Miaka Zaidi ya 15 tangu MV. Bukoba na hakuna tulicho jifunza

Mwita Matteo

JF-Expert Member
May 16, 2010
216
55
Mimi hapa kwa sababu sio mtaalamu wa mambo ya kiufundi na usalama wa Meli naomba leo niongelee hawa waokoaji walio letwa kutoka Afrika ya Kusini.

Ilipozama MV. Bukoba mwaka 1996 nikiwa form two, walikuja wataalamu wa "uokoaji" au tuite search team, kutoka Afrika ya Kusini. Mimi ni kijua baada ya tukio lile kubwa lilotia simanzi kutokea basi Askari wetu wangepewa mafunzo ya vile, ili tena tukio kubwa la vile likitokea mara moja vikosi vyetu vina respond.

Juzi tena baada ya ngudu zetu kupata maafa mazito kama yale tunaambiwa tena vikosi kutoka Afrika kusini vinasubiriwa. Jamani tujkifunze kujipanga hii ni Aibu kwa Taifa kama letu.
 
Vijana walikuwa wakijaribu kupiga mbizi bila hata miwani na viatu vya kuzamia achilia mbali mitungi ya hewa. Kibaya zaidi ni kuwa tuliunda SUMATRA ambayo inatakiwa kuangalia usalama wa hivi vyombo laki meli imeweza ku-oparate bila zana yoyote ya uokoaji. Tukubali tu kuwa viongozi wetu wako makini kupitisha bakuri la kufanikisha ushindi wa chama chao na takrima ya suti na si kuwatumikia wananchi.
 
[h=2]Ajali ya MV Bukoba tumeshindwa kujifunza![/h]
MV-Bukoba-ikizama.jpg
Ni mfano wa sinema ya kutisha iliyojaa kila aina ya ukatili.Abiria wachache walionusurika katika ajali ya kuzama kwa meli ya Mv Bukoba May 21,mwaka 1996 bado wanaamini walipona kwa muujiza.
Miaka kumi na tano baada ya tukio hilo,leo hisia zinaturudisha katika kumbukumbu za ajali hiyo ambayo ilipima uwezo na udhaifu wetu wa kukabiliana na maafa ambayo tumeendelea kuyashuhudia kwa vipindi tofauti.
Wanafunzi wa sekondari za Bwiru wavulana na wasichana wanaikumbuka sana siku hii hasa waliozoea kuoga ziwani asubuhi,kwa mbali waliona harakati za mitumbwi na meli eneo la tukio.Wengi walitoroka na kujikuta uwanja wa mpira Nyamagana wakishangaa kuwasili kwa miili ya marehemu.

Tangu kuzama kwa meli ya Mv Bukoba limebaki kuwa tukio la kihistoria ambalo athari zake ziko wazi kwa mamia ya familia waliopoteza ndugu na wategemezi wao.Inakadiliwa zaidi ya watu 800 walikufa ingawa katika nchi isiyo na mfumo mzuri wa ukusanyaji wa takwimu kwa vyovyote vile idadi hiyo haiwezi kuwa sahihi.
Kwamba meli hiyo ilikuwa imejaza kuzidi uwezo wake sio habari mpya,kwani tangu wakati huo mamia ya wasafiri wa majini wameendelea kupoteza maisha kwa tatizo lile lile la kuruhusu vyombo vilivyochoka kuzidisha abiria.
Familia zilizokuwa na uwezo ziligeuka masikini yatima,wajane na wagane wakishindwa kudai mali za ndugu zao.Wenye tamaa walitumia udhaifu wa marehemu kutoandika wosia kupora mali na kujitajirisha na hata familia za wahanga kubebeshwa mzigo wa madeni.
Tulitakiwa kujifunza kutokana na ajali hiyo kuliko kuendelea kuficha udhaifu wa vyombo hivyo kwa kuvipaka rangi mpya huku tukijua havina uwezo au vimepoteza sifa ya kusafirisha abiria na mizigo yao.
WASEMAVYO WAHANGA WA MEI 21
David Mutensa mfanyabiashara wa mjini Bukoba ni miongoni mwa abiria walionusurika ambaye hajui sehemu ya kuanzia simulizi baada ya kuelea majini kwa muda wa saa tano akisubiri kuokolewa.
Anaanza hivi:
Akiwa ni abiria wa daraja la kwanza aliona hali imekuwa mbaya mapema alfajili na meli ilipoanza kupinduka na kuzama alichukua boya dogo na kujirusha majini huku kila abiria akipigania roho yake.
“Sijui pa kuanzia kwani lilikuwa ni tukio la ghafla,meli kupinduka haijawahi kutokea duniani nilivaa boya dogo na kumwambia mwanamke aliyekuwa jirani yangu twende,akasema twende wapi mwanangu”anaeleza
Anasema alifahamu matumizi ya maboya(life jacket)baada ya kusafiri mara nyingi na meli na wakati mmoja mabaharia waliwahi kufanya mazoezi ndani ya meli jinsi ya kujiokoa kwa kutumia vifaa hivyo.
Maana yake ni kuwa wapo abiria wengi ambao hawakuwahi kuona vifaa hivyo achilia mbali kufahamu matumizi yake na kwa kuikosa elimu hiyo walishindwa kujiokoa hata kama vifaa hivyo vilikuwa mbele yao.
Huyu ni miongoni mwa abiria wengi waliolazimika kuanza upya shughuli zao za biashara na kuwa kifuta machozi cha shilingi laki moja kwa aliyenusurika na laki tano kwa waliopoteza ndugu hakikuwa kipimo sahihi ikilinganishwa na madhara waliyopata.
Simulizi ya Benezeti Benedict(46) mkazi wa kijiji cha Kashaba wilayani Missenyi inasikitisha.Ilikuwa mara yake ya kwanza kupanda meli akielekea Dar es salaam na kuwa ana umbukumbu mbaya za tukio hilo na hakuwahi kutamani kupanda tena meli.
Anasema akiwa ni abiria wa daraja la tatu pamoja na ugeni wake kwenye meli majira ya saa tisa usiku meli ilionekana kuwa na tatizo hali iliyomfanya asilale na kupakata begi kwa hofu.
Anachokumbuka ni kuwa ililala upande wa kushoto na baadaye upande wa kulia majira ya alfajili na kujikuta ameshikilia boya moja watu saba akiwemo mwanamke mmoja.
“Sikuwahi kupanda meli ,usiku nilikuwa na wasiwasi na ilizama taratibu kwa kulalia upande wa kulia nilikimbilia upande wa nyuma ya meli na kuona watu wakielea majini”anasema
Ni tukio analosema lilikuwa mwanzo wake wa kuwa na ugonjwa washinikizo la damu mpaka leo,anapokumbuka picha mbaya ya ajali hiyo.
Huyu naye alipona kimiujiza.Geofrey Francis mkazi wa kijiji cha Buhembe nje ya mji wa Bukoba alikwenda bandarini amechelewa na matokeo yake aliambulia virungu vya polisi waliokuwa wanawazuia abiria wasiendelee kujipenyeza na kupanda meli hiyo.
Anadai juhudi za kutoa kiasi kidogo cha fedha kwa askali ili aruhusiwe hazikufanikiwa na aliungana na abiria wengine watatu ambapo walichukua uamuzi wa kukodi tax na kuifuata meli hiyo bandari ya Kemondo.
Katikati ya safari ya kuelekea Kemondo yalitokea mabishano kama kweli wataiwahi meli hiyo, tofauti iliyomfanya kila mmoja kutafuta sehemu ya kulala bila shaka kujipanga kutoa maelezo kwenye familia juu ya kisa cha kuachwa na meli.
Ni baadhi ya maelezo ya walionusurika, na wakati tukikumbuka miaka kumi na tano tangu kuzama kwa meli ya Mv Bukoba yameendelea kuwepo maafa mengi kama ushahidi kuwa uwezo wa kukabiliana na majanga bado haujaimarika.
Pamoja na ukubwa wa tukio hili taifa limeshindwa kutenga hata dakika moja ya kukaa kimya kuwakumbuka wahanga waliopoteza maisha.Dakika ya kutafakari tulipokosea na kujutia uzembe wetu ambao ni chanzo cha machozi, jasho na damu.
Wakizungumzia hali ya usafiri wa majini ilivyo sasa na wakati uliopita baadhi ya wananchi wameshauri kufanyika kwa ukaguzi wa mara kwa mara na kuongeza udhibiti wa ajali za majini.
Mmojwa wa wananchi hao John Lwekanika alilalamikai ubovu wa vyombo vinavyosafiri na kuwa Mv Bukoba isingezama kama viongozi wangekuwa makini tangu ununuzi wake hadi kuruhusu matumizi.
Anadai kuwepo kwa taarifa za muda mrefu kuwa meli hiyo ilikuwa na mapungufu ambayo yalifumbiwa macho na hatimaye kusababisha maafa makubwa.
Naye mshindi wa tuzo ya uandishi wa masuala ya majanga kwa mwaka 2010 Salome Gregory,anasema taifa halina mipango bayana ya kukabiliana na majanga na kuwa matukio mengi yanaweza kukabiliwa endapo viongozi watakuwa na dhamira ya kweli.
Ni mshindi kutoka gazeti la The Citizen ambaye anaamini elimu ya majanga ikitolewa mashuleni na katika ngazi ya familia utakuwa ni msingi wa kuzalisha viongozi wa watakaoibuka na mikakati ya kuyakabili majanga.
MAJANGA NA USIRI WA TAARIFA
Kama ilivyo ada matukio mengi ya maafa huundiwa tume za uchunguzi na hatimaye matokeo yake huwa siri ya waliochunguza na wale waliopelekewa taarifa.
Mapendekezo ya tume hufungiwa kabatini na wananchi huendelea kuongozwa na hisia wakati wa kujadili utata wa tukio.
Katika nchi ambayo watendaji hugoma kuwajibika kwa kujiudhuru hata kama maafa yanahusishwa na uzembe,taarifa hizi ni muhimu kwani zinatoa mwanga kwa walioathirika kufungua malalamiko ya kulipwa fidia wakitegemea ushahidi wa tume.
Tangu kuzama kwa meli ya Mv Bukoba yamefuata maafa mengi yaliyohusisha kuzama kwa meli,mitumbi,treni, kufukiwa migodini achilia mbali maafa ya hivi karibuni katika kambi za jeshi Mbagala na Gongo la mboto.
Tulitakiwa kujifunza kutokana na makosa na haikutegemewa kuwa baada ya miaka michache meli ya Mv Nyamageni ingezama katika ziwa lile lile na kuua abiria 28,na mpaka leo taarifa ya uchunguzi wa ajali hiyo haiko wazi.
Hakuna kiongozi aliyewajibika kama ambavyo hawafikirii ,pale walipokufa abiria 281 tarehe 24,Juni 2002 baada ya treni kugongana na 73 kuzikwa makaburi ya maili mbili kule Dodoma baada ya kutotambuliwa kama wale wa Mv Bukoba waliozikwa kule Igoma jijini Mwanza.
Kama somo lingekolea ajali ya August 5,ya wanafunzi 18 kufa maji kwa mtumbwi ziwa Viktoria wilayani Sengerema wakienda shuleni isingetokea.Tukio hilo lilitanguliwa na vifo vya wanafunzi tisa waliozama mto Rufiji mkoani Pwani. Hatuwezi kukwepa ukweli kuwa ajali nyingi hazirekodiwi.
Tumeshuhudia juhudi za kujikosha kama ilivyokuwa baada ya wanafunzi 48 wa sekondari ya Shauritanga kuungua mabwenini.Shule zilipewa vifaa vya kuzima moto na kufundishwa matumizi yake.Hakuna anayejua kama ilikuwa hujuma,uzembe au vinginevyo.Mwaka jana Shule ye wasichana Rugambwa mabweni yameungua mara tatu na wanafunzi kunusurika kifo na hakuna kifaa chochote cha kuzima moto.
RAIS KIKWETE NA UJIO WA MELI MPYA
Miongoni mwa ahadi lukuki za rais Jakaya Kikwete kwa wakazi wa mkoa wa Kagera wakati akisaka mhura wa pili wa uongozi ni meli mpya kama mbadala wa Mv Bukoba. Ni kauli yenye matumaini na hakuna sababu ya kuitilia shaka kwamba ilificha hila za wanasiasa hasa pale uchaguzi usipotabilika.
Pamoja na kuimarika kwa miundombinu ya barabara kati ya Bukoba na Mwanza bado uhakika wa usafiri wa majini ni muhimu kwa ajili ya shughuli za kiuchumi. Wananchi watachagua aina ya usafiri waupendao na kuongeza ushindani katika upangaji wa bei.
Hata meli kongwe ya Mv Victoria ambayo inafanya safari zake kati ya Bukoba na Mwanza imeendelea kuwatia abiria wake majaribuni,na imekuwa ikifanyiwa matengenezo ya mara kwa mara ambapo katika kipindi hicho meli ya mizigo ya Mv Serengeti huziba nafasi hiyo kwa muda.
Mwaka 2004, meli ya Mv Viktoria iligonga mwamba eneo la Mubembe ikitoka Mwanza kuelekea Kemondo.Katika hotuba ya mpango wa maendeleo na makadirio ya matumizi ya fedha 2004/2005 aliyekuwa Waziri wa Mawasilinao na Uchukuzi Profesa Mark Mwandosya alidai ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa wafanyakazi.
Alisema uchakavu wa meli na changamoto nyingine vilisababisha lengo la makusanyo lisifikiwe kwa asilimia sita.Hata hivyo kosa moja la uzembe linaweza kuteketeza maisha ya maelfu ya watu na hali hiyo haiwezi kudhibitiwa kwa kushushwa vyeo, au uhamisho.
Kumbukumbu ya kuzama kwa meli ya Mv Bukoba iturudishe kwenye umuhimu wa kuwa na viongozi wanaowajibika kwa kauli na vitendo. Ni dakika moja ya kujuta na kutafakari.
Makala hii imeandikwa Phinias Bashaya akiwa Bukoba, Kagera
Rating: 0.0/5 (0 votes cast)




[h=3]One Response to “Ajali ya MV Bukoba tumeshindwa kujifunza!”[/h]
podius says:
September 10, 2011 at 7:58 pm
Kiukweli ajali ya meli ya mwaka 1996,mei 21 ilikuwa ni pigo la kitaifa kwani sensa ingefanyika wakati huo katika mji wa Bukoba au Mkoa wa Kagera kwa ujumla idadi kubwa ya watu ilikuwa imepote.Kama ikishatokea tunasema ni mipango ya Mungu lakini chanzo kikubwa ni wasimamizi wa vyombo vya usafiri wa majini kwani chanzo kikubwa ni mizigo kuzidi kiasi pamoja na kuwa na ubovu wa baadhi ya vifaa katika chombo husika.Jamani serikali inatutakia nini mbona tunanyanyaswa kama hatuko katika nchi yetu tena tuko huru uhuru tuliupata mwaka 1961?? Haya sasa ajali nyingine imetokea Zanzibar na ni matokeo ya (over carrying).Jamani kwa heshima na tahadhima tunaomba tusaidiwe katika kuboresha na kusimamia usafiri wa majini maana sasa umekuwa wimbo wa ajali majini..Nawapeni pole wote waliopoteza ndugu,jamaa na marafili na Mungu aziweke na kuzipumzisha roho za marehemu mahali pema peponi.AMINA.
 
Huo ndiyo ukweli wenyewe: Ingependeza kama viongozi wa serikali wangekuwa wanapitiapitia ndani ya JF wakapata haya mawazo pengine ingesaidia.
 
Back
Top Bottom