Mbuzi isokuna nazi

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,475
39,991
MBUZI ISOKUNA NAZI?
Macho puu yanitoka, nimepigwa na butwaa,
Na taya limedondoka, nimebaki kushangaa,
Moyo umenishituka, pumzi imenipaa,
Mbuzi isokuna nazi, ni bora kuiachiya!

Jikoni mumeiweka, hiyo mbuzi inang’aa,
Kwenye ghala mwatundika, eti hiyo yawafaa,
Kukuna kunapofika, mbuzi mnaiandaa,
Mbuzi isokuna nazi, bora mbali kutupiya!

Eti mbuzi ya hakika, sifa mnazitangaa,
Mwajivuna mwadundika, mbona mwaleta balaa,
Mbuzi hiyo imechoka, acheni wenu unaa,
Mbuzi isokuna nazi, haifahi kukuniya!

Mbuzi zenu zavunjika, ya kwangu miye ayeyaa,
Tena inaazimika, ikakuna kwa staa,
Na nazi ikakunika, mapishi yakakufaa,
Mbuzi isokuna nazi, ni mbuzi yao vichaa!

Nimechoka kuandika, kalamu yanidondokaa,
Ukweli huu hakika, hadharani wazagaa,
Mbuzi iloharibika, kukuna haitafaa,
Mbuzi isokuna nazi, kwanini mwaikalia?
 
MBUZI ISOKUNA NAZI.....

Salam na watolea,enyi wakubwa wakazi.
Vilingeni na vijiweni,huko mkijinafasi.
Ulaya,Asia na Marekani,Bongo mie sina wasi.
HIli jambo pembenuzi,mbona mna tupa kazi?.
Fumbo fumbia mjinga,mbuzi isokuna nazi....

Sikuzote mwaipamba,ile mbuzi chapa kazi.
Ushauri mikitoa,wala sisingizi ni iwazi.
Hata mimi kadhalika,sifa nilizitoa kwa mbuzi.
Mbuzi ile funga kazi,subirini tuone kazi.
Fumbo fumbia mjinga,mbuzi isokuna nazi.....

Kitazama rembo hasa,iking'a wazi wazi.
Majuu na Afirika,mbuzi inaenda kasi.
Majirani wa azima,migogoro kwisha kazi.
Mwana kijiji unadhima,mbona husemi wazi.
Fumbo fumbia mjinga,mbuzi isokuna nazi.....

Umeleta mgogoro,jaa umeilea mbuzi.
Si yakuka walakukunia,kazi haina mbuzi.
Jina lake maridhia,MBUZI midomo wazi.
Majilani wakunia hizo nazi,zanyumbani vipi MBUZI.
Fumbo fumbia mjinga,mbuzi isokuna nazi.....
 
Ni mbuzi ama ni buzi, ambalo halichuniki?
Nauliza wazi wazi, naomba uni hakiki
Useme kama ni buzi, ambalo halichuniki
Ambacho hakikuniki, ni mbuzi ama ni nazi?

Nahisi kama ni nazi, ambayo haikuniki
Lawama ati ni mbuzi, na tena unahamaki
Punguza pia unazi, si mbuzi isoshiriki
Ambacho hakikuniki, ni mbuzi ama ni nazi?

Si koroma wala nazi, ni dafu ukilicheki
Ni dafu la wazi wazi, na kamwe halikuniki!
Mbuzi itaweza kazi, kwa nazi kwake riziki!
Ambacho hakikuniki, ni mbuzi ama ni nazi?
 
Choveki nakusifia,bado wapamba yako mbuzi.
Inataka ushujaa,endelea kuitetea ile mbuzi.
Mbuzi ile omenoa,sikunyingi imekoa hili ulimaizi.
Nazi,dafu nazitoa,tatizo ile yako mbuzi.
Usanii yazidisha,longo longo wazi wazi.
Agenda umeiweka,utu pemwelekeo Gwiji wewe kijijini.
 
Ndugu yangu nakujibu, ni mbuzi haikuni.
Nazi inakunika, ila Lijibuzi ndio halikuni.
Tumeinoa mpaka tumechoka, lijibuzi bado halikuni.
Mbuzi isiyokuna nazi, bora kulipilia mbali.

Tumechoka kusubili, mbuzi isiyokuna nazi.
Kilichobaki kwa sasa, bora kulitupilia mbali.
Nazi zimechoka kusubiri, sasa zalalamika waziwazi.
Mbuzi isiyokuna nazi, bora kulipilia mbali.
 
Ndugu yangu nakujibu, ni mbuzi haikuni.
Nazi inakunika, ila Lijibuzi ndio halikuni.
Tumeinoa mpaka tumechoka, lijibuzi bado halikuni.
Mbuzi isiyokuna nazi, bora kulipilia mbali.

Tumechoka kusubili, mbuzi isiyokuna nazi.
Kilichobaki kwa sasa, bora kulitupilia mbali.
Nazi zimechoka kusubiri, sasa zalalamika waziwazi.
Mbuzi isiyokuna nazi, bora kulipilia mbali.


nnasemaje
hio mbuzi inakuna na kama hamuamini ptisha mkono kama hutochurizika damu.

unafanya mchezo hapa eeh.

hio mbuzi ya shamba si kukunia tu bali hata kufua nazi inafua, wengine huiita kifulio
 
Labda ni mbuzi butu, hiyo isokuna nazi,
Labda ni yenye kutu, yashindwa kufanya kazi,
Labda ni ile iso kwatu, jukumu hailiwezi,
Nazi mbona zimevunjwa, na maji yamemwagika?

Uzuri wa mbuzi kazi, si rangi wala uzuri,
Uzuri ni kwenye pozi, watu wafunga safari,
Watu wamwaga machozi, ikikuna bila shari,
Nazi mbona zi tayari, tatizo la mbuzi nini?
 
Niliiomba agenda,kwenda nnje sikutamani.
Sasa nimepata kenda,humo nataka barizi.
Fasihi umeiweka,kilaumu yako mbuzi.
Jamaa wanashaa,kichungua za nyumbani.
Mke aniuliza,je ile ile yake mbuzi.
Jikoni iking'aa,ama ile andamizi.
Mbona ile inafaa,anijibu la aziz.
Au yule twamfuga,hofu hana kwenye zizi.
Linanipiga butwaa,akiri majibu yayamaizi.
Kigano amekitwaa, anenaye huyu mbuzi.
Mifano nimeitoa,amjue wako mbuzi.
Akili imempaa,mke wangu bumbuwazi.
Anasema hili jaa,haifai hii mbuzi.
Aongeza ni balaa,kote bara na visiwani.
Wasi sina nimekaa,azisema hizi mbuzi.
 
nnasemaje
hio mbuzi inakuna na kama hamuamini pitisha mkono
kama hutochurizika damu......unafanya mchezo hapa eeh.....


Mkono kipimo tosha, wa Pwani amebaini
Tajua mumechemsha, kwa mbuzi mtabaini
Makali yake yatosha, kujua mbuzi ni nani
Mkono kipimo tosha, makali yake kujua!

Nasema pokea tano, wa kwetu mtu wa pwani
Nakupa huo mkono, umeshinda kilaini!
Kipimo bora mkono, makali kujuliani!
Mkono kipimo tosha, wabishi mkitumie!

Msilaumu ndoano, kutovua baharini
Wale samaki wa pono, wanaingia mitini
Kwani hutonoa tono!, waviziapo chamboni!
Mkono kipimo bora, makali yake kujua!
 
Pole mwanakwetu, kwa yako maswahibu
Kama ni hiyo kutu, isugue kutoa aibu
na kama ni ukurutu, hapo sina jawabu
iweje isikune nazi, na hali ni kazi ya mbuzi?

Usiseme kwa sauti, mbuzi haikuni nazi
iweje isikune nazi, na hali ni kazi ya mbuzi?
Ni ngumu kuamini, ukweli huu utaleta simanzi
Iweje isikune nazi, na hali ni kazi ya mbuzi?

Raha ya mbuzi, ni kukuna nazi
raha ya nazi, ni kukunwa na mbuzi
hata kwa wingi wa nazi, hii ni moja jukumu la mbuzi
iweje isikune nazi, na hali ni kazi ya mbuzi?


Nina wasiwasi na yako mbuzi, yangu haina ajizi
labda ni wako ujuzi, ndio maana haikuni nazi
chelea chelea wapagazi, watabeba na yako mbuzi
mbuzi hunolewa kwa mapenzi, hakika itafanya kazi
 
Bimkubwa napenda kujua,ukubwani nimewadia,
wapi ulipotelea, utamu leo watufunulia,
foramu kupotelea, wenyeji mkatukachia,
mazoea nayataka, kwako leo kunifafanulia

Rubani nilipotea, ubinafsi maswali mbele,
kundini natembelea, mbuzi kafungwa kengere,
Stivini kalowea, ufundi mbelembele,
mbuzi itanolewa, maridadi kama Pele

Ubeti naongeza, mbuzi n'sha ijulia,
kuketi kunadoda, mjuzi napalilia,
cheti nimeopoa, upembuzi wanukilia,
mengi yaningoja, mbuzi kuitunukia

SteveD. (Mwangwi wa Handaki)
 
wajuaje kuwa haikuni, wakati haijawahi kukuna naziyo
unasimanga mbuzi bure, bila ya kuuliza kwa wenzio
ningekushauri uliza, kwa waliowahi tumia mbuzi hiyo,
mbuzi hii ni safi kabisa, tena yakuna mbio mbio

kwa nini usilete naziyo, uone jinsi mbuzi ikunavyo
hakika utaridhika, nazi yako itakunika ipasavyo
tui la naziyo litachujika, litatoka utakavyo
mbuzi hii ni safi kabisa, tena yakuna vilivyo

mengi sisemi, mbuzi sitaki isifia
wewe leta naziyo, siku ukijisikia
itakunwa ikunwavyo, hakika utafurahia
mbuzi hii ni safi kabisa, kombe imejishindia
 
Mbuzi mwaisifia, kupalilia iliyo uchwara,
maridadi kujitambia, ileteni kwangu kipara,
somo nitaipatia, itambue mimi wa bara,
mbuzi naiulizia, niinoe kibarabara

Mbuzi nitaichoma, kuichuna utamu ndafu
makeke kujinoma, kuipekecha nyama dafu,
wa-pwani kuikoma, wa-bara tu-marudufu,
mbuzi naiulizia, niinoe kibarabara

SteveD. (Mwangwi wa Handaki)
 
Back
Top Bottom