Mifereji ya Dhahabu: Pasipo Silaha, Chuki wala Ukatili

Habibu B. Anga

JF-Expert Member
May 7, 2013
6,557
25,671
Sasa, unaweza kupata nakala za Kitabu changu cha "NYUMA YA ULIMWENGU WA SIRI NA UJASUSI".
kitabu kina kurasa 442 na ndani yake kuna makala 17.
Bei ya kitabu hiki ni Tsh 50,000/-

Pia waweza kupata kitabu changu cha "OPARESHENI ZA KIJASUSI ZILIZOFANIKIWA ZAIDI"
Kitabu hiki kina kurasa 214 na ndani yake nimechambua Oparesheni 6 tofauti.
Bei ya kitabu hiki ni Tsh 15,000/-

Wasiliana nami kwa namba 0759 181 457

Wako watu ambao uwepo wao katika ulimwengu wamechangia kwa namna moja au nyingine kuufanya huu ulimwengu uwe jinsi ulivyo. Wako wengine ambao wamechangia kwa kiwango kikubwa kuifanya 'mifumo' ya dunia iwe jinsi ilivyo. Mara nyingi watu hawa tunawasoma kwenye vitabu endapo kama waliishi miaka mingi iliyopita na endapo kama bado wako hai huwa ni watu tunao wahusudu na kuwachukulia kama mifano ya kuigwa.

Lakini wako watu ambao ni vigumu kuwahusudu au kuwaandika katika vitabu vya historia kutokana na jinsi ambavyo walichangia kubadilisha mifumo ya kimaisha dunia. Moja wapo ya watu hawa ni Wezi ambao mimi binafsi napenda kuwaita 'Wezi wa Daraja la kwanza' (First Class Thieves). Hawa wamekuwa toka enzi za kale na wamekuwa wanaushangaza ulimwengu kwa kiwango cha akili walichotumia na uthubutu walionao katika kutekeleza matukio.

Moja wapo kati ya wezi hawa ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kubadilisha mifumo ya kiusalama ni mtu ambaye ameandika historia katika ulimwengu na hususani taifa la ufaransa kwa kutekeleza tukio kubwa zaidi la ujambazi na lenye thamani kubwa zaidi ambayo mpaka leo hii bado hajatokea mtu mwingine katika nchi ya ufaransa aliyefanikiwa kutekeleza tukio kubwa kama hilo na kwa mafanikio. Yeye binafsi hakuiba ili tu apate kutajirika pekee na kuishi maisha ya anasa bali pia aliiba kwa kuwa aliamini huo ndio wito wake (destiny) na aliiba ili kuudhihirishia ulimwengu kuwa anaweza. Jina lake aliitwa Albert Spaggiarri.




May 1976: Nice, Ufaransa


Alfred Spaggiari moja ya watu mashuhuri kwenye jiji la Nice nchini ufaransa na swahiba mkubwa wa Meya wa jiji la Nice Bw. Jacques Medécin, Spaggiari ambaye shughuli zake alikuwa amebobea kwenye upigaji picha za mitindo na matukio muhimu zaidi ya kiserika na binafsi alikuwa ameitisha kikao kilichohudhuriwa na watu wapatao ishirini katika nyumba yake ya mapumziko ya mwisho wa wiki iliyopo nje kidogo ya jiji la Nice. Kikao hicho hakikuhusu upigaji picha au siasa bali aliitisha kikao hicho cha siri na aliwaalika wahalifu kadhaa ili awashirikishe mpango wa siri aliokuwa nao. Kati ya watu hao 20 watu watano walikuwa ni wawakilishi wa ukoo wa Mafia wa usisili ( Sicilian Mafia) aliowaakika kutoka Italia.
Akiwa anafungua kikao hicho Spaggiari aliwaeleza kuwa amewaita hapo ili awashirikishe kwenye tukio la wizi la kihistoria na ambalo anaamini litakuwa na thamani kubwa sana kiasi kwamba hawataitaji kuiba tena maishani mwao ili kuishi maisha ya hali ya juu waliyoyapenda.

Spaggiari akawaeleza kuwa amedhamiria kuiba katika Kuba (vault) ya benki ya Société Générale. Ambayo ndiyo ilikuwa benki kubwa zaidi katika nchi ya ufaransa kwa kipindi hicho na moja ya benki kubwa zaidi duniani.
Lakini kabla hajaendelea zaidi na 'hotuba' yake watu kadhaa waliokuwepo kwenye kikao hicho waliangua kicheko cha dharau na kusema kwamba walidhani kuwa wameitwa kwenye kikao hicho labda 'celebrity' Spaggiari alikuwa ana ugomvi na 'celebrity' mwenzake kwahiyo alitaka awalipe wakamfanyie 'umafia' lakini kamwe hawakutegemea mtu 'mboga saba' kama Spaggiari ati atake kuwashirikisha wao kuhusu tukio la ujambazi kwani wanaamini kuwa Spagiari hajui chochote kuhusu uhalifu wala hajui hata "a e i o u" za matukio ya ujambazi.
Spaggiari aka kaa kimya kwa sekunde kadhaa huku macho yake yakiangaza kwa wahudhuriaji wote wa kikao hicho na macho yake yakakutana na mzee mmoja wa makamo aliyekuwepo pia kwenye kikao hicho ambaye walifahamiana vyema na Spaggiari. Spaggiari akampa ishara kuwa awaeleze watu hao waliohudhuria kikao hicho kuwa yeye ni nani, yeye Spaggiari halisi ni nani, awaeleze kiundani wamfahamu Spaggiari zaidi ya yule wanayemsoma kwenye magazeti, zaidi ya Spaggiari 'mboga saba' wanaye mjua.



