Mateso ni lazima unapotafuta mwenzi wa kweli

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,314
33,108
Umeshawahi kuketi chini na kujiuliza, kama yasingekuwepo maisha yangekuwaje? Kimsingi ni swali gumu na hakuna anayeweza kulitolea jibu la moja kwa moja. Ni sawa na wanaume wanavyojiuliza kwamba wasingekuwepo wanawake wangeishi vipi.

Ninachotaka kukizungumzia leo ni kwamba mapenzi yamekuwa yakiwasumbua walio wengi katika maisha yao kiasi cha kujuta na kujilaumu kwanini walijiingiza katika uhusiano.

Wapo waliopoteza maisha, wengine wamechanganyikiwa baada ya kuathirika kisaikolojia. Kuna ndugu zetu waliopoteza kazi kutokana na kuzidiwa na mawazo. Mwandishi mmoja Saikolojia ya Uhusiano wa nchini England aliwahi kuandika kwamba Penzi ni Chungutamu (Love is Bittersweet).

Alipoandika hivyo alikuwa anamaanisha kwamba mapenzi wakati mwingine ni matamu au machungu. Yakikuendea shwari, unaweza kudhani duniani hakuna mtu mwenye amani moyoni kama wewe, lakini yatakapokuwa ndivyo sivyo, utayachukia maisha na kuyaona kama nusu jahanamu.

Pamoja na mapenzi kuleta matatizo kwa binadamu, bado mwandishi huyo alisema, uhusiano wa kimapenzi ni muhimu kwa kila binadamu mkamilifu (Love and relationship is important to every human being).

Hapo alikuwa anamaanisha kuwa hata kama umeumizwa, lakini kama umeshawahi kuonja utamu wa mapenzi, utavumilia kwa muda mchache, kabla ya kuangaza kwingine unapoona kuna uafadhali. Macho yanaona, yakishapeleka picha katika ubongo, mwili huanza kutamani.

Hata hivyo, naona ni busara niulize swali hili, Kama kila unapoingia katika mapenzi unaumizwa na mtu ambaye umempenda na ukatamani siku moja ufunge naye ndoa, kuna ulazima wa kung’ang’ania mapenzi?
Na unapong’ang’ania penzi la huyo wako anayekutesa, je italeta maana? Busara zaidi, zinahitajika katika kujibu maswali haya. Tumeumbwa na haki ya kupenda, dunia ni yetu sote kwahiyo kila mtu anastahili ëkuinjoií penzi. Hatutaki chungu wala chungutamu, tunahitaji utamu.

Kimsingi katika maisha ya sasa hasa kwa yule ambaye bado hajaolewa au kuoa, anatakiwa kuwa tayari kuumizwa kwanza, kabla ya kumpata yule mwenye mapenzi ya dhati. Ndiyo maana nikaandika ‘Mateso ni lazima unapotafuta mwenzi wa kweli’.

Mapenzi ya sasa yamejaa usanii, ukifanya uchunguzi wa haraka, utabaini kwamba watu wengi walio katika uhusiano wa kawaida yaani ‘boyfriend & girlfriend’ wanapitisha wakati, lakini uwezekano wao wa kuja kuwa kitu kimoja ni sawa na ngamia kupenya katika tundu la sindano.

Unaweza kuwa katika uhusiano na mtu akawa anakuonesha mapenzi ya kweli mpaka mwenyewe ukajiona mwenye bahati, baadaye unakuja kugundua kumbe mwenzako anakucheza shere. Inauma sana utakapobaini ‘boyfriend’ ama ‘girlfriend’ wako anakugeuza pimbi.

Sasa utajuaje kwamba huyo uliyenaye hana mapenzi ya dhati kwako? Hapo ndipo penye ngoma nzito, ndiyo maana muda mwingi tunakuwa na imani bila uhakika. Tunaamini kupitia machoni kwa sababu ya viini macho, hakuna anayeweza kupenya moyoni kujua kiwango cha mapenzi.

Napenda utambue kwamba mapenzi ya kuigiza hayawezi kudumu. Utadanyanya leo na kesho lakini ipo siku mpenzi wako atabaini kuwa amedondokea ndiko siko. Akishajua hivyo, unadhani ataendelea kukuendekeza? Akili anayo, uamuzi ataupata tu, atondoka na kukuacha solemba.

Ninachotaka kushauri ni hiki, unapotokea kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu kwa lengo la kutengeneza naye maisha, halafu mwenzako anageuka popo na kukuumiza, chukulia hali hiyo kama mwanzo wa safari yako ya kuelekea kumpata mkweli ambaye atakupenda kwa dhati.

Kuumia ni lazima, mateso hayakuanzia kwako, lakini lazima uwe na msimamo katika kusimamia ukweli. Ukivumilia kusalitiwa, baki ukijua kwamba mwenzako anakuona zoba tu. Si ajabu akawa anakutangaza hata kwenye vikao vya marafiki zake kuwa huna la kusema mbele yake. Unakubali? Dharau haifai.

Hata hivyo, baada ya kuumizwa, hutakiwi kukurupuka kutafuta mtu mwingine, kwa madai kwamba unataka kujaza nafasi hiyo. Hiyo ni mbaya, kwani unaweza kujikuta unaingia tena katika penzi chungu kuliko hata lililopita. Kaa chini jiulize, nani mkosaji, mpaka uhusiano wako ukavunjika?

Kama ni wewe lazima ujute kwanza, kisha uwe tayari kubadilika. Ukibaini kwamba halikuwa kosa lako, isipokuwa mwenzako ndiye mwenye dhambi, hilo muachie Mungu, chukulia hali hiyo kama changamoto inayokupa njia ya kumpata mwenzi wa kweli.

Hata hivyo, kuna mambo matano ambayo yanaweza kukusaidia, mara unapoachana na mpenzi wako. Ukiyazingatia ni tiba tosha kwako na wala hutokaa ukaumia.

Napenda kusisitiza, ukiachana na mwenzi wako, keti chini ujiulize zaidi ya mara mbili. Kama wewe ndiye mkosaji, jutia dhambi zako kisha uwe tayari kubadilika. Pokea yaliyopita kama changamoto ambayo si ndwele na ujipange kuganga yajayo.

Utakapobaini mkosaji ni mwenzako, wewe ni msafi angalau kwa asilimia sabini na tano, usijute. Shukuru kuachana naye kwa sababu hiyo ni hatua moja kuelekea kumpata mwenzi wa kweli. Jiamini, huwezi kumpata atakayekupenda kwa dhati kama utamng’ang’ania huyo anayekuchezea shere.

Wakati naelekeza hayo, ni vizuri nishauri kwamba si jambo jema kuachana. Jaribu kadiri uwezavyo kupigania penzi lako lisipotee, maji yakifika shingoni, basi jinasue. Mwachie Mungu, kwani atakuwa ameshaona jitihada zako na atakuongoza kumpata yule atakayetimiza njozi zako.

Nilipokuwa naelekea ukingoni kwenye gazeti la Championi Jumatatu, niliahidi kukupa mambo matano ambayo kama utazingatia, yatakusaidia kuondoa maumivu moyoni na kumsahau aliyepita. Unafikiri ni kazi ngumu? Jibu, mambo nitakayokuelekeza hapa chini ni tiba mbadala. Believe me.

MKUMBUKE KWA MABAYA TU:
Wapo wengi wameachwa na wapenzi wao lakini maisha yao bado yameendelea kuwa mazuri na Yenye furaha tele. Walichokifanya ni kusamehe na kusahau. Utabaki ukiumia kila siku endapo utakuwa unakumbuka yale mahanjam hanjama yake.

Kizuri hakikosi kasoro, mazuri yake yaweke kando na uanze kukumbuka mabaya yake moja baada ya lingine. Kufanya hivyo kutakusaidia kuzidi kumchukia badala ya kuumia na kutamani kurudiana naye. Kumbuka, safari ya maisha ni ndefu, mapenzi ni kizungumkuti.

USITHUBUTU KUONANA NAYE FARAGHA
Alikuwa mpenzi wako, mlizoeana mno, kwahiyo wakati mwingine unaweza kujisikia kama una deni moyoni la kuwa naye japo kwa mazungumzo. Chukulia hali hiyo kama hisia chafu ambazo zinataka kukufanya uusaliti uamuzi wako. Sema, sitaki kuonana naye.

