Mikakati ya udhibiti wa mianya ya wizi wa kura za wabunge na madiwani......

Tata

JF-Expert Member
Dec 3, 2009
5,799
2,725
Jana nilikuwa na mjadala wa kina wazalendo mwenzangu kuhusu mchakato wa uchaguzi wa wawakilishi wetu na mianya ya wizi wa kura ambayo ama imewekwa kwa makusudi ama kwa bahati mbaya lakini wajanja wanaitumia kufanya ujambazi wa kura za watu. Tulijikita kwenye uchaguzi wa wabunge na madiwani hasa wakati wa kupiga kura na kutangaza matokeo. Sio vibaya tukaupanua mjadala huu ili kupata njia muafaka za kudhibiti wimbi la wezi wa kura kupata nafasi za uwakilishi na hatimaye uongozi wa juu wa nchi na kugeuka kuwa wezi wa mali za nchi.

Mchakato ulivyo sasa kila mgombea/chama huteua wawakilishi wake na hawa wawakilishi wanashiriki kusimamia kura za waliowateua. Baada ya zoezi la kupiga kura kukamilika kura huhesabiwa wakiwepo wawakilishi wote ili kuthibitisha kuwa kura zote halali zimehesabiwa na matokeo yanaakisi kura zilizopigwa na kuhesabiwa. Zoezi hilo linapokamilika kila kituo kinabandika karatasi lenye matokeo yaliyoridhiwa na wawakilishi wote kwenye kituo cha wapiga kura.

Tatizo linatokea wakati wa kujumlisha matokeo ya vituo vyote ili kupata jumla kuu (consolidated outcome) ya matokeo ya vituo vyote ili kumpata mshindi halali wa uchaguzi kwenye jimbo. Baadhi ya wagombea wakipata matokeo na kugundua kuwa hawajashinda hugoma kusaini kukubali kushindwa na badala yake hulazimisha kura zihesabiwe upya.


Msimamizi hutumia mwanya huu kuagiza masanduku yote yenye kura yapelekwe kwenye kituo kimoja cha kuhesabu upya kura ili kukidhi matakwa ya kambi inayopinga matokeo yaliyoletwa toka vituoni. Ni katika huu mchakato wa kusafirisha masanduku ndipo wajanja huondoa yale masanduku halali na kuingiza masanduku yaliyochakachuliwa ili kuwafaidisha wale wagombea wajanja waliokataa matokeo.

Nina mapendekezo yafuatayo yanayolenga kuboresha mchakato huu na kuondoa mianya ya wizi/uchakachuaji wa kura:

1. Wagombea wawajibike kuwateua wasimamizi wanaowaamini wenye upeo na maadili ili kusiwe na visingizio hawa mawakala wanaposaini matokeo kwenye vituo vya kupigia kura. Kwa maana nyingine saini ya wakala (Agent) inawakilisha saini ya mgombea/chama chake.
2. Matokeo yanayotangazwa vituoni mbele ya wawakilishi wa wagombea wote yawe ni matokeo rasmi na vyombo vya habari viruhusiwe kutangaza matokeo kituo kwa kituo. Tofauti na utaratibu wa sasa wa kusubiri msimamizi wa uchaguzi kutangaza anayoyaita matokeo rasmi. Kwa maana nyingine tutakuwa tunapata updates za matokeo ya kila kituo na jumla ya kura ambazo zimepigwa na kuhesabiwa na tutajua nani ameshinda hata kabla ya matokeo rasmi yatakayotangazwa.
3. Kazi ya msimamizi iwe ni kujumlisha kura toka vituoni na kutangaza matokeo kwa mujibu wa ushahidi wa maandishi wa vituo mbalimbali.
4. Msimamizi wa uchaguzi asiruhusiwe kuamuru masanduku ya kura kusafirishwa kwenye anakotaka yeye ili kuhesabu upya kura.
5. Inapotokea mgombea hakubaliani na matokeo kama yalivyoletwa na vituo vya kupiga kura aende mahakamani kupinga matokeo hayo ikiwa ni pamoja na kuomba kibali cha kuhesabu kura kama Mahakana itaona inafaa.
NB: Kigezo pekee cha uamuzi wa mahakama wa kuhesabu kura upya kiwe ni ikiwa wakala wa mgombea alishurutishwa ama kwa nguvu au rushwa kusaini karatasi ya matokeo ya kura na mzigo wa ushahidi (burden of proof) iwe ya mgombea akisaidiwa na wakala anayedai kuwa alisaini kwa shuruti. Ikithibitishwa kuwa kweli alishurutishwa basi walioshiriki kumshurutisha wafunguliwe mashitaka mara moja na kufungwa.
6. Kuwe na muda na mahali maalum pa kutunza masanduku yenye kura zilizopigwa kutoka vituoni na zilindwe ili kuepuka kuingizwa kwa kura bandia/zilizochakachuliwa.
7. Karatasi zote za kupigia kura na za kurekodi matokeo ziwe na “serial numbers” na iwepo rekodi ya “serial numbers” za karatasi zilizopelekwa kwenye kila kituo nchi nzima. Hii itadhibiti uwepo wa karatasi bandia.

NB: Ikiwa mahakama itaamua kuwa kura zihesabiwe upya, zoezi la kuhesabu upya halitafanyika mpaka kwanza uhalali wa karatasi za kupigia kura utakapothibitishwa. Uhalali utathibitishwa kwa kuangalia serial numbers pamoja na "security features" nyingine zitakazokuwa kwenye karatasi ya kura.

8. Kila mwakilishi/chama atapatiwa nakala za matokeo yaliyosainiwa na mawakala wa kila kituo na moja ya “copy” itabakia ndani ya sanduku la kupigia kura ambalo litawekewa lakiri maalum chini ya uangalizi wa mawakala wote. "Serial mumbers" ya nakala hizi zitakuwa zinafanana kwa kila sanduku.
9. Yoyote atakaye kutwa na ama sanduku halali la kupigia kura ama nakala ya karatasi halali la kupigia kura akamatwe na kuhukumiwa kifungo cha muda mrefu usiopungua miaka saba jela. Hii haitajalisha kama aliyekutwa ni mgombea (mfano Makongoro – Ukonga) mwanachama au mshabiki wa chama.
Haya mapendekezo ni kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge na madiwani. Najipanga kuangalia utaratibu sahihi wa kudhibiti kura za rais ambazo mchakato wake unakwenda kwenye ngazi ya taifa. Naomba mawazo ya njia sahihi zaidi za udhibiti ili hatimaye tuwe na jamii ambayo kura ya mwananchi inakuwa ndiyo sauti ya mwisho juu ya mtawala anayetakiwa.
 
Back
Top Bottom