MAONI ya Upinzani Bungeni, Ofisi ya Makamu wa Rais; Muungano; A MUST READ

Tumaini Makene

JF-Expert Member
Jan 6, 2012
2,642
6,070
MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO),​
MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)​
KUHUSU
MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO) KWA MWAKA 2012/2013
(Kanuni ya 99(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,

Mwaka huu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetimiza miaka arobaini na nane tangu kuzaliwa kwake baada ya Rais wa Jamhuri ya Tanganyika Mwalimu Nyerere kutia saini Makubaliano ya Muungano na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Sheikh Abedi Amani Karume tarehe 22 Aprili, 1964.

Wakati anawasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) aliliambia Bunge lako tukufu kwamba "... katika kipindi hicho Muungano wetu umekuwa na mafanikio katika maeneo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.... Muungano wetu ndio nguzo kuu ya umoja na amani."

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri aliliambia Bunge lako tukufu kwamba, licha ya mafanikio hayo, "... zipo changamoto katika kumaliza vikwazo vinavyokwamisha shughuli za Muungano." Mheshimiwa Waziri hakuzitaja changamoto hizo.


‘MAPITO' YA MUUNGANO

Mheshimiwa Spika,

Katika Utangulizi wake kwa Chapisho la Pili la Mhadhara wa Kiprofesa (Professorial Inaugural Lecture) uliotolewa Januari 1990 na Profesa Issa G. Shivji na kupewa kichwa cha Tanzania: The Legal Foundations of the Union, Profesa Yash Ghai - aliyekuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa kwanza kutoka Afrika Mashariki - anasema kwamba kwa kuzingatia mazingira ya kuanzishwa kwa Muungano na historia yake, "... kitu cha ajabu sio kwamba umekuwa na matatizo, bali ni kwamba umedumu (licha ya matatizo hayo) – na kwenda kinyume na mwelekeo katika Afrika."

Muungano ulidumu misuguano ya miaka ya mwanzo kati ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume iliyohusu kuongezwa kwa masuala ya fedha na sarafu katika orodha ya Mambo ya Muungano. Aidha, Muungano ulidumu mauaji ya viongozi waandamizi na wajumbe wa Baraza la Mapinduzi la kwanza la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kama Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Abdallah Kassim Hanga, Waziri wa Fedha Abdul Aziz Twala, Othman Sharrif, Mdungi Ussi, Saleh Saadalla na wengine wengi.

Vile vile, Muungano ulidumu mauaji ya Sheikh Karume mwenyewe mwaka 1972; ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa' Zanzibar iliyopelekea kung'olewa madarakani kwa Rais Aboud Jumbe mwaka 1984; alichokiita Mwalimu Nyerere ‘udhaifu' wa Rais Mwinyi; na kifo cha Mwalimu Nyerere mwaka 1999.

Kwa bahati mbaya, Mheshimiwa Spika, ‘mapito' haya ya Muungano yamekuwa yanafichwa fichwa, licha ya kauli za mara kwa mara za ‘kuelimisha umma juu ya Muungano.' Kwa sababu hiyo, zaidi ya tendo la kuchanganya udongo na matukio mengine yaliyofanyika hadharani, historia halisi ya Muungano wetu haifahamiki kwa wananchi walio wengi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba wakati umefika sasa kwa Serikali kuweka wazi nyaraka mbali mbali zinazohusu historia ya Muungano wetu na ‘mapito' yake ili Watanzania waelewe masuala yote yaliyotokea yanayouhusu.

Hii ni muhimu zaidi kwa kuzingatia ukweli kwamba mataifa ya magharibi kama vile Marekani na Uingereza yalikwishatoa hadharani nyaraka za mashirika yao ya kijasusi pamoja na balozi zao za Tanzania zinazoonyesha jinsi ambavyo serikali za mataifa hayo zilihusika katika kuzaliwa kwa Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Kuanikwa kwa nyaraka zilizoko katika mamlaka mbali mbali za Serikali kutasaidia kuthibitisha au kukanusha taarifa ambazo chanzo chake ni nyaraka za kidiplomasia na kijasusi za nchi hizo kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokana na njama za kibeberu za kudhibiti ushawishi wa siasa za kimapinduzi za Chama cha Umma na viongozi wake ndani ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar la wakati huo.