Kumbuka, yeye ni kama kidonda, kuonana naye ni sawa na kukutonesha, pale ulipokuwa unaelekea kupona. Akikuita, usimtukane wala kumkaripia, mwambie kwa upole kwamba haupo tayari kuonana naye. Ukimudu kwa wiki moja, hata mwezi unaweza, ukivuka hapo ni rahisi kufikisha mwaka au kumsahau kabisa.

MHESHIMU:
Zingatia ukweli, hayo ni maisha kwa maana hiyo hata kama kakuumiza vipi, haupaswi kumgeuza ni adui yako. Wakati mwingine hutokea kwa bahati mbaya, dunia uwanja wa fujo, Shetani anazidi kuichafua na Mungu anaruhusu majaribu ili kupima imani za waja wake.

Hivyo basi, kama ulikuwa unamheshimu endelea kufanya hivyo, usibadili njia endapo mtakutana barabarani. Ukionana naye msalimie na anapohitaji msaada wako, mpe. Hata hivyo, hakikisha wakati unafanya yote, usiingiwe na hisia za kimapenzi, muone kama ndugu ama rafiki. Utashinda tu!

Wataalam wa mapenzi wanasema hivyo, lakini je, kwa mazingira ya Kibongo, ulikuwa na mpenzi wako uliyempenda, halafu akaja kukuumiza, endapo utaendelea kumsaidia, kumuonesha tabasamu lako kila mnapokutana, itakuwa inaleta maana? Mtihani gumu!

JIAMINI UTAPATA MWENZI WA KWELI:
Mapenzi ni safari, ni wachache ambao wameingia katika uhusiano wa kimapenzi kwa mara ya kwamza na kisha wakaoana. Yawezekana mpaka unakuja kumpata mume ama mke wako tayari umeshawahi kuumizwa mara kadhaa huko nyuma.

Kama huyo uliyempenda amekutosa ama wewe umemuacha baada ya kuona hakufai, basi jiamini utampata mwenzi wa kweli. Ukijenga hilo kichwani, kisha ukajiwekea utaratibu wa kusali na kumuomba Mungu akuoneshe chaguo sahihi, hiyo ni tiba kamili ya kisaikolojia.

JUKUMU LA MAISHA NI LAKO TU:
Ndiyo! Kwanini ukubali kuyaharibu maisha yako kwasababu ya binadamu mwenzako. Kama ulimpenda lakini yeye akashindwa kuthamini mapenzi yako, muache aende. Kama wewe ni msafi, basi ipo siku atajuta na kutamani arudi kwako ili atubu.

Unashindwa kula, huna njaa? Kamua msosi kadiri unavyoweza, endelea kufanya kazi zako vizuri na uache kuhuzunika. Mmeachana ona kama amekupunguzia mzigo, safisha ubongo kwa ajili ya kuanza maisha mapya. Jukumu la maisha ni lako tu na mafanikio ni yako, yapiganie.

Elewa mapenzi ni sehemu ya maisha, hivyo usiyape nafasi ya kuharibu upande mwingine. Hayo wanasema wataalam wa mambo ya mapenzi. Je, kwa mazingira yetu yalivyo, unapoachwa na mpenzi wako unaweza kula kwa raha, kulala usingizi mnono na kufanya kazi zako kwa ufasaha? Mtihani mgumu!

Nihitimishe kwa kusema kwamba inauma sana kumkosa yule uliyemtarajia kuwa mwenzi wako wa kudumu maishani, lakini hakuna furaha zaidi ya kumpata mtu mwenye mapenzi ya kweli juu yako, ingawa baadhi yetu, huingiwa na tamaa, hivyo kuwaacha wale wanaotupenda kwa moyo mmoja.

Fikiria maisha ya kudumu na mwenzako kwa maisha marefu, mfunge ndoa na mzae watoto kisha mzikane. Mlioachwa na kuumizwa poleni, lakini zingatieni somo hili. Mungu atawabariki
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom