Mbeya: Polisi aliyeua mwanafunzi atiwa mbaroni!

kipusy

JF-Expert Member
May 7, 2010
639
321
Askari polisi anayetuhumiwa kumuua mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU) kilichopo jijini Mbeya, ametiwa mbaroni na kuwekwa rumande katika kituo kikuu cha polisi kati.

Habari zilizopatikana kutoka katika kituo hicho cha mkoa, zimedai kuwa askari huyo, (jina tunalihifadhi), amewekwa rumande kituoni hapo siku ya tatu sasa wakati tuhuma za mauaji dhidi yake zikiendelea kufanyiwa uchunguzi.

"Ni kweli askari mwenzetu yupo hapa amewekwa rumande baada ya tukio la mauaji ya mwanafunzi lililotokea hivi karibuni," alisema askari mmoja aliyetaka jina lake lisitajwe kwa kuwa si msemaji wa Jeshi la Polisi wakati akizungumza na NIPASHE kwa simu jana kutoka kituoni hapo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, jana hakupatikana kuzungumzia habari hizo, simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa hadi tunakwenda mitamboni.

Mwanafunzi huyo, Daniel Godluck Mwakyusa (31), anadaiwa kuuawa na askari huyo kwa kumpiga risasi sehemu kadhaa za mwili wake akimtuhumu kuwa ni jambazi katika tukio lililotokea Februari 14, mwaka huu.

Askari anayedaiwa kufanya mauaji hayo ambaye alikuwa na wenzake wakifanya doria, inadaiwa kuwa baada ya kumuua mwanafunzi huyo, walimpora fedha Sh. 300,000 pamoja na simu ya mkononi.

Juzi Kamanda Nyombi akizungumza na NIPASHE kwa simu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi wa tukio hilo umeanza na kuongeza kuwa ukikamilika, jalada litapelekwa kwa Wakili wa Serikali ambaye ndiye ataamua kama suala hilo lipelekwe mahakamani au la.

Habari zilizopatikana awali zinadai kuwa mwanafunzi huyo alipigwa risasi na askari baada ya kuwakuta na wanafunzi wenzake wakipata vinywaji katika moja ya baa jijini Mbeya.

Habari kutoka eneo hilo zinadai, polisi hao baada ya kuwakuta wanafunzi hao, yalitokea majibishano baada ya kuwatuhumu kuwa ni majambazi, hali iliyomlazimisha askari aliyekuwa na bunduki aina ya SMG kufyatua risasi na kumuua Mwakyusa.

Habari zaidi zinadai kuwa askari hao baada ya kumuua mwanafunzi huyo, walimpora fedha hizo na simu ya mkononi.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, baada ya askari kudaiwa kufanya mauaji hayo, walichukua mwili wa marehemu na kuupeleka Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na kuwaeleza wauguzi na wahudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti kwamba wameokota mwili wa jambazi.

Kwa mujibu wa watoa habari wetu, wahudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti walielekezwa kwamba kwa sababu mwanafunzi huyo hafahamiki jina, maiti yake iwekewe lebo, ingawa alikutwa na vitambulisho vinavyoonyesha kuwa ni mwanafunzi wa TEKU na polisi inadaiwa walivificha.

Habari kutoka hospitalini hapo zinadai kuwa, mwili huo ulipelekwa katika chumba cha kufanyia uchunguzi na inadaiwa kuwa ndugu wa marehemu hawakuruhusiwa kuingia, badala yake walikuwepo polisi na Mwanasheria wa Serikali pekee yao.
Kutokana na mwanafunzi huyo kuuawa katika mazingira ya kutatanisha, Jeshi la Polisi lilitoa usafiri wa gari lenye namba za usajili T 138 AFK aina ya Toyota Coaster kwa ajili ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Kyela kwa mazishi, baada ya uchunguzi wa daktari kuthibitisha kuwa aliuawa kwa kupigwa risasi.

Baba mzazi wa marehemu huyo, Pastory Mwakyusa, aliliambia NIPASHE kuwa amesikitishwa sana na mauaji ya mtoto wake kwa kuwa hakuwa na tabia ya wizi wala ujambazi. Aliiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina kwa lengo la kubaini sababu za kuuawa kwa mtoto wake.
CHANZO: NIPASHE, 23rd Feb, 2012
 
Police ni watu wabaya sana,nchi zingine police ni watu wa kulinda usalama wa raia na mali zao,lakini hapa kwetu police ndio wahalifu wa kwanza,wanafanya mauaji ya raia wema na kupora mali zao lakini hawawajibiki,na wakubwa zao wako kimya tu sijui wanafurahia?Jeshi la police hatuna imani nalo kabisa ni bora ukutane na simba kuliko police.
 
Inauma sana kazi ya polisi wa tz ni kukamata na kuwauwa ambao hawausiki na kuwasakizia mikosa yasiyo yao. Tutafika tu.
 
Si ajabu ukichunguza hapo chanzo wanagombania mwanamke na huyo askari amefanya makusudi kumdelete mume mwenzake kuondoa upinzani!!
 
kwa nini tunaua binadamu wenzetu jamani! tuwe na huruma na maisha ya wenzetu. poleni wafiwa! naomba hao polisi washitakiwe bila huruma maana tabia ya kulindana ndio inalea mambo haya!
 
:A S embarassed: inauma sana jamani....hii nchi ni kama uchafu dampo.... hatuna serikali
 
Back
Top Bottom