UTAMBULISHO MFUPI WA "MPIGA PICHA" ALBERT SPAGGIARI

Albert Spaggiari alizaliwa Desemba 14, 1932 katika mji mdogo wa Hyerés ambapo mama yake alimiliki duka kubwa la mavazi ya ndani ya wanawake (lingerie).
Akiwa bado yuko katika shule ya upili, katika shule yao Spaggiari alitokea kumpenda msichana ambaye alikuwa ni mtoto wa Mkuu wa shule. Mara nyingi Spaggiari alijikuta anaingia kwenye matatizo na walimu kutokana na kumshushia kipigo kijana mmoja wa kisenegali ambaye alipata ufadhili wa kusoma shuleni hapo lakini naye alionyesha hisia za kumpenda binti huyo. Kutokana na Spaggiari kuingia kwenye matatizo mara kwa mara na walimu hakufanikiwa kumaliza shule kwani alifukuzwa baada ya walimu kuchoshwa na tabia zake.

Licha ya kutokuwepo shuleni Spaggiari aliendeleza uhusiano wake na yule mtoto wa Mkuu wa shule
Katika juhudi za Kutaka kumuonyesha huyo binti kwamba yeye sio hoe hae Spaggiari akamuahidi huyo binti kumnunulia pete ya almasi yenye thamani kubwa sana. Uhalisia ni kwamba Spaggiari hakuwa na hela lakini kutoka moyoni alipania kuitekeleza ahadi huyo ili azidi kumfanya mpenzi wake ampende zaidi.

Hivyo basi Spaggiari akamshawishi rafiki yake mmoja kuwa usiku wa siku moja ana mpango wa kuiba pete ya almasi katika duka mojawapo hapo mjini kwao.. Rafiki yake akakubali na wakapanga siku wakatekeleza tukio lakini kwa masikitiko makubwa wakakamatwa.
Baada ya kukamatwa na kushtakiwa mahakamani, Spagiarri alihukumiwa kwenda jela.
Lakini kutokana na umri wake mdogo wa miaka 17, serikaki na Spagiarri wakakubaliana kuwa akajiunge na jeshi badala ya kukaa jela.
Hivyo basi Spaggiarri akajiunga na jeshi kitengo cha wanajeshi wa kutumia parashuti.

Mwaka 1953 Spaggiari alishiriki katika vita ambayo majeshi ya Ufaransa yaliivamia koloni lao la Indochina (Vietnam ya sasa na maeneo yanayoizunguka). Spaggiari alikuwa ni mwanajeshi hodari na aliwahi kujeruhiwa mara mbili katika mapambano na kutokana na uhodari wake alitunukiwa nishani ya heshima.
Lakini ni kana kwamba wizi ulikuwa ndani ya vinasaba vya Spaggiari kwani akiwa huko huko Vietnam na kabla vita haijaisha yeye pamoja na rafiki yake walivamia duka moja mjini Hanoi na baada ya upelelezi walibainika.
Hii ilipelekea Spaggiari kufukuzwa jeshini na kurudishwa ufaransa na kufunguliwa mashtaka na akahukumiwa miaka mitano.

Spaggiarri akatumikia kifungo na mnamo mwaka 1957 akarudi uraiani.
Baada ya kurudi uraiani Spaggiari akajihusisha na kufanya kazi katika viwanda vya kutengeneza makabati ya kuhifadhi vitu vya siri (Safes) na pia akafanikiwa kupata msichana mrembo aliyeitwa Marcelle Audi ambaye kwa kipindi hicho alikuwa anafanya kazi kama Nesi na akafanikiwa kumuoa.
Baada ya kumuoa waliondoka ufaransa na kuelekea nchini Senegal ambapo kwa kipindi hicho bado lilikuwa ni koloni la Ufaransa na wakaishi mjini Dakar. Kwa bahati mbaya hawakufanikiwa kukaa sana Senegal kwani mwaka 1960 Senegal ilipata Uhuru na ikawalazimu warejee tena Ufaransa.

Baada ya kurejea Ufaransa Spaggiarri akaanza kujihusisha na vikundi vya uzalendo vya nchi za ulaya ambavyo vilikuwa vinapinga wazungu kuachia makoloni ya Africa.
Kikundi ambacho kilimvutia sana Spaggiarri kiliitwa OAS (Organisation de al'rmée Secrète). Kikundi hiki kilijihusisha na shughuli za kishushushu kusaidia kushawishi serikali ya ufaransa isiachie koloni la Algeria na pia kilifanya shughuli zake kudhoofisha harakati za watu wa Algeria kudai Uhuru. Spaggiari akajiunga na kikundi hiki mwaka 1961.
Rais wa ufarasa wa kipindi hicho (Rais De Gaulle) mwanzoni alikiunga mkono kikundi hiki lakini kadiri muda ulivyoenda na kuonekana wazi kuwa suala la kuipatia Uhuru Algeria haliepukiki, Rais De Gaulle akakipiga marufuku kikundi cha OAS na vikundi vingine vyote vyenye mlengo huo.

Baada ya harakati zao za OAS kupigwa marufuku Spaggiari akabakia na kinyongo kikubwa sana dhidi ya Rais De Gaulle. Hivyo basi mwaka huo huo wa 1961 akasafiri mpaka nchini Hispania kwenda kuonana na mmoja wa waanzilishi wa kikundi cha OAS mzee aliyeitwa Jenerali Pierre Lagaillarde. Sababu kubwa ya kumfuata ni kwamba Spaggiari alikuwa anahitaji apewe ruhusu ya kumdungua kwa risasi Rais De Gaulle ili kulipiza kisasi kwa "kuwasaliti" OAS na 'raia' wa Ufaransa kwa kuunga mkono Algeria kupewa Uhuru.
Jenerali Pierre akamwambia kuwa ampe 'ramani' yake jinsi alivyopanga ni namna gani atampiga risasi Rais De Gaulle.
Bila kusita Spaggiari akamueleza mpango wake, kuwa msafara wa Rais De Gaulle huwa unapita katika mji mdogo wa Hyerès na huwa wanapita mbele ya duka la mama yake Spaggiari (mama yake Spaggiari alikuwa ni mfanyabiashara wa mavazi ya ndani ya akina mama (langarie)). Hivyo Spaggiari akamueleza Jenerali Pierre kuwa atakaa juu ya paa la duka la mama yake na atakaa na bunduki ya wadunguaji na Msafara wa Rais ukupita atampiga risasi Rais De Guelle.

