Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,268
- 33,040
Hali hii ilijitokeza baada ya Mkapa kusema wakati wa uzinduzi wa kampeni cha CCM katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki Machi 12, mwaka huu kwamba Vecent Nyerere hana undugu na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Kauli hiyo ilijibiwa na Madaraka Nyerere ambaye ni mtoto wa marehemu Nyerere aliyethibitisha kuwa Vicent ni mtoto wa baba yao mdogo hivyo ni ndugu yao kabisa.
Baada ya ufafanuzi Madaraka, Vicent alijibu kwa kumshangaa Mkapa huku akimkebehi kwa kauli yake iliyoonesha wazi kuwa alikosea kutamka maneno hayo hadharani, jambo ambalo lilionyesha kuwa hakujua ukweli kuhusu uhusiano wa Vecent na Marehemu Baba wa Taifa.
Si hivyo tu, rais mstaafu huyo ameshambuliwa kwenye majukwaa ya kampeni za Chadema na nje ya jukwaa kutoka wa wanaharakati na wadau mbalimbali hapa nchini ambao kwa nyakati tofauti walishangaa ni kwa nini aliingia katika siasa hizo chafu ambazo zimemshushia hadhi na heshima aliyojijengea katika nchi hii kutokana na mambo mazuri aliyoifanyia Tanzania kwa kipindi cha miaka 10 alipokuwa rais.
Tunajua Mkapa bado ni mwanachama hai wa CCM, ambaye anaheshimika sana kwani mbali ya kuwa Rais, alikuwa Mwenyekiti wa chama hadi alipomaliza kipindi chake cha urais, hivyo anastahili kukisaidia chama chake kinapokuwa katika kampeni mbalimbali za uchaguzi.
Lakini je, katika nafasi ya rais aliyofikia katika uongozi wa nchi hii anatikiwa kushiriki kampeni? Je, ni halali rais mstaafu anayeheshimiwa apelekwe hata kwenye kampeni za uchaguzi mdogo jimboni ambao siasa zake mara nyingi ni za kupakana matope badala ya kunadi sera za kuwakomboa wananchi?
Kwa bahati mbaya katika chaguzi mbili alizoshiriki Mkapa(wa Igunga mwishoni mwa mwaka jana na huu wa Arumeru Mashariki), alishambuliwa na kukashifiwa kwa maneno machafu ya siasa za uchaguzi wa ngazi hiyo, ambayo kwetu tunaona kuwa anashushiwa hadhi.
Kilichojitokeza kwamba, Mkapa alitumia propaganda ambazo ni za chini ikilinganishwa na nafasi, ufahamu, hekima na heshima yake. Tunadhani alifanya hivyo kwa sababu alitaka kufikisha ujumbe kwa mashabiki na wapiga kura kwa lugha aliyoamini atakubalika kutokana na vuguvugu la siasa za uchaguzi katika ngazi hiyo kutawaliwa na maneno ya kuchafuana, kama wanavyoropoka viongozi wengine katika kampeni zinazoendelea sasa huko Arumeru Mashariki.
Kuonyesha kuwa Mkapa hakustahili kusema hayo, kauli hiyo ingetolewa na mtu mwingine kama ambavyo viongozi wengine wanavyosema, hakuna ambaye angeshtuka wala kushangaa na kuanza kumshambulia.
Hiyo inadhihirisha kwamba, Mkapa kama rais mstaafu amewekwa kwenye nafasi ya juu ambayo hategemewi kusema maneno rahisi kama hayo, bali walitegemea angemwaga sera za chama chake.
Kutokana na hali hiyo, sisi tunaona kwamba, marais wastaafu kushiriki katika kampeni za uchaguzi mdogo ni kuwadhalilisha na zaidi ya hapo, hao ni viongozi wa kitaifa ambao kwa nafasi yao wanabeba jukumu la kuwa walezi na washauri wa kitaifa yanapotokea mambo magumu; ndiyo maana CCM ilishaamua kuwaondolea majukumu mengine katika chama na kubakia kuwa wazee na washauri wa chama, ili wanapoombwa kutoa ushauri na kufanya usuluhishi wasitiliwe shaka na upande wowote.
Hata kama chama chao kinawahitaji wakati wa kampeni hizo, isiwe kwa kupanda jukwaani bali wasaidie kwa kuwashauri na kuwapa mbinu za ushindi kuliko kupanda jukwaani ambapo kila analosema hupewa uzito wa juu na kisha kumhusisha nalo moja kwa moja.
Kwa sababu hiyo basi, tunashauri kwamba marais wastaafu wasitumiwe kwenye kampeni za uchaguzi hasa ngazi ua uchaguzi mdogo ili kulinda heshima yao.
Marais wastaafu wasishiriki kampeni za uchaguzi ndogo