Marekani na ushirikina

vukani

JF-Expert Member
Dec 30, 2009
245
165
Wakati sayansi na teknolojia vikiwa juu kabisa katika ngazi ya vitu ambavyo vimefikia mafanikio makubwa kule Marekani, jambo la kushangaza limeripotiwa. Hivi karibuni wachunguzi wa masuala ya imani, wamebaini kuwa imani za ushirikina zimetopea kwenye jamii hiyo.

Watu wengi nchini humo wanaamini katika mambo ya ajabu na yasiyoelezeka kisayansi, kama vile mizimu, laana, viumbe wa ajabu, majini na mengine kama hayo. Taarifa za utafiti huo uliofanywa na shirika la BRS ambazo zimetolewa hivi karibuni zinaonesha kwamba robo tatu ya Wamarekani hivi sasa wanaamini kwamba watu wanaweza kupona kwa matumizi ya nguvu za ziada badala ya dawa.

Nusu ya Wamarekani wanaamini kwamba ndoto huwa zina ujumbe na zinasema kuhusu mambo ambayo yanaweza kutokea kweli. Robo ya watu wanaamini kwamba viumbe kutoka dunia nyingine, maarufu kama UFO wapo kweli na wanatoka kweli dunia nyingine ambayo binadamu hajaigundua.

Kiasi cha asilimia 37.2 ya Wamarekani wanaamini kwamba kuna nyumba zenye mizimu au majini. Asilimia 28 wanaamini kuwa inawezekana kabisa mtu akakunja au kuvunja kitu kwa kutumia nguvu ya mawazo yake.

Asilimia 20 ya wamarekani wote wanaamini kwamba, kuna uwezekano wa mtu kuwasilianana wafu au mfu wake na hii hufanywa kwa kutumia ubao maarufu kama ouija board.

Asimia 18 wanaamini kwamba kuna viumbe wa ajabu ambao wakitajwa kwamba, wamewahi kuonwa nchini humo na kwingine duniani. Asilimia 13 ya Wamerikani wanaamini katika nguvu ya nyota , utabiri wa karata na mengine ya aina hiyo. Kwa ujumla, idadi hiyo inaamini kwamba kuna watu wenye uwezo wa kuwatabiria wengine kuhusu maisha yao ya baadae, yaani wapiga ramli.

Taarifa ya utafiti huo yenye ukubwa wa kurasa 74 inaonesha kwamba suala la imani ya kuwepo maajabu, miujiza, nguvu za ziada na mengine ya aina hiyo hayahusiani sana na maendeleo ya sayansi au teknolojia na pia hayahusiani na kuwa na fedha au hapana.

Pamoja na maendeleo ya sayansi na pia kipato kupunguza imani ambazo zinaonekana wazi zinatokana na ujinga na ukosefu wa mahitaji yamsingi, bado inaonekana binadamu ameumbwa ili kuwa na imani za uwepo wa nguvu nyingi na kubwa zaidi zisizo na maelezo ya kimaabara..
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom