Miaka 50 ya Uhuru ------------ Siungi mkono hoja

MussaBubu

Member
Dec 23, 2011
20
4
Waraka wa Bubu-0002
Miaka 50 ya Uhuru--------Siungi Mkono Hoja

UTANGULIZI
Mwaka 2011 tumeshuhudia sherehe nyingi za kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika Wizara,Taasisi,Mikoa,Wilaya,Kata na vijiji mbalimbali na hata imepelekea baadhi ya watu nikiwamo mimi kuuita ‘’Mwaka wa Sherehe’’.Sina tatizo kwa kufanyika maadhimisho hayo ya Uhuru tatizo langu ni namna na staili iliyotumika kuandaa maadhimisho hayo na hatimaye kuligharimu Taifa mabilioni ya shilingi na kuacha Serikali ikiwa imefilisika.
Maamuzi hayo yalifikiwa na viongozi wetu,huku wakijua wazi kuwa nchi yetu ni moja ya nchi maskini sana na ikiwa katika tatu bora ya nchi ombaomba Duniani ikiongozwa na Iraq na Afghanistan zilizoathiriwa sana na vita.
Mwalimu Nyerere mwaka 1969 aliwahi kusema ‘’Tufanye uchaguzi katika vitu vizuri,na sio katika vitu vizuri na vibaya:Kupanga ni kuchagua’’Ni Dhahiri kuwa viongozi hawakuzingatia maneno hayo ya Mwalimu na hivyo kuamua kupeleka fedha nyingi katika maadhimisho ya sherehe za Uhuru na hata kuongeza malipo kwa wabunge kutoka 150,000/= hadi 330,000/= kwa kikao kimoja ambazo hazikuwa muhimu sana na kuyapuuza mambo muhimu kama vile kuongeza vocha za ruzuku kwa wakulima.
Pia katika sherehe hizo tumesika kauli mbiu ya ‘’TUMEDHUBITI,TUMEWEZA,NA TUNASONGA MBELE’’ ikibebwa na mambo matatu muhimu yaani UHURU,AMANI na MAENDELEO makubwa yaliyofikiwa.Hivyo,kwa kuwa sasa watu wametulia na sherehe zimeshakwisha,ni vizuri sote kwa pamoja tutafakari kauli mbiu hii tukilinganisha na hali halisi ilivyo kwa sasa katika nyanja mbalimbali.
UHURU
Kama Mwalimu alivyowahi kusema katika hotuba yake ya Uhuru na Maendeleo hapo mwaka 1968 kwamba‘’Uhuru na maendeleo vinamahusiano kama alivyo kuku na yai! Bila kuku hupati mayai; na Bila yai hautapata kuku.Hivyohivyo,Bila uhuru huwezi kupata maendeleo na Bila maendeleo utapoteza uhuru wako mara moja’’.Mwalimu aliendelea kusema ‘’Tunamaanisha nini tunapoongelea Uhuru?Kwanza,Kuna uhuru wa kitaifa;Uwezo wa watanzania kupanga juu ya maisha yao,na kujitawala wenyewe bila kuingiliwa na wasio Watanzania.Pili,Kuna uhuru dhidi ya njaa,magonjwa,na umaskini,Na tatu,Kuna uhuru binafsi kwa mtu mmoja mmoja;yaani haki ya kuishi na mtu mwingine katika utu na usawa,Uhuru wa kuongea ,Uhuru wa kushiriki katika maamuzi ya mambo yanayohusu maisha yake .Vitu hivyo vyote ni sehemu ya Uhuru,na Wananchi wa Tanzania hawataweza kuwa na uhuru wa kweli mpaka pale mambo hayo yote watakapokuwa wamehakikishiwa’’
Miaka 50 ya Uhuru,Serikali imeshindwa sio tu kusimamia lakini pia kujiamulia mambo yake yenyewe.Imeshindwa katika manunuzi mbalimbali,kama vile ya rada,imeshindwa kuandika mikataba yenye maslahi kwa Taifa,imeshindwa kusimamia ukusanyaji wa kodi,imeshindwa kutoa ajira kwa vijana,imefikia hatua inawakopa wafanyakazi,inawakopa wakulima wa mahindi ,inagawa ardhi yetu kama kanzu,inasafirisha wanyama wetu nje ya nchi,mfano twiga, imeua viwanda na mashirika mbalimbali na imeamua kubadilishana Madini ya Uranium na Net.Lakini hata pale ufisadi wa rada ulipogundulika bado serikali haikuwa tayari kufuatilia,na mpaka Waingereza walipoamua kutusaidia kurejesha fedha hizo serikalini na hatimaye kutupangia matumizi.
Miaka 50 ya Uhuru,Watanzania bado hawana chakula cha kutosha na kila mwaka huwa tunashuhudia baa la njaa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.Mkoa wa Ruvuma ,moja ya mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa mahindi bado kaya nyingi zinakosa chakula cha kutosha kwa mwaka mzima.Ukienda mahakamani haki haitendeki,Rushwa imetawala kila kona na maskini wengi hupoteza haki zao.Hukumu ya mwizi wa kuku inachukua siku chache kusikilizwa kuliko mwizi wa mabilioni ya shilingi.Tumeshuhudia mafisadi wakubwa wanapojisafisha na kusafishwa kwa jeuri ya fedha,na wakati mwingine kupigiwa debe na hata kiongozi mkuu katika uchaguzi na tuhuma zao kutafsiriwa kama ajali tu ya kisiasa.
Miaka 50 ya Uhuru,Tunashuhudia serikali inavyotumia nguvu nyingi kupitia jeshi la Polisi kupambana na maskini kama vile wamachinga,wakulima wadogo na wafugaji badala ya kupambana kuondoa umaskini uliokithiri kwa Watanzania.Tunashuhudia jinsi vijana wanavyokosa nafasi za masomo katika vyuo mbalimbali kama vile Ualimu ngazi ya cheti,uuguzi ,utabibu na nyinginezo nyingi sio sababu hawana sifa bali ni kwasababu tu hawana pesa za kutoa rushwa kwa wanaohusika au hawana mkubwa yeyote anayeweza kuwasaidia.
Miaka 50 ya Uhuru,Tumeshuhudia tunaletewa bajaji kama gari ya kubebea akina mama wajawazito kwenda hospitali (ambulance) wao wanapelekwa INDIA hata wakitokwa tu na chunusi usoni.Wakati wakulima wa Pamba,mahindi,tumbaku,kahawa na mazao mengine wakihangaika kupata pembejeo na kupata masoko ya kuuza mazao yao,Wabunge wanaongezewa posho kwa asilimia 155 kinyemelanyemela.Wanafunzi wa vyuo vikuu wanagoma kila leo kwa ajili ya kucheleweshea pesa za kujikimu,utafiti ,na mafunzo ya vitendo, serikali inawapiga mabomu na kuwafukuza vyuo,na kwa bahati mbaya sana watoto hao ni wale wa wakulima wadogowadogo na wafugaji,hivyo wakati nyumbani wazazi wao wanateseka kwa maisha magumu na huko vyuoni watoto wao wanapigwa mabomu, ama kweli haya ni machozi,jasho na damu.
Miaka 50 ya Uhuru,Tunashuhudia nyumba za udongo na nyumba za suti za bati ndio makazi ya polisi wetu .Wakati mafisadi wanaita bilioni 25 ni vijisenti ,wafanyakazi wa Serikali wakiwemo polisi,walimu, askari wa JWTZ na wengineo wanalipwa shilingi zisizozidi milioni 30 kama mafao baada ya kustaafu.Majeshi yetu yamekuwa ni makada wa CCM ndio maana mara baada ya kustaafu huteuliwa kushika nafasi mbalimbali kupitia CCM .Polisi hufanya kazi zao kinyume na mafunzo yao,mfano,Polisi wanaacha kuwawinda majambazi badala yake wanatumia kodi za watanzania kuwawinda na kuwasulubu vijana wanaofanya biashara ya BODABODA au YEBOYEBO ambao kimsingi wanajitafutia riziki.Polisi husahau kabisa kwamba hawa wanaowasulubu ni vijana wenzao,kaka zao,baba zao,mama zao na hata babu zao,inasikitisha sana.Na kwa bahati nzuri maisha haya magumu yanamgusa kila Mtanzania wa kawaida bila kujali ni polisi,Kijana,Mzee,Mwanamke,Mwanaume,mtoto,mkubwa,kada wa CCM,kada wa CDM,kada wa NCCR N.K.Na sasa kutokana na umaskini wetu tumepewa masharti na David Cmeroon,Waziri Mkuu wa Uingereza ili tuweze kupewa misaada tunatakiwa kukubali ndoa za jinsia moja,na ndio maana naungana na Mwalimu kwamba usipokuwa na maendeleo unapoteza uhuru wako mara moja.
MAENDELEO
Wanazuoni mbalimbali wametafsiri maendeleo kama ifuatavyo ikitegemea sana mazingira husika;
· Ni mabadiliko ya watu juu ya namna ya kuishi au kufanya vitu kwa ubora zaidi.
· Ni mabadiliko chanya ya fikra na mitazamo ya watu katika masuala mbalimbali
· Ni hali ya kukua au kusonga mbele katika mambo mbalimbali yanayomgusa binadamu
Tafsiri hizo zote hapo juu,zimegusia mambo 2 ya msingi sana,yaani Mabadiliko na Watu,Hivyo maendeleo ya kweli ni yale yanayobadili maisha ya watu kutoka kwenye ufukara wa kupindukia kwenda kwenye maisha bora,yaani kuweza kupata huduma bora za jamii bila kusahau uhakika wa chakula.Na kwa mujibu wa Mwalimu anaamini kwamba ‘’Ukiwaendeleza Watanzania utakuwa umeindeleza Tanzania’’.Hapa ni muhimu tujiulize kama kweli watanzania tumeendelezwa vyakutosha katika mambo mbalimbali kama vile elimu,maji,huduma za afya kilimo na n.k, Je,tunasonga mbele au tunarudi nyuma?
Katika hotuba yake Uhuru na Maendeleo mwaka 1968,Mwalimu anasisitiza kwamba ‘’Ukweli ni kwamba Maendeleo maana yake ni maendeleo ya watu.Barabara,majengo,kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao na vitu vingine kama hivyo,sio maendeleo,bali ni nyenzo tu za maendeleo_Ongezeko la idadi ya majengo ya shule itatafsiriwa tu kuwa ni maendeleo iwapo tu majengo hayo yatatumika kuendeleza akili na ueledi wa watu.Ongezeko la uzalishaji wa mazao kama vile ngano,pamba,mkonge,tumbaku,mahindi,kahawa au maharage na mengineyo itatafsiriwa kuwa ni maendeleo iwapo tu itapelekea watu hao kuwa na afya bora.Kuongezeka kwa pamba,kahawa,tumbaku,mahindi na mazao mengine,yataitwa maendeleo iwapo tu yatauzwa,na pesa zitakazopatikana zitatumika katika mambo mengine ambayo yataboresha afya ,yatafanya watu wawe na furaha na yatawezesha watu kuelewa masuala mbalimbali.Maendeleo ambayo sio maendeleo ya watu yaweza kuwa ni maendeleo kwa faida ya Wanahistoria katika miaka 3000 ’’.
Ni wazi kuwa maneno haya ya Mwalimu juu ya maendeleo yanapingana sana na majigambo ya viongozi wetu kwamba kwa miaka 50 ya uhuru tumepiga hatua kubwa kimaendeleo kwani maendeleo haya tunayoyashuhudia ni ya watu wachache ambayo yamepelekea kuwa na Taifa lenye
Matabaka mawili,yaani walionacho na wasionacho,au matajiri na maskini.Matabaka hayo yamejidhihirisha wazi katika nyanja ya elimu,ambapo leo hii kuna shule za maskini yaani zile za kata na wazazi na zile za matajiri na viongozi wa serikali ambazo wanafunzi wanafuatwa na magari ya shule nyumbani na kurudishwa tena jioni.Wakati Shule za msingi za watu maskini wanasoma kwa kiswahili na walimu wakiwa wachache,huku kwa matajiri na viongozi wanafundishwa kwa kiingereza yaani English medium na walimu wakiwa wakutosha kwa sababu wanalipwa vizuri.Karo za shule hizo ni kubwa mno lakini kwa wao kuzilipa ni rahisi tu kwani wanapata fedha nyingi sana kwa njia chafu,mfano ni zile walizoiba kupitia EPA , Meremeta,uuzwaji nyumba kule Italy , Richmond , Dowans , Rada , kuuza wanyama nje kama vile twiga, chui na Tembo na malipo ya posho na nyingine nyingi.
Matabaka mengine yamejionesha katika ubora wa maisha kati ya vijijini na mijini.Serikali imewasusa watu wa vijijini na mpaka imefikia hatua watu wa vijijini wanaamini hawastahili kuendelea kwa kuwa tu wapo vijijini,kitu ambacho sio kweli.Kutokana na maisha magumu ya vijijini hata wafanyakazi hawataki tena kwenda kufanya kazi huko na hivyo matumaini ya watu wa vijijini na pembezoni ya nchi kama vile mkoa wa Ruvuma,maendeleo kwao imebaki kuwa kitendawili kila kukicha na sasa hata hizo ajira zenyewe zimepunguzwa kwa 50% na maana yake ni kwamba watoto wa walewale Watanzania maskini wataendelea kubakia benchi bila ajira kwa kuwa hawana mitaji na mazingira mazuri ya kujiajiri ndio maana siungi mkono hoja.
AMANI
Bila kuwa na uhuru wa kweli ni vigumu kuwa na amani.Na kwa kuwa Maendeleo pia hutegemea sana uhuru wa kweli,hivyo basi huwezi kuwa na amani kama unashindwa kumudu mahitaji muhimu ya kila siku bila kusahau makazi bora. Ni vizuri tujiulize ni Watanzania wangapi leo mijini na vijijini wanauwezo wa kujenga nyumba nzuri za kuishi ambazo zitapelekea kuondokana na magonjwa?
Mwaka 1968,katika hotuba yake ya kuukaribisha mwaka mpya,Mwalimu aliwahi kusema hivi ‘’Sasa hivi amani ni jambo muhimu kila mahali na kwetu sote;kwa furaha yetu,na kwa uchumi wetu na kuendelea kwetu kijamii, amani inahusika’’Mwalimu aliendelea kusema’’Bado amani peke yake haitoshi kuleta ari ya binadamu kama tunamaanisha kutokuwepo tu kwa migogoro yenye machafuko.Kwa kuamini hivyo,amani ingeweza kuwa kama msamaha tu unaotokana na utulivu wa kijamii ambao unapelekea kunyang’anywa kwa haki nyingi za kibinadamu.Amani na haki za binadamu zinamahusiano na zinapaswa kuhusiana’’
Hali kadhalika,Maneno haya ya Mwalimu yanatofautiana sana na mbwembwe za viongozi wetu.Ni dhahiri kuwa watanzania hatuna amani ya kweli isipokuwa tuna utulivu.Utulivu huu unatokana na woga tulionao na ni ukweli usiopingika kwamba Woga ni jela mbaya kuliko gereza la kitai,keko na ukonga.Pia mwoga hufa mara nyingi,lakini jasiri hufa mara moja.Amani hii inayosifiwa na kuhimizwa na viongozi wetu ni amani inayowawezesha wao kutumia vibaya rasilimali zetu kwa maslahi yao binafsi na sio ya Taifa.Ndio maana leo ukibahatika kuwa Rais wa nchi basi watoto nao lazima wawe mabilionea,Lakini hatukuona hayo wakati wa Mwalimu.Ama kweli nakubaliana kabisa na Mh.Godbless Lema kwamba ‘’ Ni heri ya vita inayotafuta haki na usawa, kuliko amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa mwanadamu’’.Tumeshuhudia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na wageni kuthaminiwa zaidi kuliko Watanzania wenyewe.Kwa hili , ‘’Niko tayari kufa huku nimesimama kuliko kuishi huku nimepiga magoti’’Watanzania tunaishi huku tukiwa tumepiga magoti bila kujielewa
KWANINI NAITAJA CCM NA SERIKALI YAKE?
Usishangae kwanini naitaja sana CCM na Serikali yake,kwani wahenga husema ‘’ Mbwa akikonda anayelaumiwa ni mfuga mbwa’’ na viongozi wetu wanapoulizwa kwanini Tanzania maskini hali ya kuwa tuna rasilimali nyingi wanasema hawajui kwanini sisi bado ni maskini. Majibu haya ni ushahidi tosha kwamba hawataweza kuleta maendeleo hapa nchini kwasababu uwezo wao wa kufikiri umefikia kikomo.Rais Kagame aliwahi kunena ‘’Kama angeteuliwa kuwa waziri wa bandari wa Tanzania angeilisha Afrika Mashariki yote yaani Tanzania,Uganda,Kenya,Rwanda na Burundi’’ Maneno haya ni ushahidi tosha kwamba CCM, imeambukizwa virusi vya ufisadi,inaumwa,imezeeka,imechoka na imechakaa.Isaidiwe ife salama isituachie vita.
Wabunge wa CCM wameshindwa kuwatetea wananchi waliowachagua,Mfano,Wabunge wa CCM walitetea kwa nguvu zote mswaada uliokua unatoa mwanya wa kununua mashine chakavu hata katika manunuzi ya kawaida.Kwa kukubali kipingele hicho ina maana wametoa mwanya kwa watendaji wasio waaminifu wakishirikiana na viongozi kufanya ufisadi katika manunuzi ya vifaa mbalimbali na kuwaacha wananchi wakiandamwa na umaskini wakupindukia
Katika hotuba yake mwaka 1968 akiwa Uganda,Mwalimu alisema ‘’Chama Lazima kiwasemee watu,Kazi ya Chama imara cha siasa ni kuwa daraja kati ya watu na Serikali walioichagua na kwa serikali kwa watu wanaotarajia kuwahudumia’’Mwalimu aliendelea kusema ‘’Lakini chama pia inabidi kihakikishe kwamba Serikali inakuwa karibu na hisia,matatizo na matumaini ya watu’’Bado Mwalimu alisistiza kwa kusema ‘’Na inabidi kielimishe watu na kuwasaidia kuona nini maana ya matendo ya Serikali juu ya usalama wao na fursa zao katika siku zijazo’’ ama kwa hakika CCM imeshindwa kuwasemea wananchi badala yake chama kinaangalia maslahi yake zaidi katika kuhakikisha kinabaki madarakani kwa gharama yeyote ile bila kujali athari zinazoweza kujitokeza. Mwalimu aliendelea na hotuba yake hiyo kwa kusema ‘’Lakini Wabunge wanaweza kuwakilisha watu tu kama watasaidiwa na chama imara chenye mamia kwa mamia ya wabunge wake kwa waume wachapakazi,wenye akili na wasio wabinafsi’’.Aliendelea kusema kwamba ‘’Na kama viongozi kama hao wanatumia vibaya nafasi zao,au wanakuwa mbali na watu,kwa kiasi kikubwa ni kwasababu chama kinashindwa kuwasemea watu na kuwa mlinzi wa rasimali za watu’’.
Na kutokana na ukweli huu ndio maana CCM na Serikali yake sio tu imeshindwa kuwatetea watu, lakini pia kimeshindwa kuwachukulia hatua viongozi mbalimbali wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndio maana gamba limekuwa gumu kuvulika kwani wahenga husema ‘’Utazuia vipi ongezeko la wimbi la ukeketaji wakati ngariba ni Diwani wa kata na ndio mwenye kijiji’’
Huku majimboni nako mambo hayaeleweki,Mfano,Jimbo la Songea mjini Mbunge wa jimbo hilo anadiriki kuiba kura katika uchaguzi wa Meya,ili tu apatikane Meya atakayelinda maslahi ya Mbunge huyo na sio ya Wananchi.Naibu Meya naye alikimbia na kura halali kwenyekimkoba chake,na huku Mkurugenzi nae akijifanya yupo bize na simu haoni kinachotendeka.Katika mazingira hayo viongozi hao hawawezi kusimamia maendeleo ya jimbo hilo kwani hakuna msafi miongoni mwao.Mkuu wa Wilaya nae kwa upande mwingine anaendelea na tabia yake ya ubabaishaji katika vocha za pembejeo.Huko bungeni nako wakati Pinda anatetea posho kwa wabunge,Makinda nae anasema posho hazitoshi ziongezwe kwa 155% kwa sababu maisha ni magumu kwa wabunge.Ama kweli ’’Ukistaajabu ya Pinda,utashangaa ya Makinda’’ .Wanasongea nawaambia’’ Ukitaka kuepuka nzi tupa kibudu’’
 
Back
Top Bottom