Jenerali Pierre akakubaliana naye kuwa arudi ufaransa na akatekeleze mpango huo lakini akampa onyo kuwa siku hiyo atayotakaa juu ya paa la duka la mama yake, asifyatue risasi kabla hajapata amri ya moja kwa moja kutoka kwake (direct command). Spaggiari akakubali na kurejea ufaransa.
Siku ya siku ikafika, Spaggiari akakaa juu ya paa la duka la mama yake, msafara wa Rais ukapita mbele ya duka, Spaggiari akasubiri 'direct command' kutoka kwa Jenereli Pierre ili amfyatulie risasi Rais De Guelle, akasubiri na kusubiri, amri haikuja na msafara wa Rais ulitokomea mbali na macho yake.
Wiki chache baadae Spaggiarri akakamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya kujihusisha na vikundi vya 'kigaidi'. Spaggiarri akagundua kuwa Jenerali Pierre 'alimuuza'.
Mahakama ikamuhukumu kifungo cha miaka minne jela. Spaggiari akatumikia miaka yote.

Siku ya kutoka jela ni mke wake Audi pekee aliyemkuta nje ya geti la jela akimsubiri waende nyumbani. Spaggiari akamuapia mkewe kuwa hataki tena kujihusisha na harakati zozote wala siasa. Kuanzia sasa kitu pekee anachokitaka ni kuwa mume bora kwake.
Spaggiarri hakuwa anatania, akafungua ofisi yake ya upigaji picha katika jiji la Nice. Akafanya kazi kwa bidii usiku na mchana na ndani ya miaka michache akaibukia kuwa ndiye mpiga picha bora zaidi katika jiji la Nice, na harusi zote za hadhi ya juu ni Spaggiari ndiye alipiga picha, matukio yote muhimu ya kiserikali na binafsi, tenda ya kupiga picha alipewa Spaggiari. Punde si punde Spaggiari akawa moja ya watu mashuhuri zaidi katika jiji la Nice, na akafahamiana na kila mtu muhimu kwenye jiji la Nice. Mpiga picha Spaggiari akawa moja ya raia wanaoheshimika zaidi jijini Nice.
Lakini licha ya mafanikio na heshima yote, kana kwamba uhalifu umeandikwa kwenye vinasaba vyake, roho ya Spaggiari ilitaka zaidi! Sio pesa zaidi, sio umaarufu zaidi, hapana roho ya Spaggiari ilitamani kuiba! Kufanya tukio moja kubwa kuudhihirishia ulimwengu umahiri wake katika wizi.
Roho ya Spaggiari iliwasha kwa kiu ya kutaka kuiba, na alijua bayana roho yake haitotulia mpaka pale atakapo tekeleza walau tukio moja maridadi la wizi. Na ili kujiridhisha Spaggiari akaamua kuwa atafanya tukio la wizi ambalo litasimuliwa vizazi na vizazi.



Turejee kwenye Kikao cha "Mpiga Picha" Spaggiari na wenzake


Baada ya wote waliokuwepo kwenye kikao hicho kusikia historia hiyo ya Spaggiari walishikwa na bumbuwazi. Wote waliduwaa kwani baadhi yao waliwahi kusikia minong'oni mtaani kuwa mpiga picha Spaggiari ni 'mtundu mtundu' lakini hawakutegemea kama huo 'utundu' wake aliwahi kuhusika kwenye maisha ya hatari kama jinsi ambavyo wamesimuliwa kwenye kikao hicho.
Kwa ufupi kwa historia hiyo fupi, Spaggiari alivuna heshima kutoka kwa watu wote ambao walikuwa wamehudhuria kikao hicho lakini swali moja likabaki hewani, je mpango wake ni upi juu ya utekelezaji wa kuiba benki hiyo ya Société Générale, naye Spaggiari akawajibu kuwa hicho ndicho alichowaitia hapo kuwa wakae chini wote watoke na mpango kabambe wa kuiba katika benki hiyo na yeye yuko tayari kusikia mawazo yao kwanza.

Baadhi ya waliokuwepo kwenye kikao kile hasa wale wanachama watano kutoka ukoo wa Mafia wa usisili, wakatoa maoni yao. Wakasema kuwa kama anaweza kuwapa uhakika kuwa katika tarehe fulani mahususi benki hiyo itakuwa na kiwango kikubwa cha fedha basi wao wanaweza wakasaidia wapate silaha na kuweka mpango madhubuti wa kuivamia hiyo bank na kupora hela. Baada ya wanachama hao wa Mafia kutoa maoni hayo Spaggiari akawapa jibu la kuwashangaza sana, kuwa hakubaliani na mkakati huo kwasababu anataka kwamba tukio hilo watakalotekeleza anataka waweke mpango wa kutumia akili zaidi badala ya kutumia mabavu na silaha.

Baada ya maoni hayo kukataliwa wengine nao wakatoa maoni kwamba labda wamteke mtoto au mke wa meneja wa benki kisha watumie kigezo hicho kumshawishi meneja awasaidie kuiba katika benki yake. Wazo hili nalo lilipingwa na Spaggiari na akawaeleza kuwa hataki ukatili wowote utumike katika kutekeleza tukio hili. Mzee mmoja veterani wa kikundi cha OAS ambaye alikuwepo yeye akasema kuwa anatamani afahamu siku ambayo benki yoyote kubwa inakuwa na kiwango kikubwa cha fedha kisha wailipue ili kuikomesha serikali kwa 'kusaliti' kikundi chao cha OAS. Spaggiari akamjibu kwa kifupi tu kuwa kama akitaka afanye tukio lolote kwa ufanisi anatakiwa aweke hisia za chuki pembeni. Hivyo wazo lake hilo la kulipua benki kwa kisasi alikuwa analipinga.

