Mbunge amshangaa Waziri Mkuchika kwa kupindisha ukweli wa Gazeti Mwananchi

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,720
21,779
Mbunge amshangaa Waziri Mkuchika kwa kupindisha ukweli wa Gazeti Mwananchi





Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo,George Mkuchika, ambaye anamshangaza Mbunge wa Chadema, Dr Wilbrod Slaa, kwa kupindisha ukweli kuhusu kuzomewa kwa makada wa CCM katika kampeni za uchaguzi mkoani Mwanza.

Na Kizitto Noya

KATIBU mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amehoji uadilifu wa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika na kumtaka aeleze tatizo alilonalo dhidi ya gazeti la Mwananchi kiasi cha kulituhumu kusema uongo kutokana na kuripoti habari ya kuzomewa kwa viongozi wa CCM.


Mwananchi iliripoti habari za kuzomewa kwa makamu mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa na kada wa chama hicho, John Malecela wakati walipokuwa kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika Nyarugusu.


Baada ya kusoma habari hiyo, Dk Slaa alipiga simu ofisi za Mwananchi jana na kueleza kushangazwa na kitendo cha Mkuchika, ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa CCM na kumtaka Mkuchika asichanganye ushabiki wake wa kisiasa na dhamana ya uongozi aliyopewa.


"Mkuchika aache kuupotosha umma. Hatumzuii kuwa shabiki wa siasa, lakini ushabiki wake usivuruge uwajibikaji wake katika dhamana tuliyompa," alisema Dk Slaa na kuongeza:


"Katika hili ni vyema akawa wazi kusema ana tatizo gani na gazeti la Mwananchi. Aseme kama ana shida na mwandishi wa habari ile au nguvu ya gazeti lenyewe kwani kilichoripotiwa ni sahihi tena kiliripotiwa na vyombo vingi vya habari, na sio Mwananchi peke yake."


Dk Slaa alisema Malecela na Msekwa walizomewa katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea katika jimbo la Busanda kama ilivyoripotiwa na wananchi wana haki ya kujua kama walivyokuwa na haki kujua namna yeye (Dk.Slaa) alivyozomewa bungeni.


"Kwa nini Dk. Slaa alipozomewa bungeni hakuitisha press Conference (mkutano na waandishi wa habari) na kuvikanya vyombo vya habari? Kwa nini wakizomewa wapinzani iwe sahihi, lakini ikizomewa CCM ni kuvunja sheria," alihoji.


Mbali na Msekwa na Malecela, mgombea wa chama hicho katika uchaguzi huo mdogo wa jimbo la Busanda, Lolencia Maselle Bukwimba na mumewe Maselle Buziku, walizomewa wakati walipotambulishwa kwenye mkutano huo wa kampeni.


Tukio hilo limetokea siku moja baada ya chama hicho kujikuta kikiwa na watu wachache wakati wa mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni zake kwenye kata ya Kaseme. Vyama vya upinzani vya Chadema na CUF vimekuwa vikisomba watu.


Pamoja na kukanusha, viongozi wa CCM wamekaririwa wakisema kuwa Chadema imekuwa ikituma vijana wake kwenye mikutano ya CCM ili wawazomee viongozi na kufanya fujo.


Dalili za hali mbaya katika mkutano huo zilianza wakati viongozi hao wakiingia eneo la Nyarugusu ambalo ni maalumu kwa wachimbaji wa dhahabu. Viongozi hao walipokelewa kwa alama ya vidole viwili kila walikopita. Alama ya vidole viwili hutumiwa na Chadema.


Zomea zomea hiyo iliwakabili viongozi hao wa CCM wakati walipokuwa wakimnadi mgombea wao. Hali mbaya ilianza kwa katibu mwenezi na uhamasishaji, Simon Mangelepa wakati aliposimama jukwaani na kuanza kutambulisha wageni walioambatana nao na kufuatiwa na mbunge wa viti maalum mkoani Mwanza, Maria Hewa ambaye alizomewa baada ya kuwaeleza wananchi kuwa wanapaswa kutulia.


Kutokana na hali hiyo mwenyekiti wa CCM mkoani Mwanza, Clement Mabina alisimama jukwaani kabla ya kumkaribisha Malecela ili amnadi mgombea wa chama hicho na kuwaeleza kuwa anazo taarifa kuwa kuna watu ambao wamepangwa hapo kwa ajili ya kuzomea, naye akazomewa.


Ndipo ilipofika zamu ya Msekwa kumnadi mgombea na baada ya kupanda jukwaani alimkaribisha mgombea ambaye naye alimsimamisha mumewe, Maselle Buziku, ambaye naye alitamba kuwa wakimchagua atatumia nafasi yake kwenye taasisi ya SEDA kuhakikisha wanapata mikopo, lakini akajikuta akizomewa.
 
Busanda kama Tarime vile....CCM wajiandae kuiba ama la wakishindwa baaasi tena wameula wa chuya
 
Back
Top Bottom