Mauaji ya Polisi

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,315
33,111
Songeafujo(1).jpg

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa Ruvuma wakimshikilia mmoja wa vijana waliodaiwa kuandamana kinyume cha sheria mjini Songea kupinga mauaji ya raia.


Damu ya raia imemwagika tena baada ya polisi kufyatua risasi za moto kukabiliana na waandamanaji katika mji wa Songea mkoani Ruvuma na kuua watu watatu, kujeruhi zaidi ya 20 na wengine zaidi ya 56 kukamatwa.
Tukio hilo lililotokea jana asubuhi mjini hapa lilisababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa Manispaa ya Songea hasa kutokana na mabomu ya machozi yaliyorushwa kuwatawanya wakazi wa mji huo ambao walikuwa wamekusanyika karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kupinga mfululizo wa matukio ya mauaji ambayo yametetemesha mji wa Songea katika siku za hivi karibuni.
Kabla ya maandamano ya jana, kulikuwa na matukio matano ya mauaji ya kutisha yaliyosababisha baadhi ya wananchi kuandamana bila kibali kwenda kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Songea, Thomas Ole Sabaya Februari 20, mwaka huu baada ya idadi ya watu waliouawa katika mazingira ya kutatanisha kufikia watano.
Katika kilio chao walichokitoa mbele ya mkuu huyo wa wilaya, wananchi hao walisema kuwa hali ya mauaji hayo inazidi kuongezeka siku hadi siku, hali ambayo imewafanya waishi kwa hofu kiasi kwamba baadhi ya watoto wao wanashindwa kwenda shule kutokana na hofu.
Walimweleza kuwa baadhi ya wazee wamekuwa wakilazimika kujifungia ndani ya nyumba zao kwa hofu inayotokana na kasi hiyo ya matukio ya mauaji. Baada ya kuelezwa malalamiko hayo, Sabaya aliwaomba wananchi hao wawe watulivu wakati Serikali kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wakichukua hatua za kuwatambua wahusika wa mauaji hayo.
Aidha, Sabaya aliwaahidi wananchi hao kuwa hatua nyingine ya kushughulikia tatizo hilo ingekuwa ni kuwakutanisha viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya mtaa, kata na wilaya.
Wakati taratibu hizo zikiendelea kufanywa, juzi usiku yalitokea mauaji mengine ya mtu mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika na mwili wake ulikutwa ukiwa umetupwa kwenye maji katika eneo la Matarawe-Bombambili mjini hapa. Hali hiyo ilizidisha hasira za wananchi hao na kuamua kuandamana jana mpaka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambayo iko eneo moja na ofisi ya Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma. Hali hiyo iliyosababisha ofisi zote kutumia walinzi waliokuwepo
kufunga mageti ili kuzuia umati mkubwa wa watu uliokuwa umezingira huku wengine wakirusha mawe.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi lililazimika kuingilia kati kwa kutumia mabomu ya machozi kwa ajili ya kuwatawanya wananchi, lakini wananchi walikaidi amri na kuendelea kurusha mawe dhidi ya askari, hali iliyowalazimu askari kutumia risasi za moto.
Mapambano baina ya wananchi hao na polisi yalisababisha vifo vya watu wawili waliouawa kwa risasi za moto na miili yao kuhifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma mjini Songea.
Mauaji hayo yalitokea katika eneo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa nje ya ukumbi wa mikutano wa Songea Club majira ya saa 3:45 asubuhi ambako askari waliokuwa na silaha walikuwa wakiwataka wananchi hao waingie ndani ya ukumbi kwa ajili ya kuzungumza na viongozi wa serikali ya mkoa, lakini hawakuwa tayari kuingia kwenye ukumbi huo kwa kuhofia kukamatwa.
Badala yake, wananchi hao waliendelea kuwarushia polisi mawe na magari mengine ya serikali yaliyokuwepo eneo hilo.
Jana shughuli zote za kiuchumi zilisimama katika mji wa Songea kuanzia asubuhi saa 3:30 kwa siku nzima.
KAULI YA RC
Tukio hilo liliwasababishia hofi wakazi wa mji wa Songea huku Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, akisema kuwa Serikali itahakikisha inashirikiana na vyombo vyote vya dola, viongozi wa ngazi zote na wananchi kuhakikisha amani inakuwepo mjini Songea na mkoani Ruvuma kwa ujumla.
RPC: HAYAKUWA MAANDAMANO
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamuhanda, alisema kuwa kitendo kilichofanywa na wananchi hao hakikuwa maandamano, bali zilikuwa ni fujo ambazo zimesababisha maafa na uharibifu wa mali katika maeneo mbali mbali ya mji wa Songea.
Kamuhanda alisema kuwa wananchi hao waliharibu mali mbalimbali kwa kurusha mawe zikiwemo za watu binafsi, ofisi za serikali na vyama vya siasa.
WATU 20 WAJERUHIWA
Alisema kuwa Jeshi la Polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya, lakini hakuwatii amri hiyo ndipo askari polisi walipolazimika kutumia risasi za moto na kusababisha vifo vya watu watatu huku wakiwajeruhi zaidi ya 20.
Kamanda Kamuhanda alisema kuwa majeruhi hao walikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma na kwamba wanaendelea kupatiwa matibabu.
56 WATIWA MBARONI
Alisema kuwa mpaka sasa watu zaidi ya 56 wanashikiliwa na Polisi kuhusiana na tukio hilo na kuongeza kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk. Benedict Ngaiza, akithibitisha kupokelewa kwa miili ya watu watatu waliouawa katika tukio hilo na majeruhi ambao wanaendelea kupelekwa hospitalini hapo na kwamba idadi kamili itatolewa baadaye.
Katika tukio lingine, wananchi hao waliishambulia kwa mawe nyumba ya mkuu wa kituo cha polisi kilichopo karibu na Kituo cha Polisi Kati huku kundi lingine likizingira eneo lote la kituo hicho na ofisi za jirani ikiwemo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Mjini na kuvunja mlango na vitu mbali mbali vilivyokuwemo ndani.
Tukio hili linakumbusha mauaji mengine ya watu watatu waliouawa na polisi waliotumia risasi za moto Januari 5, mwaka jana baada ya kuwataka kutawanyika wakiwa kwenye maandamano ya kupinga uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha.



CHANZO: NIPASHE
POLISI WA KIBONGO KWA KUPENDA KUTOA ROHO ZA WATU!!!!!! KASHESHE KWELI POLISI WETU WABAYA.
 
Back
Top Bottom