Wale jamaa watano wanachama wa ukoo wa kihalifu wa Mafia, ambao walisafiri kutoka Itali kuja kuhudhuria kikao hicho wakainuka wote kwa pamoja na kumwambia Spaggiari kuwa wanaondoka. Wanahisi kuwa licha ya kuwa ni kweli kama walivyosikia kwenye kikao hicho kuwa amewahi kushiriki katika mipango ya hatari katika maisha yake lakini wanahisi kuwa kwasasa Spaggiari ana ndoto za mchana na hayuko kwenye uhalisia kwasababu kama anakataa maoni yote yaliyotolewa hawaoni uwezekano wowote wa kikao hicho kuzaa mkakati wenye uhalisia wa kutekeleza tukio la ujambazi.
Spaggiari akawasisitiza kuwa wakae chini wasikilize maoni mengine yakiwemo maoni yake lakini wanachama hao wa Mafia wakamwambaia kuwa hawako tayari kuendelea na kikao hicho kwani wanadhani mkakati wowote utakaowekwa hapo utakuwa ni kana kwamba wanaenda kujitoa sadaka kwani haiingii akilini watu muwe na dhamira ya kuiba benki alafu msitumie silaha. Mafia hao wakainuka, wakaaga na kuondoka.

Kwahiyo Spaggiari akabakia na watu 15 pekee kwenye kikao hicho wengi wao wakiwa ni wanachama wa zamani wa kikundi cha OAS. Na alivyowaangalia nyuso zao aligundua dhahiri kuwa ndani ya dakika chache kama hatowapa mpango wowote wa kuwashawishi kuhusu hilo tukio nao wangeweza kuinuka na kuondoka.
Spaggiari akaenda mpaka kwenye kabati la pembeni lililopo kwenye sebule hiyo na kutoka na boksi dogo la saizi ya kati na kulibeba kwa mikono miwili mpaka kwenye meza iliyokuwepo katikati ya sebule na kisha akawaomba wote wainuke na kusogea karibu na meza.
Baada ya wote kusogea karibu na meza Spaggiari akatoa makaratasi kadhaa kutoka kwenye lile box na kayatandaza juu ya meza.

Makaratasi yale yalionyesha ramani na mpango mji wa jiji la Nice. Kuna makaratasi yalionyesha nyumba kwa nyumba na jengo kwa jengo kwa jiji lote la Nice. Makaratasi mengine yalionyesha juu ya mifumo ya barabara ya jiji zima. Makaratasi mengine yalionyesha juu ya mfumo ya maji taka ya jiji zima na hapa katika karatasi hizi za mifumo ya maji taka ndipo hasa Spaggiari aliwataka awaeleze kuhusu mpango wake anao ufikiria. Katika karatasi hiyo inayoonyesha mfumo wa maji taka, Spaggiari akawaonyesha mahali ambapo benki ilipo na akaweka alama kwenye karatasi kisha akawaonyesha mfereji wa maji taka wa chini kwa chini ( Sewer) ambao unapita karibu kabisa na benki hiyo na pia akaweka alama kwenye mfereji huo kisha akawafafanulia zaidi. Akawaeleza kuwa upande ambapo mfereji huo unapita na kupakana na benki ni takribani mita 5 tu kutoka kwenye mfereji mpaka kwenye Kuba (Vault) ya benki. Hivyo basi kama wataweza kuchimba shimo la chini kwa chini (tunnel) lenye urefu wa mita 8 kutoka kwenye mtaro huo wa maji taka kuelekea upande wa benki basi watakuwa wamefika katikati ya sakafu ya vault ya benki ya Société Générale na kitu pekee kitakachobaki ni kutoboa tundu dogo kwa kwenda juu na watakalolitumia kuingilia ndani ya vault kutoka kwenye tunnel walilochimba kutoka mtaroni. Huo ndio ulikuwa mkakati wake.
Spaggiari aliwaangalia nyuso za wale waliokuwepo kwenye hicho kikao na alikuwa na uhakika kuwa wamevutiwa na mkakati huo ingawa walikuwa na maswali kadhaa.

Spaggiari akatoa fursa waulize maswali na swali la kwanza lililokuwepo kwenye vichwa vya wengi lilikuwa je, watakapokuwa chini wanachimba hilo shimo (tunnel) hawatashtukiwa kutokana na makelele na mitetemo watakayo sababisha. Spaggiari akawajibu kuwa japokuwa tunnel la urefu wa mita 8 wanaume kama wao 15 wana uwezo wa kulichimba ndani ya siku hata 3 lakini ili kuzuia kusababisha kelele na mitetemo amepanga kuwa shimo hilo litachimbwa taratibu kana kwamba wanakula chakula kwenye sahani kwa kutumia kijiko. Haijalishi itachukua wiki au miezi mingapi.

Swali lingine lilikuwa je itakuwaje kama vault ina 'sensors' za kuhisi mitetemo au sauti? Spaggiari akawajibu kuwa kuhusu hilo wampe kama siku tatu atafahamu hiyo vault ina 'sensors' zipi na ni namna gani watakavyo jiahami nazo.

Spaggiari akauliza kama kuna swali lingine. Hakukuwa na swali. Kisha akawaukiza, "who is in?" ("Nani atashiriki nami kwenye hili?") wote 15 waliobakia kwenye kikao hicho walikubali kushiriki katika tukio hilo.
Spaggiari akawaeleza kuwa anawapa wiki moja kila mtu akamalize ratiba zake alizokuwa nazo, mwenye familia akaage na kudanganya anavyoweza kwani wakikutana baada ya hiyo wiki moja watakuwa na wiki kadhaa au pengine miezi kadhaa ya kutekeleza tukio hilo ambalo halijawahi kufanyika kabla.
Wakaagana, wakatawanyika.



SPAGGIARI NA GENGE LAKE WANAINGIA 'KAZINI'



Wakati wenzake wakiwa wamerudi makwao kuaga familia zao ili warejee baada ya wiki moja kwa ajili ya 'kazi', yeye Spaggiari kesho yake alifika mpaka kwenye benki ya Société Générale na akaomba kuwa mteja afunguliwe sanduki jipya kwa ajili ya kuhifadhi vitu vyake vya faragha/siri ( safe deposit box) katika vault. Baada ya kukamilisha taratibu zote za kujaza nyaraka za maandishi na kulipia gharama za huduma hiyo hatimaye akapelekwa na muhudumu wa benki mpaka kwenye vault na kuonyeshwa kisanduku ambacho kitakuwa chake. Kisha muhudumu akatoka nje ya mlango ili kumpa faragha Spaggiari ahifadhi vitu vyake. Baada ya kuachwa peke yake Spaggiari akatoa saa kubwa ya muito (alarm clock) ambayo ilikuwa kwenye kibegi kidogo alichokuja nacho. Saa hii ilikuwa na ukubwa wa kufanana kabisa na saa kubwa ya ukutani. Lakini ilikuwa nzito zaidi. Na ilitengenezwa kuwa saa ya muito ambayo muda uliotegeshwa ukifika Saa inaita na kutetema (vibration). Spaggiari akaitegesha saa hiyo iwe inaita usiku wa manane. Kisha akaiweka kwenye kisanduku chake alichoonyeshwa. Kisha akakifunga kisanduku, akatoka nje akakabidhi funguo ya kisanduku kwa muhudumu na kurudi nyumbani.

Baada ya wiki moja kupita na wenzake kurudi kwa ajili yakuanza kazi, kwanza kabisa Spaggiari akawapa muhtasari juu ya alichofanikisha mpaka mda huo. Akawaeleza kuwa hawahitaji kuhofu kuhusu 'sensor' za mitetemo au sauti kwakuwa ameng'amua kuwa vault hiyo haina 'sensor' zozote zile. Walipo muuliza amejuaje, akawaeleza kuhusu Saa ya muito aliyoiweka kwenye hiyo vault na kuitegesha iwe inaita muda wa usiku. Na akawaeleza kuwa kwa siku kadhaa amekuwa akichunguza na hajaona taharuki yoyote kutoka kwa walinzi au alarm za ulinzi za benki zikilia hivyo ana uhakika kabisa hakuna 'sensors' zozote kwenye hiyo vault.

Spaggiari alikuwa sahihi kabisa kwani vault hiyo ni kweli haikuwa na sensor zozote, wenyewe wenye benki waliamini kuwa vault hiyo ilikuwa haiingiliki kwa namna yoyote (utterly impregnable) kwasababu mlango wake wa chuma ulikuwa mnene zaidi ya kuta tatu za nyumba ya tofali zikiunganishwa pamoja na mtu alihitajika kuingiza namba maalumu (combination) na kutumia funguo kubwa mbili maalumu ili aweze kuufungua. Pia kuta za hiyo vault zilikuwa haiwezekani hata mtu kuzigusa akiwa nje kwani vault ilikuwa kati kati ya jengo la benki na kuta zake zilikuwa nene kiasi kwamba zinazidi hata unene wa kuta tatu za nyumba ya kawaida.

Baada ya Spaggiari kuwapa wenzake muhtasari huo, kawaeleza kuwa hivyo basi saa hiyo ya muito watakuwa wanaitumia kama muongozo wa ziada ili wawe wanachimba kwa usahihi zaidi kuekekea chini ya sakafu ya vault (pinpointing). Baada ya kupeana muhtasari, Spaggiari akaondoka na wenzake ili akawaonyeshe eneo la kazi.

Walitumia boti ndogo kusafiri katika mto Rivera mpaka mahali ambapo kiwango kidogo cha maji ya mto yanachepuka na kuingia katika mtaro mkubwa wa maji taka unaokusanya maji na kupita karibu na benki waliyotaka kuiba. Walipofika hapa walitumia maboya kuelea juu ya maji machafu ya mtaro yaliyojaa kinyesi cha binadamu na uchafu mwingine, walielea kuelekea mbele kwa takribani dakika ishirini wakiwa na ramani zao mikononi mpaka walipofika sehemu waliyoihitaji.

Baada ya kufika hapo Spaggiari akawapa maelekezo kuwa wanatakiwa wachimbe moja kwa moja bila kupindisha hata kidogo kwenda mita 8 ndani na kama watakuwa sahihi baada ya kufikisha mita 8 hizo alarm aliyoiweka kwenye vault ikilia basi wataisikia juu ya vichwa vyao, ikimaanisha kwamba wako chini ya sakafu ya vault.
Pia Spaggiari akawagawanya wenzake kwenye shift za kufanya kazi. Akawaambia kuwa kutakuwa na makundi mawili, kila kundi litafanya kazi kwa masaa kumi wakati huo wengine watakuwa wamelala na akawasisitiza kuwa ni lazima walale kwa masaa kumi. Kwahiyo shifti zilikuwa mbili, masaa kumi kazini na masaa kumi kulala. Pia akawakataza wasiguse kabisa pombe au kahawa kwa muda wote ambao watakuwa wanafanya hiyo kazi.

Siku iliyofuata kazi ilianza. Kazi ilifanyika bila papara, taratibu na kwa umakini mkubwa. Kazi ikaendelea kwa siku kadhaa, wiki kadhaa na baada ya miezi miwili hatimae walifikisha tanuru (tunnel) la urefu wa mita 8. Baada ya kufikisha umbali huo Spaggiari akawaambia wasubiri usiku wa manane kusikiliza saa ya muito ili wajue kama wako sahihi au la. Ilipofika usiku wa manane alarm ya saa iliyowekwa kwenye vault na Spaggiari iliita, na waliisikia juu ya vichwa vyao kabisa. Wakapongezana kwani sasa walikuwa na uhakika asilimia mia moja kuwa wako sahihi, walikuwa wako chini ya sakafu ya vault na kilichobakia ilikuwa ni kutoboa hiyo sakafu na kuchukua 'mwali wao'.
Spaggiari akawaambia wenzake kuwa inabidi wapumzike kwa siku mbili kuisubiria Bestille Day ndipo watoboe sakafu na kuchukua mwali wao.

