Marufuku kusafirisha nje Tanzanite ghafi`

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,080
Ngeleja1%289%29.jpg

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.



Serikali imepiga marufuku usafirishaji nje ya nchi wa madini ya Tanzanite ghafi kwa vile hayawanufaishi sana Watanzania kutokana na kuuzwa kwa bei ndogo yakiwa katika hali hiyo.
Madini Tanzanite yaliyopigwa marufuku kusafirishwa nje ya nchi, ni yale yanayoanzia gramu moja na zaidi yenye ubora wa kusanifiwa na kwamba, yatakatwa na kusanifiwa hapa hapa nchini kwa vile tathmini imeonesha kuwa uwezo wa kufanya hivyo upo.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema amri hiyo inafuatia malalamiko ya wananchi kwamba madini hayo yananufaisha mataifa mengine.
“Mfanyabiashara yeyote atakayekiuka agizo la serikali akigundulika, madini yake yatataifishwa na pia leseni yake itafutwa mara moja pamoja na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yake,” alisema Waziri Ngeleja.
Hata hivyo, Ngeleja alisema madini ghafi ya Tanzanite yatakayoruhusiwa kuafirishwa nje, ni yale yenye michongo ya asili, ambayo yanaweza kutumika kwenye majumba ya makumbusho, vyuo vya madini na mavazi ya kifalme yanayouzwa kwa bei kubwa kutokana na ubora wa rangi, usafi, mchongo wa asili na uzito.
Alisema madini yasiyopitisha mwanga kabisa yasiyoweza kusanifiwa nchini ambayo hutengeneza shanga pia, yataruhusiwa chini ya idhini ya Kamishna Mkuu wa Madini.
Tanzanite ambayo ni madini ya vito adimu sana duniani yanapatikana Tanzania pekee, eneo la Mererani, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Arusha, yamekuwa yakichimbwa na kuuzwa nje ya nchi hususan katika nchi za India, Afrika Kusini, Thailand, Ujerumani na Israeli yakiwa ghafi kwa bei ndogo kuliko stahili yake. Serikali inapata asilimia tano ya thamani ya Tanzanite ghafi kama mrabaha.



CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom