Mbowe ambana Waziri Mkuu atoe kauli juu ya masuala yanayokwaza demokrasia na utawala bora

Tumaini Makene

JF-Expert Member
Jan 6, 2012
2,642
6,071
HOTUBA YA KIONGOZI WA UPINZANI BUNGENI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHE. FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB) KUHUSU MAPITIO YA KAZI ZA SERIKALI KWA MWAKA 2011/2012 PAMOJA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA OFISI YA WAZIRI MKUU MWAKA WA FEDHA 2012/2013

1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
huku nikitambua na kuamini kuwa "Nyumba asiyoilinda Mwenyezi Mungu, wote wailindao wafanya kazi bure," naomba kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai, ulinzi na nguvu na hivyo kuniwezesha kusimama hapa kwa mara nyingine tena kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu mapitio ya kazi za Serikali katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa fedha 2011/2012 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi hii kwa mwaka 2012/2013, kwa mujibu wa kanuni za Kudumu za Bunge toleo la mwaka 2007, kanuni ya 96(6).


Mheshimiwa Spika, ni wajibu kwangu kutoa shukrani kwa wabunge wenzangu wa upinzani kwa ushirikiano wao na kwa niaba yao wote nawiwa kutoa shukrani kwa Viongozi wenzetu walio nje ya Bunge, Makamanda, wanachama, wepenzi na waumini wote wa mageuzi nchini. Tunawashukuru kwa namna wanavyotutia moyo kwa njia mbalimbali. Tunawaahidi kuwa tutaendelea kuwawakilisha ndani ya Bunge hili kwa unyenyekevu mkubwa kwa nguvu za hoja ili hatimaye nchi yetu ipate neema aliyokusudia Mwenyezi Mungu juu yake.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii vilevile kuwapongeza wale wote waliopewa dhamana ya kuwa Mawaziri kufuatia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri. Ni imani yangu watakuwa wa baraka kwa nchi yetu na kamwe hawatakuwa wa laana. Nawaomba watambue kuwa kambi ya upinzani ina nia njema na kila Mtanzania bila kujali itikadi yake na kwa maana hiyo watayapokea kwa dhamira njema yale yote tutakayoshauri kupitia hotuba hii na nyingine zote tutakazowasilisha rasmi kwa kila wizara.

Mheshimiwa Spika, kwa uzito mkubwa sana, nawashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Hai. Nawaahidi kuendelea kuwatumikia wao na nchi yetu yote kwa uadilifu mkubwa. Mwisho lakini kwa uzito wa kipekee, naishukuru sana familia yangu hususan mke wangu Dr. Lillian na watoto wetu Denis, Nicole na Dudley. Mungu atawalipa kwa kumkosa baba kwa muda mrefu. Mbarikiwe sana.

2.0 OFISI YA WAZIRI MKUU

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu imeanzishwa kwa mujibu wa ibara ya 52 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara, Gazeti la Serikali Na. 494 kama lililochapishwa tarehe 17/12/2010 kuhusu Wizara zilizoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano na Gazeti la Serikali Na. 494A kuhusu majukumu ya kila Wizara.

2.1 MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2011/12
Mheshimiwa Spika,
taarifa za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, zimeendelea kuonyesha upungufu mkubwa juu ya mipango, matumizi na taarifa za utekelezaji mipango hiyo katika ngazi zote za serikali na idara zake, zikiwemo serikali za Mitaa. Ni lazima hali hii itafutiwe mbinu ya kukidhi haja na idhibitiwe ipasavyo. Tatizo kubwa ni kwamba mapendekezo ya CAG yamekuwa hayatekelezwi na serikali au yanatekelezwa kwa kiwango kidogo.


Mheshimiwa Spika, tukiangalia randama ya Ofisi ya Waziri Mkuu, fungu 37, Mwaka wa fedha 2011/2012, tunaona kuwa Bunge liliidhinisha jumla ya Shilingi 109, 404,476,000 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa fungu husika. Lakini hadi Aprili Mwaka 2012, fungu hilo lilipokea jumla ya Tshs. Billion 15,351,640,429.12 ambazo ni sawa na asilimia 14.03 ya bajeti iliyopangwa. Mwaka huu wa fedha, kwa fungu hilo linaomba Tshs.billioni108,271,972,000. Kambi ya Upinzani ina hoji, ni kwa kiasi gani maombi haya yanawiana na utekelezaji wa mipango yetu?

Mheshimiwa Spika, aidha, serikali ilipanga shilingi 134,375,960,000/- kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika fungu ya 27 (Vyama vya siasa) fungu 37 (Ofisi ya Waziri Mkuu) fungu 42 (Mfuko wa Bunge), Fungu 91 (Tume ya Kuratibu Dawa za Kulevya) na Fungu 92 (Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania). Hata hivyo, hadi Aprili 2012 na Tshs. Billion 24,301,571,108 zilikuwa zimetolewa, na zilizotumika ni Tshs. 19,689,920,292.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Randama ya Taarifa ya Waziri wa Nchi Sera, Uratibu na Bunge uk.9 nanukuu "Jedwali Na. 3 linaonyesha mchanganuo wa Matumizi ya Miradi ya Maendeleo hadi Aprili, 2011".

Mheshimiwa Spika, tukiangalia jedwali tajwa hapo juu, tunaona kuwa badala ya kuonyesha miradi ya maendeleo kwa 2011/2012 linaonyesha mgawanyo wa fedha kwa mafungu tajwa. Aidha, taarifa ya utekelezaji wa miradi kwa fungu 37, uk.10-12 wa randama ya Waziri wa Nchi, haionyeshi mchanganuo wa fedha kwa kila mradi, jambo ambalo linatia shaka kwa matumizi au kuwepo wa miradi husika.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo ingekuwa mfano wa kuigwa katika uwazi wa utekelezwaji wa miradi, ili wananchi waone thamani ya fedha kwa miradi husika, lakini kwa mujibu wa randama hiyo imekuwa ni kinyume. Hivyo basi, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuweka wazi gharama za utekelezaji kwa kila mradi kama miradi ilivyowasilishwa kwenye Kamati ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona hapa kuna tatizo kubwa sana, kwani katika bajeti iliyopitishwa na Bunge kwa Mafungu tajwa hapo juu, fedha zilizotolewa hadi April, 2012 ni asilimia 18.08 tu. Je, ni kweli kuwa serikali itaweza kutoa asilimia 81.92 zilizobaki kwa miezi iliyobaki toka April hadi Juni (mwezi unaokaribia kuisha) ili kutekeleza miradi iliyokuwa imepangwa? Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu shughuli za maendeleo zilizoathirika na ucheleweshwaji huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, jambo la kushangaza ni kwamba katika mwaka huu wa fedha, zimeombwa jumla ya Tshs 109,906,972,000/-kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kama mwaka uliopita zilitengwa Tshs Billioni 134,375,960,000/- kwa miezi 9 wakatapa asilimia 18.08, ni kwamba waheshimiwa wabunge wanapoteza muda kupitisha mafungu hapa lakini utekelezaji haufikii hata aslimia 20. Hii inaonyesha kuwa bajeti inayopitishwa siyo halisi, kama mafungu hayo yameweza kuishia asilimia 18 ya maombi yake, hakuna haja ya kumpa fedha kulingana na maombi yake.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe ufafanuzi wa kina na mchanganuo wa matumizi katika miradi yote hasa kwa fungu la 37 ili Mafungu hayo kwa Waziri Mkuu yaweze kithinishwa

2.2 UTAWALA BORA NA DEMOKRASIA

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa sasa nchi yetu imeamua kuendelea na utamaduni wa kutokuheshimu misingi ya utawala bora na demokrasia ya mfumo wa vyama vingi. Jambo hili linakuwa la hatari zaidi kama Ofisi ya Waziri Mkuu ndio inaongoza kwa kutoa maelekezo na miongozo ya kukiuka misingi ya utawala bora na Demokrasia .

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo kimsingi Msajili wa Vyama vya Siasa anawajibika kwayo moja kwa moja, inapoamua kusimamisha chaguzi za kiserikali kwa kuwa eti CCM kinaendesha uchaguzi wake wa ndani ni jambo ambalo halipaswi kufumbiwa macho hata kidogo. Na hili ni sehemu ya uthibitisho wa madai yetu ya muda mrefu kuwa vyombo vya kusimamia chaguzi havipo huru na huwa vinakipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na maelekezo wanayopewa.

Mheshimiwa Spika, naomba ninukuu sehemu ya barua ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Ndugu B.B Kichinda, ya tarehe 23 Mei 2012 Kumb. Na FA.291/300/08/25 kwenda kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na nakala zake kusambazwa kwa wakuu wote wa Wilaya za Mkoa wa Mara iliyokuwa na kichwa kisemacho "YAH:KUSIMAMISHA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA ,VIJIJI NA VITONGOJI KATIKA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA".

"Nyote mnataarifiwa kuwa kutokana na mwingiliano wa uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi katika ngazi mbalimbali na ule wa Serikali za Mitaa, mnatakiwa kusimamisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kupisha uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa nafasi zilizo wazi ufanyike mara baada ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi"

Mheshimiwa Spika, kwa barua hii ni dhahiri kuwa Katibu huyu amepewa maagizo kutoka ngazi ya juu na kwa mujibu wa tangazo la Serikali Na 51 la tarehe 17 Disemba ,2010 mwenye dhamana ya kutoa maelekezo hayo ni Waziri Mkuu kwani ndio msimamizi mkuu wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, barua hii ilifuatiwa na agizo la wakurugenzi watendaji wa Halmashauri mbalimbali za Wilaya za Mkoa wa Mara na kusimamisha chaguzi hizo.

Kambi ya Upinzani, inamtaka Waziri Mkuu:
i. Kutoa kauli ya Serikali juu ya kusimamishwa kwa chaguzi zinazojitokeza za serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ili kupisha uchaguzi wa CCM.
ii. Ni lini chaguzi hizo zitafanyika, kwani nchi nzima zimesimamishwa.
iii. Anachukua hatua gani kutokana na jambo hili ambalo ni kinyume cha katiba, sheria na misingi ya utawala bora.


2.2 SHEREHE ZA KITAIFA

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina matukio mengi ya kihistoria, pamoja na matukio mengine ya kimataifa, ambayo kutokana na unyeti wake, imepelekea kila mwaka matukio hayo kuadhimishwa kitaifa. Maadhimisho hayo yanahusisha kusherehekea kumbukumbu za Tanganyika kupata Uhuru wake, maadhimisho ya siku ya Muungano, maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei mosi), maadhimisho ya sabasaba, maadhimisho ya nanenane, maadhimisho ya sikukuu ya mashujaa, n.k.

Mheshimiwa Spika, maadhimisho hayo yote hufanyika kuanzia ngazi ya Taifa hadi ngazi ya Wilaya kwa kufanya sherehe mbalimbali zinazohusisha viongozi wa kiserikali, na hivyo ni dhahiri matumizi ya kodi za wananchi hutumika. Kambi ya Upinzani inasema kuwa matukio hayo ya kihistoria ni muhimu yaeleweke kwa vizazi vyetu vya sasa na vijavyo.

Mheshimiwa Spika, katika kufikia azma hiyo si lazima tutumie fedha nyingi za walipa kodi wakati Serikali inashindwa kutimiza wajibu wake muhimu zaidi wa kutoa huduma za msingi kwa wananchi wake, kama vile huduma ya maji safi na salama, elimu bora kuanzia ngazi ya msingi hadi elimu ya juu, kupeleka nishati kwenye maeneo ya uzalishaji na kwa Watanzania waishio vijijini n.k.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali badala ya kufanya maadhimisho ya Sherehe hizo zote tuchague ni sherehe zipi zinatoa tija kwa Watanzania na zipi hazileti tija na maadhimisho yake yafanyike kila baada ya miaka miwili au mitatu.

Mheshimiwa Spika, taarifa iliyoandikwa na Ndg. Mkinga Mkinga na kutolewa na "Gazeti la The Citizen" linalochapwa na Kampuni ya Mwananchi Communication ya Jijini Dar es Salaam, zilidai kwamba mwaka jana Serikali ilitumia kiasi cha TSh bilioni 64 kwa ajili maadhimisho ya sherehe za uhuru. Tangu kumalizika kwa sherehe hizo, Serikali haijapinga taarifa hiyo na haijatoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu matumizi hayo.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe tamko kuhusu matumizi hayo pamoja na mchanganuo wake ili kutekeleza dhana nzima ya uwazi na ukweli, ambayo ni msingi muhimu wa Utawala Bora. Ni vyema vilevile taarifa za gharama za sherehe hizi za Kitaifa zikawekwa hadharani, zikiwemo gharama za mbio za mwenge ili umma wa Watanzania waweze kuchambua na kuona kama kweli bado ni tija na kipaumbele kwa Taifa kuendeleza sherehe hizi kwa mfumo tulio nao leo.

2.3 BUNGE KAMA MUHIMILI WA KUISIMAMIA NA KUISHAURI SERIKALI

Mheshimiwa Spika, mamlaka ya Bunge yameainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara za 62 hadi 64. Lakini kwa kufanya kazi ya kuisimamia na kuishauri Serikali Ibara ya 63(2). Hili ni jukumu kubwa sana ambalo linahitaji kuwa na raslimali na umakini katika utekelezaji wake.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inauliza ni kwa vipi Bunge linaweza kuisimamia na kuishauri Serikali wakati Bunge (Wabunge) halina taarifa za kutosheleza kuhusiana na utendaji wa Serikali? Ni mara nyingi Bunge limedai kupatiwa nakala za mikataba ambayo Serikali imeingia na Makampuni na wadau mbalimbali lakini ombi hilo limeshindikana. Aidha, Kifungu cha 10 cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge ya mwaka 1988 na marejeo yake ya mwaka 2002, kinatoa haki kwa mbunge kuomba na kupatiwa taarifa kutoka kwa mtumishi yeyote katika taasisi za Umma.

Mheshimiwa Spika, ni mara chache sana kifungu hiki kinaheshimiwa na watendaji kwani waheshimiwa wabunge mara kadhaa wamekuwa wakiomba kupatiwa taarifa kutoka kwa watendaji Serikalini bila mafanikio. Kambi ya Upinzani inauliza ni kwa vipi tutaisimamia Serikali kama hatuna taarifa sahihi kuhusiana na utendaji wa Serikali? Pengine serikali itamke wazi ni nini kifanywe na wabunge ili upatikanaji wa taarifa zake usiwe wa vikwazo kama ilivyo sasa.

2.4 KATIBA MPYA NA CHANGAMOTO ZAKE

Mheshimiwa Spika, kwa kuangalia uzoefu wa nchi nyingine ambazo zimepitia mchakato wa mabadiliko ya katiba katika miaka ya hivi karibuni, ni vyema kutambua kuwa mchakato huu siyo mwepesi. Ni mchakato unaohitaji kupambanua mapema changamoto zinazoweza kujitokeza katikati ya mchakato na hivyo kuandaa mazingira mbadala ya kukabiliana na changamoto husika.

Mheshimiwa Spika, pamoja na nia njema ya kuwa na katiba mpya ifikapo 2014, ni dhahiri kuwa hakuna uhakika wa asilimia mia moja wa kuipata kwa wakati. Aidha, kupata katiba mpya ni jambo moja, na kuanza kuitumia ni jambo jingine. Kuanza kuitumia katiba mpya kutahusisha mabadiliko ya sheria nyingine kadhaa zikiwemo za uchaguzi na taasisi zinazohusiana na uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, uchaguzi ni jambo tete wakati wote. Ni dhahiri kuwa ushuhuda uliopatikana katika chaguzi ndogo za marudio za ubunge katika majimbo ya Igunga Mkoani Tabora na Arumeru Mashariki Mkoani Arusha pamoja na uchaguzi wa marudio wa madiwani katika kata kadhaa nchini; uchaguzi wa mjumbe wa Baraza la wawakilishi katika Jimbo la Uzini, Zanzibar zimeonyesha ushindani ambao ufumbuzi wake ni kuwa na taasisi makini sambamba na mifumo ya haki katika kuzisimamia. Matumizi ya nguvu za ziada za vyombo vya dola hususan polisi katika kuthibiti chaguzi hizi hautoi viashiria vizuri vya uwepo wa amani katika chaguzi siku za usoni.

Mheshimiwa Spika, malalamiko mengi katika chaguzi hizi yamegusa maeneo yafuatayo:

  • Daftari la kudumu la wapiga kura. Raia kadhaa wenye umri na sifa nyinginezo za kupiga kura wamezuiwa haki yao ya kikatiba ya kupiga kura bila sababu za msingi.
  • Tume ya uchaguzi kuonyesha vitendo mbalimbali vya upendeleo wa wazi kwa chama tawala. Ni dhahiri kuwa Tume ya Uchaguzi haiku huru na ni hatari kuendelea kuitegemea kwa njia yeyote kuratibu chaguzi zozote za mbele.
  • Kushindikana kwa kiasi kikubwa kutekelezwa kwa sheria ya gharama za uchaguzi kunakoendana na mkanganyiko wa sheria yenyewe baina ya Uchaguzi mkuu na chaguzi ndogo.
  • Kushindikana kwa kiasi kikubwa kutekelezwa kwa maadili ya uchaguzi kunakosababishwa pamoja na mambo mengine upendeleo wa taasisi kadhaa zenye dhamana ya kusimamia chaguzi mbalimbali ndani ya nchi.

2.5 MAPENDEKEZO YA MAREKEBISHO YA KATIBA YA MPITO

Mheshimiwa Spika, ili kuweka tahadhari ya kudumisha amani na utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi, hatuna budi kama Taifa kuchukua hatua za dharura kurekebisha usimamizi wa chaguzi zetu kati ya sasa na hapo tutakapokuwa na katiba mpya. Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuwa na marekebisho ya mpito ya Katiba yetu yatakayowezesha tume yetu ya uchaguzi kuwa huru.

2.6 MALIPO YA PENSION KWA WAZEE

Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa maelezo zaidi naomba kunukuu kauli ya Waziri Mkuu aliyoitoa hapa Dodoma akiwahutubia Wazee wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya wazee Duniani tarehe 1 Oktoba 2009. Nanukuu: "Serikali inatambua umuhimu wa wazee katika maendeleo ya Nchi yetu, inatambua Wazee ni rasilimali na hazina kubwa katika kukuza uchumi wa nchi yetu na kuleta mabadiliko ya kiuchumi. Wazee ndio mliotujengea misingi ya Taifa tuliyonayo hivi sasa". Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inakubaliana kabisa na kauli hiyo ya Mhe.Waziri Mkuu, hoja ya msingi ni kuiuliza Serikali ni kwanini Wazee ambao ni rasilimali na hazina kubwa ya Taifa letu iendelee kufa kihoro wakati walikwishawekeza zamani katika nchi hii?

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani wakati tunawasilisha hotuba yetu kwa Wizara ya Kazi mwaka 2011/2012 tulisema yafuatayo, nanukuu: "Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa dhana ya hifadhi ya jamii ni pana sana, Kambi ya upinzani tunaitaka serikali kuzingatia pendekezo letu kuweka mfumo utakaowafanya wazee wote kupata pesheni (Universal pension) kila mwezi kwa kiasi cha shilingi ishirini elfu kwa kuanzia ili kuwapunguzia wazee wetu hasa waishio vijijini gharama kubwa za maisha". Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasisitiza kuwa pensheni hii ni muhimu kwa kuwa itasaidia kuongeza kipato kwa wanaoishi vijijini ambako umasikini wa kipato umejikita na kupunguza umasikini kwa kiwango cha takriban asilimia 57.9 kwa wazee walio na umri zaidi ya miaka 65.

Kwa mujibu wa Kauli ya Waziri Mkuu kuwa "Idadi hii ya wazee inajumuisha waliokuwa wanafanya kazi za kuajiriwa, au waliojiajiri wenyewe na walioko vijijini wakijishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali. Hili ni kundi kubwa ambalo likitumiwa vizuri na hasa kwenye maeneo maalum linaweza kuinua kasi ya maendeleo ya Taifa hili".

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya utafiti ulifanywa na Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya wazee liitwalo (HelpAge International) na kutolewa mwezi May 2010. Idadi ya wazee ni 1,327,883. Tunaamini hili linawezekana kutekelezwa katika mwaka huu wa bajeti kama serikali ina nia ya kweli ya kulitekeleza.

Kwa mahesabu rahisi ni kwamba kwa jumla ya wazee 1,327,883, kama kila mmoja akipata sh. 20,000/- (kiasi kinachopendekezwa) kwa mwezi malipo yatakuwa shilingi 1,327,883 x 20,000 = 26,557,660,000/- (bilioni 26.557) na kwa mwaka malipo yatakuwa shilingi 26,557,660,000/- x 12 = 318,691,920,000/- (bilioni 318.691).

Kama tukiongeza 5% ya fedha hizi kama gharama za utawala kuhakikisha wazee wote wanapata fedha hizo kwa mwaka taifa litatumia shilingi 334,626,516,000/- (bilioni 334.626) kwa kuanzia.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uzito wa Kauli aliyoitoa Waziri Mkuu wakati akiwahutubia Wazee tarene 1,Oktoba 2009 kuwa, "Wazee ni rasilimali na hazina kubwa katika kukuza uchumi wa nchi yetu na kuleta mabadiliko ya kiuchumi" ni dhahiri kiasi hicho kwa mwaka Serikali inauwezo wa kukipata. Kwa kuwa tunatarajia kufanya sensa mwaka huu pamoja na kuanzisha utambuzi wa wananchi wote kwa kutoa vitambulisho vya uraia, Kambi ya Upinzani inaona kuwa takwimu halisi na za kuaminika za wazee wetu zitapatikana.

2.7 UTAWALA BORA NA HAKI ZA BINADAMU

2.7.1 Mauaji ya raia

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani katika hotuba yetu ya mwaka uliopita katika ofisi hii tulitoa takwimu na majina ya wananchi waliouwawa kutokana na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa na vyombo vya dola likiwemo jeshi la polisi kama ifuatavyo; naomba kunukuu:
"Mheshimiwa Spika, mauaji ya raia mikononi mwa polisi yameendelea kuongezeka kwa kasi ya kutisha sana kutoka matukio ya kuuawa watu 5 mwaka 2008, watu 15 mwaka 2009 hadi watu 52 mwaka 2010. Kwa kasi hiyo hiyo, mwaka huu pekee, Kwa miezi ya Januari hadi Mei 2011, tayari watu 9 wameripotiwa kuuawa Na Polisi katika eneo moja tu la Nyamongo, Tarime na kushuhudia matukio ya unyama wa kutisha yakifanyanywa na chombo cha dola kwa kutupa miili ya marehemu hao barabarani na kuitelekeza.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunataka hali hii ichukuliwe hatua na kuangaliwa kwa umakini mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa mwaka huu pia kumefanyika mauaji ya raia 3 huko Arusha ambao walipigwa risasi na Polisi kwa kile kilichodaiwa kuwa walitaka kuleta vurugu na uvunjaji amani.
Wananchi wengine 9 wameshauawa Tarime, wawili Kisarawe, mmoja Sumbawanga na mwingine Tabora. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matukio haya yameainishwa kama ifuatavyo;
(i) Mnamo Januari 5, 2011 watu watatu ambao ni Denis Michael, Ismail Omary na Paul Njuguna Kaiyele waliuwawa na wengine 21 kuumizwa vibaya wakati wa maandamano mjini Arusha.
(ii) Mnamo tarehe 16 Mei, 2011 polisi waliwaua watu 5 katika eneo la Mgodi wa North Mara Wilayani Tarime unaomilikiwa na Kampuni ya African Barrick Gold Mine na kufanya idadi ya watu waliouliwa katika eneo hilo toka mwaka 2009 hadi Juni 2011 kuwa 34. Kama hiyo haitoshi, mnamo tarehe 9 Juni, 2011 kijana ajulikanaye kama Nyaitore mkazi wa kijiji cha Nyangoto wilayani Tarime alipigwa risasi ya bega na polisi wa mgodi na kulazwa hospitali ya Sungusungu.


(iii) Mwezi Mei, 2011 katika kijiji cha Namanga wilayani Nachingwea, askari wa Wanyama pori walimpiga risasi kwenye miguu yote Juma James (27) ambaye anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea.

(iv) Mkoani Tabora wilayani Urambo mnamo tarehe 28 Mei, 2011 askari polisi walimuua Juma Saidi na kujeruhi wengine kadhaa katika kijiji cha Usinge. Tukio Hilo lilitanguliwa Na kipigo Kwa Mwenyekiti WA kijiji cha Shela Na wenzake mnamo tarehe 26 Mei, 2011 vitendo vilivyofanywa na askari walioenda kukamata mifugo.
(v) Mnamo Aprili 2, 2011, mkazi wa kijiji cha Mwanza Buriga kata ya Kukirango wilaya ya Musoma vijijini Mwabia Zome(40) aliuawa kwa kupigwa risasi chini ya titi la kushoto na askari magereza wa gereza la Kiabakari.
(vi) Watu wengine wa umri kati ya miaka 25- 30 walipigwa risasi tarehe 7 Machi, 2011 ambapo Sese Kabanzi, alifia njiani wakati akipelekwa hospitali na July Hamisi alikufa hapo hapo baada ya kupigwa risasi
maeneo ya kifuani.
(vii) Mnamo tarehe 5 Februari, 2011 Askari wa Wanyama Pori katika Hifadhi ya Selou wameripotiwa kuuwa watu wawili na kujeruhi mmoja Wilayani Kisarawe Mkoani Pwani. Waliokufa ni Hamisi Boy na Mohamed Suta na anayeuguza majeraha ni Mohamed Kigwiso.

Mheshimiwa Spika, kuna ushahidi kuwa askari hawa wanashutumiwa kwa kuendeleza matukio ya ukatili dhidi ya wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo kwa makusudi huku Jeshi la Polisi likishindwa kuwasaidia raia kulinda usalama wao. Wilayani Kisarawe askari hawa wanadaiwa kuwauwa Na kuwatupa mtoni Na kupelekea raia wafuatao waliwe Na mamba, ambao Ni Ndugu Majengo, Mohamed Kibavu, Adamu Feruzi, Semeni Abdala Kube, Hemed Kassim, Mzee Hussein, Ramadhani Mgeto na Bwana Mkala.
Mheshimiwa Spika, cha kusikitisha zaidi kuna matukio mengi ambapo ndugu za waathirika hao wa ukatili wamekuwa wakinyanyaswa pale wanapofuatilia haki au uwajibikaji katika vyombo vya usalama. Aidha, matukio ya uchomaji moto miili ya marehemu, kulishwa mamba na kutupwa na kutelekezwa barabarani maiti ni matukio yanayotuingiza katika historia mpya ya kutojali haki za binadamu.
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha miezi mitano ya mwaka 2011 tayari watanzania 21 wameuwawa kwa kupigwa risasi maeneo mbalimbali ya nchi yetu na wengine wengi kuumizwa kwa kupigwa risasi wakiwemo wanafunzi wa shule za Sekondari na Vyuo Vikuu mbalimbali hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani, inaitaka serikali ifanye mambo yafuatayo ili kukomesha mauaji haya;
(i) Kulipa Fidia stahili kwa mujibu wa sheria husika za nchi kwa ndugu na/au jamaa wa wale wote waliouawa kutokana na vitendo vya Jeshi la Polisi la Tanzania na kwa wale wote walioumizwa kwa namna yoyote ile na/au kuharibiwa mali zao kutokana na vitendo hivyo;
(ii) Kuwachukulia hatua askari Polisi, askari Magereza na wale wa Wanyamapori ambao wamehusika katika mauaji haya kwani hali hii ikiachwa iendelee kama ilivyo sasa ni hatari kwa usalama wa watanzania na inalifanya Taifa letu kuingia kwenye rekodi mbaya ya kukiuka haki za binadamu.
(iii) Iundwe Tume huru ya uchunguzi ya kimahakama (Judicial Commission of Inquiry) itakayoundwa na majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania iundwe ili kufanya uchunguzi huru. Tunapenda kusisitiza kuwa tunataka iundwe tume ya uchunguzi ya kimahakama kwani hufanya kazi zake kwa uwazi na huruhusu wananchi kuhudhuria na/au kushiriki moja kwa moja katika kazi za tume kama mashahidi na/au kwa kuhoji mashahidi wengine wanaotoa taarifa kwenye tume hiyo".


Chanzo: Taarifa ya Mwenendo wa Haki za Binadamu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ya mwaka 2010." Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, Naomba kunukuu kauli ya Waziri Mkuu aliyoitoa wakati akifanya majumuisho ya hoja yake katika Bunge la Bajeti Julai Mosi mwaka uliopita kama inavyoonekana katika taarifa rasmi za Bunge hili (Hansard) kama ifuatavyo:
"Mheshimiwa Spika, katika madai yaliyowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge, hususan wa kutoka Kambi ya Upinzani kuhusu mauaji yanayodaiwa kufanywa na baadhi ya Vyombo vya Dola, ni vyema ikaeleweka kuwa, Serikali haina nia ya kupuuza shutuma hizi za mauaji ya raia wake. Katika kulishughulikia suala hili, suala la mauaji ya raia yanayodaiwa kufanywa na baadhi ya Vyombo vya Dola, Serikali imefikia uamuzi sasa wa kuvichunguza vifo hivyo kwa kupitia Sheria husika ya Inquest kwa kadri itakavyowezekana. Inawezekana kwa muda mrefu utaratibu huo hauzingatiwi lakini kwa sasa, ni lazima tuufuate na ni lazima sasa tuutekeleze ili kutokana na maamuzi ya uchunguzi huo watu waweze kupelekwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi pale itakapobainika kwamba vifo hivyo au mauaji hayo hayakuwa na sababu za msingi."


Mheshimiwa Spika, ni muhimu tukatambua kuwa kila kifo cha mtu ni tofauti na cha mwingine, na hutokea katika mazingira tofauti. Hivyo, kwa kuzingatia kilio cha wananchi ambao Serikali ina wajibu wa kuwalinda, vifo vyote ambavyo vimetokea kwa sababu ya matumizi ya nguvu, kikiwamo kifo cha raia kilichotokea akiwa chini ya uangalizi wa Vyombo vya Dola, ni vema serikali ikazingatia mazingira husika.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kauli hii nzito ya Waziri Mkuu ambaye ndiye kiongozi wa shughuli zote za serikali ndani ya Bunge, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa agizo hili juu ya hatua stahiki zilizochukuliwa dhidi ya mauaji ya raia kama tulivyoonyesha katika hotuba yetu mwaka uliopita.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2011 hali ya kuheshimu na kuzingatia haki za binadamu haikuwa tofauti na mwaka 2010 kwa sababu bado taarifa zinaonyesha kuwa yapo mauaji yenye kutia shaka ambayo yaliripotiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu 2011 uk. 17 na 18 kipengele cha 2.1.2, kutoka mwezi Januari hadi Desemba takribani watu 25 wamefariki wakiwa mikononi mwa polisi na maafisa wengine wa ulinzi. Hali kadhalika Matukio yote haya yamewaacha zaidi ya watu 50 kubaki na majeraha.

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa zilizopo ni kuwa mauaji yameripotiwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo mwendelezo wa mauaji katika mgodi wa North Mara, unyanyasaji wa polisi wa tarehe 28/05/2011 na kuwaweka kizuizini viongozi wa CUF akiwemo Mh. Magdalena Sakaya (Mb), mauaji ya mtu mmoja eneo la Ubaruku katika Wilaya ya Mbarali na manyanyaso ya polisi kwa wachimbaji wadogowadogo katika Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi (Taarifa ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu 2011 uk. 19, 20 kipengele cha 2.1.2.2).

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunatambua kuwa taarifa hizi za mauaji zinawagusa Askari Polisi pia kwa kuwa kwa mwaka uliopita katika maeneo ya Tarime, Tabora, Shinyanga, Arusha na Rukwa polisi watano waliuwawa na wananchi (Taarifa ya Kituo cha Haki za Binadamu mwaka 2011uk. 18 kipengele cha 2.1.2).

Mheshimiwa Spika, taarifa hizi kwa ujumla wake zinaligusa Jeshi letu la Polisi kwa kiasa kikubwa. Kambi ya Upinzani tunaamini kuwa kuacha kuchukua hatua dhidi ya polisi wachache wanaolichafua jeshi la polisi kwa ujumla inasababisha picha mbaya ya taifa letu kitaifa na kimataifa.

2.7.2 Mauaji na unyanyasaji wa Kisiasa

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumekuwa na manyanyaso na hata mauaji ambayo kwa namna moja ama nyingine yamekuwa yakihusishwa na siasa dhidi ya wananchi wanaojiunga na vyama vya upinzani. Hili linadhihirika hasa katika chaguzi ndogo za madiwani na ubunge au hata za vijiji na vitongoji hapa nchini. Hivi karibuni wabunge wa CHADEMA (Mhe. Highness Kiwia- Ilemelela na Mhe. Salvatory Machemli- Ukerewe) walikatwa mapanga wakati wa uchaguzi mdogo wa Udiwani wa Kata ya Kirumba Jimbo la Ilemela Mkoani Mwanza na wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi, huku polisi wakishindwa kuzuia hali hiyo pamoja na kuwa walifika katika eneo la tukio tena wakiwa na silaha.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa kesi ya kuwajeruhi waheshimiwa wabunge ipo Mahakamani, Kambi ya Upinzani imeona ni vema kurejea tukio hilo kwa kuwa linahusiana moja kwa moja na hali ya siasa nchini. Manyanyaso hayo yanazidi kushamiri siku hadi siku ambapo mpaka sasa katika Wilaya ya Kilosa wanachama na baadhi ya viongozi wa CHADEMA wapo jela na kuwekewa masharti magumu ya dhamana kwa sababu za kisiasa. Katika Wilaya Rungwe waliokuwa wagombea udiwani katika baadhi ya Kata wamebambikiwa kesi mbalimbali zinazohusishwa na siasa na pia katika kijiji cha Bermi Wilaya Babati, baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Meatu ambapo wafuasi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakibambikiwa kesi za uongo mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, katika chaguzi ndogo za Igunga na Arumeru Mashariki vifo vilivyotokea kwa sababu za kisiasa viliripotiwa mathalani kifo cha marehemu Mbwana Masoud na taarifa kupelekwa polisi lakini hadi leo hakuna hatua zilizochukuliwa. Mara tu baada ya uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki yalitokea mauaji mengine ya kiongozi wa CHADEMA Msafiri Mbwambo na vifo vingine vinne ambapo mauaji hayo yanahusishwa na siasa.

Mheshimiwa Spika, manyanyaso haya hayawezi kuvumiliwa tena ni lazima kama taifa tujue kuwa nchi hii ni ya vyama vingi vya siasa na hivyo kila raia ana haki ya kujiunga na chama chochote cha siasa bila shinikizo. Hii ni kwa sababu bado mikutano ya kisiasa na hata mikutano ya waheshimiwa wabunge wa upinzani inavamiwa mara kwa mara mathalani uvamizi aliofanyiwa Mbunge wa Iringa Mjini Mhe. Mchungaji Peter Msigwa.

2.7.3 Hali ya Magereza na Haki za Wafungwa

Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala ya mwezi Septemba 2011 kama ilivyonukuliwa na taarifa ya Haki za Binadamu ya Marekani kuhusu Tanzania ya (United States, Department of State, Human Rights Report- Tanzania May 2012 pg 4-5) kuwa kuna matatizo makubwa sana katika Magereza yetu nchini ambapo matatizo kama msongamano wa kutisha, magonjwa mbalimbali, mahabusu wengi kukaa muda mrefu gerezani bila kesi zao kusikilizwa, na chakula kibovu.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya mahabusu wa gereza la Keko Jijini Dar es Salaam wamewasilisha malalamiko yao kwa Jaji Mkuu kwa barua yao ya tarehe 11/07/2011ambapo wameonyesha kuwa tatizo kubwa lao kubwa ni;
i. Msongamano uliokithiri unaosababishwa na kusuasua kwa uendeshaji wa kesi kutoka Mahakama za Mwanzo, Wilaya, Mkoa na Mahakama Kuu.
ii. Kubambikiwa kesi na Jeshi la Polisi hasa kitengo cha upelelezi.
iii. Rushwa iliyokithiri kwa baadhi ya maofisa na makarani wa Mahakama.


Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona kuwa kwa hali hii ya gereza moja tu katika Jiji la Dar es Salaam ni wazi kuwa Magereza mengi nchini yapo katika hali mbaya sana. Mathalani Gereza la Karanga lililopo mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro linakabiliwa na msongamano mkubwa kutokana na kuwahifadhi wafungwa kutoka Wilaya za Hai, Rombo, Moshi Mjini, Moshi Vijijini na Siha.

Mheshimiwa Spika, gereza la Karanga pia linakabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri ambapo lipo gari moja (Karandinga) linalotumika kuwapeleka na kuwarudisha mahabusu katika Wilaya zote. Kwa maana hii, karandinga huhudumia Wilaya moja kwa siku na kusababisha mahabusu wote wa wilaya nzima kusubiri siku yao mara moja tu kwa wiki.

Mheshimiwa Spika, hali hii ya magereza nchini imesababisha wafungwa wengi kukaa Gerezani kwa muda mrefu kwa kisingizio cha kusubiri kesi zao kusikilizwa au kutokamilika kwa upelelezi.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza yafanyike marekebisho ya kisheria ili uwepo ukomo wa ukaaji katika magereza wakati mtuhumiwa akisubiri hicho kinachoitwa upelelezi kukamilika. Hii itapunguza tatizo la msongamano katika magereza mengi nchini na kuhakikisha kila mtuhumiwa/mfungwa anatendewa haki kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Mheshimiwa Spika, matatizo haya pia yanachangiwa na kuwepo kwa maslahi madogo wanayoyapata Askari Polisi na Askari Magereza hata baada ya kufanya kazi katika mazingira magumu na makazi duni.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali kuboresha maslahi ya Jeshi la Polisi na Magereza kwa sababu kwa kushindwa kufanya hivyo kunawaathiri wananchi wengine ambao kwa namna ama nyingine ndio waathirika wakubwa wa matatizo hayo. Kambi ya upinzani tunaamini kuwa hata kushindwa kuboresha mazingira ya kazi kwa Askari Polisi na Askari Magereza ni kinyume na haki za binadamu kwa upande mwingine.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuleta taarifa rasmi ya namna ya kuboresha hali ya magereza nchini ili kukidhi dhana ya chuo cha mafunzo na sio chuo cha unyanyasaji na ubambikaji wa kesi kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, matatizo ya magereza nchini yamesababisha watu wengi kufariki magerezani, kupata ulemavu wa kudumu na wengi kukaa magerezani muda mrefu bila kupata haki.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunasisitiza serikali kuchukua hatua za haraka kunusuru idara ya magereza na kutoa taarifa katika Bunge hili na kama hatua za haraka hazitachukuliwa tutalazimika kuleta hoja binafsi ili kuliomba Bunge kuazimia kuunda Tume Maalumu kushughulikia mateso na ukiukwaji mkubwa wa haki za mahabusu na wafungwa kwa upande mmoja na Askari Magereza kwa upande wa pili.

3.0 GHARAMA ZA UENDESHAJI SERIKALI

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa hapa Bungeni tarehe 14 Juni 2012, katika bajeti ya Sh. trilioni 15.1, shilingi trilioni 10.6 ni gharama za uendeshaji na salio la trilioni 4.5 ndio linaloenda kwenye maendeleo. Kwa uhalisia huu ni wazi kwamba maendeleo yatakuwa kwa kasi ndogo sana.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani haipingi matumizi ya kawaida ya msingi katika Serikali ila inapinga matumizi ambayo kimsingi sio ya lazima. Kwa mfano posho za vikao ni matumizi ambayo si ya lazima kwa sababu mtumishi anayelipwa mshahara, kuhudhuria vikao ni sehemu ya kazi yake. Jedwali hapa chini linaonyesha posho za vikao katika Idara za Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo fedha hizo zingeweza kutumika katika shughuli za maendeleo kama posho hiyo ingefutwa:


KASMAIDARAPOSHO YA VIKAO
210314Utawala95,000,000
Fedha na Uhasibu20,250,000
Sera na Mipango31,500,000
Ukaguzi wa Ndani17,400,000
Habari, Elimu na Mawasiliano3,000,000
Ugavi20,000,000
Sheria1,500,000
Menejimenti ya Mifumo ya Habari800,000
Uratibu wa Maafa39,000,000
Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa47,000,000
Bunge na Siasa15,000,000
Maendeleo ya Sekta Binafsi24,000,000
Uratibu wa Shughuli za Serikali100,500,000
Mpiga Chapa wa Serikali55,100,000
470,050,000
Chanzo: Randama Ofisi ya Waziri Mkuu, Fungu 37

Mheshimiwa Spika, jumla ya shilingi 470,050,000 zitatumika kama posho ya vikao katika Ofisi ya Waziri Mkuu fungu 37 peke yake. Hapa hatujaangalia fungu 56 ambalo pia liko chini ya Ofisi yake, na Wizara zingine. Hii ina maana kwamba kuna fedha nyingi sana zinazotumika kama posho ya vikao kwa watumishi ambao tayari wana mishahara. Kuna matumizi mengine ambayo Kambi ya Upinzani inaona pia kuwa si ya lazima kama posho ya mavazi kwa safari za nje, sare za kazi n.k.

Mheshimiwa Spika, sambamba na matumizi makubwa ya Serikali katika posho mbalimbali, na mbali na kutokuwepo kwa sera madhubuti inayosimamia ununuzi na aina ya magari kwa kada mbalimbali katika utumishi wa umma, Serikali ina tatizo jingine kubwa la matumizi makubwa yasiyoratibiwa katika matengenezo na ununuzi wa mafuta ya magari. Kwa mujibu wa Ripoti ya Kiufanisi na Kiuchunguzi kama ilivyotolewa na CAG ya tarehe 31Machi, 2012 ni kwamba Wizara ya Ujenzi ndio yenye jukumu la kununua, kusajili na kufanya matengenezo ya magari ya Serikali, ikisaidiana na Wakala wake TEMESA (Tanzania, Electrical, Mechanical and Electronics Services Agency).

Mheshimiwa Spika, taarifa ya CAG inaonesha kwamba Wizara ya Ujenzi haijaweka mfumo wa kusimamia matengenezo ya magari. Pia hakuna sera yoyote ya ununuzi na matengenezo ya magari na hivyo hakuna mwongozo toshelezi juu ya usimamizi wa ununuzi na matengenezo ya magari. Wizara haijatoa mwongozo kwa TEMESA juu ya hatua na michakato ya kufuata na wala Wizara haisimamii utendaji wa TEMESA ipasavyo.Wizara pia haina kumbukumbu za kila wakati kama chombo cha usimamzi wa matengenezo ya magari. Mfumo wa matengenezo ya magari ya Serikali hausimamiwi ipasavyo na TEMESA kwa kuwa magari ya Serikali hayakaguliwi kabla na baada ya matengenezo.

Mheshimiwa Spika, mapungufu haya ya Wizara na TEMESA katika kusimamia matengenezo ya magari ya Serikali kunapelekea Serikali kupoteza fedha nyingi sana kwani licha ya kuwa hakuna usimamizi wa kutosha lakini pia hakuna taarifa au kumbukumbu za matengenezo ya magari na gharama zake.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitishwa na mtumizi makubwa ya fedha za walipa kodi kwa matengenezo ya magari ya Serikali ambayo hayana usimamizi madhubuti. Gharama kubwa sana inatumika kwa mafuta na matengenezo ya magari kama jedwali linavyoonyesha hapa chini:




Mafuta na Matengenezo
IDARA KASMA 220300KASMA 230400
MAFUTAMATENGENEZO
Utawala126,500,00091,000,000
Kitengo cha Fedha na Uhasibu13,250,0004,150,000
Sera na Mipango30,000,00020,000,000
Ukaguzi wa Ndani10,920,00012,000,000
Habari, Elimu na Mawasiliano15,000,00015,000,000
Ugavi9,627,50010,000,000
Kitengo cha Sheria5,625,000
Menejimenti ya Mifumo ya Habari550,0001,000,000
Uratibu wa Maafa45,000,00019,400,000
Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa25,000,00011,000,000
Bunge na Siasa30,000,00036,000,000
Maendeleo ya Sekta Binafsi51,000,00020,000,000
Uratibu wa Shughuli za Serikali49,500,00039,000,000
Mpiga Chapa wa Serikali45,000,00025,080,000
JUMLA456,972,500303,630,000
JUMLA KUU760,602,500
Chanzo: Randama, Ofisi ya Waziri Mkuu, Fungu 37

Mheshimiwa Spika, mimi mwenyewe ni mhanga wa tatizo hili. Kwa miezi sita niliacha kutumia gari la serikali aina ya Toyota Landcruiser V8 ambalo nilipewa kwa matumizi ya kazi kwa nafasi yangu kama Kiongozi wa Upinzani Bungeni nikitaka nipewe gari la gharama nafuu zaidi. Stahili hii niliipata kupitia waraka wenye masharti ya kazi ya Kiongozi wa Upinzani, Bungeni uliotolewa 25 0ctoba 2010, kabla hata ya uchaguzi mkuu wa 2010. Mazingira kama haya yalimfika pia Waziri Mkuu, Mheshimiwa Pinda siku za nyuma ilipodaiwa kukataa kutumia gari aina ya Landcruiser VX na akakusudia kutumia gari ya gharama nafuu zaidi.


Mheshimiwa Spika, suala la magari ni suala la kisera zaidi kuliko la utashi wa mtu binafsi. Pamoja na kususa kwa muda gari hili, Serikali haikujali kubadilisha sera yake ya matumizi ya magari ya gharama kubwa pamoja na kutoa matamko mara kwa mara kuashiria azma hiyo. Wakati mimi kwa nafasi yangu sikuwa na uwezo wa kubadilisha sera, upande wa Mheshimiwa Waziri Mkuu ni dhahiri mamlaka ya kubadilisha sera anayo na amekuwa akishuhudia Serikali anayoiongoza ikiendelea kununua na kutumia magari haya ya gharama kubwa.Leo tumemsikia Waziri Mkuu akitoa ahadi nyingine ambayo tunasubiri utekelezaji wake.

4.0 MSHIKAMANO WA TAIFA

4.1 Vyama vya Siasa
Mheshimiwa Spika,
vyama vya siasa nchini vinasimamiwa na Sheria namba 5 ya mwaka 1992 pamoja na marekebisho yake. Sheria hii, kifungu cha 9 (2) inakataza uwepo wa vyama vya siasa vilivyopo kwa misingi ya ukabila, udini, au ukanda. Msajili wa vyama vya siasa amepewa mamlaka na sheria kusimamia msingi huu muhimu wa mshikamano wetu kama Taifa.


Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana, kumekuwepo propaganda nyingi na za kimkakati na kwa bahati mbaya zaidi zikiongozwa na baadhi ya viongozi wa Chama Tawala na vyama washirika wake kueneza chuki miongoni mwa Watanzania kuwa vyama makini vya upinzani ni vya kikabila, kidini na hata vya kimaeneo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa propaganda hii inakusudia kujenga uhalali wa chama tawala na washirika wake dhidi ya upinzani makini, ni hakika kuwa inapanda mbegu mbaya ya chuki na mpasuko miongoni mwa Watanzania kwani maneno huumba.

Mheshimiwa Spika, matukio mbalimbali ya siasa za aina hii barani Afrika yanatukumbusha mauaji ya halaiki Rwanda 1994 baina ya Wahutu na Watusti, Sudan haswa eneo la Darfur, Nigeria mapambano baina ya Waislamu na Wakristo, Somalia na hata Kenya machafuko ya mwaka 2008 baada ya uchaguzi yalisababishwa na kuchochewa sana na siasa za kibaguzi na kikabila baina ya watokao mlima Kenya na watokao eneo la Bonde la Ufa.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na kauli mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya wanasiasa zikiashiria kuwagawa watanzania katika misingi ya udini, ukabila na ukanda. Hata katika mijadala yetu ndani ya Bunge hili tukufu dalili za baadhi ya masuala haya yameanza kujitokeza, kwa waheshimiwa wabunge katika kujadili masuala mbalimbali kujikita kwenye siasa za ukanda na hata mara nyingine ukabila.

