Mbunge CHADEMA aibua Deci bungeni; NAIBU Waziri wa Fedha, Gregory Teu, ameshindwa kujibu swali

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Imeandikwa na Shadrack Sagati, Dodoma; Tarehe: 29th June 2011

NAIBU Waziri wa Fedha, Gregory Teu, leo ameshindwa kujibu swali lililomtaka aeleze hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusu maofisa walioshindwa kutekeleza wajibu wao hadi taasisi ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI) ikafanya shughuli zake kinyume cha sheria.

Swali hilo liliulizwa na Mbunge wa Kawe Halima Mdee (Chadema) ambaye awali aliuliza swali la msingi kuhusu DECI.

Katika swali hilo la nyongeza, Mdee alisema, DECI ilifanya shughuli zake kwa miaka mitatu za kuchukua amana za wananchi bila kuwa na kibali cha kufanya hivyo.

“Serikali inatoa kauli gani juu ya maafisa wake ambao walikuwa wanajua suala hilo lakini hawakuchukua hatua zozote? alihoji Mdee.

Katika swali lingine la nyongeza Mbunge huyo aliuliza kuwa, kwa kuwa fedha zinazoshikiliwa ni za wanachama na waliofanya uhalifu huo ni watu watano, na kwa vile thamani ya fedha inashuka kwa nini wanachama ambao hawakuwahi kuvuna hata mara moja wasikabidhiwe fedha hizo?

Katika majibu yake alisema: “Fedha zinazodaiwa na wanachama ni nyingi wakati fedha zilizoko kwenye akaunti za wakurugenzi ni kidogo.”

Baada ya kujibu hivyo alienda kukaa ndipo Spika wa Bunge Anne Makinda akamkumbusha kuwa hajajibu sehemu nyingine ya swali hilo kuwa maofisa wa serikali ambao walizembea hadi Deci wakaendesha shughuli zao kinyume cha sheria wamechukuliwa hatua gani?

Ndipo Naibu huyo aliporudi kwenye eneo la kujibia na kusema “Nafikiri walikuwa bado hawajaandikishwa,” alisema naibu waziri huyo na kuwafanya wabunge kuangua kicheko.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge huyo, Teu alisema Serikali haijachukua fedha za Deci bali fedha hizo, Sh bilioni 14.81 zimezuiliwa katika akaunti zilizomilikiwa na wakurugenzi wa Deci katika benki mbalimbali nchini.

Katika swali hilo Mdee alitaka kufahamu hatma ya fedha za wananchi. Alisema fedha hizo ni asilimia 37.77 ya ambazo zinadaiwa na wanachama wa Deci ambazo ni Sh bilioni 39.3.

Alisema, uamuzi wa kuzizuia uliotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikiwa ni hatua mojawapo ya uchunguzi dhidi ya Deci ambayo ilikuwa inaendesha mchezo wa upatu.

“Napenda kuliarifu Bunge lako kuwa kesi ya Deci iliyofunguliwa mwaka juzi katika mahakama ya Kisutu inaendelea kusikilizwa,” alisema Teu na kuongeza: “Hivyo hatma ya fedha hizo za wananchi itategemea hatma ya kesi hiyo kwani Deci ilikuwa na matawi 40 katika mikoa 18 ya Tanzania Bara”.

Alisema, usikilizwaji wa mashahidi wa Dar es Salaam umekamilika na hatua za kuwapata mashahidi kutoka mikoa mingine zimeanza.

Alisema, Deci ilikuwa na wanachama 649,859 na sehemu ya wanachama hao watahitajika kutoa ushahidi mahakamani.
 
Kwa tz ukiwa wazr umeula ndo maana utawaona siku ya kuapishwa wanaambatana na familia zao na wapambe wao wanaenda kujipongeza.Baada ya hapo ni kwenda bungeni KUDANGANYA WANANCHI NA BUNGE.Angalau sasa hv wameanza kubanwa ndo vichekesho vinajitokeza. Kwa wazungu ukiwa waziri si nafasi ya kufurahia sana kwa sababu utatumika
 
Back
Top Bottom