Matukio ya mauaji yaibuka Zanzibar

X-PASTER

JF-Expert Member
Feb 12, 2007
11,610
1,810
na Mwandishi Wetu

KUMEIBUKA mauaji ya kutatanisha katika Manispaa ya mji wa Zanzibar ambapo katika kipindi cha wiki moja watu sita wamekutwa wamekufa akiwemo mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya Kiasia, aliyekutwa ameuawa kwa kuchomwa visu tumboni na maiti yake kutelekezwa chumbani kwake, Mtaa wa Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Mfanyabiashara huyo, Nassor Abdallah Khalfan (50), alikutwa jana chumbani kwake akiwa na majeraha makubwa tumboni yaliyosababishwa na kuchomwa na kitu chenye ncha kali na kuvunjwa mbavu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kiongozi wa Serikali ya Mtaa wa Kikwajuni, Ibrahim Ali, alisema mwili wa marehemu ulikutwa na ndugu zake, saa nne asubuhi baada ya kwenda nyumbani hapo na kukuta mlango ukiwa wazi.

Alisema akiwa nyumbani alipokea ujumbe kutoka kwa Diwani wa wadi ya Kikwajuni ambaye ni Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar kuwa kuna mauaji yametokea katika eneo lake na kumtaka kufuatilia suala hilo kwa undani.

“Nilipofika hapa kwa kweli nilishtuka baada ya kumkuta marehemu akiwa ameuawa kwa kupigwa visu vya tumbo, ” alisema Sheha wa Kikwajuni.

Kiongozi huyo wa mtaa alisema marehemu Nassor hakuwa na ugomvi na mtu isipokuwa alikuwa ni mpole na mcheshi katika kipindi chote cha uhai wake.

Alisema katika nyumba hiyo ya ghorofa moja, marehemu alikuwa akiishi peke yake na hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Yahaya Rashdi Bughi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kwa ajili ya kubaini chanzo na waliohusika na mauaji hayo.

Gazeti hili lilishuhudia madaktari wakiufanyia uchunguzi mwili wa marehemu nyumbani kwake na baadaye maiti hiyo kuchukuliwa kwa mazishi yaliyotarajiwa kufanyika katika eneo la Fuoni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Hata hivyo, watu waliofanya mauaji hayo hawakuchukua kitu chochote kutoka katika nyumba hiyo.

Habari zaidi kutoka kwa baadhi ya wanafamilia zinasema kwamba kabla ya tukio hilo marehemu alionekana na kijana mmoja wakinywa kahawa ukumbini kwake wakati ndugu yake mmoja alipokwenda kuweka mzigo wake wa simu za mikononi.

Wakati huohuo, Mohamed Abdallah Mwalimu (30) mfanyakazi wa Mradi wa Uhifadfhi wa Mazingira Kanda ya Pwani (MACEMPO), amefariki dunia usiku wa kumkia juzi baada ya kupigwa jiwe alipokuwa akiendesha pikipiki. Tukio hilo lilitokea juzi, eneo la Sogea, mjini unguja.

Tangu kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, matukio ya watu kuokotwa wakiwa wamekufu yamekuwa yakijitokeza Zanzibar na kuleta hali ya wasiwasi kwa baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Zanzibar

__________________
Habari hii inapatikana hapa: Tanzania Daima - Matukio ya mauaji yaibuka Zanzibar
 
Back
Top Bottom