Mawaziri wa JK watia aibu

Selous

JF-Expert Member
Jan 13, 2008
1,325
144
Wavamia makampuni makubwa kuomba fedha za kampeni

na Mwandishi Wetu


IKIWA imebaki siku mbili kabla ya kuanza mwaka mpya, homa ya uchaguzi mkuu mwakani inazidi kupanda huku baadhi ya wagombea wakiwemo mawaziri wakihaha kusaka fedha kwa ajili ya kugharamia kampeni zao.
Homa hiyo imesababisha baadhi ya mawaziri kuvamia ofisi za wawekezaji wa makampuni makubwa pamoja na wafanyabiashara maarufu nchini, kuomba fedha kwa ajili ya kugharamia uchaguzi huo.
Mbali ya mawaziri, wengine wanaopita kwenye makampuni ya wawekezaji wakubwa kuomba fedha za kampeni za uchaguzi ni pamoja na wabunge wa sasa wanaotaka kutetea majimbo yao na baadhi ya watendaji wanaotarajia kustaafu serikalini.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano, umebaini kuwa makampuni na wawekezaji wakubwa wanaosumbuliwa na wanasiasa hao, ni pamoja na yale yenye migogoro na jamii au serikali ambapo mawaziri na wanasiasa hao hujiingiza kwa nia ya kutaka kuwasaidia.
Mbali ya makampuni yenye migogoro na jamii, mawaziri hao pia huyaomba msaada wa kifedha makampuni mengine makubwa nchini, hali ambayo imeelezwa kuwa kero.
Kwa mujibu wa habari hizo, moja ya kampuni zenye mgogoro katika jamii na ambayo imekuwa ikisumbuliwa sana ni ya kuchimba madini ya Barrick.
Vyanzo vyetu vya habari kutoka ndani ya Barrick, vinasema baadhi ya mawaziri na wabunge, wamekuwa wakitumia mgogoro wa kampuni hiyo kuhusishwa na utiririshaji wa maji ya sumu kwamba wana uwezo wa kuumaliza.
“Hiyo ni kweli kabisa wanasiasa wanapigana vikumbo kutaka hela. Wengi wanakuja kwa gia ya kutaka kuisaidia kampuni, wakiahidi kule bungeni watasimama kidete kututetea, lakini nao wanataka wasaidiwe pesa kwa ajili ya miradi yao ya jimbo na wanaomba pesa nyingi,” alisema mmoja wa maofisa wa Barrick.
Kwa mujibu wa habari hizo hali hiyo imewafanya baadhi ya wakurugenzi wa kampuni hizo wawe na namba zaidi ya moja za simu ili kukwepa usumbufu wa wanasiasa hao wenye uchu wa kurudi madarakani kwa kutumia pesa.
Kampuni ya kupakia na kupakua makontena ya TICS, ambayo hadi sasa bado iko kwenye mgogoro mkubwa na serikali, nayo imekuwa ikiandamwa kuombwa misaada na wanasiasa hao.
Mmoja wa viongozi wa juu wa kampuni hiyo, ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema ni jambo la kawaida kwa kampuni yake kuombwa misaada ya fedha na wanasiasa.
“Hatuwezi kutaja majina ya mawaziri na wabunge waliotuomba msaada, lakini wapo, baadhi tumewasaidia ingawa wakati mwingine si kwa kiwango walichoomba, na hadi sasa maombi yaliyopo mezani ni mengi,” alisema ofisa huyo.
Kampuni za bia nchini; TBL na Serengeti Breweries (SBL) na kampuni za simu za mkononi ni sehemu ya makampuni mengine yenye maombi lukuki ya misaada ya fedha kutoka kwa mawaziri na wabunge.
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima Jumatano imezipata kutoka kwa viongozi wa juu wa kampuni hizo, zinasema hali hiyo imekuwa kero kwao na baadhi wamefikia hatua ya kumwandikia Spika wa Bunge Samuel Sitta kulalamikia hali hiyo.
Hata hivyo, Spika na katibu wake hawakuweza kupatikana jana kuthibitisha kama wamewahi kupata malalamiko kutoka kwa baadhi ya makampuni nchini kuhusu hali hiyo.
Akizungumzia kuwapo kwa hali hiyo, Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), alikiri kuwapo kwa hali hiyo kwa wanasiasa na kuwataka wapanue wigo wa kupata pesa kwa ajili ya majimbo yao badala ya kuomba kwenye makampuni.
“Hii ni aibu na ndiyo maana mimi nimejitahidi kupanua wigo wa kuwa na marafiki nje ambao wanaweza kukusaidia. Kwa mfano hivi karibuni nimepata msaada wa magari mawili ya wagonjwa kutoka kwa rafiki zangu nchini Uingereza, na wengine pia wapanue wigo,” alisema Chegeni.


Source: Tanzania Daima
 
Ukienda IPP Media kwa Mengi pia utakuta lundo la Wabunge wameomba huko. Hapo bado Rostam, Manji na matajiri wengine

Wanasiasa wetu kila mmoja wao anategemea wafanyabiashara ili kuokoka jimboni, ni aibu kweli kweli.
 
Kuna mtu wa kampuni ya sigara (TCC) aliniambia kwamba kuna kundi la wabunge walienda kutembelea kiwanda hicho pamoja na kwamba wengi wao hawakuwa wavutaji hata hivyo waliomba na kupewa sigara nyingi tu. Walizipeleka wapi? Your guess is good as mine! Wabunge wetu ni kama watoto wa shule kitabia.
 
Kuwategemea wabunge na mawaziri wa namna hii watakuwa fair katika kufanya mambo yao sio rahisi. Kwani ni lazima watakuwa biased kwa watu walio wasaidia au kutowasaidia na wao wakiamini kwamba wana uwezo wa kufanya hivyo. Ndio maana wengi wao hawako huru sababu ya u omba omba wao.
 
Back
Top Bottom