Maswali alfu lela na moja kwa Rais Kikwete

mpangwa1

JF-Expert Member
Jul 19, 2009
278
8
HII ni sehemu ya mwisho ya maswali alfu lela na moja kwa rafiki yangu, Rais Jakaya Kikwete, ambayo anapaswa kuyajibu kabla ya Oktoba 31 ili niwe nimeyasahihisha na kutangaza maksi atakazokuwa amepata.
Maksi hizo ndizo zitakazomsadia kushinda au kushindwa katika mtihani rahisi wa kuendelea kubaki madarakani kwa sababu kwa pamoja, mimi na wachokonozi wengine wote uswahili tunatarajia kutumia maksi hizo kumpima kama ana uwezo wa kuendelea na ngwe ya pili ya ukuu wa kaya yetu au lah.
Hata hivyo, haitakuwa ajabu akafeli lakini akaendelea na ngwe na pili kwa sababu zinazofahamika. Zinatumiwa na watahiniwa wengi wasiojiweza kichwani, ikitokea hivyo asiwepo wa kushangaa, ieleweke vile vile kuwa hiyo ndiyo staili yetu Watanzania, ujanja ujanja.
Kabla sijaendelea na maswali, nitumie fursa hii kueleza masikitiko yangu kutokana na hatua ya meneja wa kampeni za uchaguzi za rafiki yangu kuutangaza umma kuwa chama chetu cha maulaji hakina mpango wa kumruhusu mgombea wetu kuhudhuria mdahalo wa kupimana uelewa wa mambo rahisi kabisa na wasomi wenzake.
Ndugu meneja, amekaririwa na wanahabari siku chache tu baada ya msisitizo nilioutoa kuhusu umuhimu wa rafiki yangu kushiriki mdahalo huo akieleza kuwa, eti! mgombea wetu hawezi kushiriki kwa sababu muda haupo hivyo wagombea wengine wa urais wanaweza kufanya mdahalo wenyewe.
Kama hakukaririwa vibaya na waandishi wa habari na kama kumbukumbu zangu ziko sahihi, alisema eti, mdahalo huo hauna msingi kwa sababu mgombea wetu anafahamika, hivyo wasiofahamika ndio wafanye mdahalo. Mambo ya ajabu kabisa!
Kwamba rafiki yangu anafahamika kwa wananchi bila kujali kuwa anafahamika kwa mazuri au mabaya, kwa kushindwa au kushinda kutekeleza majukumu yake. Anafahamika kama kiongozi dhaifu au jasiri na pengine kama mchekeshaji au mtu makini.
Katika ‘issue’ ya mdahalo anafahamika lakini kwenye kuitangaza sura yake kwa Watanzania ili wampigie kura hafahamiki! Ndiyo maana chama chetu kimelazimika kutumia mabilioni ya pesa kusambaza picha zake Tanzania nzima ili wapiga kura wamuone, wamfahamu, wampigie kura.
Mabango yenye picha zinazomuonyesha katika taswira mbali mbali yamesambawa hadi vijijini ili kumtambulisha kwa wapiga kura wanaomfahamu. Huu ni utamaduni mpya wa mtoto anaelelewa na baba yake, akimuona kila siku nyumbani, akienda na kurudi kazini, inapowadia sikukuu ya mavuno ambapo wageni hualikwa nyumbani kwa mkulima hodari kusherehekea, mtoto anajumuishwa na wageni waalikwa kutambulishwa kwa baba yake mzazi anayeishi naye nyumba moja.
Hizi ndizo sura mbili tofauti ninazolazimishwa kuziona kwa rafiki yangu. Katika mdahalo na katika kusaka ulaji. Ni picha mbaya ambazo naamini hata yeye hapendi aonekane hivyo.
Wanamlazimisha aonekane mtu mwenye shaka ya kuchaguliwa tena, asivyojiamini mbele ya wasomi wenzake kiasi cha kukacha kufanya mdahalo nao kwa sababu ambazo mimi naamini hazina mashiko.
Najua ipo siku atakataa kwa sababu kushinda atashinda, hilo sina shaka nalo. La kushabikia mdahalo ni kuondoa dhana potofu ambayo imekuwa ikijengwa na wambea kuwa hayuko ‘fit’ katika mambo fulani fulani ya wenye akili.
Tuendelee na maswali; swali la 501; rafiki yangu, unaifahamu EPA? Jibu liwe ndiyo au hapana. (b) EPA ni nini? Hapa eleza kwa kirefu pamoja na shughuli zake. Swali la 502; Eti? Ni kweli ulimuomba kaka Ben aidhinishe ukwapuaji wa fedha za EPA ili zikusaidie kuwahonga wapiga kura wakati ukiwania ukubwa mwaka 2005?
