Migogoro ya kisiasa yazidi kuitafuna Mbeya

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,906
22,050
Migogoro ya kisiasa yazidi kuitafuna Mbeya

Mwandishi Wetu, Mbeya Oktoba 7, 2009


Baadhi ya wakazi wamkumbuka Matheo Quaresi

HIVI karibuni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisimamia harambee kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya ambako zilipatikana zaidi ya Shilingi milioni 320.

Makisio ya uongozi wa Wilaya hiyo, harambee ya siku hiyo ililenga kukusanya Shilingi milioni 350 ikiwa ni sehemu ya mahitaji ya zaidi ya Shilingi milioni 900 zinazohitajika kwa ajili ya miradi mbalimbali ya elimu wilayani humo.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya shule za sekondari wilayani humo yakiwemo majengo ya maabara, vyumba vya madarasa na nyumba za walimu.

Ni wazi hiyo ni miongoni mwa mikakati ya kuinusuru sekta ya elimu wilayani humo, sekta ambayo kimkoa imekuwa ikiporomoka kwa kasi ya kutisha tangu mwaka 2007.

Taarifa ya ufaulu kwa Wilaya ya Mbozi pekee inaonyesha kuwa mwaka 2005 wanafunzi waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi nchini walikuwa 10,140, kati ya hao wanafunzi 5,480 sawa na asilimia 61.7, walifaulu. Mwaka uliofuata waliofanya mtihani huo walikuwa 11,346 ambapo kati ya hao, wanafunzi 7,836, sawa na asilimia 69.1, walifaulu.

Lakini kuanzia mwaka 2007 hali ya ufaulu wa wanafunzi ilishuka kwa kasi ambapo kati ya wanafunzi 11,118 waliofanya mtihani mwaka huo ni 5,480 tu ndiyo waliofaulu, ikiwa ni sawa na asilimia 54 . Kwa mwaka jana waliofanya mtihani walikuwa 16,782 ambapo kati yao ni wanafunzi 8,393, sawa na asilimia 50, ndio waliofaulu.

Sura ya kimkoa katika maendeleo ya elimu haitofautiani sana na ile ya Wilaya ya Mbozi; kwani kufikia mwaka jana ufaulu wa wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi nchini ulifikia asilimia 55 kutoka ufaulu wa zaidi ya asilimia sabini kabla ya mwaka 2007 ambapo mkoa huo ulitamba nchini kiasi kwamba iliifanya nafasi ya kwanza kitaifa kuwa ‘mali’ yake.

Jambo linalosikitisha kuhusu hali hiyo ni pale katika miaka hiyo hiyo ya kuporomoka kwa elimu, mkoa huo ulivyoweza kujipambanua kuwa kinara wa migogoro ya kisiasa isiyoisha, migogoro iliyojaa visasi na kukomoana iliyosambaa takribani mkoa mzima.

Hivi karibuni mwandishi wa habari wa gazeti la Daily News, Jonas Mwasumbi aliamua kuvunja ukimya pale alipowapasha wanaoitwa ‘Wazee wa Mkoa wa Mbeya’ kuwa wawaeleze wanasiasa wao kuwa wanakoupeleka mkoa siko. Kwamba wamefikia hata hatua ya kuwagawa hata waandishi wa habari.

Ujumbe wa Mwasumbi ni kwamba iwapo kweli wazee wale waliowaita waandishi wa habari kukanusha yaliyoandikwa kwenye vyombo vya habari kuhusu wao kuombwa kuwa wasuluhishi wa mgogoro wa kisiasa mkoani humo, basi wawaite wanasiasa wao na kuwaeleza kuwa wananchi wamechoshwa na migogoro isiyoisha badala ya kukubali kutumika kuendeleza migogoro kama wafanyavyo sasa.

Mtazamo wa viongozi walio wengi uko kwenye ujenzi wa miundombinu ya shule; kama vile vyumba vya madarasa, maabara, nyumba za walimu na vyoo, wakisahau kuwa utulivu na upendo miongoni mwa wadau wote wa elimu ni moja ya misingi muhimu katika maendeleo ya elimu.

Sio siri tena, hivi sasa watu wanazikumbuka enzi za uongozi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Mateo Quresi, kwamba pamoja na mapungufu yake yote aliyokuwa nayo, lakini aliupandisha mkoa huo kielimu kwani ni katika kipindi cha uongozi wake aliyekuwa Afisa Elimu wa Mkoa huo, Elisifa Mafole, aliufanya mkoa huo utambe nchini kwa kuongoza katika mitihani ya taifa ya kuhitimu elimu ya msingi.