Mheshimiwa Spika, hali hii ni ya hatari sana na italigawa taifa letu kama sisi viongozi hatutachukua hatua mapema na kama tukiendeleza kuukoleza wimbo huu wa udini , ukabila na ukanda hakika Tanzania yetu haitakuwa moja tena .

Kambi ya Upinzani inataahadharisha vyama vyote vya siasa na viongozi wote ambao katika kuficha udhaifu wa vyama vyao na utendaji wao wamekuwa wakijikita kwenye propaganda hizi waache mara moja kwani Watanzania ni wamoja na tusifiche madhaifu yetu kwa kuwagawa Watanzania katika misingi ya kidini, kikanda na kikabila kwani madhara yake ni makubwa sana na hakuna hata mmoja wetu ambaye atakuwa salama.

Aidha, tunamtaka msajili wa vyama vya siasa nchini kuchukua hatua mara moja dhidi ya vyama na viongozi wa vyama ambao wamekuwa na tabia hii ya uchochezi kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa. Kadhalika, kama kweli kuna chama chochote kinachoonekana kuwepo kwa misingi hii ya kibaguzi kifutwe haraka ili kuliepusha Taifa letu na uchafu huu.

4.2. Taasisi za Dini
Mheshimiwa Spika,
hatari ya kuligawa Taifa sasa haiko katika siasa pekee, bali hata ndani ya dini zetu. Yanayowasukuma baadhi ya viongozi wetu wa dini kuendeleza na kukoleza vita hii ya ki-imani ni pamoja na udhaifu wa serikali kukemea na kuchukua hatua stahiki kadri matukio yanavyojitokeza. Kuna ushahidi tosha vile vile kuwa baadhi ya viongozi wetu wa dini wametumiwa na kufadhiliwa na watu mashuhuri wakiwepo wafanyabiashara wakubwa kwa niaba ya viongozi wa Kiserikali na Vyama vya siasa kueneza propaganda hizi kwa malengo ya kisiasa.


Vipo vyombo vya habari vinavyomilikiwa na taasisi za dini ambavyo wakati mwingine vimekuwa vikieneza uchochezi wa wazi dhidi ya dini nyingine bila mamlaka za Kiserikali kuchukua hatua stahiki. Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka serikali itoe tamko kukemea hali hii na iahidi ndani ya Bunge kutokuvumilia dini, kiongozi au muumuni yeyote wa dini yeyote atakayeshindwa kuheshimu haki ya mwenye imani tofauti.

5.0 UNYANYAPAA WA FIKRA VYUO VIKUU.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasikitika sana kuwa hadi sasa baadhi wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) waliokuwa wanapinga kumaliza Masomo yao bila kufanya elimu kwa njia ya vitendo (Field Practical) wako majumbani baada ya kusimamishwa masomo na uongozi wa Chuo.

Mheshimiwa Spika, kumbukumbu zinatuonyesha kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi walikutana na viongozi wa Wanafunzi na wakakubalina na madai ya wanafunzi kuhusiana na wanachuo kupatiwa mafunzo kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa kumekuwepo na juhudi za Serikali kwa kutumia baadhi ya viongozi wa vyuo vikuu hususan vya umma, kuwanyima haki za ki-fikra wanafunzi wanaohisiwa kuwa wafuasi au wapenzi wa vyama vya upinzani. Hoja ya kupiga marufuku siasa vyuoni inaonekana kuwahusu tu wale wasio wa Chama cha Mapinduzi.

Mbali na kujenga tabaka la kibaguzi miongoni mwa vijana wetu, hakika vitisho, manyanyaso na hofu wanayojengewa vijana hawa inawadumaza kifikra vijana wetu katika kuhoji, kudadisi na hata kuthubutu. Tunaharibu viongozi wa kesho na hakika dhambi hii italitafuna Taifa letu hususan watekelezaji wa mkakati huu kwa miaka mingi ijayo.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa kauli ya ni kwa nini ubaguzi huu unaendekezwa katika vyuo vyetu vikuu na kwa kupitia uongozi wa chuo cha UDOM kuwarudisha chuoni wanafunzi wote wapatao 260 ili wamalizie masomo yao.

5.1. BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 19 (1) cha sheria No. 9 iliyoanzisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, ni wajibu wa kila mtu aliyenufaika na mikopo ya elimu ya juu kurejesha mkopo serikalini kupitia Bodi ya mikopo. Pamoja na changamoto ya urejeshwaji wa mikopo kwa walionufaika, bodi imeshindwa kuwa na mfumo wezeshi wa kuirejesha mikopo kwa wakati. Zoezi la kutafuta kampuni za madalali wa minada ili kukamata mali za wahusika, ni kuonyesha kushindwa kuwa na njia mbadala ya kurejesha mikopo na kuiongezea bodi gharama zisizo za msingi pia kutowatendea haki Watanzania wasio na ajira rasmi.

Mheshimiwa Spika, Serikali lazima itambue walionufaika na mikopo wengi ni vijana wasio na mali,na tatizo la kutorejesha mikopo ni kukosekana kwa ajira kwa wahitimu wa elimu ya juu. Kambi ya upinzani inaishauri serikali kutumia mfumo rafiki wa urejeshaji mikopo kwa kutumia technolojia ya benki na mitandao ya simu kama M-PESA,TIGO PESA, Airtel Money n.k, kuwarahisishia wadaiwa walioko pembezoni mwa Dar es Salaam kwa kuainisha viwango vya ulipaji kwa wadaiwa pamoja na serikali kulitafutia ufumbuzi tatizo la ajira ili mikopo irejeshwe kwa kasi zaidi.

6.0 SERIKALI KUHAMIA DODOMA
Mheshimiwa Spika,
kauli ya Serikali kuhamishia shughuli za kiserikali Dodoma imekuwa na miaka mingi sana, na kauli hiyo ndiyo ilipelekea kuundwa kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa tangazo la Serikali Na. 230 la tarehe 12 oktoba, 1973. Hadi mwaka huu ni miaka 39, Ni kweli kuna mipango ambayo inaweza kutumia muda wote huo kabla ya kutekelezwa na kuendelea kuitwa mpango! Wakati huohuo serikali hii inajenga mji mpya Kigamboni kule Dar Es Salaam, kwanini nguvu hizo zisingewekezwa Dodoma kama kuna dhamira ya kweli?


Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itangaze rasmi kuwa mpango huo umeshindwa kutekelezeka na hivyo ikubaliane na Sera na Mpango wa CHADEMA kuwa Dodoma uendelee kuwa Jiji la Elimu na Bunge, Dar es Salaam uwe ni mji Mkuu wa Biashara na Utendaji wa shughuli za Serikali.

Mheshimiwa Spika, TAMISEMI ndio Wizara kiungo kati ya Serikali kuu na wananchi (Halmashauri), hivyo ni ukweli uliowazi kuwa mashauriano ya karibu kati ya wizara mbalimbali zilizo Dar es Salaam ni muhimu sana katika kufanikisha taarifa kutoka juu hadi chini.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa TAMISEMI ndio Wizara kiunganishi na Wizara nyingine zote zilizopo Dar es Salaam, kwa namna moja au nyingine imekuwa ikiingia ikitumia gharama kubwa kwa ajili ya kufanya uratibu ili miongozo yote inayotolewa Serikali Kuu iwafikie watendaji walioko ngazi za chini.

Mheshimiwa Spika, katika hili tufikirie kuwa kila siku gari liko safarini (posho ya mkurugenzi na dereva, mafuta na uchakavu wa gari). Kwa umbali ni kilimeta 450 kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam, kwa magari ya land cruiser kwa safari hii litatumia lita 100 kwenda tu. Hivyo kwa mwezi mmoja wa siku 22 za kazi kwa safari ya kwenda na kurudi mafuta ni Tshs. 9,680,000/= kwa mwaka mzima kwa mafuta ni Tshs.116,160,000/-. Hizi ni gharama za mafuta tu kwa gari moja, hapo bado gharama za kuwawezesha wakurugenzi au maafisa kuishi Dodoma ama Dar es Salaam. Hii ni mojawapo ya sababu zinazosababisha fungu linaloombwa na TAMISEMI kwa ajili ya mafuta yanayoombwa kwa mwaka 2012/2013 kufika Tshs.709,887,000/

Mheshimiwa Spika, wakati Waziri Mkuu akihitimisha hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2011/2012 hapa Bungeni alisema , nanukuu "Kwa maelekezo haya ya Mheshimiwa Rais uamuzi wa kuhamia Dodoma hauna budi kutekelezwa. Kwa maana hiyo, hata kama fedha zimetengwa, napenda kuwahakikishia kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu itajengwa Dodoma. Aidha, Wizara zote ambazo zimetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi zianze kujenga Dodoma. Jambo muhimu ni kuvuta subira. Tutaendelea kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais kwa lengo la kuhamia Dodoma kama ilivyokwishapangwa" Kambi ya Upinzani tunahoji utekelezaji wa kauli hii umefikia wapi ?

6.1 Hadhi Ya Dar Es Salaam Kuwa Na Sheria Yake

Mheshimiwa Spika , Serikali pamoja na kutangaza adhma yake ya kuhamishia shughuli zake makao makuu dodoma toka mwaka 1973, Lakini bado shughuli zake zote zinafanywa Dar es Salaam. Nchi nyingi hutaja miji yake mikuu kwenye katiba na kuitungia sheria maalum ya kuiongoza hii inasaidia utendaji na maendeleo ya miji mikubwa kama Dar es Salaam kupata "attention" ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, Dar es Salaam ina muundo wa kipekee duniani, ambapo kuna Halmashauri tatu za kiutendaji (Manispaa ya Ilala,Temeke,Kinondoni) na Halmashauri moja ya kiitifaki "ceremonial" inayoitwa Halmashauri ya Jiji la DSM na wala haina madaraka ya Jiji. Ina majukumu ya kuitambulisha Dar es Salaam kiitifaki. Ili kujiendesha imepewa mapato ya UDA,soko la Kariakoo,Ubungo bus terminal, DDC . Halmashauri hii haina wananchi wala Madiwani! Inaundwa na madiwani watatu watatu toka kila Manispaa, Mameya na Wabunge. Kinachotokea ni kuifanya ifanye mambo shaghalabaghala kwa kuwa haina "political responsibility".
30 Nov 2010 kupitiia GN No 416/2010 Serikali ilivunja Halmashauri ya Jiji.


Mheshimiwa Spika, Cha kushangaza serikali imeendelea kupeleka fedha kwenye chombo ambacho hakipo. Kwa kushtuka na kuendesha mambo holela 3 feb 2012 kupitia GN No 36/2012 serikali imetangaza kuunda halmashauri ya jiji la DSM bila kulihusisha bunge. Hapa ndipo wameongeza tatizo badala ya kupunguza tatizo.
Sasa kwa kuwa ni dhahiri Serikali imeshindwa kuhamia Dodoma,sasa itangaze rasmi kuwa Dodoma ni Jiji la Bunge na DSM itangazwe mji Mkuu wa kiutawala na kibishara na itungwe sheria maalum ya utawala wa DSM ili iwe na viongozi na watendaji mahiri, wabunifu na wenye nguvu ya sheria ili mji huu upate heshima,uwe msafi,na huduma zifanane na hadhi ya majiji mengine duniani.


7.0 UWEKEZAJI NA UWEZESHAJI.

7.1 Sekta ya Kilimo

Mheshimiwa Spika, nchi yetu bado ni nchi ya Kilimo licha ya kwamba mchango wa sekta nzima ya Kilimo katika Pato la Taifa umeshuka mpaka asilimia 23.7 mwaka 2011 kutoka asilimia 24.1 mwaka 2010. Kushuka huku kwa mchango wa sekta ya Kilimo katika Pato la Taifa ni matokeo ya kuendelea kuporomoka kwa sekta ya Kilimo na kuongezeka kwa kasi kwa sekta ya huduma katika Uchumi wa nchi yetu.

Hata hivyo Kilimo bado kimeendelea kuwa Sekta inayoendesha maisha ya Watanzania wengi, takribani asilimia 75 ya Wananchi wote. Hivyo kitendawili cha Umasikini katika Uchumi unaokua kitateguliwa na sekta ya Kilimo na hivyo kuwaondoa Watanzania katika dimbwi la Umasikini. Mipango ya Uwekezaji katika Uchumi na Uwezeshaji wa wananchi ni lazima uzingatie Sekta Mama katika nchi yetu ambayo ni Kilimo.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2011 umeshuhudia kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa uzalishaji kwenye mazao makuu ya chakula nchini ambayo ni Mahindi na Mpunga/Mchele. Wakati Uzalishaji wa Mahindi umepungua kwa asilimia 3 kutoka tani 4.5 milioni mwaka 2010 mpaka tani 4.3 milioni mwaka 2011, uzalishaji wa Mchele ulipungua kwa asilimia 14.1 kutoka tani 1.7 milioni mwaka 2010 mpaka tani 1.4 milioni mwaka 2011. Uzalishaji wa Mazao mengine ulikuwa wa kuridhisha kiasi. Ni dhahiri kwamba uwezo wa nchi kuzalisha chakula ni mkubwa sana na hata mara 20 ya kiwango kinachozalishwa sasa. Tanzania inao uwezo wa kuzalisha Chakula kwa matumizi ya nyumbani na hata kuuza nje ziada na kupata fedha za kigeni.

Mheshimiwa Spika, uwekezaji wa Serikali katika miundombinu ya Kilimo ili kuwezesha wananchi kuzalisha chakula kingi zaidi ni mdogo mno. Serikali imegubikwa na suala la Kilimo Kwanza na hasa mpango wa SAGCOT kama mwarobaini wa kuongeza uzalishaji wa Kilimo. Kambi ya upinzani Bungeni inaamini kwamba uzalishaji endelevu utakaoondoa umaskini vijijini ni uzalishaji utakaofanywa na wananchi wakulima wadogo wadogo na wa kati badala ya Mashirika makubwa ya kimataifa ambayo yanaendeshwa kwa lengo la kupata faida zaidi. Uzalishaji endelevu ni ule unaowafanya wananchi wamiiliki ardhi yao badala ya ule unaowafanya wananchi kuwa ‘manamba' katika Nchi yao wenyewe.

Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao yote ya Biashara uliongezeka ingawa kwa baadhi ya mazao isipokuwa Karafuu, bei katika soko la Dunia liliathiri sana thamani ya mauzo yetu nje. Mazao ya Kilimo yanachangia dola za kimarekani 669 milioni tu, yaani chini ya dola za kimarekani bilioni moja kwa mwaka. Ni dhahiri kwamba iwapo tukiongeza uzalishaji kilimo kinaweza kuchangia mara tatu ya sasa katika mapato ya fedha za kigeni.

Mheshimiwa Spika, zao la Tumbaku ndiyo linaoongoza kwa mauzo nje likiingiza dola za kimarekani 281 milioni, likifuatiwa na Kahawa kwa kuingiza dola 143 milioni, Korosho dola 107 milioni, Pamba 61.6 milioni, Chai dola 47.2 milioni na Karafuu dola 29 milioni. Mauzo ya Katani katika soko la Dunia yalikuwa ni madogo sana kiasi cha kutoonyeshwa katika Kitabu cha Hali ya Uchumi mwaka 2011.

Mheshimiwa Spika, iwapo tukiweka mkakati maalumu wa kuongeza uzalishaji katika kilimo na kuongeza thamani hapa nchini ni dhahiri kwamba tutaweza kuongeza mauzo yetu nje na kuwafanya wakulima wetu wapate fedha na kuweza kuboresha maisha yao.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa tuliyonayo ni kwamba mfumo wetu wa Kilimo cha mazao ya biashara kimehodhiwa na Bodi za Mazao ambazo kazi yake kubwa ni kunyonya (extractive behaviour) wakulima badala ya kuwaendeleza. Bodi za Mazao yote hapa nchini kama zilivyoundwa baada ya kuvunja Mamlaka za Mazao zimeonyesha kushindwa kabisa kusimamia Mazao yao. Mkulima ndio anaathirika na Bodi za Mazao kutokana na maamuzi yao ambayo hayazingatii haki za Wakulima na bodi hizi kuongozwa kisiasa zaidi na makada wa CCM wakiwamo Wabunge kuliko utaalam. Ni hakika basi kuwa Chama cha Mapinduzi hakiwezi kukwepa lawama ya kilio cha wakulima nchi hii kwa kushindwa kuongoza bodi hizi na kuzigeuza vitegauchumi.

Mheshimiwa Spika, vile vile sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma katika Sekta ya Kilimo ilitekelekezwa vibaya kiasi cha kutapanya hovyo mali za Taifa kwa kuuza hovyo viwanda vilivyojengwa kwa mkakati maalumu wa kulifanya Taifa kuongeza thamani ya Mazao, kuuza Mashamba ya Umma hovyo bila hata kujali wenyeji waliotoa Ardhi kwa Shirika la NAFCO (rejea migogoro ya Mashamba ya Basutu na Kapunga ambapo Serikali iliuza mpaka kijiji na wananchi wake kwa mwekezaji) na kuachia mali zingine za Umma bila uangalizi (Mfano wa Vinu cha kusaga nafaka Iringa, Mwanza na Arusha).

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba tuangalie upya namna tunavyoendesha Sekta ya Kilimo kupitia Bodi za Mazao. Ni lazima tuangalie upya majukumu ya Bodi za Mazao katika kuendeleza Mazao wanayoyasimamia ikibidi kuondokana kabisa na Bodi za Mazao na kurejesha Ushirika wenye Nguvu, unaoendeshwa na wananchi wenyewe bila kuingiliwa na wanasiasa.

Mifano ya Chama cha Ushirika cha Kanyovu kule Kigoma ni moja ya mifano inayoweza kutumika katika kuangalia upya usimamizi wa Mazao yetu ya Kilimo. Chama hiki kinajiendesha kibiashara, kimejenga kiwanda chake cha kukoboa Kahawa na hata kupata soko la kuuza ‘specialty coffee' moja kwa moja kwa makampuni makubwa kama Sturbacks huko Marekani kwa jina la Gombe Coffee.

Mheshimiwa Spika, chama changu kilipotembelea mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara kabla ya Bunge hili la Bajeti tumeshuhudia umasikini wa kutupwa wa wananchi wetu. Wananchi wa Lindi na Mtwara wangekuwa wanafahamu kwamba zao la Korosho ni zao la Tatu kwa kuingiza fedha za kigeni nchini (Dola 107 milioni mwaka 2011) baada ya Tumbaku na Kahawa, hakika wasingekubali kubaki katika umasikini wa namna ile.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo juhudi za Serikali ya awamu ya kwanza ya nchi yetu kujenga viwanda vya Korosho ili kuongeza thamani na kumfanya mwananchi apate fedha zilikwamishwa na sera mbovu za ubinafsishaji. Katika Viwanda 12 vya korosho nchini, ni viwili tu vinafanya kazi.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana korosho ya thamani ya zaidi ya dola 185 milioni ilibaki kwenye maghala bila kuuzwa. Wakulima walipewa bei ndogo ilhali bei katika soko la Dunia ilipanda kutoka dola 963 kwa tani mpaka dola 1110 kwa tani. Bodi ya Korosho iliendelea na ukiritimba wa kutoa zabuni ya kuuza dawa ya Sulphur kwa wakulima kwa bei kubwa isiyoendana na uhalisia. Kambi ya Upinzani inataka kuwepo na mfumo bora wa soko la Korosho ikiwemo kuzuia kuuza nje Korosho ghafi na kujenga viwanda vidogovidogo vya kubangua korosho vijijini ambavyo mbali na kuongeza thamani ya zao la korosho, vitaongeza kwa kiasi kikubwa ajira kwani viwanda vya kubangua korosho ni "labour intensive."

Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia wabunge wanaotoka mikoa inayolima Pamba wakiongea kwa uchungu kuhusu bei ya Pamba. Ni dhahiri kwamba Bei ya Pamba katika Soko la Dunia imeporomoka sana. Mara ya Mwisho tumeangalia soko la Liverpool tumeona bei imefikia senti za dola za Marekani 67 kwa pauni moja. Hivyo ni dhahiri kwamba Bei ya Pamba mwaka huu itakuwa ni mgogoro mkubwa sana. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iweke mkakati maalumu ili kuepuka mkulima kuumizwa na wanunuzi wa pamba ambao wengine ni wanasiasa. Serikali iangalie uwezekano wa kuanzisha mfumo maalumu wakuweka sawa bei za Mazao (stabilization Fund) ili kuhakikisha mkulima analindwa na kubadilika kwa bei katika soko la Dunia. Hata hivyo silaha kubwa kuliko zote ya kudhibiti bei ni kuongeza thamani hapa nchini kwa kufufua viwanda vyote vya nguo na kutoa motisha maalumu kwa wenye viwanda wa ndani ili wazalishe kwa kutumia malighafi za hapa nchini.

7.2 Uwekezaji

Mheshimiwa Spika, mazingira ya uwekezaji nchini bado hayaridhishi kutokana na sababu mbalimbali , Kwa kipindi cha mwaka 2011/2012 wizara iliweza kuanzisha kituo kimoja tuu cha utoaji huduma kwenye bandari ya Dar Es Salaam, na bado mizigo imeendelea kukaa bandarini kutoka siku 12-13 mwezi Mei 2011, hadi kufikia siku 9 mwezi Machi,2012.

Mheshimiwa Spika, Jambo hili linafanya uwekezaji katika nchi yetu kuwa mgumu sana haswa kutokana na mizigo kukaa muda mrefu bandarini na hivyo wawekezaji kujikuta wanakaa muda mrefu bila kupata mizigo yao na hivyo kuchelewesha miradi ya wawekezaji. Pia wawekezaji wamejikuta wakiwa na vikwazo vya kudumu katika barabara kuu wakati wa kusafirisha mizigo yao mbalimbali kutoka bandarini na haswa kutokana na kukosekana kwa usafiri wa reli nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Nchi uwekezaji na uwezeshaji ni kuwa kwa kipindi cha mwaka 2011/2012 jumla ya shilingi bilioni 9.9 zilitolewa kwa wawekezaji kwa ajili ya mradi wa kukuza ushindani wa sekta binafsi (PSCP), na fedha hizi walipewa wajasiriamali 2,780 na kupewa ruzuku ya mbegu na mitaji. Wakati huo huo jumla ya shilingi bilioni 7.8 zilitolewa kwa kampuni 786 chini ya mpango uitwao programu ya ruzuku ya kuchangia (Matching Grants Programme).

Mheshimiwa Spika, imekuwepo mifuko mingi sana ambayo inaasemekana kukusudia kuwezesha wananchi kushiriki shughuli za kiuchumi. Mifuko hii kama vile MEF (Mwananchi Empowerment Fund), JK Fund (Mabilioni ya Kikwete), SELF, ECGS (Export Credit Guarantee Scheme), Dirisha la Kilimo TIB, Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) nk imekuwa ikitoa mikopo na misaada mingi katika mfumo wa usiri mkubwa.
Watanzania walio wengi hawaelewi uwapo wa mifuko hii tukiwemo sisi wabunge. Mifuko hii ni mingi mno inayofanya kazi inayofanana na ingeweza kuunganishwa na kuokoa fedha nyingi ambazo sasa zinaishia katika utawala. Mifuko hii vilevile inahudumia Watanzania na hata wasio Watanzania wanaounga mkono kwa njia moja au nyingine itikadi moja. Ubaguzi huu ni bora uangaliwe usilete madhara kwa umoja wetu kama Taifa.


Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani , inataka kujua utaratibu ambao umekuwa ukitumiwa na serikali katika kuchagua wajasiriamali hawa na kampuni hizi kwani ni kiasi kikubwa sana cha fedha za walipa kodi kwa mabilioni ambacho kimekuwa kimetolewa. Hii itasaidia Watanzania wengine kujua njia wanazopaswa kutumia ili waweze kupata fedha hizo.

