wa kutoa huduma za jamii kama kujenga shule barabara, vyuo, huendesha huduma za afya kama ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hata hospitali kubwa za rufaa, kutaja kwa uchache tu.
Kwa bahati mbaya, serikali haifanyi biashara, na hata pale inapomiliki mashirika yake, wajibu wa kuyaendesha huachiwa bodi za wakurugenzi na watendaji wanaounda menejimenti, ili katika kujiendesha ufanisi na tija vizingatiwe kwa mapana yake; serikali pia hunufaika na kodi katika utekelezaji wa majukumu ya mashirika haya na wakati mwingine pale faida inapopatikana hupata gawio.
Miongoni mwa kundi kubwa katika jamii ambalo halina ujanja wa kukwepa ulipaji kodi ni wafanyakazi ambayo hukatwa fedha zao moja kwa moja katika mfumo wa kodi ijulikanayo lipa kadri unavyopata (Pay As You Earn- PAYE), hawa kila mwezi hata kabla ya kupata ujira wao kodi yao hukatwa moja kwa moja na mwajiri.
Kimsingi ulipaji kodi ni wajibu, katika mataifa yaliyoendelea mwananchi hufurahi kulipa kodi kwani ni wajibu kwa taifa lake, ni ulipaji kodi huo huwahakikishia barabara nzuri, reli za kuaminika na kila huduma ya umma ambayo ni wajibu wa serikali kuitoa.
Wakati huo ukiwa ni wajibu muhimu wa wananchi na ukiwa ndio chimbuko la kuwapo kwa mabunge (uwakilishi) katika vyombo vya kutunga sheria, kuna dalili kwamba hapa nchini tabia ya watu kutafuta kona za kukwepa kulipa kodi, hasa kwa wafanyabiashara, ni mtindo ambao unaendekezwa sana na mamlaka za serikali.
Kwa mfano, Ripoti ya Mdhbiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2009/2010 imebainisha kwamba kiasi cha Sh. bilioni 690 sawa na asilimia 14.7 ya mapato ya serikali kwa mwaka huo, kilisamehewa kodi.
Hizi kwa hesabu za harakaharaka ni takribani mapato ya mwezi mmoja na nusu ya serikali kulingana na takwimu za ukusanyaji wa kodi ya wastani wa Sh. bilioni 400 kwa mwezi.
Kwa hiyo ni sawa na kusema kwamba kwa mwezi mmoja na nusu wa mwaka wa fedha wa 2009/2010 serikali iliamua kuacha kukusanya kodi zote. Kwa upeo wetu na pengine kwa upeo wa Watanzania wengi hizi ni fedha nyingi mno kusamehewa bila kulipiwa kodi.
Kumekuwako na mjadala mpana sana juu ya misamaha ya kodi kama kweli inatolewa kwa manufaa ya umma, au ni njia nyingine ya matumizi mabaya ya madaraka kunufaisha watu binafsi. Tunasema haya kwa kuwa katika mazingira ya kawaida, misamaha ya kodi ingepaswa kuwa ni kidogo sana kwa taifa kama Tanzania ambalo takribani asilimia 43 ya bajeti yake ni misaada kutoka kwa nchi wahisani na mashirika ya kimataifa.
Mara nyingi misaada hii hupatikana kwa mbinde, wakati mwingine kwa masharti magumu na yanayoelekea kuuza uhuru wetu kama taifa katika kupanga na kuamua vipaumbele vyetu, tunakubali kudhalilika hivyo wakati mabilioni ya Shilingi yakisamehewa kwa sababu nyepesi mno.
Tunaamini ripoti ya CAG imetufungua macho ili kama taifa tujielekeze kutathmini kama kweli misamaha hii ni muhimu kiasi hicho ili sasa tubane zaidi kwa nia ya kuongeza uwezo wa kifedha wa serikali ambao utajitafsiri katika uwezo wake wa kutekeleza majukumu yake muhimu kwa umma.
Serikali kupitia vyombo vyake mbalimbali vinavyohusika na ulipaji wa kodi, kama Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato (TRA) ijielekeze kutibu ugonjwa huu wa misamaha ya kodi, na badala yake kuelemisha jamii itambue kwamba ulipaji kodi ni wajibu wa kila mwananchi wa kujivunia.
Hata hivyo, serikali itambue kwamba ili wajibu huo uwaingie vilivyo wananchi, ni lazima waone kodi zao zikileta mabadiliko ya kweli kweye ustawi wa maisha yao, na si kuwaneemesha wachache waliokalia ofisi za umma. Ni kwa njia hiyo tu tunaweza kugeuza mwelekeo wa sasa wa kila mtu kutamani msamaha wa kodi hata kwa mambo ya binafsi mno.
 
Back
Top Bottom