Wanahistoria wanaamini kuwa ni jambo jema kurejea nyuma; kwani husaidia kubaini mbinu zilizotumika kufikia mafanikio yaliyopatikana wakati huo, na hapo ndipo viongozi wa mkoa huo wanapopaswa kujihoji walipojikwaa.

Mmoja wa Wakurugenzi Watendaji waliopata kufanya kazi mkoani humo enzi za Quresi alipata kutaja moja ya siri ya mafanikio yao wakati huo. Aliitaja siri hiyo kuwa ni kutokutoa nafasi kwa majungu katika utendaji.

Anasema: “Wakati ule tulichapa kazi kweli kweli, yule mzee (Quresi) hakuruhusu majungu. Mtu akipeleka jungu aliumbuka, hivyo Halmashauri tulifanya kazi zetu kwa uhuru na amani. Ukikosea alikueleza pale pale na yaliisha. Hakuwa anaweka mambo moyoni, anakwambia yanaisha, mnasonga mbele.”

Mkurugenzi huyo anabainisha kuwa majungu mengi kwenye serikali za mitaa ni ya kisiasa hivyo ukiyaendekeza unawafanya watendaji wasijiamini, unawakosesha raha ya kazi, wanakosa amani na katika mazingira ya aina hiyo huwa hakuna ufanisi.

Mtazamo wa Mkurugenzi huyo ndiyo ulinifanya nitafakari zaidi kuhusu hali ya Mkoa wa Mbeya hivi sasa ambapo kiwango cha elimu kinashuka huku malumbano ya kisiasa yakizidi kushika kasi, nami najihoji hivi hawa viongozi wetu hapa mkoani wanaelewa mambo yaliyowaelemea wananchi wao kweli? Ni swali ngumu lakini rahisi.

Naelewa ni ukweli mchungu, lakini uongozi wa Mkoa wa Mbeya umekubali kuyakumbatia majungu, na ukweli huu unajidhihirisha katika kauli na matendo yao. Hawako tayari kukaa pamoja na kuyamaliza.

Pengine moja ambalo wanapaswa kuelewa ni kwamba wananchi wanafuatilia kila kitu kinachoendelea, na sasa wamefikia hatua ya kuushutumu uongozi huo kuwa umekaidi hata maagizo ya Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akihitimisha ziara yake mkoani humo.

Baada ya kuzungumzia kwa ujumla mgogoro wa kisiasa ulipo mkoani humo, aliwaeleza kuwa wao ni watu wazima hivyo wamemuelewa. Matarajio ya wananchi baada ya maelezo hayo ya Rais, ambayo kiutawala ni maagizo, ni kwa uongozi wa mkoa wa Chama tawala na Serikali yake kuitisha kikao cha pamoja kati yao na wabunge wote wa mkoa huo na kuyamaliza.

Hilo halijafanyika hadi leo, lakini elimu inaendelea kushuka tena kwa kasi huku migogoro ya kisiasa ikizidi kushika kasi, na kadiri siku kuelekea Uchaguzi Mkuu mwakani zinavyozidi kupungua, ndivyo na uwezo wa viongozi wetu kushughulikia migogoro hiyo unavyozidi kupungua.

Pamoja na kauli ya hivi karibu ya Mkuu wa Mkoa huo, John Mwakipesile kuwa hataki malumbano tena, bado wanatakiwa kwenda hatua mbele zaidi, kukaa pamoja na kuyamaliza kwa dhati ya mioyo yao pasipo chembe ya unafiki.

Naelewa ukweli huu hautawapendeza, lakini huo ndio mtazamo wa wananchi mkoani humo, wamechoka na wanaumia zaidi pale elimu inapoporomoka kwa kasi. Wakiufikiria mustakabali wa watoto wao, hawapati matumaini; kwani mbele wanaona giza kwa sababu elimu inaporomoka lakini migogoro ya kisiasa ndio inazidi kushika kasi.

Ni wazi kwamba pamoja na harambee za kina Pinda kwa ajili ya Wilaya ya Mbozi, na mikakati mbalimbali inayochukuliwa na wilaya za mkoa huo katika kuimarisha miundombinu ya shule, bado mkoa haujakaa sawa na hakuna mabadiliko yoyote yatakayopatikana katika mazingira ya sasa.

Wakazi kadhaa wa Mbeya waliohojiwa wanataka mkoa ufungue ukurasa mpya wenye kuleta matumaini kwa watoto, wajukuu na vitukuu vyao.

Mmoja alifikia hatua ya kukumbusha kauli ya: “Mkubwa asipokuwa tayari, hata kama mdogo atasema yameisha; hayawezi kuisha.”
 
Back
Top Bottom