Maswali kwa rais Kikwete na yatokanayo

Invisible

Robot
Feb 11, 2006
9,075
7,873
jk_1.jpg


Naam,

Tido Mhando anaongea lakini sauti ilikuwa haisikiki vema na wamerekebisha.

Toka magazetini:

RAIS Jakaya Kikwete, amesema kuwa hajawafunga midomo wabunge na badala yake amewataka waendelee kuikosoa serikali kwa misingi iliyo sahihi.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi kwa staili yake mpya ya kujibu maswali ya papo kwa papo kwa kutumia simu, ujumbe mfupi wa simu (sms) na barua pepe kupitia televisheni na redio.

Akijibu swali lililoulizwa kwa njia ya barua pepe kwamba kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kililenga kuwaziba midomo wabunge pamoja na Spika wa Bunge, Samuel Sitta, Rais Kikwete alisema kilichotokea mjini Dodoma ni mazingira ambayo yameonekana kama vile ni uhusiano usioridhisha kati ya wabunge wa CCM na serikali yao.

Alisisitiza kuwa kamwe serikali yake haina nia na haiwezi kuwaziba midomo wabunge wake.

"Kweli tulikuwa na mjadala mkali sana, wengine wakatajana majina, lakini kilichoonekana ni mazingira ambayo yameonekana kama vile ni uhusiano usioridhisha kati ya wabunge wa CCM na serikali yao. Lingine ni mazingira ya kuchukiana sana kati ya wabunge wa CCM, wanachukiana kiasi kwamba wanashindwa hata kuachiana glasi za maji.

"Lakini pia NEC iliona kwamba kwenye kamati ya chama ya Bunge, ilitokea hisia kwamba haifanyi kazi ipasavyo, hivyo tukasema tutafanyaje kuondoa hali hii ya kuchukiana sana, na tufanye kamati yetu ya chama ifanye vizuri.

"Basi hatimaye tukakubaliana kwamba lazima mambo hayo tuyashughulikie, tukamwomba Msekwa, Mwinyi na Kinana, tukasema basi waangalie hali hii ili kuondoa tofauti hizo. Hicho kwa kweli ndicho kilichotokea Dodoma. Mimi naamini baada ya wazee wetu hawa tutafika pazuri, nataka wabunge wetu waikosoe serikali ili kukijenga chama na serikali na hakukuwa na juhudi za kuziba watu midomo," alisema.

Akijibu swali la Solomoni Natal wa mjini Arusha kuhusu kuwapo makundi ndani ya CCM, Rais Kikwete alisema hakuna makundi bali kilichopo ni kwamba kuna uwazi zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.

Kuhusu waraka wa Kanisa Katoliki na ule wa Waislamu uliotolewa na Shura ya Maimamu, Rais Kikwete alisema kuwa umeitisha serikali yake, na sasa viongozi wakuu wa taifa wanafanya utaratibu wa kukutana na viongozi wa dini.

Alisema hayo akijibu swali aliloulizwa kwa njia ya simu na Zombo Kamkala wa jijini Dar es Salaam.

Katika swali lake la msingi, Zombo alihoji sababu za rais kuwa kimya baada ya Kanisa Katoliki na Waislamu kuzindua nyaraka zao zinazoelekeza waumini wao jinsi ya kuchagua viongozi wakati wa uchaguzi mkuu mwakani.

"Mheshimiwa Rais, hawa jamaa mbona wanatupeleka mahala pabaya na nyaraka zao, na mbona serikali imekaa kimya?" alihoji Zombo.

Akijibu swali hilo kwa hisia, Rais Kikwete alisema kuwa waraka wa Katoliki na baadaye mwongozo wa Waislamu, umeishitua sana serikali yake kiasi cha kuleta hofu, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

"Hili jambo ni kweli limetushtua sana na kuleta hofu kubwa, hasa kule tunakoelekea kwenye uchaguzi, kwani kuna hatari ya Watanzania kupiga kura kwa maelekezo ya dini zao, Wakristo na Waislamu.

"Hii inatia hofu sana na hata kwenye kikao cha NEC mjini Dodoma, tumezungumza na kwa pamoja tumeiona hofu hiyo, kwani kama tukiendelea hivi, hatutakuwa na taifa, badala yake kutakuwa na ushindani wa kidini.

"Si mwelekeo mzuri sana, Mwalimu amelijenga taifa hili bila ubaguzi, tutazamane kwa Utanzania wetu na si kwa dini zetu," alisema.

Rais Kikwete ambaye ni mara yake ya kwanza kuzungumzia suala la waraka wa Wakatoliki na Waislamu hadharani, alisema kuwa NEC, imeagiza viongozi wakuu wa taifa, akiwamo yeye mwenyewe, makamu wake na Waziri Mkuu, kukaa meza moja na viongozi wa dini ili kujadili hatma ya taifa hili kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu mwakani.

Mbali ya kuagiza kukutana na viongozi hao wa dini, Rais Kikwete alisema NEC pia imeagiza viongozi wa siasa kuacha kulumbana hadharani juu ya nyaraka hizo na kuwataka waumini wa dini zingine kutofanya hivyo kwa sasa.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, tayari serikali imeshaanza mawasiliano na viongozi na kusisitiza kuwa katika kipindi hiki, viongozi wengine wa madhehebu mengine ya dini, wasitoe nyaraka zaidi.

Rais Kikwete katika mazungumzo hayo, pia alizungumzia suala la ufisadi na kutamba kuwa katika dunia, Tanzania inaweza kuingia kwenye rekodi ya kuthubutu kwa kuweza kuwafikisha mahakamani zaidi ya vigogo 27 wa serikali.

Akijibu swali la Jacob Mkama wa Ukerewe, kwamba serikali haijafanya juhudi katika kukabiliana na mafisadi, Rais Kikwete alisema madai hayo si sahihi, kwani juhudi ambazo serikali yake imefanya katika kukabiliana na rushwa na ufisadi, zinaonekana.

"Ningeshangaa sana kama nisingeweza kuulizwa swali hili. Mimi natazama suala hili katika hatua mbili, kwanza kujenga chombo cha kuongoza mapambano, yaani TAKUKURU. Usipokijenga, hatutafika mbali. Kwanza tukaanza na sheria, tuliyokuwa nayo ni ya mwaka 71, sasa tuna sheria mpya," alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alitamba kuwa hivi sasa serikali yake imeimarisha utendaji kazi wa TAKUKURU kwa kuajiri watumishi zaidi na kuwapa mafunzo pamoja na vifaa vya kufanyia kazi.

"Tumejenga mazingira ya kuwataja walarushwa, hivi sasa kuna kesi 578 toka kesi 50 zilizokuwepo mwaka 2005, taarifa nyingi zaidi zinapatikana. Wengine wanasema tunashughulika na dagaa tu, mbona papa hakuna? Tumefanya kesi za EPA, BoT, watendaji wakuu wa serikali 27 wako mahakamani na naweza kusema Tanzania tunaweza kuingia kwenye rekodi duniani ya kuthubutu," alisema Rais Kikwete.

Alitoboa siri kuwa hivi sasa kuna kesi kubwa tatu ambazo zimekamilika na wakati wowote TAKUKURU itawafikisha wahusika mahakamani.

Alitamba kuwa hakuna rafiki katika vita dhidi ya ufisadi, na kwamba hana ndugu wala rafiki, kwani tayari baadhi ya rafiki zake wa karibu, hivi sasa wako matatani.

Akizungumzia suala la ujenzi wa shule na matatizo ya walimu, Rais Kikwete alisema serikali yake imejenga shule nyingi katika kipindi kifupi, hivyo kusababisha uhaba wa walimu pamoja na vifaa.

Hata hivyo, alielezea mikakati ya kukabiliana na kasoro hizo ili kutoa fursa zaidi kwa wananchi kupata elimu.

Kuhusu matatizo ya madai ya walimu na mradi wa ujenzi wa nyumba zao kama alivyoulizwa na Pascal Justine, Rais Kikwete alisema baada ya muda mfupi matatizo hayo yatakuwa historia.

Alisema atajibu maswali yote aliyoandikiwa kwa ujumbe mfupi, barua pepe na kwamba atatafuta muda mwingine wa kuzungumza na wananchi kwa staili hiyo.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya taifa hili kwa kiongozi wa nchi kuzungumza na wananchi wake kwa staili ya kuulizwa maswali.

Hata hivyo, rais alijibu maswali yasiyozidi 15 kutokana na urefu wa majibu kwani alitumia karibu saa mbili kujibu maswali hayo.


Chanzo: Tanzania Daima.
 
So kwenye hii thread tunatakiwa kuandika maswali yetu halafu yafowadiwe kwa raisi?
 
Tido anasema wameshapata maswali takribani 2,500 ya sms na karibu emails kama 500 hivi.

JK anasema atawajibu mmoja baada ya mwingine hata baada ya kipindi.

Atatafuta namna nyingine ya kujibu maswali baadae hata isipokuwa kwa njia ya Television
 
ameikana Ilani aliyochotea kura kuwa hakuiandika yeye na kama angiandika yeye ..... anaogopa sana

Swali la kwanza kutoka kwa tido guess what? Shule za Loawassa na mafanikio yake na mkuu anashusha data dalili za kwamba alishaambiwa kabla
 
JK anasema kama ni yeye basi shule za kata asingeziingiza kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM lakini kwakuwa CCM anayegombea haandai ilani basi hana budi kuitekeleza.
 
Shalom, jamaa hapo kachemka. Nadhani Tido hakumwandaa juu ya swali hilo!
 
Sidhani kama issue ya takwimu ina msaada sana na inapoteza muda wa kujibu maswali mengi... Hapa washauri wake wangemwambia namna ya kutumia dakika 90 hizi
 
Naona Rais anamwaga takwimu kama vile Maswali ya Tido alikuwa anayajua
 
JK ametoa weakness kubwa ya CCM kwamba mgombea haruhusiwi kuhusika ktk kazi ya kuandaa ilani ya uchaguzi. Pia ame-disown ilani anayoitekeleza sasa. Kwamfano anasema ingekuwa ilani imeandaliwa naye asingeweka suala la Sekondari kila kata.

Binafsi naona amekuwa muungwana kuonyesha tatizo/matatizo yanayotokana na ilani hiyo.
 
leo kazi ipo, naona mh ameshaikana ilani ya ccm kuwa yeye hakuandaa, kwahiyo kuna uwezekano mkubwa akakwepa kujibu swali lolote linalohusianb na ahadi zake kipindi cha
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom