Mchezo mchafu wahusisha familia ni wakati wa NEC Dodoma; Kuchukulia hatua dagaa kuacha Mapapa

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Mchezo mchafu UVCCM Dodoma
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, wabunge zaidi ya wanne akiwamo Saidi Mtanda wa Mchinga, mkoani Lindi na Dk. Hamis Kingwangala wa Nzega, mkoani Tabora, ni miongoni mwa waliokuwa tayari kufichua mchezo mchafu wa matumizi ya mamilioni ya fedha kuhonga baadhi ya vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM.

Wakati mchezo huo unafanyika wabunge hao na wenzao walikuwapo Dodoma ambako kabla ya vikao vya CCM walikuwa wakishiriki shughuli za Bunge.

Inaelezwa ya kuwa hata hivyo, licha ya kuwa tayari wabunge hao walishindwa kupewa nafasi ya kufichua siri hiyo mbele ya NEC-CCM, inayotajwa kuhusisha familia ya kigogo huyo kupitia kwa mtoto wake mmoja.


Mtoto huyo ambaye kwa sasa jina lake tunalihifadhi kutokana na kushindwa kumpata kwenye simu yake ya mkononi, anatajwa kuwa mmoja wa walipaji posho kwa vijana wa CCM inayofikia hadi Sh milioni moja kwa mjumbe mmoja, fedha ambazo zinatajwa kutoka katika familia yake na watu wengine wasiojulikana.


Mtoto huyo pia anadaiwa kuwa kambi moja na Mwenyekiti wa UVCCM mkoani Arusha, James ole Millya, katika vurugu za mara kwa mara zilizokuwa zikiibuka UVCCM-Arusha ambazo hata hivyo, zilisuluhuhishwa na Steven Wassira, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.


Kwa mujibu wa taarifa za uhakika, alikuwa Nape Nnauye (Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM) aliyemtaka Mwenyekiti Rais Jakaya Kikwete kumpa mwongozo kuhusu kundi la vijana wa CCM kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania waliosafirishwa, kulipwa posho nono na gharama za malazi, wako Dodoma kwa shughuli gani na kwa sababu gani.


Nape anatajwa kueleza bayana kwamba ushahidi wa vijana hao kuwapo Dodoma kwa kuitwa na kundi la mafisadi upo, ushahidi ambao hata Kikwete anatajwa kuutambua na baada ya Nape kuhoji hivyo, Kikwete alimhoji Beno Malisa; fedha hizo wamezipata wapi.


Beno, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa UVCCM anatajwa pia kushambuliwa na mawaziri, William Lukuvi na Steven Wassira ambao hata hivyo walikuwa wakitoa lugha zenye mwelekeo wa kumuonya na si kutaka ashughulikiwe kwa mujibu wa kanuni za UVCCM au chama hicho.


Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baada ya Malisa kupigwa mashambulizi ndani ya siku ya kwanza ya vikao hivyo, alifikisha taarifa hizo kwa wenzake waliosafirishwa "kwa kazi maalumu" Dodoma na baadhi yao walitishika na kuanza kufunga safari ya kurudi mikoa walikotoka.


"Vijana hawa walisafirishwa kuletwa hapa kwa kazi kubwa mbili. Kwanza kuna maneno waliambiwa uongozi wa UVCCM unavunjwa, lakini pili kuna hofu kwamba wale viongozi mafisadi watang'olewa katika kikao hicho cha NEC.


"Kwa hiyo walikuja kutibua masuala hayo mawili kwa vitisho kwamba kama ingekuwa hivyo wangehamia Chadema, lakini baada ya Rais Kikwete kusema kwenye kikao wasitutishe, waende hata kesho baadhi ya vijana waliogopa wakakimbia wengine usiku kurudi walikotoka," anaeleza mtoa habari wetu.


Katika mchakato huo wa mawasiliano, gazeti hili limeshuhudia ujumbe wa simu ya mkononi kutoka kwa mmoja wa viongozi wa vijana katika moja ya mikoa ya Kanda ya Juu Kusini, ambaye pia ni mwalimu katika moja ya vyuo vikuu nchini.


Kiongozi huyo ndiye aliyekuwa akisambaza ujumbe wa kuita vijana wafuasi wa viongozi wanaopaswa kujiuzulu ili wakusanyike Dodoma ambapo kwa mikoa ya mbali kama Kigoma, Raia Mwema imeelezwa kuwa tiketi za ndege kwa vijana waliokuwa tayari kuelekea Dodoma zilikuwa zikipatikana kwa masharti tu, ukifika Dodoma uungane na kundi hilo.