Aidha, nyaraka hizo zitatoa mwanga juu ya kilichowasibu viongozi waandamizi wa chama hicho ambao bila uwepo wao kutambuliwa rasmi, historia ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Muungano inabaki pungufu. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, miaka karibu hamsini ya Muungano ni umri wa kutosha kwa taifa la Tanzania kuambiwa ukweli wote juu ya kuzaliwa kwake na mapito ambayo limepitia katika kipindi hicho.

UKIUKWAJI MAKUBALIANO/SHERIA YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,

Makubaliano ya Muungano ya tarehe 22 Aprili 1964 yalikuwa ni mkataba wa kimataifa kati ya nchi mbili huru zilizokubaliana kuunda ‘nchi moja huru', kwa mujibu wa ibara ya (i) ya Hati ya Muungano. Ili kutekeleza Makubaliano ya Muungano, Bunge la Jamhuri ya Tanganyika lilitunga Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, 1964, Sura ya 557 ya Sheria za Tanzania. Kifungu cha 4 cha Sheria hiyo kilitangaza kuunganishwa kwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuwa ‘Jamhuri moja huru itakayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.'

Kwa upande wa Zanzibar, Baraza la Mapinduzi – ambalo ndio lilikuwa ‘Bunge' la Zanzibar wakati huo – halikutunga sheria ya kuridhia Makubaliano ya Muungano. Jambo hili limekuwa chanzo cha mjadala mkali katika duru za kitaaluma na kisheria juu ya uhalali wa Muungano wenyewe. Kwa vyovyote vile, matokeo ya kusainiwa Makubaliano ya Muungano ni kwamba Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zilikufa na nchi moja – iliyokuja baadae kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - kuzaliwa.

Mheshimiwa Spika,

Kwa mujibu wa aya ya (iv) ya Makubaliano ya Muungano na kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Muungano, Mambo ya Muungano yaliyokubaliwa kwenye Makubaliano ya Muungano yalikuwa kumi na moja. Haya ni mambo yaliyoko katika vipengele vya 1 hadi 11 vya Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Muungano. Hata hivyo, kati ya mwaka 1964 and 1973 mambo mengine sita – yanayoonekana katika vipengele 12 hadi 16 vya Nyongeza ya Kwanza – yaliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano.

Hivyo basi, mwaka 1965 masuala ya fedha, sarafu na benki yaliongezwa; mwaka 1967 leseni ya viwanda na takwimu, elimu ya juu na mambo yaliyokuwa katika Nyongeza ya X ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliongezwa; mwaka 1968 yaliongezwa mambo ya maliasili ya mafuta, petroli na gesi asilia; na mwaka 1973 mambo yanayohusu Baraza la Mitihani la Taifa yaliongezwa.

Aidha, Mheshimiwa Spika, Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya mwaka 1984 yaligawa kipengele cha Nyongeza ya X ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutengeneza vipengele vinne vinavyojitegemea katika orodha ya Mambo ya Muungano, yaani usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, utabiri wa hali ya hewa na takwimu.

Vile vile, Mabadiliko hayo yaliongeza kitu kipya katika orodha ya Mambo ya Muungano: Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Aidha, kipengele cha 3, yaani ulinzi, kilifanyiwa marekebisho na kuwa ‘ulinzi na usalama.' Na mwaka 1992 ‘uandikishwaji wa vyama vya siasa' nao uliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Mambo yote yaliyoongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano baada ya mwaka 1964 yalikuwa nje ya Makubaliano ya Muungano na nje ya Sheria ya Muungano na kwa hiyo yalikuwa batili. Hii ni kwa sababu Sheria ya Muungano – na sio Katiba za Muda za 1964 au 1965 au ya sasa - ndio Sheria Mama iliyozaa Muungano na kuweka mgawanyo wa madaraka kati ya mamlaka za Jamhuri ya Muungano na mamlaka za Zanzibar. Sheria ya Muungano ilitungwa na Bunge la Katiba tofauti na sheria za kawaida.

Aidha, Katiba ya Muda, 1965 iliyotawala Tanzania hadi 1977 iliiweka Sheria hiyo kama Nyongeza ya Pili katika Katiba na kuweka masharti kwamba Sheria hiyo haiwezi kurekebishwa bila marekebisho hayo kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote wa Tanganyika na wale wa Zanzibar. Vile vile, Katiba ya Muunganoinataja, katika Orodha ya Kwanza ya Nyongeza ya Pili, kwamba moja ya Sheria ambazo mabadiliko yake yahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote ni "Sura ya 557 (Toleo la 1965), Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964."