8.0 KITUO CHA UWEKEZAJI TANZANIA (TIC)

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi Januari 2011 ha di Aprili 2012 TIC imetekeleza majukumu mbalimbali , mojawapo likiwa ni kuhamasisha wawekezaji kutoka nje ambapo waliweza kupata wawekezaji katika miradi mitatu ambayo ni mradi wa makaa ya mawe mchuchuma na chuma liganga,mradi wa makaa ya mawe ngaka na mradi wa Kilwa Energy Co.Ltd unaotarajiwa kuwekeza katika kuzalisha umeme kiasi cha Megawati 318 kwa kutumia gesi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na World Investment Report 2011, mitaji kutoka nje imeongezeka kutoka Dola za Marekani 646 Milioni mwaka 2009 hadi kufikia Dola za Marekani 700 Milioni mwaka 2010.Hii ni sawa na ongezeko la dola 53 milioni kwa mwaka mzima . Taarifa hii imekuja wakati ambapo nchi yetu imekuwa na wawekezaji kwenye sekta ya gesi na mafuta ambao wamejitokeza katika kipindi husika . waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwahi kusema, na nanukuu: "Tubadilishe tabia, itabidi tujitolee tu kama vile mtu anataka kujiua na tuwasaidie wakulima, wafugaji na wavuvi… katika bajeti tusiulizane, tuelekeze nguvu katika maeneo hayo…" Akifungua mkutano wa siku tatu wa wadau wa mifugo
mjini Dodoma (Jumatatu, Sept. 28, 2009)


Mheshimiwa Spika, taarifa za ''Doing Business Report'', inayoandaliwa na Benki ya Dunia, pamoja na ile ya "Global Competitiveness Report'', inayoandaliwa na World Economic Forum, zinaonyesha kuwa Tanzania haifanyi vizuri katika kujenga mazingira ya kuvutia wawekezaji, hali hii inachangiwa sana na Urasimu wa taasisi za serikali katika kuwahudumia wawekezaji ili kutoa huduma bora na za haraka , ukosefu wa miundombinu kama maji ,barabara , umeme , usafiri na haswa ikizingatiwa kuwa ikishafika saa kumi na mbili jioni uchumi wan chi yetu huwa unalala kwani hakuna usafiri ama wa ndege au mabasi kwa muda wa usiku, n.k.

Kambi ya Upinzani , inahoji kama kwa mwaka mzima mitaji inaongezeka kwa kiwango hicho , kuna haja gani ya serikali kuendelea kusisitiza kuwa ziara za rais nje ya nchi zimekuwa na mafanikio makubwa ya kuvutia wawekezaji ? je ni kiasi gani cha fedha kilitumika katika mwaka husika kwa ajili ya ziara za rais na viongozi wengine nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta wawekezaji?

Hata kama raisi akienda nje kila siku kama hatujaboresha mazingira ya uwekezaji katika nchi yetu tutakuwa tunaendeleza matumizi mabaya ya rasilimali za taifa letu tuu . Pamoja na rais kwenda G8 na kurejea akisema kuwa tumepata mafanikio makubwa lakini taarifa ya benki ya dunia ya mazingira ya kufanya biashara inaonyesha kuwa Tanzania mwaka 2011 ilikuwa ya 125 na mwaka huu 2012 imekuwa nafasi ya 127 huku ni kurudi nyuma , nah ii ni dalili ya wazi kuwa kwenda nje ya nchi sio suluhisho la kupata wawekezaji bali njia pekee ni kuboresha mazingira yetu ya uwekezaji haswa kwa kuimarisha miundombinu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Hapa ndio maneno ya waziri mkuu yanakuwa na maana; nanukuu: "kama Bunge, lakini mmoja mmoja kama watumishi wa umma, tunao wajibu mkubwa sana wa kuishi na kutenda kwa mfano. Tujiepushe na tamaa zinazoweza kuliingizia Taifa hili hasara kubwa". Kauli ya Waziri Mkuu kuhitimisha mjadala wa Richmond,
Mkutano wa 18 wa Bunge, Februari 10, 2010


8.1 Gesi Asilia

Mheshimiwa Spika, nchi yetu sasa imebarikiwa kuhusiana na suala la Mafuta na Gesi Asilia. Hivi sasa kuna Mikataba 29 na Leseni 18 zimetolewa kwa kampuni mbalimbali za kimataifa kutafuta Mafuta na Gesi asilia kwa niaba ya Shirika la Petroli Tanzania (TPDC). Kwa taarifa za TPDC hivi sasa nchi yetu ina utajiri wa Gesi Asilia wa jumla futi za ujazo 29.5 trillioni (Trillion Cubic Feet – TCF).

Mheshimiwa Spika, kwa bei ya sasa ya Gesi katika Soko la Dunia, Tanzania yaweza kuwa na gesi asilia yenye thamani kati ya zaidi ya dola za kimarekani 3.5 trillioni kwa kuchukua kiwango cha chini cha ‘recoverable gas' na 6 trillioni. Ugunduzi zaidi bado unaendelea ambapo Kampuni za BG/Ophir, Ophir/Mubadala na Shell/Petrobras zinaendelea na zoezi la utafutaji zaidi. Katika eneo la Ziwa Tanganyika kampuni ya Beach Petroleum imeanza zoezi la kukusanya ‘seismic data'.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la vitalu namba 9, 10, 11 na 12 Mashariki mwa kisiwa cha Unguja na eneo la Pemba channel shughuli za Utafutaji bado hazijaanza kufanyika kutokana na mgogoro usiokwisha wa suala la Mafuta na Gesi kuwa suala la Muungano au hapana. Kambi ya Upinzani Bungeni inapenda kuitahadharisha Serikali kwamba masuala ya utafutaji wa Mafuta na Gesi ni masuala ya Msimu na hivyo kuchelewa kutoa maamuzi kuhusu suala la Mafuta na Gesi kuwa suala la Muungano au la kunaweza kuondoa uwezekano wa eneo hili la Zanzibar kufanya zoezi la utafutaji hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inatoa mapendekezo yafuatayo katika kuimarisha na kuboresha sekta ya gesi na mafuta hapa nchini ili kuitayarisha nchi kwa utajiri huu mkubwa:
i. Suala la mafuta na gesi ni muhimu sana likawekewa utaratibu maalum na hatua zichukuliwe haraka ili kuandaa sera na sheria ya sekta ya gesi itakayosimamia uendeshaji wa sekta hii muhimu kwa uchumi wa taifa. Muswada wa sheria husika uwasilishwe kwenye Bunge mapema iwezekanavyo. Kumekuwa na ahadi nyingi za Serikali kuhusu jambo hili, sasa utekelezaji ufanyike


ii. Pawepo na Mpango maalum wa Maendeleo ya Gesi (Gas Master Plan) nchini kuanzia utafutaji, uchimbaji na umuhimu wa gesi asilia kwa manufaa ya Taifa na kukuza uchumi wetu. Lengo ni kujua ni gesi kiasi gani tutaitumia kuzalisha Umeme, kuzalisha Mbolea na bidhaa nyingine, matumizi ya viwandani na kiasi gani tutauza nje ya nchi.

iii. Wananchi wanaozunguka maeneo yanayopatikana au yanayopitia gesi asili wawe sehemu ya mipango ya maendeleo ya gesi asili na hivyo kunufaika na matumizi ya gesi badala ya kuachwa, hali inayoleta manunguniko na tishio la uendelevu wa sekta husika na haswa ikizingatiwa kuwa uwekezaji unaofanywa katika sekta hii kama wananchi hawataona kuwa na wao ni wafaidika ni rahisi sana kuweza kuhujumu miundombinu hii na kuhatarisha usalama na hata uhai wa wananchi wengine .

iv. Ujenzi wa miundombinu ya gesi uwe unazingatia mahitaji ya muda mrefu ili kupunguza gharama na kuondokana na uhaba na uharibifu wa maliasili, mfano bomba la Songosongo liliwekwa bila kuzingatia mahitaji asili ya gesi na hivyo kujikuta kuwa wanashindwa kusafirisha gesi ya kutosha kutumiwa na wahitaji wote;

v. Tuwekeze kwenye kuwapa elimu na maarifa vijana wa Kitanzania na haswa kwenye Sekta ya gesi ili waweze kupata utaalamu wa jinsi ya kusimamia sekta hii kama ambavyo nchi majirani zetu wa Uganda na Msumbiji wamefanya kwa kuwapeleka vijana wao nje ya nchi ili kupata utaalamu juu ya uendeshaji wa sekta hii.

Tunasisitiza umuhimu wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtwara ambacho kitajikita kuwaandaa Watanzania kuwa wataalamu wa sekta ya Mafuta gesi kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Ieleweke Chuo hiki hakitahusika na masomo ya Sayansi peke yake bali pia Sheria, Uchumi na Menejimenti ili kuhakikisha kwamba Taifa linakuwa na rasilimali watu ya kutosha. Mradi huu wa Chuo Kikuu cha Mtwara uanze mara moja.

vi. Serikali iliahidi kwa Shirika la Fedha la Kimataifa kwamba Sheria ya usimamizi bora wa Fedha za Mafuta na Gesi (Petroleum Revenue Management act) italetwa Bungeni mnamo mwezi Novemba. Kambi ya Upinzani inasisitiza kwamba Sheria hii iletwe haraka ili kuweka wazi mapato yatokanayo na utajiri huu na namna bora ya kutumia fedha hizi ili kuzuia uchumi kuathiriwa na pia kuzuia ufisadi. Hatutaki Tanzania iwe kama nchi nyingine za Kiafrika ambazo utajiri wa Mafuta na Gesi umekuwa ni laana badala ya Neema.

vii.Serikali iweke mazingira bora ya kujenga uwezo wa Watanzania kutoa huduma kwenye kila hatua ya utafutaji wa Mafuta na Gesi. Hivi sasa kuna zaidi ya wageni 1200 kwenye Meli za kutafuta Mafuta na Gesi katika Pwani ya Mtwara, Lindi na Pwani. Kwa masikitiko makubwa sana wageni hawa wanakula hata nyanya, mchicha na vitunguu kutoka nje ya Tanzania.

viii. Vile vile tudhibiti makampuni ya Ulinzi kutoka nje kuwa na silaha kali kali kwa kujenga uwezo wa Jeshi letu la Majini (Navy) ili liwe na kikosi maalumu kwa ajili ya kulinda meli za kutafuta mafuta na Gesi na Makampuni haya yatozwe tozo maalumu. Ni hatari sana makampuni ya kigeni kuwa na masilaha makubwa ndani ya ramani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

…………………………………..
Freeman A. Mbowe (Mb)
Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Msemaji Mkuu wa Kambi-Ofisi ya Waziri Mkuu
25.06.2012

 
Habar wakuu!
Kutokana na vuguvugu la udini ambalo linazidi kusambazwa na baadhi ya viongozi wa kidini hapa nchini pamoja na vyombo vya habari, mhe Mbowe amesema haya yote yanatokana kutokana na serkali dhaifu ambayo inashindwa kukemea mambo kama hayo ambayo madhara yake ni makubwa kwa nchi pia amekemea vikali tabia ya viongozi wa CCM kuwagawa watu kidni na kiukanda na kikabila kwa maslahi mafupi ya chama chao.

Source Mbowe mwenye kwenye hotuba yake bungeni.
Wachovu wa mawazo huwa kutwa kucha ni kulala tu.

Yeye Mbowe sera zake za kuendesha serikali bila udini zinasemaje? Sijamsikia akikemea Uamsho na SMZ kwa kuchoma makanisa.
 
Wachovu wa mawazo huwa kutwa kucha ni kulala tu.
Yeye Mbowe sera zake za kuendesha serikali bila udini zinasemaje?
Sijamsikia akikemea Uamsho na SMZ kwa kuchoma makanisa.

CDM haina serikali/dola ambayo ndiyo ingestahili kuchukua hatua stahiki kulingana na udini. Kulizungumzia hili Bungeni ndiyo jukwaa lake sahihi kuliko angeongelea vichochoroni.
 
CDM haina serikali/dola ambayo ndiyo ingestahili kuchukua hatua stahiki kulingana na udini. Kulizungumzia hili Bungeni ndiyo jukwaa lake sahihi kuliko angeongelea vichochoroni.

