Mbunge Kilasi amwaga fedha, baiskeli jimboni

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,082
Kilasi.jpg

Mbunge wa Mbarali, mkoani Mbeya, Esterina Kilasi (CCM).



Mbunge wa Mbarali, mkoani Mbeya, Esterina Kilasi (CCM), amezua mjadala na malalamiko kutoka kwa wanachama na viongozi wa chama hicho katika wilaya hiyo, baada ya kuwamwagia makatibu wa siasa na uenezi wapatao 11 wa jimbo hilo Sh. 100,000 kila mmoja watakazozitumia kama nauli ya kwenda kutembelea Bunge mjini Dodoma mwezi ujao.
Kilasi amekuwa ni mbunge wa pili wa CCM kulalamikiwa na wananchi na wanachama wa CCM kwa kutoa fedha kwa viongozi wa chama ngazi ya kata katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu, hatua ambayo inatafsiriwa kuwa ni rushwa.
Mbali na Kilasi kutoa kiasi hicho cha fedha kwa makatibu wa siasa na uenezi, pia aligawa baiskeli kwa makatibu kata 11 wa CCM wa jimbo lake ili ziwarahisishie kufanya kazi za chama kwenye kata zao katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Katibu wa CCM Wilaya ya Mbarali, Zacharia Bageorge, alithibisha mbunge huyo kutoa fedha na baskeli na kufafanua kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya alipofanya ziara ya kutembelea wilaya hiyo makatibu kata walimuomba baiskeli ambapo Katibu wa Siasa na Uenezi, Bashir Madodi, alikwenda kumwambia mbunge atoe msaada huo kwa niaba ya chama mkoa.
Bageoge alisema kimsingi, Kilasi hajafanya kosa kutoa msaada huo kwa sababu ni moja ya majukumu yake ya utekelezaji wa ahadi zake alizoahidi mwaka 2005. Mbunge wa kwanza kulalamikiwa alikuwa ni Mbunge wa Rungwe Magharibi, Profesa David Mwakyusa, ambaye kwa upande wake alimwaga fedha taslimu Sh. 500,000 kwa kata 10 za jimbo lake zisaidie kuimarisha chama, hali iliyozua mjadala mkali kutoka kwa wananchi na wanachama wa CCM wa Wilaya ya Rungwe.
Akizungumza na Nipashe kwa simu, Kilasi alithibitisha kutoa kiasi hicho cha fedha pamoja na baiskeli kwa viongozi hao wa chama wa kata na kwamba kufanya hivyo haimaanishi kuwa amefanya kosa, bali ni sahihi kwa sababu yeye bado ni mbunge aliyoko madarakani ambaye anaruhisiwa kutoa misaada kwa chama na viongozi wake.
“Ni kweli makatibu wa uenezi nimewapa Sh.100,000 ambazo zitawasaidia kwenda bungeni Dodoma kutembea na kujifunza, nilishawahi kuwapeleka makatibu kata kutembea Dodoma: Sasa zamu hii ni ya makatibu wa uenezi,” alisema Kilasi ambaye hata hivyo, hakufafanua mambo ambayo viongozi hao watakwenda bungeni kujifunza.
Alisema watu wanaolalamika hawana hoja na kwamba kama wanaona amefanya kosa kutoa msaada huo waende Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Mkamba, ili waelezwe utaratibu ulivyo ndani ya chama hicho tawala.
Mbunge huyo alisema misaada anayoitoa kwa viongozi hao wa CCM wa kata ni utekelezaji wa ahadi alizoziahidi wakati anagombea ubunge mwaka 2005 na kwamba haoni kama kuna kosa wakati yeye bado ni mbunge halali wa Mbarali hadi hapo Bunge litakapovunjwa.
Kilasi alisema wanaolalamikia misaada anayoitoa ni wapinzani wake, ambao wanataka kugombea ubunge katika Jimbo la Mbarali na kwamba anawashangaa kwa sababu baadhi yao wamekuwa wakifanya vikao vya siri na kuwahonga watu ili ikifika wakati wa uchaguzi wawachague. “Wanaolalamikia mambo hayo ni wanachama wanaotaka kugombea ubunge, lakini mbona wao wanagawa kalenda na fedha kwa wanachama wa CCM na viongozi, lakini nimetulia kimya,” alisema Kilasi na kuongeza: “Hata hivyo, hali ikizidi itabidi niwashitaki.”
Alisema wabunge waliopo madarakani wataendelea kutekeleza ilani ya CCM mpaka hapo Rais Jakaya Kikwete atakapolivunja Bunge na kwamba kwa hali hiyo hawezi kuacha kutoa misaada katika jimbo lake na hakuna anayeweza kumzuia.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom