Misaada na mikopo vitahatarisha uhuru wetu

engmtolera

JF-Expert Member
Oct 21, 2010
5,150
1,437
japo kama tungeweza kuzipata; hivyo ndivyo tunavyotaka kweli? Kujitawala ni kujitegemea. Kujitawala kwa kweli hakuwezekani ikiwa Taifa moja linategemea misaada na mikopo ya Taifa jingine kwa maendeleo yake. Hata kama pangetokea Taifa au mataifa ambayo yako tayari kutupa fedha zote tunazohitaji kuendesha mipango yetu ya maendeleo isingekuwa sawa kwa nchi yetu kuipokea misaada hiyo bila kujiuliza matokeo yake yatakuwa nini kwa Uhuru wetu na uzima wetu. Msaada ambao ni kama chombo cha kuongeza juhudi, au nyenzo ya juhudi, ni msaada ambao una manufaa. Lakini msaada unaoweza ukawa sumu ya juhudi si msaada wa kupokea bila kujiuliza maswali. Kadhalika mikopo. Kweli mkopo ni bora kuliko misaada ya "bure". Mkopo nia yake ni kuongeza jitihada au kuifanya jitihada itoe matunda mengi zaidi. Sharti moja la mkopo huwa ni kuonyesha jinsi utavyoweza kuulipa. Maana yake ni kwamba sharti uonyeshe kuwa unakusudia kuufanyia kazi itakayoleta manufaa ya kukuwezesha kuulipa. Lakini hata mikopo ina kikomo. Sharti upime uwezo wa kulipa.

Tunapokopa fedha kutoka nje mlipaji ni Mtanzania. Na kama tulivyokwisha sema Watanzania ni watu maskini. Kuwabebesha watu maskini mikopo ambayo inawazidi kimo si kuwasaidia bali ni kuwaumiza. Na hasa inapokuwa, mikopo hiyo ambayo wanatakiwa walipe haikuwafaidia wao, bali ilifaidia watu wachache tu. Na Viwanda vya wenye raslimali zao je? Ni kweli tunavitaka. Hata tumepitisha katika Bunge sheria ya kulinda raslimali ya wageni wanaoanzisha mipango mbali mbali ya uchumi katika nchi yetu. Nia

yetu na matumaini yetu ni kuwafanya waone kuwa Tanzania ni nchi inayofaa kuingiza raslimali zao. Kwani raslimali yao itakuwa salama italeta faida. Na faida hiyo wenyewe wataweza kuiondoa bila vipangimizi. Tunayo matumaini ya kupata fedha za maendeleo mbali mbali kwa njia hii. Lakini hatuwezi kupata za kutosha. Lakini hata kama tungeweza kuwaridhika kabisa Wageni hao na Makampuni hayo mpaka yakubali kuanzisha mipango yote ya uchumi tunayohitaji katika nchi yetu, hivyo ndivyo tunavyotaka kweli? Kama tungeweza kushawishi wenye raslimai wa kutosha kutoka Amerika, na Ulaya kuja kwetu na kuanzisha Viwanda vyote, na mipango mingine yote ya uchumi tunayohitaji katika nchi hii, hivi kweli tungekubali bila kujiuliza maswali? Tungekubali kweli kuacha uchumi wetu wote uwe mikononi mwa wageni kwa ajili ya kupata faida na kuipeleka katika nchi zao? Hata kama wasingedai kuhamisha faida na kupeleka makwao, bali faida yote watakayopata wataitumia hapa hapa Tanzania kwa maendeleo zaidi. Hivi kweli tungekubali jambo hili bila kujiuliza hasara zake kwa Taifa letu? Huu Ujamaa tunaosema kuwa ndiyo shabaha yetu tungeujengaje? Twawezaje kutegemea nchi za nje na Kampuni za nje kwa misaada na mikopo na raslimali kwa maendeleo yetu bila kuhatarisha uhuru wetu? Waingereza wana methali isimayo "Amlipaye mwimbaji ndiye huchagua wimbo". Tutawezaje kutegemea nchi za kigeni na Makampuni ya kigeni kwa sehemu kubwa ya maendeleo yetu bila
kuzipa nchi hizo na makampuni hayo sehemu kubwa ya uhuru wetu wa kutenda tupendavyo. Ukweli wenyewe ni kwamba hatuwezi. Tukariri basi. Tumefanya makosa kuchagua fedha, kitu ambacho hatuna, kiwe ndicho chombo kikubwa cha mipango yetu ya maendeleo. Tunafanya makosa kudhani kuwa tutapata fedha kutoka nchi za kigeni. Kwanza, kwa sababu kwa kweli hatuwezi kupata fedha za kutosha kwa maendeleo yetu. Na pili, hata kama tungeweza, huko kutegemea wengine kungehatarisha uhuru wetu na siasa nyingine za nchi yetu.
 
Back
Top Bottom