Mbaroni kwa kukutwa na bunduki, risasi 10

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
POLISI mkoani Arusha wamewakamata watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na bunduki aina ya Rifle ikiwa na risasi 10 wilayani Longido.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na jeshi hilo mkoani hapa, umebaini kuwa silaha hiyo ilitumika katika tukio moja la utekaji wa magari ya wafanyabiashara maarufu mkoani hapa.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Thobias Andengenye amesema watu hao walikamatwa juzi saa 8.45 usiku katika eneo la mbuga nyeupe Kata ya Engikareti wilayani Longido.

Kamanda Andengenye amewataja wao kuwa ni Tolomayani Salievo (50) mkazi wa Namanga pamoja na Senu Most (29) mkazi wa Sombetini jijini Arusha, ambapo walikamatwa kutokana na doria iliyofanywa na polisi.

Alisema bunduki hiyo ilikuwa imefutwa nambari zake za usajili ambapo ilikuwa na risasi 10 ndani yake huku akibainisha ya kuwa polisi inachunguza kwa kina umiliki wa silaha hiyo.

Hata hivyo, Andengenye alisema polisi katika uchunguzi wa awali, imebaini ya kuwa silaha hiyo ilitumika katika utekaji wa gari mojawapo la wafanyabishara lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita mkoani hapa.

“Tayari uchunguzi wa awali tumebaini ya kuwa hii silaha ilitumika katika tukio la utekaji wa gari la wafanyabiashara wawili lililotokea wiki iliyopita mkoani Arusha hivyo bado tunachunguza kwa kina hata hivyo,” alisema Andengenye.

Katika tukio jingine, Kamanda Andengenye alisema mkazi wa Mianzini, Robert Lomayani (55), amefariki baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani usiku wa kuamkia leo.

Mtu huyo alijinyonga saa 8.30 usiku ambapo alimuaga mkewe kuwa anaenda nje kujisaidia, lakini katika hali isiyo ya kawaida, alikawia kurejea ndipo mkewe, Juliana Robert alitoka nje ili kujua nini chanzo.

Kamanda Andengenye alisema baada ya mkewe kutoka nje ya nyumba wanayoishi alimuona mumewe akining’inia kwenye mlango mkuu wa kuingilia na aliposogea karibu kujua chanzo, alibaini ya kuwa tayari alikuwa ameshakata roho. Mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
 
Back
Top Bottom