Maswali Magumu: Hata wachache Wanashinda

Mzozo wa Mizozo

JF-Expert Member
May 26, 2008
426
12
Hata wachache wanashinda
*
Ansbert Ngurumo

ALAMA za nyakati sasa zinaonyesha kuwa walio wengi wakitetea uongo, wachache wakatetea ukweli; wachache watashinda.
Sijui kama serikali imezisoma, kuzitafsiri na kuzitafakari vizuri. Lakini dalili zinaonyesha wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameanza kuziona na kuzielewa.
Baadhi ya wabunge wa CCM wamegundua kwamba kwa muda mrefu wamekuwa wakitumika kulinda maslahi ya walio madarakani na kuwagandamiza wananchi maskini.
Kwa muda mrefu wamekuwa wasaliti kama wenzao wengi, lakini sasa wameanza kuona mwanga, na wameanza jitihada binafsi za kujinasua katika kundi la kutetea watawala wachache, kwa sababu wamegundua kwamba ukweli haukai mioyoni, vichwani wala mifukoni mwa walio madarakani.
Wameanza kung’amua kuwa ukweli na haki viko vijijini na mitaani wanakoishi wananchi wanyonge, maskini wa Tanzania katika nchi iliyojaa rasilimali nyingi zinazofyonzwa na mafisadi, wakisaidiwa na sheria, kanuni na mikataba inayowekwa na kulindwa na walio madarakani.
Tayari lipo kundi la wabunge wa CCM ambao sasa wamechoka kutetea uongo. Wametamani na wameamua kuwa wakweli, na wameanza kuonyesha cheche, kuitikisa serikali na hata kuhatarisha maisha yao binafsi.
Ni kitu gani kimeutafuna woga wao na kujenga upya dhamiri zao? Ni nguvu gani imewaingia na kuwakumbusha kuwa nchi hii si ya watawala bali wananchi, wapiga kura? Ni jambo gani limewakumbusha kuwa kazi ya mbunge si kuungana na watawala bali kuwabana, kuwahoji na kuwasimamia watekeleze wajibu wao kwa umma? Tunaweza kutilia shaka nia yao, au tunaweza kuwaunga mkono na kuwapa moyo wasirejee walikotoka.
Vyovyote itakavyokuwa, tutakapokuwa tumetafakari matukio, hali na mazingira ya kisiasa na kiuchumi ya mwaka mmoja uliopita nchini mwetu; tukielekeza macho yetu huko tunakoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka kesho na uchaguzi mkuu miaka miwili ijayo, tutapata mahali pa kuanzia kutafakari mwamko huu mpya wa wabunge wa CCM.
Tunachoweza kusema kwa sasa ni kwamba, kelele za wananchi walio wengi zimewafikia watawala na wabunge wa CCM kupitia kwa wabunge wachache wa vyama vya upinzani, ambao kwa mwaka mzima wameiweka serikali msalabani, na matokeo yake yameonekana.
Kwa mwaka mzima uliopita, serikali haikuwa na ajenda ya maendeleo, bali kujitetea dhidi ya tuhuma za ufisadi zilizoibuliwa na wapinzani bungeni na kwenye mikutano ya hadhara. Machungu ya bajeti iliyopita, yakichochewa na kauli za wapinzani, yameiweka serikali pabaya.
Wapinzani waliposema bajeti haimpi mwananchi nafuu, serikali ilisema bajeti inamkomboa mwananchi. Serikali imetumia pesa nyingi kujisafisha na kuitetea bajeti, imeshindikana. Imetumia baadhi ya wabunge wa CCM kuitetea, wamezomewa.
Wamejaribu kushindana na ukweli, wameshindwa. Uchache wa wapinzani bungeni, haukuzuia hoja zao kupenya hadi mioyoni mwa wananchi. Kanuni za Bunge na mabavu ya kamati ya wabunge wa CCM, havikutosha kuwatetea watawala dhidi ya wananchi.
Tazama ukweli ulivyo na nguvu. Miongoni mwa wabunge wote 323, CCM ina wabunge 279; wapinzani ni 44. Kwa mazoea, hata kama wapinzani wana hoja nzuri namna gani, inabezwa na kuachwa kwa sababu zikipigwa kura watakaoshinda ni wale wa CCM walio wengi.
CCM imekuwa ikitumia wingi wao kunyamazisha wapinzani na wananchi kwa ujumla. Viongozi wakuu wa njama hizi za CCM wamekuwa wawili: Spika wa Bunge (kwa kutumia kanuni za Bunge) na waziri mkuu (ambaye ni msimamizi wa shughuli za serikali bungeni) kwa kutumia kamati ya wabunge wa CCM.
Mazoea hayo ndiyo yalitumika katika kumdhibiti na kumwadhibu Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, na baadaye kumtisha Mbunge wa Karatu (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.
Lakini sote tunajua kilichotokea. Wananchi waliungana na wapinzani hao wachache kuitetemesha serikali kwa mwaka mzima sasa.
Na baada ya hapo, wananchi wamefunguka macho, na sasa wameanza kujua namna ya kuishughulikia serikali yao. Hoja za wabunge hao na wengine wa upinzani kuhusu ufisadi, zimewaongezea wananchi ujasiri wa kuikosoa na kuilaani hadharani.
Zimeleta mwamko mpya katika siasa za Tanzania; na zimeua propaganda kongwe na dhaifu ya CCM juu ya mwelekeo wa serikali ya awamu ya nne.
Wingi wa wabunge wa CCM, mabavu ya serikali na matumizi mabaya ya pesa kuwatuma mawaziri nchi nzima kupinga hoja wa wapinzani, havikuondoa dhiki ya wananchi.
Wala havikuifanya bajeti ya mwaka jana kuwa bora zaidi. Katika hili, mkweli na mwongo walionekana. Sasa serikali inajua hili; na CCM inakiri.
Na wabunge wa CCM wameshtuka na kukumbuka wajibu wao kwa umma. Ndiyo maana nao sasa wanatoa kauli nzito kuipinga na kuikosoa serikali, na hata kuitaka ichukue hatua kali dhidi ya mafisadi - kauli ambazo hazikudhaniwa kuwa zingetoka kwa wabunge wa CCM dhidi ya serikali ya awamu ya nne.
Hatimaye, wabunge wa CCM wamelazimika kujiunga na wapinzani kutetea maslahi ya taifa, wakizingatia usemi kwamba: ‘kama huwezi kuwashinda, jiunge nao.’ Wachache wameshinda.
Lakini kilishowafanya washinde ni hoja zilizoungwa mkono na wananchi walio wengi. Wabunge wachache wa upinzani wamekuwa watetezi wa wananchi walio wengi, wanaowaona watawala kama wanyonyaji, wabadhirifu wa mali za umma, ‘wanadishaji wa nchi’ kwa wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje, na watu wasiojali maslahi ya taifa.
Si kwamba CCM haina wabunge makini, wazalendo na wapenda maendeleo. Wamo! Lakini wengi wamekuwa waoga wa mikiki mikiki na ubabe wa chama chao. Wamekuwa wakiburuzwa kuunga mkono mambo wasiyoyakubali kwa mioyo yao yote.
Wamekuwa walalamishi wa pembeni pembeni. Lakini sasa wamepata funzo kwa wapinzani. Wameanza kujitokeza na kuchomoza. Na serikali imeanza kuhisi joto lao. Haya ni mageuzi, hata kama hayajakamilika. Laiti kungekuwa na wabunge 150 wa upinzani.
Kuna mambo ambayo serikali ingeogopa kuyapeleka na kuyajadili bungeni, maana ingejua kwamba kule kuna hoja nzito na idadi inayoweza kutikisa Bunge, ambayo ikiongezewa kidogo tu na wengine wa CCM wanaoshawishiwa na hoja, inaweza kuzuia kabisa upuuzi wa serikali - unaowafanya wakubwa washibe! Mfano wa pili wa ushindi wa wachache unapatikana katika vyombo vya habari. Hadi katikati mwa mwaka 2006, ndani ya mwaka mmoja wa serikali ya awamu ya nne, vyombo vya habari karibu vyote viliegemea kwa serikali.
Vilikuwa na mapenzi binafsi yasiyomithilika kwa Rais Jakaya Kikwete. Mtu mmoja alitania akisema vilimsifu na kumuimba kwa utukufu uliokaribia wa kidini! Wakati huo huo, wahariri na waandishi wadogo na wakubwa walimuogopa aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa.
Hawakumpenda kwa dhati, na katika mazungumzo, walimsingizia Lowassa kwamba ‘haandikiki’, ziliundwa njama za kujenga uandishi mpya wa kipropaganda kuisaidia serikali.
Watafiti wakirejea habari na makala nyingi za kipindi hicho katika magazeti, redio na televisheni, wataibuka na ushahidi mkubwa wa hiki ninachokizungumzia hapa.
Nguvu yao ilikuwa kubwa maana ilitanda nchi nzima. Walimbeza yeyote asiyekubaliana nao. Ilipobidi walimtisha. Na waliwapata wengi. Vyombo karibu vyote vikabaki kutafuta jinsi ya kusifia kasi mpya na ari mpya ya serikali mpya.
Lakini walikuwapo waandishi wachache sana (nadhani hawakuzidi 10 nchi nzima) waliosema ‘hapana!’ walisema kazi tunayo, hatuhitaji kufanya uandishi wa ‘kuomba kazi serikalini’.
Wakasema “endeleeni kuonyesha uzuri na uwezo wa serikali, mtuache sisi tuonyeshe upande mwingine wa serikali.” Wengi hawa walibeza uchache wa wenzao, hawakuangalia hoja na sababu zao. Walitilia shaka hata uzalendo wa wachache hao.
Na kwa haraka haraka, wengi hao walishirikiana na serikali kuunda muswada wa kuanzisha sheria ya uhuru wa habari, lakini ulipochunguzwa ukaonekana ulikuwa na lengo la kulinda zaidi maovu ya wakubwa, kutukuza ufisadi kwa kuminya zaidi uhuru wa habari unaotetewa.
Wachache wakakataa, wakapiga kelele nchi nzima; wadau wakawaunga mkono, ushindi ukapatikana. Jambo moja lilikuwa wazi. Wengi walitaka kuufanya uandishi kuwa ukarani wa kuwasaidia walio madarakani.
Wachache walitaka kuzingatia dhana kwamba vyombo vya habari ni muhimili wa nne wa dola baada ya serikali, Bunge na mahakama; kama ilivyoasisiwa na Thomas Carlyle, mwandishi na mwanahistoria Mwingereza wa karne ya 19.
Vyombo vya habari vinaweza na vinapaswa kutetea haki na kulaani dhuluma, huku pia vikijenga na kusimika ajenda za kisiasa kwa manufaa ya umma.
Wachache hawa waliamini kwamba ikiwa vyombo vya habari vyote vitakuwa mirefeji ya taarifa za propaganda za serikali na CCM; iwapo waandishi na wachambuzi wote watakuwa midomo ya watawala; nani atakuwa sauti ya wananchi? Wachache hawa walizingatia kuwa iwapo waandishi watafikiri kwa kutumia akili za watawala; uhuru na demokrasia tulivyopigania kwa muda mrefu, vitakuwa vimezikwa kaburi moja! Walitambua kwamba jitihada hizi za wale wengi zilikuwa chafu, na zililenga kuficha udhaifu wa walio madarakani, na kuupa fursa ufisadi ushamiri bila wananchi kujua.
Walitambua kuwa uandishi wa karne ya 21 lazima utofautiane na ule wa miaka ya 1960 baada ya uhuru, zama za propaganda kali za chama cha TANU na utumwa wa mawazo (maana tunajua kuwa yaliyopingana na ya watawala hayakupewa nafasi!).
Wachache hawa walizingatia kauli ya mwanadiplomasia na mwandishi mahiri Henry Anatole Grunwald, aliyewahi kuwa mhariri mtendaji wa jarida maarufu la TIME la Marekani, kwamba uandishi wa habari haupaswi kamwe kunyamaza. Alisisitiza: “Unapaswa kusema, na kusema pale pale, wakati miangwi ya mishangao, madai ya utukufu na dalili za hofu vinapokuwa bado vibichi.” Hatukutaka kureja tulikotoka. Kipaumbele cha wachache kiliwekwa katika kulinda na kutetea maisha na ustawi wa muda mrefu wa ndugu zetu, wazazi wetu na watoto wetu (Watanzania kwa ujumla wao), si ya watawala.
Leo, baada ya miaka miwili, waliokuwa wanadhihaki wenzao ndio wanaochekwa na kubezwa. Upepo umebadilika. Sifa na uwezo halisi wa watawala wetu vimeonekana wazi. Ukweli wa wachache umeshinda. Hatimaye, mweleko wa jumla wa uandishi juu ya utendaji wa serikali umebadilika.
Uandishi wetu sasa umegeuka na kuwapa wananchi sauti waliyonyimwa muda mrefu, wakaanza kuwamulika watawala wao, kuwahoji na hata kuwazomea inapobidi. Hatimaye, vyombo vya habari vimewaunganisha tena wananchi.
Vinawapa taarifa na habari muhimu; na wananchi wanazitumia kujijenga upya kifikra kupambana na mafisadi na kujikwamua kisiasa, kiuchumi na kijamii. Huu nao ni mwanzo mwingine wa mageuzi.
Na haya yamewezekana tukiwa bado na sheria mbaya zinazosimamia uandishi na utangazaji nchini. Yamewezekana bila sheria nzuri ya uhuru wa habari. Hali ingekuwaje kama tungekuwa huru? Kwa wabunge wachache na waandishi wachache kushinda makundi ya wengi katika mazingira ya sasa; na ukweli kwamba hata hao wengi sasa wamefika mahali wamefumbuka macho na wameanza kuwa jasiri katika kukemea ufisadi wa serikali, ni hatua ambayo mwaka huu wa fedha unaomalizika sasa hauwezi kupita bila kukumbushana na kujiweka sawa katika mwaka unaoanza.
Imani yangu ni kwamba, huko tuendako nguvu ya umma itakuwa kubwa na yenye kishindo kikubwa zaidi. Itawapa wananchi matumaini yaliyopotea, ambayo tumekuwa tunayatetea katika miaka miwili iliyopita.
Fundisho tunalopata hapa ni kwamba hata wachache, iwapo watasimamia ukweli, watashinda na hatimaye wataungwa mkono na wananchi walio wengi. Maana wingi wa dhuluma hauwezi kushinda ukweli na haki inayotetewa na wachache.

ansbertn@yahoo.com
www.ngurumo.blogspot.com
+447853 850 425
 
Asante sana kwa ujumbe huu mzito na uliojaa ukweli. Huu ni mwanzo tutafika safari yetu ndefu ya ukombozi
 
Asante sana kwa ujumbe huu mzito na uliojaa ukweli. Huu ni mwanzo tutafika safari yetu ndefu ya ukombozi

Mapinduzi ya kweli yataletwa na Mashujaa wachache ambao tutakuwa tumeamua kuweka Our Hopes above our Fears!!!

Mpaka Kieleweke!
 
Katika kugombania nguvu ya dola si rahisi kiongozi wa dola akaweka masilahi ya kitu/mtu yeyote zaidi kake binafsi mbele.
ni kawaida na ndio ilivyo power inapendwa na wanasiasa wote, hata wewe ukiingia kwenye siasa unatafuta power na recognition.
Utaonekana wa maana kwa kufanya mambo mbalimbali, mfano kusaidia mahitaji ya wananchi kupatikana, kujinadi nchi nyingine, kuhakikisha wananchi wanaishi kwa usalama nk.
Haya yote ni ili tu kujihakikishia dola lako linatawalika.
si kwamaba una huruma sana.
ukiingia kwenye siasa kichwa kichwa utafilisika mara moja tutakusahau.
Ndio kina mrema, walipenda nchi zaidi wasahau kujikinga wenyewe.
 
Back
Top Bottom