Bastille Day (siku ya Uhuru wa Ufaransa) ambayo husheherekewa kila mwaka tarehe 14 July na kwa mwaka huu 1976 ilikuwa inaangukia siku ya alhamisi, hivyo hii ilifanya kuwe na siku nne za mapumziko (alhamisi na ijumaa (sherehe za Bastille Day) Jumamosi na jumapili (mapumziko ya mwisho wa juma)). Kwahiyo Spaggiari alitaka wapate muda wa kutosha kwa siku nne ili wachukue fedha na vitu vingi kadiri wawezavyo.

Hatimaye alhamisi ikawadia na Spaggiari na genge lake wakamalizia kutoboa sakafu ya vault na kuingia ndani. Jambo la kwanza walilolifanya baada kufanikiwa kuingia ndani ya vault ni kuchomelea mlango wa vault kwa ndani ili mtu aliyepo nje asiweze kuufungua.
Kazi ikaanza na Spaggiari kwa kutumia uzoefu aliokuwa nao wa kufanya kazi kwenye viwanda vya kutengeneza 'safes' akawaongoza wenzake katika zoezi la kufungua visanduku. Kazi ilifanyika mchana na usiku kwa siku ya kwanza ya alhamisi na kesho yake siku ya Ijumaa Spaggiari akawaambia wenzake wapumzike kwa masaa machache ili nao washerehekee sikukuu ya Bastille kama wenzao walioko huko mitaani. Hivyo basi Spaggiari akatoka kwenye vault na kurudi mtaani kununua mvinyo pamoja na vyakula vya anasa na kurudi navyo kwenye vault kwa ajili ya kusheherekea. Baada ya kumaliza kula na kunywa kazi iliendelea usiku na mchana siku hiyo ya ijumaa, jumamosi na ilipofika jumapili mchana walikuwa wamefanikiwa kufungua yapata visanduku 400 vilivyokuwa na fedha taslimu, vito vya thamani, hati fungani na vitu vinginevyo vya thamani kubwa. Inakadiriwa kuwa thamani ya 'mzigo' wote ambao Spaggiari na genge lake walipata unafikia Faranga Milioni 60 za ufaransa (60 million French Frans).

Ilipofika muda wa mchana siku ya Jumapili mvua ilianza kunyesha na Spaggiari akahisi mitaro waliyotumia kuingilia inaweza kujaa maji na hivyo kufanya zoezi la kutoka kuwa gumu hivyo basi akawaamuru wenzake waondoke kabla mvua haijawa kubwa. Lakini kabla hawaondoka aliwaambia wenzake kuwa anahitaji kufanya jambo moja la muhimu la mwisho. Huku akionekana akiwa na hisia na msisimko wa hali ya juu, spaggiari alichukua kopo la rangi alilokuwa amekuja nalo pamoja na brashi ndogo ya kapakia rangi, kisha akausogelea ukuta mmoja ndani ya vault na kuandika maandishi makubwa yaliyo someka; "SANS ARMES, NI HAINE, NI VIOLENCE" ("Without weapons, nor hatred, nor violence" ("Pasipo silaha, wala chuki, wala ukatili")).
Hiyo ndio 'falsafa' aliyotaka kuifikisha kwa ulimwengu mzima kujitambulisha yeye ni 'mwizi daraja la kwanza' wa dizaini gani.
Baada ya hapo wakafungasha mizigo yao, wakatokomea.


'Maisha' Baada ya Tukio..

Siku ya jumatatu benki ya Société Générale ilifunguliwa na shughuli ziliendelea kama kawaida pasipo yeyote kung'amua kuwa kuna jambo lilitokea ndani ya vault. Na kama ilivyo ada ilipofika majira saa Tatu na nusu asubuhi wafanyakazi wawili walielekea kwenye chumba cha Vault kukifungua ili kuruhusu wateja kuhifadhi vitu na wengine kuchukua vitu walivyohifadhi. Walipofika mlangoni wakaingiza namba maalumu na kisha kama ilivyo utaratibu wakaingiza funguo mbili katika matundu mawili juu ya mlango na kuzungusha funguo lakini jambo la ajabu mlango haukufunguka. Walihangaika kuzungusha funguo karibia nusu saa lakini mlango haukufunguka.

Baada ya juhudi zote hizo bila mafanikio wakaamua watoe taarifa kwa meneja msaidizi wa benki aliyeitwa Pierre Bigou. Bw. Pierre baada na yeye kuhakikisha kuwa mlango ulikuwa haufunguki ikabidi aagize aitwe muhunzi ili aje kuwasaidia. Dakika chache baadae muhunzi alifika na akaanza kuukagua mlango, na ndani ya dakika kumi na tano akawa ameng'amua kuwa mlango umechomelewa kwa ndani na hakuna namna ambayo wanaweza kuufungua wakiwa nje.

Sehemu ya mapokezi baadhi ya wateja walikuja kwa ajili ya kutumia visanduku vyao vya kwenye vault walianza kupaniki na ilimbidi meneja mwenyewe wa benki ahusike kuwatuliza na kuwaondoa wasiwasi. Meneja alitumia maarifa yake yote ya huduma kwa wateja kuwaondoa hofu wateja wake na kuwataka wawe watulivu, " Nothing to worry about monsieur. A minor technical problem madame. Your valuables are quite safe but there may be a slight delay" ("ondoa hofu muheshimiwa. Ni tatizo dogo tu la kiufundi. Vitu vyenu viko salama ila itachukua muda kidogo kurekebisha.") Meneja wa benki Bw. Jacques Guenet alisikika akiwatuliza wateja wake.

Baada ya muhunzi kugundua kuwa mlango huo hautaweza kufunguka kwa nje akapendekeza kuwa watoboe ukuta ili kuingia ndani. Viongozi wa benki wakakubali na kazi kutoboa ukuta ikaanza. Kutokana na unene wa ukuta na kutoboa kwa makini ili wasisababishe hasara nyingine, ilichukua takribani masaa matatu kutoboa tundu kubwa kiasi la kumuwezesha mtu kupita. Yule muhunzi ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuchungulia ndani na alipochungulia alipatwa na mshangao kana kwamba amepoteza fahamu kwa sekunde kadhaa. Hakuamini alichokuwa anakiona ndani ya vault. Huku bado akiwa na mshangao alimgeukia Meneja wa Benki aliyekuwa amesimama nyuma yake na kumwambia kwa mshangao, "Merde de putain" ("you have been robbed" ("Mmeibiwa")).

Baada ya wote bumbuwazi kuwaisha kutokana na kutoamini macho yao walichokuwa wanakiona mbele ya macho yao, hatimae wakapiga simu polisi na haraka sana polisi wakawasili. Baada ya Polisi kuwasili na kuingia ndani ya vault nao pia hawakuamini kile walichokuwa wanakiona mbele ya macho yao. Wote kwa pamoja macho yao yaliganda kwenye Ujumbe ulioandikwa kwenye ukuta, "sans armes, ni haine, ni violence" (Pasipo silaha, chuki wala ukatili).



KUKAMATWA, KUSHTAKIWA NA KUWA 'HURU' TENA

Ndani ya miezi miwili polisi walifanikiwa kugundua kuwa Spaggiari ndiye muhusika mkuu wa tukio lile. Haijulikana hasa ni namna gani polisi walifanikiwa kugundua kuwa Spaggiari ndiye alikuwa 'mastermind' wa tukio lile, kwani kumekuwa na maelezo mengi sana yanayokinzana lakini angalau ufafanuzi unaoonyesha uhalisia kidogo ni kwamba mmoja wapo wa watu walioshiriki tukio lile alipopewa mgao wake wa fedha pia alipewa na miche kadhaa ya dhahabu (gold bars) na bila kutumia akili au kuwa na subira akauza mche mmoja ndani ya wiki chache baada ya tukio. Baada ya siku kadhaa mtu aliyeununua mche huo aliripoti polisi kuwa ameuziwa mche wa dhahabu unaofanana kabisa na moja ya miche inayoripotiwa kuwa imeibiwa kwenye vault ya benki ya Société Générale.
Polisi wakamfatilia huyo mtu na wakafanikiwa kumtia nguvuni na baada ya kumuhoji kwa siku kadhaa akawataja wenzake wote akiwemo Albert Spaggiari.

Polisi waliposikia kuwa Spaggiari ndiye alikuwa kiongozi wa tukio hilo, walishikwa na butwaa kwani Spaggiari alikuwa ni moja ya watu mashuhuri na anayeheshimika zaidi jijini Nice. Na kipindi wanapata taarifa hii alikuwa yuko safarini mashariki ya mbali akiwa amemsindikiza rafiki yake Meya wa jiji Bw. Jacques Médecin, katika ziara ya kiserikali.

Siku ambayo Meya na Spaggiari wanarejea Nice kutoka mashariki ya mbali, Spaggiari alikamatwa hapo hapo uwanja wa ndege na kufunguliwa mashtaka ya kuhusika kupanga na kushiriki tukio la ujambazi katika benki ya Société Générale.

Kesi hii ilitikisa vyombo vya habati ulimwengu mzima na umaarufu wa Spaggiari ukaongezeka maradufu na mwenyewe alionekana kufurahia haswa jinsi alivyokuwa anazungumziwa kila kona ya Dunia.

Wakati kesi ikiwa inaendelea Spaggiari akatunga hadithi ambayo kwa bahati mbaya Jaji aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo aliiamini na akawa anatamani kujua kiundani. Spaggiari aliwaeleza kuwa alifanya tukio hilo ili kukiwezesha kiuchumi kikundi cha siri cha wazalendo kilichoitwa 'Catena' (neno la kifaransa linalomaanisha 'Chain' (mnyororo)).

Spaggiari akawaeleza kuwa hayuko tayari kuwapa taarifa za kikundi hicho Polisi kwani hawaamini bali yuko tayari kutoa taarifa kwa Jaji huyo peke yake. Hivyo basi ikawekwa ratiba maalumu ambayo Spaggiari alikuwa anapelekwa ofisini kwa Jaji na kila walipokutana alikuwa anampa kikaratasi alichokiandika kwa mafumbo (coded message) na ilikuwa inamlazimu Jaji akune kichwa haswa ili kung'amua kilichoandikwa na Spaggiari kuhusu siri za hicho kikundi cha 'Catena'.

Katika moja ya vikao vyao na Jaji, Jaji akiwa 'bize' kung'amua Ujumbe huo wa mafumbo Spaggiari aliinuka kutoka kwenye kiti kana kwamba anataka kumkaribia Jaji ili ampe ufafanuzi. Lakini jambo la ajabu alikimbia kwa spidi ya ajabu mpaka dirishani na kujirusha nje kwa uhodari wa hali ya juu (kumbuka aliwahi kuwa mwanajeshi kitengo cha Parashuti). Ofisi ya Jaji ilikuwa juu ghorofa ya Tatu katika hilo Jengo la mahakama, lakini kutokana na Spaggiari kujirusha kwa uhodari alitua chini juu ya paa la gari bila kudhurika. Kisha akakimbia kuvuka barabara na kulikuwa na piki piki inamsubiri.

Baada ya kukwea juu pikipiki akageuka kuwaangalia juu dirishani maaskari pamoja na Jaji waliokuwa wanachungulia wakiwa hawaamini kilichotokea ndani ya sekunde chache. Spaggiari akapayuka kwa nguvu "Au revoir" (kwaherini). Kisha akatabasamu kwa dharau na inasemekana akawaonesha kidole cha kati. Kisha kwa mwendo wa kasi na uhodari pikipiki ikapotea mbele ya upeo wa macho yao. Hiyo ndio ilikuwa mara ya mwisho kwa mamlaka za serikali za ufaransa kumuona Spaggiari.

Wiki mbili baadae mtu mwenye gari ambalo Spaggiari alitua alipo ruka kutoka ghorofani alipokea cheki ya thamani ya faranga 5,000 pamoja na kikaratasi kikisema ni kwaajili ya matengenezo ya paa la gari lake.
Pia kuna tetesi ambazo zimeenea mno toka kipindi hicho mpaka sasa kuwa mtu aliyempakia Spaggiari kwenye pikipiki na kumtorosha alikuwa Christian Estrosi bingwa wa Dunia wa mbio za pikipiki ambaye baadae alikuja kuwa waziri katika serikali ya Ufaransa.

Baada ya kutoroka Spaggiari alielekea nchini Argentina na kuishi huko na kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha muonekano (plastic surgery). Inasemekana Spaggiari alikuwa anarudi mara kwa mara nchini Ufaransa kumuona mkewe Audi na Mama yake.

Akiwa nchini Argentia inasemekana kuwa alikuwa karibu sana na CIA akiwasaidia kufanikisha shughuli ambazo CIA hawakutaka kujihusisha nazo moja kwa moja kwa kuhofia jina la idara yao kuchafuka ikitokea siri kuvuja.
Mfano mzuri ni jinsi ambavyo Spaggiari (au daniel jina walilotumia CIA kumtambua (code name)) alishirikiana na Michael Townley afisa wa DINA (kitengo cha ushushushu cha nchi ya Chile) kuchora mchoro na kulipua gari la balozi wa Chile nchini Marekani.

Skandali hii ilichangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha mahusiano ya kidiplomasia kati ya marekani na Chile na hakuna aliyejua uhusika wa CIA mpaka pale mwaka 2000 ambapo CIA waliweka hadharani nyaraka kadhaa za siri baada mda wake wa usiri kupita.

Albert Spaggiari alifariki June 8, 1989 kwa kansa ya koo kutokana na matumizi ya sigara.
Fedha, Vito vya thamani, hati fungani na nyaraka nyingine za siri zilizoibwa na Albert Spagiari na Genge lake havijapatika mpaka leo hii. Tukio hili limebakia katika vichwa vya Wafaransa kama tukio kubwa pekee la wizi wa vitu vya thamani ya juu zaidi na lililotekelezwa kwa umaridadi na akili nyingi au kama Spaggiari mwenyewe alivyolielezea; "Sans armes, ni haine, ni violence" (Pasipo silaha, chuki wala ukatili").



Jiunge na Group langu la WhatsApp kusoma simulizi mpya kila siku. Kuna malipo ya 5,000/- kwa mwezi. Wasiliana nami 0759 181 457




Mwisho.


The Bold

Shukrani kwa; The NewYork Times, Le Firago (Le cerveau de casse du Nice), The Independent, Fric-Frac, Wikipedia & Les égouts du paradis.
 
The bold Shukrani kwa Kunitag, For Sure umejitahidi sana tena saaana mkuu.
hongera kwa kazi nzuri uliyoifanya aisee,.
Tukirudi kwenye
Sans armes, ni haine, ni
violence...
Aisee spaggiari amepiga wizi kama alioupiga Natorbartolo(if am not mistaken) Au unaonaje mkuu?
 
The bold Shukrani kwa Kunitag, For Sure umejitahidi sana tena saaana mkuu.
hongera kwa kazi nzuri uliyoifanya aisee,.
Tukirudi kwenye
Sans armes, ni haine, ni
violence...
Aisee spaggiari amepiga wizi kama alioupiga Natorbartolo(if am not mistaken) Au unaonaje mkuu?
Yeah ni 'kazi' matata kama ya Nortarbatollo! Akili zaidi kuliko nguvu..
 

714937580550ef7a38138f2719150416.jpg
0ace990b0af4f8e3233b8aae4d6fd191.jpg
The bank job movie hiyo
 
Ama kweli usimdharau usiyemjua...
Hii pia imenifanya nitafakari 'vita' kubwa iliyokuwepo baina yetu (author The bold & I) mwaka jana.
Siamini kama ungekuja kuwa mtu ninayeheshimu masimulizi yake namna hii.
Nasikitika sikuona uwezo wako mkubwa wa akili kwa kipindi kile...
Leo hii wewe ni mmoja kati ya watu ninaowaheshimu sana humu JF.

Hivyo basi....mkasa wa Spaggiari sio tu kwamba umeniburudisha,umenifunza pia.
Heshima kwako The bold
 
Ama kweli usimdharau usiyemjua...
Hii pia imenifanya nitafakari 'vita' kubwa iliyokuwepo baina yetu (author The bold & I) mwaka jana.
Siamini kama ungekuja kuwa mtu ninayeheshimu masimulizi yake namna hii.
Nasikitika sikuona uwezo wako mkubwa wa akili kwa kipindi kile...
Leo hii wewe ni mmoja kati ya watu ninaowaheshimu sana humu JF.

Hivyo basi....mkasa wa Spaggiari sio tu kwamba umeniburudisha,umenifunza pia.
Heshima kwako The bold
Yeah nakumbuka ile 'vita' ya mwaja Jana hahaaha!! Aiseee..
Nashukuru sana Nifah kwa pongezi, that means alot, especially coming from you moja ya watu muhimu zaidi humu JamiiForum..
Asante sana Mkuu
 
Back
Top Bottom