Taarifa zinabainisha kuwa bajeti ya mamilioni ya fedha ilitengwa na kutumika katika kugharimia vijana hao kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.


Kwa mujibu wa taarifa hizo, mpango huo pia ulikuwa ukiratibiwa na kijana mwingine ambaye ni mtumishi katika moja ya kampuni za aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Azizi.


Hujuma zilianza mapema

Taarifa za kiuchunguzi zinaelekeza kuwa mpango wa kuhakikisha mchakato wa kujivua gamba unahitimishwa kwenye kikao cha NEC uliandaliwa na kundi la watuhumiwa wa ufisadi, ukiratibiwa na mmoja wa wajumbe wa Sekretariati ya CCM (jina linahifadhiwa).

Kigogo huyo ndani ya sekretariati ndiye aliyepewa jukumu la kuandaa waraka maalumu kuhusu hali ya kisiasa ambamo ndimo masuala ya kujivua gamba na mengine yanapaswa kuhusishwa.


Kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka kitengo cha maadili, jukumu la kuandaa waraka huo lililikuwa la kitengo hicho lakini baadaye lilikasimiwa na mjumbe huyo wa sekretariati, ambaye anadaiwa kufanya ‘uchakachuaji' ili kupenyeza matakwa ya mtandao wa kifisadi.


Hata hivyo, taarifa za kina zinabainisha kuwa waraka huo ulikataliwa mara kadhaa na Kikwete ambaye alikuwa anaukataa kupitia kwa Katibu Mkuu, Wilson Mukama.


Kutokana na kiongozi huyo kijana wa sekretariati kusumbuliwa kila mara kwa kurudishwa akatengeneze vizuri waraka huo; huku akishindwa kujua yalikuwa ni maagizo ya Kikwete na si Mukama, kuna wakati anatajwa kutishia kujiuzulu kutokana na kusumbuliwa akiamini ulikuwa ni usumbufu unaosababishwa na Mukama pekee.


Taarifa zinabainisha kuwa ingawa hatimaye alifuta maelezo yenye kuhujumu mpango wa kujivua gamba ndani ya waraka huo kama walivyotaka watuhumiwa wa ufisadi, lakini alikuwa akichomekea mawazo hayo wakati alipokuwa akifanya uwasilishaji kwenye vikao husika, vikiwamo vya Kamati ya Maadili iliyoketi kabla ya Kamati Kuu.


Mikakati ya kubadili upepo

Kumekua na juhudi kubwa za kubadili vita ya ufisadi kwa kuiwekea kinga ya kuwa chanzo chake ni vita ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015, ukihusisha watu wanaotajwa kuwania kumrithi Rais Jakaya Kikwete.

Juhudi hizo zinazoendeshwa kwa gharama kubwa, zinalenga kuwasafishia njia watuhumiwa wa ufisadi ili kuweza kuingia katika mbio za urais na hatimaye kuingia madarakani baada ya Kikwete kwa gharama zozote zile.


Madai hayo yameanza kwa kujaribu kuuaminisha umma kwamba chimbuko la hali mbaya ya kisiasa ndani ya CCM ni wanamtandao walioshiriki kumpitisha mgombea Jakaya Kikwete mwaka 2005.


Katika kuuaminisha umma, watuhumiwa wa ufisadi wamefanikiwa kuwaaminisha watu kwamba tuhuma dhidi yao ni za kupikwa na kwamba baada ya kumpitisha Kikwete na baada ya kuwa na hakika ya ushindi dhidi ya Upinzani, wanamtandao mmoja mmoja walianza kujitathimini juu ya uwezekano wa wao wenyewe kuwania urais baada ya Kikwete.


Vinara wa kundi hilo walikuwa Edward Lowassa, Samuel Sitta, Rostam Aziz, Getrude Mongella, Zakia Meghji, Abdulrahman Kinana, Bernard Membe, Juma Jamaldin Akukweti (sasa marehemu), Kingunge Ngombale Mwiru, Philip Marmo, Emmanuel Nchimbi, Ali Karavina, Juma Mwapachu, Henry Shekifu, Ponsian Nyami, Makongoro Mahanga, Nazir Karamagi, Stephen Wassira na Sophia Simba.

Sasa maelezo ya watuhumiwa yanaanza kulikumbushia kundi hilo kwa kudai kwamba, kundi hilo lilikuwa pia likijipanga kwa ajili ya nafasi karibu zote za uongozi wa juu wa serikali na mihimili mingine baada ya uchaguzi wa mwaka 2005.

Pamoja na kuwa sababu hasa ya minyukano ndani ya CCM inapotoshwa, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma ya kuwa "hali ya siasa ndani ya chama ni shwari lakini si shwari sana".


Kwa mujibu wa Mukama, makundi kinzani yameshamri ndani ya chama hicho na sasa yanapangana safu za uongozi kwa kutumia fedha jambo ambalo alisema ni kansa ambayo inakitafuna chama hicho polepole.


Alisema kwa ajili hiyo chama kilikuwa kimeamua katika kikao cha NEC kutafuta dawa ya tatizo hilo na kwa kuanzia tuhuma zote za viongozi wote zitashughulikiwa kwa ngazi mbalimbali chini ya kamati za maadili husika na ambao tuhuma zao zitathibiti watachukuliwa hatua bila kuchelewa.


Akinukuu waraka wa NEC, Mukama alisema: "Kwa kutambua kuwa suala la ufisadi limekuwa mzigo mkubwa sana kwa Chama cha Mapinduzi licha ya juhudi kubwa ambazo Serikali ya CCM imezifanya katika kupambana na tatizo hilo, NEC iliamua kuwa viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wajipime na kuchukua hatua wenyewe kwa maslahi ya Chama. Wasipofanya hivyo Chama kiwawajibishe bila kuchelewa.


"Ni dhahiri kuwa azimio hili lililenga viongozi wote wa Chama, katika ngazi zote cha chama chetu, kuanzia ngazi ya Taifa hadi Tawi. Ni dhahiri pia azimio hilo lilikusudiwa liwe sehemu ya utamaduni wa kusimamia maadili ya viongozi na wanachama wa chama chetu, yaani kwamba viongozi au wanachama, wanavunja maadili watachukuliwa hatua zinazostahili bia kuchelewa.

"Hali ilivyo hadi sasa, takriban miezi saba baada ya azimio hilo kupitishwa hatujapata mwitiko wa kuridhisha kutoka kwa viongozi wa ngazi yoyote ambao ni walengwa wa azimio hilo. Bila shaka wakati sasa umefika kwa chama kutekeleza ile sehemu ya pili ya azimio husika kwa kuwawajibisha wahusika. Lakini utekelezaji wake utafanyika vipi ili haki ionekane inatendeka? Jibu ni kwamba utekelezaji huo hauna budi ufanyike kwa kufuata utaratibu uliowekwa na kanuni za CCM za uongozi na maadili."

Aliongeza Mukama: "NEC imeagiza kupitia Kamati za Usalama na Maadili zianze mara moja mchakato wa kutekeleza azimio hilo kwa mujibu wa kanuni na taratibu na vilevile kwamba zoezi hilo lifanyike bila kuchelewa."

Kauli hiyo ya NEC ilikuja siku moja baada ya mmoja wa watu ambao wamekuwa wakituhumiwa kwa ufusadi Lowassa kuzungumza mkutanoni akisema alikuwa ametuhumiwa sana kwa kuitwa fisadi ili hali yeye si fisadi na kwamba alijiuzulu katika kashfa ya Richmond kulinda heshima ya CCM na serikali yake.

Aidha ilikuja baada ya NEC kutangaza ya kuwa ilikuwa imemvua madaraka Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kirumbe Ng'enda, ambaye alikuwa anatuhumiwa kuvuruga zoezi la kura za maoni katika chaguzi za wabunge na madiwani mkoani kiasi cha kuwashusha baadhi ya wagombea waliopata kura nyingi. Uamuzi huo umeelezwa kuwa ni, "kuchukulia hatua dagaa na kuacha mapapa."
 
Mchezo mchafu UVCCM Dodoma
.......
Inaelezwa ya kuwa hata hivyo, licha ya kuwa tayari wabunge hao walishindwa kupewa nafasi ya kufichua siri hiyo mbele ya NEC-CCM, inayotajwa kuhusisha familia ya kigogo huyo kupitia kwa mtoto wake mmoja.

Mtoto huyo ambaye kwa sasa jina lake tunalihifadhi
kutokana na kushindwa kumpata kwenye simu yake ya mkononi, anatajwa kuwa mmoja wa walipaji posho kwa vijana wa CCM inayofikia hadi Sh milioni moja kwa mjumbe mmoja, ........



Who owns this rag?
 
Back
Top Bottom