Swali hili usilielewe vyovyote vinginevyo, ni la kawaida tu na nimekuuliza kwa sababu wengi wanataka kujua kama tuhuma zilizosambaa sasa huku uswahilini za wewe kuhusika katika jambo hili ni kweli.
Ni vizuri ukaelewa kuwa wapiga kura wanashauku ya kujua mabilioni yaliyotumika katika uchaguzi wa 2005 kwenye kampeni zako yalitoka wapi? Yalitoka katika vitega uchumi ambavyo chama chetu kimewadhulumu Watanzania? Yalitolewa na serikali au kuna wafadhili walichanga!?
Swali la 503; Kwanini ulipotajwa katika orodha ya watuhumiwa 11 wa ufisadi kule Mwembeyanga hukujibu tuhuma hizo wala kuchukua hatua? Hapa pia ni vema ukatoa maelezo kwa kirefu kwa sababu tuhuma zilizotolewa ni nzito.
Kuna shaka kubwa kuwa ni za kweli kwa sababu hata baadhi ya waliotajwa pamoja na wewe kwenye orodha hiyo walijaribu kutishia kwenda mahakamani lakini hadi sasa hawajatekeleza nia hiyo.
Hili linaonyesha kuwa waliowatuhumu walituhumu ukweli ndiyo maana inakupasa kutoa maelezo marefu kadri inavyowezekana ili kufuta kabisa hisia hizi. Kwa unyeti wa swali lenyewe, maelezo hayo yatakuwa yamejibu maswali mengine 54.
Swali la 557; litakuwa kosa mtu akikuita fisadi kwa kushindwa kujibu tuhuma za ufisadi zinazo na zilizokwishaelekezwa kwako? Naamini swali hili halitaleta hisia zozote mbaya kwa sababu fisadi ni neno ambalo hivi sasa linatumika vizuri hapa nyumbani.
Swali la 558; kamilisha majina ya watu hawa? Mabere….., Dk. Ringo…., Malegesi …… swali la 559; unafikiri kwa nini nimekuuliza swali la 558? Swali la 560; Jibu kwa kirefu.
Utajisikiaje madudu ya EPA na kinachosemwa juu yako na wenzako kuhusu EPA kikianza kuanikwa katika ukurasa huu ili kila mwananchi akisome katika kipindi hiki?
Swali la 561; Ulitumia busara zipi kuwasamehe waliokwapua fedha za EPA? Swali hili linahusiana na mambo ya kisheria na majibu yake yajumuishe maelezo yako na yaliyokwishatolewa na wasaidizi wako kuwa kuwakamata wezi wa EPA kunaweza kuliyumbisha taifa na mengine yote unayoyajua kuhusu EPA. Ukilijibu kwa usafaha utakuwa umejibu maswali mengine 150.
Swali la 711 hadi 720; chagua jibu lililo sahihi. Watanzania wanaishi (a) Maisha bora (b) Maisha bomu (c) Bora maisha. Ninategemea jibu litazingatia ukweli halisi wa maisha ya sasa ya Watanzania bila kujali kama umetimiza ahadi ya kuwaletea maisha uliyowaahidi au la!
Rais Mstaafu wa Marekani alipokuja Tanzania alituletea (a) Vyandarua (b) Fedha za mkopo (c) Vitabu na wataalamu wa elimu. Hakuna haja ya kuona aibu kuchagua jibu sahihi hata kama jamaa huyo alituletea peremende.
Ikiwa hivyo utakuwa umewakata kilimilimi wale wanaohoji manufaa ya safari zako nje kwa sababu hawajui huko huwa unakwenda kuomba nini na zaidi hawana shukrani kwa sababu rafiki wa baba akikuletea zawadi ni lazima ushukuru pasipo kuhoji chochote.
Usafiri salama kwa mama mjamzito ni (a) Gari la wagonjwa (b) Bajaj (c) Tela la kukokotwa na ng’ombe. Unajua kila kundi la jamii au watu fulani linahitaji usafiri unaoendena nalo. Kwa mfano wewe pale Ikulu usafiri wako ni magari ya kifahari aina ya Benz, BMW na Toyota, Land Cruiser za bei mbaya.
Huu ndiyo usafiri wa hadhi yako hata kama unatoka hapo magogoni kwenda nyuma tu pale Karimjee. Ni lazima utumie usafiri huu wa gharama iliyopindukia hata kama sisi wenzako huku tunalalia mihogo ya pilipili kwa kikombe cha maji. Unastahili, ni lazima iwe hivyo.Kwa mawaziri wao wanastahili mashangingi yenye thamani ya zahanati nne kama tunavyoelezwa na wenye akili. Ni lazima watumie mashangingi hata kama kuna wajawazito wanaokata roho katika zahanati kwa kukosa dawa.