Mbimbinho says Thanks for this useful Answer. Kudos:mod:
 
Ndu wana JF
Katika hali ya kusikitisha kabisa,Kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni Mh.Freeman mbowe amezungumzia swala la uhusiano ndani vyama vya siasa hapa Tanzania, katika maneno yake amegusia swala la propaganda za kikanda ndani ya vyama vya siasa hasa chadema.

Mh.mbowe ameonekana akipinga na kukanusha kuwa chadema haina ukanda kama inavyofikiliwa na watu waliwengi hapa nchini.

Naomba kumshangaa(mbowe) kupinga swala hili la ukanda ndani ya chama chake Mbowe,kwa sababu yeye ndiye anaye plan na kutoa pesa za vijana wake wa ukanda wa kaskazini ambao bila aibu wala soni wamekuwa wakieneza ukanda huo kwenye mikutano yao ya chama kwa vitendo.

Naomba kudhibitisha hili kwa mkutano mmoja tu au miwili ambayo imekuwa ikifanyika hapa Jijini Dar es salaam na safari ya kusini mwa Tanzania.

Mkutano wa Jumamosi Tar.23 /06 /2012 pale SINZA UZURI kama kawadia safu ya ukanda wa kaskazini ndio waliongoza a-z ya mkutano ule.Ndugu Kilewo (katibu wa chadema mkoa maalumu wa kinondoni) ndiye anayeenezaa ukanda huu unao UA chama ndani kwa ndani.Katika mkutano ule aliwasimamisha kuhutubia wakaskazini tu,,mfano alimsimamishwa Mkaskazini mmoja(ambaye alizua gumzo kwa jukwa kuu na wanafunzi wa elimu ya juu waliofika pale mara baada ya kuanza kumtetea kikwete nanukuu "tatizo sio rais wala serikali tatizo ni wabunge wetu" na kutangazwa kuwa ni mpiganaji wa chama na alihutubia kwa muda mrefu.Pia akafuta Antoni Komu,akafuta lema,akafuta mzee ndesambulo ambaye alikuwa mtu wa mwisho.

Lema alijitambulisha kama mjumbe wa kamati kuu..ilihalli ni uongo,kwa sababu ujumbe wa kamati kuu alisha poteza sifa zake mara baada ya kupoteza kiti cha ubunge pale arusha.kwa sababu alikuwa mjumbe wa kamati kuu kwa kuwakilisha wabunge wa chadema.
Katika mkutano huu kulikuwepo viongozi mbalimbali, madiwani na mwenyekiti wa vijana wa kinondoni hawakupewa nafasi kabisa,,pia kulikuwepo na wanaharakati wazoefu wengi tu lakini hawakupewa nafasi licha ya muda kuruhusu nafasi hiyo.

Pia kwenye mkutano wa manzese waliohutubia siku ile ni wakaskazini ,watu amabo si wakaskazini kama Heche alipewa nafasi ile kwa sababu no way out HECHE NI MWENYEKITI WA BAVICHA hivyo ilikuwa si rahisi kumkwepa.

Kubwa zaidi ni kwenye mikutano iliyokuwa inaendelea kusini mwa Tanzania..katika ROSTER ile ni wa kaskazini ndio walipewa nafasi ya mbele katika kwenda na kwenye kuutubia

Pia ona katika swala la malipo kwa wanaharakati wa kati(middlemen)...waliku wanalipwa Ali bananga na Ole millya(wakaskazini) ndio walikuwa wanalipwa kwenye kundi la wanaharakati wa kati..wanaharakati wengine wote hawakulipwa.

Pia mafunzo yaliyokuwa yanaendeshwa nchi nzima kwa madiwani wa chadema,yamekuwa yakifanywa na watu wa kaskazini ..ambao ni katibu wa Mbunge wa Moshi mjini,John Mrema na Antoni komu.Hii ni dhahili hapa kunaajenda ya ukanda inayoenezwa na watu flani kama mbowe na watoto wake a kina kilewo.

Nasisitiza ukanda upo..kwenye mkutano wa UZURI SINZA ambao ulikuwa maalumu kwaajiri ya CHASSO kanda maalumu ya Dar es salaam..Vyeti vilishindwa kutolewa kwa sababu mkutano ule uliendeshwa kipropaganda (kikanda)

Kisa ni Kilewo ambaye aliufanya mkutano ule sehemu ya wakaskazini kujifua kisiasa.

Mwisho.
Nasisitiza kwamba chadema kwa mwenendo huu wa vijana wenu hasa Huyo anayejiita Kilewo mtaua chama kabisa..au mtazalisha kizazi cha chadema chenye mpasuko wa kikanda.Kuna makamanda wengi na wanaharakati ambao si wakaskazini wanajua na niwazoefu wa siasa hizi za kujenga chama..wakitumiwa vizuri dhana ya ukanda haitaendelea kuitafuna chadema.

Asanteni.
 
CDM haina serikali/dola ambayo ndiyo ingestahili kuchukua hatua stahiki kulingana na udini. Kulizungumzia hili Bungeni ndiyo jukwaa lake sahihi kuliko angeongelea vichochoroni.
Kisingizio cha kukosa akili kabisa.
Kama ingekuwa hivyo hata kina Nyere wasingwalaumu wakoloni kwa vile walikuwa hawana dola.

Mshaurini Mbowe kuwa akiwa kiongozi ni lazima awe na sera na mikakati inayoeleweka kuendesha nchi.

Kulalama na kupiga filimbi hilo awaachie kina Sugu.
 
Kisingizio cha kukosa akili kabisa.
Kama ingekuwa hivyo hata kina Nyere wasingwalaumu wakoloni kwa vile walikuwa hawana dola.
Mshaurini Mbowe kuwa akiwa kiongozi ni lazima awe na sera na mikakati inayoeleweka kuendesha nchi.
Kulalama na kupiga filimbi hilo awaachie kina Sugu.

Siungi mkono hoja.
 
ndio maana tunasema chadema ipo kupigania ukristo, wakiguswa wakristo lazima chadema watasema, wakiguswa waislam kimya!!! ni juzi tu hapa baraza la mitihani limefanya madudu, mbona cdm hawasemi?
Kuwa na akili japo kidogo ndo maana wanpigania wawatoe ccm mfumo kristo na mengine yote yatafuata na nyie mko mkuweka vizingiti acheni kulalamika wacha wawanyoshe sana mpaka mkija shituka ndo mtajuwa kumbe Cdm walikuwa sawa.
 
Pendeni kuwa wakweli, tena napenda kutoa wito kwa Watanzania wote tuwe tunatafakari kwa kina na kujadili, pamoja na kupima mambo. Mimi ningependa watu watakao ingia kwenye siasa waingie kufuatana na hisia zao pamoja na msukumo wao wa kisiasa na si kwa ukanda wao. Hatuwezi kujenga nchi kwa kuacha watu ambao ni wazoefu au wanauwezo fulani eti kwa sababu ni wa kanda fulani, pia hatuwezi kuacha kutumia watu waliokomaa kisiasa na waadilifu halafu tukachukua watu ambao bado hawajakomaa kisiasa baadae zikatoka kauli za kukidhoofisha chama halafu tuseme eti itifaki ya ukanda ilizingatiwa.

Ili mafanikio yapatikane ni lazima kuwe na watu ambao wana hofu ya Mungu, wachapa kazi, waadilifu na wazalendo hivyo itakuwa rahisi kwa watu wa namna hii kupigania ukweli, na si vinginevyo.

kama mkutano umefanyika na watu waliopatikana kwa siku hiyo ndio hao, pengine wengine walishindwa kufika hakuna tatizo, na pengine hao waliokuwepo hawakuwa wamejiandaa sasa utalazimisha mtu azungumze.

tusipende kutumika na chama cha ccm kwa kuleta mijadala ambayo haina mantiki, nchi inaisha huku tunatumia sababu ambazo hazina msingi kuchafua chadema. Tulete hoja zenye mashiko mwisho wa siku wangezungumza watu mbalimbali mngesema waislamu walikuwa wengi kuliko wakristo au wakristo mbona walikuwa wengi kuliko waislamu.

Mtu anapojiunga na chama huwa akubaliwi au akataliwi kwa sababu ya kabila lake au dini yake bali kwa sababu ya utashi wake yeye mwenyewe na ana haki zote za kugombea nafasi za chama na kuwa kiongozi hivyo vvyote vinapatikana kulingana na sifra za mgombea huyo na si vinginevyo. sasa mnataka mtu akiwa anafaa akataliwe kwa sababu ya ukanda, huu ndio utakuwa ubaguzi.
 
ndio maana tunasema chadema ipo kupigania ukristo, wakiguswa wakristo lazima chadema watasema, wakiguswa waislam kimya!!! ni juzi tu hapa baraza la mitihani limefanya madudu, mbona cdm hawasemi?

....ulitaka cdm iseme nn,wakati serikali ipo na imekaa kimya?mbona watu wavivu wa kufikiri?
 
hao hawafai hata kupewa nchi, wakipewa nchi wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, mawaziri wote watatoka kaskazini. tenda zote za serikali zitapelekwa kaskazini, makabila mengine mtabaki watazamaji.

ajabu sana kuona watu ambao mikoa yao inakaribia kufa kutokana na umaskini japokuwa wana rasirimali za kutisha wanaishabikia CCM, hivi wewe mtu wa Kigoma unaipendea nini CCM inayosababisha mkoa wenu uwe mfano wa umaskini hapa Tz?
 
Huyu mleta mada inaonekana ni miongoni mwa watu waliohudhuria mkutano huo na kunyimwa fursa ya kuzungumza kwa sababu hana wadhifa wowote ndani ya chama na ndio maana analalamika hivyo.

Pili , kuhusu mafunzo kwa madiwani ni kweli yalifanyika kwa madiwani wote wa nchi nzima 578 na yaliendeshwa kwa kanda tatu tofauti, moja ilikuwa na wakufunzi wafuatao, Silivester Masinde, Antony Komu, Josephat Isango,Alex Kasurura ,Kunty ....nyingine ilikuwa na Benson Kigaila,Lazaro Maasay,Jaffar Michael,na wengine na ya tatu ilikuwa na Nyangaki Shilungushela,John Mrema,Shaba, Basil Lema ,Anna Mghwira, Dadi Kombo .

Sasa huyu yeye anapaswa kufanya utafiti kuwa hao watu walitokea kanda gani na wengine walienda kwa sababu ya nafasi zao kwenye chama .

huyu inawezekana ni msaidizi wa Tuntemeke.......
 
Wenyewe wakija watakuwa wakali kwani ukweli unauma lakini mimi napita tu sina zaidi
 
udini ni singo ya ccm iliyochuja. ni wadaifu na hawaoni mbali na pia hawana wema kwa nchi hii. je!! hivi ccm na wabaguzi wengine watafanyaje ikiwa wakristo na wasio na dini wataamua kulipa moto kwa moto?
 
Huko tunakoelekea sio salama kabisa hasa kama tuna watu kama Nape wanaongea bila kufikiri madhara ya matamshi yao. Kama viongozi wa nchi wana nia ya dhati ya kunusuru taifa hili na mipasuko ya kidini, ukanda, ukabila ningeshauri yafuatayo wenyeviti na makatibu wa vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu wakutane na kuweka framework/miongozo kuhusu yafuatayo:

1. Iwe ni marufuku kwa mwanasiasa yoyote kujiingiza kwenye shughuli za kidini. Hakuna mambo ya harambee, wala kusalimia waumini, au kiongozi wa kisiasa (including rais) kuwa mgeni rasmi kwenye shughuli za dini. Kama anaenda kwenye ibada aende kama mtu wa kawaida na sio vinginevyo.

2. Tuondoe mambo yote yanayohusu dini kwenye elimu, kuanzia vitabu vilivyoandaliwa kwa misingi ya dini. Somo la dini liwe ni suala la mtu binafsi hivyo lisiwe chini ya NECTA. Dini na mambo yote yanagusa dini yawe mambo binafsi.

3. Wanasiasa wakubaliane mambo ambayo ni muhimu kwa umoja wa taifa hivyo kuachana na kauli za kugawa watanzani. Hapa ningeomba nimtaje Nape maana ameonesha kupenda siasa za kugawa watu.

Nchi yoyote iliyostaarabika huwa wanakubaliana mambo muhimu yanatakiwa kuzingatiwa na wanasiasa wote.
 
Back
Top Bottom