Sasa kwa mama zetu wajawazito ambao serikali yetu imekuwa ikisisitiza kuwapenda sana hadi tunawapatia vyandarua visivyokidhi viwango kwa hati punguzo, ni vema ukaeleza mwenyewe usafiri unaofaa kwao kutumika.
Kipi kinafaa kuanza kujengwa ili kuondoa adha ya usafiri kwa Watanzania (a) Barabara za uhakika (b) Viwanja vya ndege (c) njia ya reli. Hapa hakuna maelezo, chagua tu jibu sahihi. Adui namba moja wa Watanzania kwa sasa ni (a) Umaskini (b) Maradhi (c) Ufisadi. Tanzania ni nchi (a) Maskini (b) Tajiri (c) Fukara. Na hata swali hili halina ufafanuzi kwa sababu linajitosheleza.
Mama Salma Kikwete ni (a) Kiongozi wa Serikali (b) Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA (c) Mke wa Rais (d) Mwanasiasa. Nadhani swali linaeleweka, tunaendelea. Tanzania ni nchi inayoongozwa (a) Kidini (b) Kikatiba (c) Kiholela. Hili rahisi sana.
Katika uchaguzi mkuu wa 2005, mgombea gani wa urais alidaiwa kutumia vyombo vya habari kuchafua wenzake (a) CHADEMA (b) CCM (c) CUF. Kazi ya Sheikh Hussein ni (a) Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa (b) Mnajimu (c) Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya rais. Swali hili lina umuhimu wa kipekee.
Mwanasiasa mzuri ni aliyebobea katika (a) Kudanganya (b) Kutoa ahadi zisizotekelezeka (c) Kuzungumza ukweli.
Swali la 721; serikali iliyoko madarakani ina yapi ya kujivunia iliyofanya katika kipindi cha miaka mitano iliyokaa madarakani. Jibu la swali liguse sekta zote kuanzia ya uchumi hadi michezo. Nalo limejumuisha maswali 250, hivyo kufanya idadi ya maswali kuwa 971.
Swali la 972; Eleza kwa kirefu, kwa nini serikali imefeli kwa kiwango cha kusikitisha kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa na serikali ya awamu ya tatu? Hapo pia kuna maswali 24 zaidi ambayo utakuwa umeyajibu kulingana na uzito wa swali lenyewe.
Swali la 997; Mwaka 2005 mfumuko wa bei ulikuwa asilimia ngapi? Swali la 998; Mwaka 2009 mfumko wa bei ulikuwa asimilia ngapi? Swali la 999; Tangu 2005 hadi 2009 pato la taifa limepanda kwa asilimia ngapi?
Swali la 1000; Katika kipindi cha miaka mitano ya awamu ya nne, kwa nini ufanisi wa ukusanyaji mapato wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) umekuwa wa kusuasua?
Swali la alfu lela na moja; kwanini serikali nyingi za Afrika huwa zinaamini kuwa haziwezi kupinduliwa kupitia sanduku la kura?
Source Tanzania Daima
Malaria sugu na wezako mnaweza kuandaa deza kwa boss wenu iliaweze kujibu haya maswali
 
kwanini serikali nyingi za Afrika huwa zinaamini kuwa haziwezi kupinduliwa kupitia sanduku la kura?
jibu rahisi.......wewe waweza kubali na kuamini kiti ulichokalia,na tena unanufaika nacho mwingine anaweza kukichukua kwa sanduku la kura????HAKUNA SERIKALI AFRIKA AMBAYO INAAMINI HILO,90% YA SERIKALI ZA AFRIKA VIONGOZI WAKE NI WABINAFSI,WAZANDIKI,WACHOYO,WAROHO WA MADARAKA,......HAWAKO TAYARI KUONA WANAPINDULIWA WAKO TAYARI KULINDA NAFASI ZAO KWA GHARAMA YEYETO HATA IKIBIDI KWA DAMU,KUIBA KURA,ULINZI WA SHEHE YAHAYA NK.
NAKINACHOWAPAKICHWA ZAIDI KUENDELEA KUAMINI HILI NI NGUVU NDOGO YA MAAMUZI DHABITI,UJINGA,LACK OF INFORMATION KWA WAPIGA KURA.WHAT WE NEED TO CHANGE THE CURRENT POSITION IS EMPOWERNMENT!!!!!
 
Back
Top Bottom