Mambo yote haya, Mheshimiwa Spika, yanaifanya Sheria ya Muungano kuwa na haiba ya Katiba. Kama alivyosema Profesa Issa Shivji katika The Legal Foundations of the Union: "Kila mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa sheria amefundishwa kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapatikana katika waraka unaoitwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Lakini, nachelea kusema, kila mwanafunzi amefundishwa visivyo.

Katiba ya Tanzania inapatikana sio katika waraka mmoja, bali katika nyaraka mbili. Sheria ya Muungano, Sura ya 557 ya Sheria za Tanzania na Sheria ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.... Vivyo hivyo, Katiba ya Zanzibar inapatikana katika (1) Sheria ya Muungano na (2) Katiba ya Zanzibar, 1984
." Katika masuala yanayohusu Muungano, kwa mujibu wa Profesa Shivji, waraka unaotawala ni Sheria ya Muungano.

Hii ndio kusema kwamba panapotokea mgongano kati ya Katiba au Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Muungano, ni Sheria ya Muungano ndio inayokuwa na Katiba au Katiba ya Zanzibar inakuwa batili kwa kiasi cha ukiukaji wake wa Sheria ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Kifungu cha 5 cha Sheria ya Muungano, ambacho ndicho chenye misingi mikuu ya Muungano hakijawahi kurekebishwa tangu Sheria yenyewe ilipotungwa mwaka 1964. Badala yake, Bunge limekuwa na tabia ya kukwepa kuigusa kabisa Sheria ya Muungano na badala yake limekuwa likifanya marekebisho ya orodha ya Mambo ya Muungano iliyowekwa kwa mara ya kwanza katika Katiba za Muda za mwaka 1964 na 1965 kwa kuongeza vipengele katika orodha hiyo. Lengo la marekebisho haya, Mheshimiwa Spika, limekuwa mara zote ni kuinyang'anya Zanzibar mamlaka yake chini ya Sheria ya Muungano.

Ndio maana katika Mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya CCM Kuhusu Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yaliyotolewa tarehe 27 Januari, 1983, CCM ilitamka kwamba "... msingi wa kuwa na orodha ya mambo ya muungano katika Katiba ni kuonyesha mamlaka ya Serikali ya Zanzibar ambayo yalikabidhiwa kwa Serikali ya Muungano; na msingi wa kuongeza mambo zaidi katika orodha ya mambo ya muungano, kama ambavyo imefanyika mara kwa mara, ni kuhamisha mamlaka zaidi ya Serikali ya Zanzibar kwenda kwa Serikali ya Muungano."

Mheshimiwa Spika,

Profesa Shivji anasema - katika The Legal Foundations of the Union - kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano halikupewa mamlaka ya kuongeza Mambo ya Muungano bali lilipewa mamlaka ya kutunga sheria zinazohusu Mambo ya Muungano kama yalivyofafanuliwa katika Sheria ya Muungano. Kwa maana hiyo, nyongeza zote zilizofanyika katika orodha ya Mambo ya Muungano tangu mwaka 1964 zilikiuka Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano na ni batili. Ndio maana, kwa muda mrefu, Wazanzibari wamelalamikia masuala haya, hasa hasa masuala ya fedha, sarafu na mafuta na gesi asilia.

Mheshimiwa Spika,

Vitendo vya kupuuza Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano vilifikia kilele chake tarehe 21 Novemba, 2000 pale Mahakama ya Rufani ya Tanzania ilipotamka – katika kesi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar dhidi ya Machano Khamis Ali na Wenzake 17 – kwamba Zanzibar sio nchi na wala sio dola. Bali, kwa mujibu wa Mahakama ya Rufani, ‘hakuna ubishi wa aina yoyote kwamba Jamhuri ya Muungano ni nchi moja na dola moja.'

Kama tulivyokwisha kuonyesha, suala la Mahakama ya Rufani ya Tanzania yenyewe kuwa suala la Muungano liliingizwa kwenye orodha ya Mambo ya Muungano kinyemela na kinyume na Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano. Jibu la Wazanzibari juu ya ukiukwaji wa muda mrefu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano hayo lilikuwa ni kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar mwaka 2010.

KATIBA YA MUAFAKA AU KATIBA YA UHURU?​
Mheshimiwa Spika,

Misukosuko ambayo imeukumba Muungano wetu tangu mwaka 1964 hailingani na hatari kubwa inayoukabili hivi sasa. Kama tulivyomweleza Rais Kikwete katika waraka wetu wa tarehe 27 Novemba, 2011, "Muungano wetu upo katika hatari kubwa ya kuvunjika kwa sababu ya mabadiliko makubwa ya kikatiba ambayo yamefanyika katika Katiba ya Zanzibar, 1984 na kutokana na Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Hii ni kwa sababu Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba, 2010, inaashiria tafsiri mpya ya Makubaliano ya Muungano na ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inahoji misingi ya Jamhuri ya Muungano kama nchi moja, mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, na mambo muhimu ya Muungano....
" Ili kufahamu jambo hili vizuri, ni muhimu kuelewa kwa undani yaliyomo katika Sheria hiyo ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,

Tarehe 13 Agosti, 2010, wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano likiwa limevunjwa kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilipitisha Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar, 1984. Mabadiliko haya yaliweka msingi wa kikatiba wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar inayoshirikisha CCM na Chama cha Wananchi (CUF). Kwa sababu hiyo, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imepigiwa upatu kama Katiba ya Muafaka na, kwa kiasi fulani, hii ni kweli.

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba imekwenda mbali zaidi. Sheria hii sio tu imehoji uhalali wa orodha ya Mambo ya Muungano ya tangu mwaka 1964 na nyongeza zake zilizofuata, bali pia imehoji pia misingi muhimu ya Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano ya Muungano. Kwa mtazamo huu, Katiba ya sasa ya Zanzibar inaelekea kuwa ni tangazo la uhuru wa Zanzibar zaidi kuliko waraka wa muafaka kati ya vyama viwili vilivyokuwa mahasimu.

Mheshimiwa Spika,
Aya ya (i) ya Makubaliano ya Muungano na kifungu cha 4 cha Sheria ya Muungano vilitangaza muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuundwa kwa ‘Jamhuri moja huru itakayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.'

Huu ndio msingi wa maneno ya ibara ya 1 ya Katiba ya Muungano kwamba ‘Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.' Na huu ndio ulikuwa msingi wa maneno ya ibara ya 1 ya Katiba ya Zanzibar ya kabla ya Mabadiliko ya 2010 kwamba ‘Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.' Sasa msingi huu wa Muungano umehojiwa na maneno ya ibara ya 2 ya Katiba mpya ya Zanzibar yanayotamka kwamba ‘Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.'

Mheshimiwa Spika,

Ibara ya 2(2) ya Katiba ya Muungano inampa Rais wa Jamhuri ya Muungano – kwa kushauriana kwanza na Rais wa Zanzibar - mamlaka ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya au maeneo mengineyo. Vile vile, ibara ya 61(3) ya Katiba ya Muungano inampa Rais wa Zanzibar mamlaka ya kuteua Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Zanzibar ‘baada ya kushauriana na Rais.' Masuala ya mgawanyo wa nchi katika mikoa na mamlaka za mikoa hiyo sio, na hayajawahi kuwa, Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Muungano.

Vile vile hayapo katika orodha ya Mambo ya Muungano. Ni wazi kwa hiyo, kwamba ibara za 2(2) na 61(3) za Katiba ya Muungano zilikuwa zinakiuka matakwa ya Sheria ya Muungano na kwa hiyo ni batili. Sasa wazanzibari ‘wamejitangazia uhuru' kwa kutangaza – katika ibara ya 2A ya Katiba mpya ya Zanzibar – kwamba "... Rais (wa Zanzibar) aweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi." Aidha, kwa ibara ya 61(1), Rais wa Zanzibar hawajibiki tena kushauriana na Rais wa Muungano pale anapofanya uteuzi wa wakuu wa mikoa ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,

Wakati ambapo Sheria ya Muungano ilikuwa imetambua na kuhifadhi mamlaka ya Rais wa Zanzibar kama mkuu wa dola ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Tanzania – katika Kesi ya Machano Khamis Ali na Wenzake – ilitishia moja kwa moja msingi huo kwa kutamka kwamba Zanzibar sio nchi na wala sio dola na kwa hiyo haiwezi kutishiwa na kosa la uhaini.

Sasa ibara ya 26(1) ya Katiba mpya Zanzibar ‘imerudisha' dola ya Zanzibar kwa kutamka kwamba "kutakuwa na Rais wa Zanzibar ambaye atakuwa Mkuu wa Nchi ya Zanzibar, Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi." Aidha, kwa kutambua kwamba ‘Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano' sio moja ya Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Muungano, Katiba ya sasa ya Zanzibar imetamka kwamba katika kesi zinazohusu ‘kinga za haki za lazima, wajibu na uhuru wa mtu binafsi', uamuzi wa majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar "... utakuwa ni wa mwisho na hautokatiwa rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Tanzania."

Mheshimiwa Spika,

Kifungu cha 5(1)(a)(iii) na (iv) cha Sheria ya Muungano kinataja ‘ulinzi' na ‘polisi' kama sehemu ya mambo kumi na moja ya Muungano. Na hivyo ndivyo inavyosema aya ya (iv)(c) na (d) ya Makubaliano ya Muungano. Ijapokuwa ‘ulinzi' ulichakachuliwa baadae kwa kuongezwa maneno ‘na usalama', bado ni sahihi kusema kwamba masuala ya ulinzi na polisi ni masuala halali ambayo Sheria ya Muungano iliyakasimu kwa Serikali ya Muungano.

Na kwa sababu hiyo, ni sahihi kwa Katiba ya Muungano kutamka – kama inavyofanya katika ibara ya 33(2) - kwamba ‘Rais (wa Jamhuri ya Muungano) atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.'

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, katika kile kinachoonekana kama hojaji kubwa ya msingi huu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano, ibara ya 121 ya Katiba ya sasa ya Zanzibar imeunda majeshi ya Zanzibar inayoyaita ‘Idara Maalum.'

Majeshi haya, kwa mujibu wa ibara ya 121(2) ni Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU); Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM); Chuo cha Mafunzo (cha wahalifu), na Idara Maalum nyingine yoyote ambayo Rais wa Zanzibar anaweza kuianzisha ‘ikiwa ataona inafaa....' Kuthibitisha kwamba Idara Maalum ni majeshi, ibara ya 121(4) inakataza watumishi wa Idara Maalum '... kujishughulisha na mambo ya siasa....' Makatazo haya hayatofautiani na makatazo ya wanajeshi kujiunga na vyama vya siasa yaliyoko katika ibara ya 147(3) ya Katiba ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Sio tu kwamba Katiba mpya ya Zanzibar inaanzisha majeshi bali pia inamfanya Rais wa Zanzibar kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi hayo. Kwa mujibu wa ibara ya 123(1) ya Katiba hiyo, "Rais atakuwa Kamanda Mkuu wa Idara Maalum na atakuwa na uwezo wa kufanya chochote kile anachohisi, kwa maslahi ya Taifa (la Zanzibar), kinafaa." Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 123(2), mamlaka ya Rais wa Zanzibar chini ya ibara ndogo ya (1) yanaingiza "... uwezo wa kutoa amri ya kufanya shughuli yoyote inayohusiana na Idara hiyo kwa manufaa ya Taifa."

Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, haya ni mamlaka ya kutangaza au kuendesha vita ambayo, kwa mujibu wa ibara ya 44(1) ya Katiba ya Muungano, ni mamlaka pekee ya Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama tafsiri hii ya ibara ya 123 ya Katiba mpya ya Zanzibar ni sahihi.

Na kama ni sahihi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe tamko Bungeni ni kwa nini imeiruhusu Zanzibar kujinyakulia mamlaka juu ya mambo ya ulinzi na usalama ambayo kwa historia yote ya Muungano yamekuwa ni mamlaka pekee ya Serikali ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Kifungu cha 5(1)(b) cha Sheria ya Muungano kilitamka kwamba muundo wa Serikali ya Zanzibar utakuwa kama utakavyoamuliwa na sheria za Zanzibar pekee. Na hivyo ndivyo ilivyokubaliwa katika aya ya (iii)(a) ya Makubaliano ya Muungano. Hata hivyo, licha ya muundo wa Serikali ya Zanzibar kutokuwepo katika orodha ya Mambo ya Muungano, Katiba ya Muungano imetenga Sura ya Nne nzima kuzungumzia ‘Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.'

Kwa mujibu wa Profesa Shivji katika The Legal Foundations of the Union, Sura ya Nne ya Katiba ya Muungano "... haina ulazima wowote na ni kuingilia, bila kualikwa, kwenye mambo ambayo yako ndani ya mamlaka pekee ya Zanzibar." Ndio maana Katiba mpya ya Zanzibar – kwa usahihi kabisa - imefanya mabadiliko katika muundo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar bila ya kuzingatia matakwa ya Sura ya Nne ya Katiba ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Katiba mpya ya Zanzibar sio tu kwamba ‘imetangaza uhuru' wa Zanzibar kwa kuhoji misingi muhimu ya Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano, bali pia imehakikisha kwamba uhuru huo utalindwa dhidi ya tishio lolote la Serikali ya Muungano. Hii imefanywa kwa kuweka utaratibu wa kuwepo kura ya maoni ya wananchi wa Zanzibar kuhusu mabadiliko ya vifungu kadhaa vya Katiba ya Zanzibar. Kwa mujibu wa ibara ya 80A(1) ya Katiba hiyo, "... Baraza la Wawakilishi halitaweza kufanya mabadiliko ya Katiba kuhusiana na sharti lolote lililomo katika kifungu chochote kilichoainishwa katika kijifungu cha (2) cha kifungu hiki, mpaka kwanza mabadiliko hayo yakubaliwe na wananchi kwa kura ya maoni."

Vifungu vinavyohitaji kura ya maoni ni vifungu vyote vya Sehemu ya Kwanza ya Sura ya Kwanza inayohusu Zanzibar kama nchi na/au dola; kifungu cha 9 kinachohusu Serikali na watu wa Zanzibar; vifungu vyote vya Sura ya Tatu inayohusu kinga ya haki za lazima, wajibu na uhuru wa mtu binafsi; na kifungu cha 26 kinachohusu Rais wa Zanzibar na mamlaka yake.

Vifungu vingine ni pamoja na kifungu cha 28 kinachohusu muda wa urais; Sehemu ya Pili na ya Tatu ya Sura ya Nne zinazohusu Makamu wawili wa Rais, Baraza la Mawaziri na Baraza la Mapinduzi; kifungu cha 80A kinachohifadhi haki ya kura ya maoni; na vifungu vya 121 na 123 vinavyohusu Idara Maalum na mambo yanayohusiana nayo.

Mheshimiwa Spika,

Kuweka masharti ya kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya vifungu tajwa vya Katiba mpya ya Zanzibar kuna athari ya moja kwa moja kwa uhai wa Muungano wetu. Hii ni kwa sababu hata vifungu ambavyo tumeonyesha kwamba vinakiuka misingi mikuu ya Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano haviwezi kubadilishwa bila kura ya maoni ya Wazanzibari.

Kwa maneno mengine, kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, masuala ya kama Tanzania ni nchi moja au la, majeshi ya ulinzi, polisi, n.k. ambayo yamekuwa Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano sio Mambo ya Muungano tena hadi hapo wananchi wa Zanzibar watakapoamua – kwa kura ya maoni – kuyarudisha kwa mamlaka ya Muungano. Huku, Mheshimiwa Spika, ni kutangaza uhuru wa Zanzibar bila kutaja neno uhuru! Huku ni kuua Muungano bila kukiri hadharani!

Mheshimiwa Spika,

Kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, hatuna tena nchi moja inayozungumzwa katika Katiba ya Muungano bali tuna nchi mbili. Kwa mtazamo huo huo, masuala ya ulinzi na usalama, polisi, n.k. sio tena Mambo ya Muungano kwa sababu sasa kila nchi ina majeshi yake na kila moja ina Amiri Jeshi Mkuu wake. Aidha, tuna marais wawili, wakuu wa nchi wawili viongozi wa serikali wawili. Haya yote yanakiuka moja kwa moja Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano.

Kwa upande mwingine, kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, Rais wa Muungano hana tena mamlaka ya kugawa mikoa na wilaya kwa upande wa Zanzibar, na wala hawezi kumshauri tena Rais wa Zanzibar anapoteua Wakuu wa Mikoa wa Tanzania Zanzibar. Aidha, Mahakama ya Rufani ya Tanzania – licha ya kuwa moja ya Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya Muungano - haina tena mamlaka ya kusikiliza na kuamua rufaa zinazohusu haki za msingi na uhuru wa mtu binafsi zinazotoka Zanzibar. Yote haya hayapo katika Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano lakini yapo katika Katiba ya Muungano.

KURUDISHWA KWA SERIKALI YA TANGANYIKA

Mheshimiwa Spika,

Katika maoni yetu kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilionyesha jinsi ambavyo "tafsiri hii mpya ya Makubaliano ya Muungano na Katiba ya Jamhuri ya Muungano imetiliwa nguvu kubwa na Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo imeipa Zanzibar nafasi na ushawishi mkubwa katika utungaji wa Katiba Mpya."

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilionyesha kwamba, kwa mujibu wa Sheria hiyo, "Rais wa Zanzibar sio tu kwamba ana mamlaka karibu sawa na Rais wa Jamhuri ya Muungano bali pia ana kura ya turufu katika mchakato mzima wa Katiba Mpya." Aidha, tulithibitisha jinsi ambavyo "... ushawishi mkubwa wa Zanzibar hauishii katika kura ya turufu aliyo nayo Rais wa Zanzibar pekee yake (bali) Zanzibar ina ushawishi mkubwa vile vile kutokana na nafasi kubwa iliyo nayo katika vyombo vingine vinavyoundwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba...."

Mheshimiwa Spika,

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia tena tahadhari iliyoitoa wakati huo kwamba: "Masharti haya ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yana athari kubwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu yanakiuka Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano na hata Katiba ya sasa ya Zanzibar...." Na kama tulivyosema wakati huo, "... tafsiri hii mpya ya Makubaliano ya Muungano na ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inarudisha mezani mjadala juu ya muundo wa Muungano wetu na nafasi ya iliyokuwa Tanganyika katika Muungano huo."

Mheshimiwa Spika,

Kama ilivyo kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba katika mazingira ambayo upande mmoja wa Muungano umejitangazia uhuru kama ambavyo tumeonyesha hapa, huu ni wakati muafaka kuanzishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika.

Katika mazingira ambayo upande mmoja wa Muungano sio tu una Serikali kamili, Bunge kamili, Mahakama kamili, wimbo wa taifa, bendera ya taifa, na sasa una nchi kamili yenye mipaka na eneo la bahari linalojulikana, una majeshi yake na Amiri Jeshi Mkuu wake, huu ni muda mzuri kwa Serikali ya Tanganyika kuzaliwa upya. Katika mazingira kama haya, Mheshimiwa Spika, upande wa pili wa Muungano unatakiwa kuwa na vitu vyote hivyo pia ili uweze kujadiliana na upande wa kwanza katika hali ya usawa.

Huu ni wakati wa kurudishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika kama ilivyopendekezwa na Tume ya Rais ya Chama Kimoja au Vyama vingi mwaka 1991 na Tume ya Kissanga mwaka 1998, na kama ilivyopendekezwa na Kundi la Wabunge 55 wa Bunge hili tukufu na kuungwa mkono na Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi kabla ya hoja hiyo kutunguliwa na Baba wa Taifa mwaka 1993!

KURA YA MAONI JUU YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaielekeza Tume ya Katiba kuongozwa na misingi mikuu ya kitaifa ya kuhifadhi na kudumisha ‘kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano.' Hata hivyo, baada ya kujitokeza kwa wananchi wanaopinga kuendelea kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba amesema kwamba wale wanaopinga Muungano nao wajitokeze kutoa maoni yao kwa Tume.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu ni namna gani maoni ya wale wanaotaka kiini macho hiki cha Muungano kiishe yatashughulikiwa na Tume ambayo imepewa jukumu kisheria la kukihifadhi na kukidumisha kiini macho hicho? Ni kipi kitakachoizuia Tume ya Warioba kupuuza maoni ya watu hao kwa hoja kwamba Sheria inaielekeza Tume kuratibu na kukusanya maoni na kutoa mapendekezo ya kuhifadhi na kudumisha Muungano?
Mheshimiwa Spika,

Katika miezi ya karibuni kumejitokeza makundi ya wananchi, hasa kwa upande wa Zanzibar, ambayo yamedai kwamba iitishwe kura ya maoni ya wananchi ili kuamua kama bado kuna haja ya kuendelea na Muungano. Makundi haya, yakiongozwa na kundi la Uamsho, yameshambuliwa sana hadharani kwa kudaiwa kwamba yanataka kuvunja Muungano. Na watu ambao wameongoza mashambulizi dhidi ya wana-Uamsho ni viongozi waandamizi wa CCM, wakiwemo viongozi wakuu wastaafu wa chama hicho.

Mheshimiwa Spika,

Katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tulisema kwamba "... hofu ... ya kuwaudhi ‘Wazanzibari' ndio imepelekea kimya kikuu – ndani ya CCM na ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano - juu ya ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano uliofanywa na Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar, 2010." Naomba nikiri kwamba tulikosea kusema hivyo.

Tulichotakiwa kusema wakati ule, na tunachokisema sasa, ni kwamba kimya kikuu ndani ya CCM na ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya ukiukwaji mkubwa wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano pamoja na Katiba kinatokana sio tu na ‘hofu' ya kuwaudhi Wazanzibari bali pia kinatokana na ukweli kwamba viongozi waandamizi wa CCM pamoja na wa Serikali yake walishiriki katika ukiukwaji huo!

Wao ndio wanaoongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ndio waliondaa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar. Na wao ndio wanaoongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano waliokula kiapo cha kuihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Na kwa hiyo wao ndio walioiruhusu Zanzibar kutangaza uhuru kwa Mabadiliko haya ya Katiba yake.


Mheshimiwa Spika,

Kwa viongozi hawa na chama chao kuibuka sasa na kuwatuhumu wana-Uamsho na makundi mengine kwamba wanataka kuvunja Muungano kwa kudai kura ya maoni ya wananchi wakati wao wenyewe wamekaa na kupitisha marekebisho ya Katiba ambayo tayari yamevunja Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano ni kilele cha juu cha unafiki wa kisiasa. Mashabiki hawa wa Muungano waeleze walikuwa wapi wakati Zanzibar inatangaza uhuru wake kwa kuchanachana Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano.

Mheshimiwa Spika,

Kwa wale wanaodai kwamba wana-Uamsho wanataka kuvunja Muungano kwa sababu tu ya kudai kura ya maoni, tunaomba tuwakumbushe yafuatayo. Kwanza, kwa mujibu wa Baba wa Taifa katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania: "Huko nyuma baadhi ya viongozi wa Zanzibar wapinzani wa Muungano wamewahi kudai tufanye referendum kwa Zanzibar kuhusu Muungano. Tukakataa kwa sababu safi kabisa."

Hapa Mwalimu alikuwa anamzungumzia aliyekuwa Rais wa Zanzibar Alhaj Aboud Jumbe
, Waziri Kiongozi Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Bashir Ebassuah Kwaw Swanzy waliong'olewa madarakani mwaka 1984 baada ya ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa.'

Aidha, Mheshimiwa Spika, katika kitabu hicho hicho Mwalimu Nyerere anasema yafuatayo juu ya kilichotokea kwenye Bunge hili hili wakati wa Bunge la bajeti la mwaka 1993: "Tarehe 30 Julai, 1993 wakati wa mkutano wa bunge la bajeti ukiendelea, zaidi ya wabunge 50 kwa pamoja walitoa taarifa ya kusudio la kuwasilisha hoja Bungeni ambayo inadai (kwamba) kuendelea na mfumo huu wa Muungano usiowaridhisha wananchi wengi wa upande mmoja ni kuhatarisha kuendelea kudumu kwa Muungano....

Hivyo basi wabunge hawa wanaliomba Bunge ... liazimie kwamba Serikali ... ilete Muswada Bungeni kabla ya Februari 1994, kurekebisha katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kuwezesha uundaji wa ‘Serikali ya Tanganyika' ndani ya Muungano.... Tarehe 20 Agosti, 1993 wabunge wahusika waliwasilisha taarifa nyingine ... iliyokuwa inalitaka Bunge ... liazimie kwamba Serikali ... iandae kura ya maoni ambayo itafanyika kabla ya 31 Desemba, 1994 ili kupata maoni ya wananchi wa Tanzania juu ya kuundwa kwa "Serikali ya Tanganyika" ndani ya Muundo wa Muungano....
"


Pili, Mheshimiwa Spika, Katiba ya sasa ya Zanzibar ambayo mashabiki wa Muungano wameileta kwa kupitia Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba tayari imewapa wananchi wa Zanzibar haki ya kuamua, kwa kura ya maoni, mambo mbali mbali yanayoihusu nchi hiyo na namna itakavyoongozwa. Mashabiki hawa wa Muungano wakubali kuvuna walichopanda, wasibeze wale wote wanaotaka kutumia haki ya kura ya maoni kuamua hatma ya Muungano na nafasi ya Zanzibar ndani au nje yake.

Mheshimiwa Spika,

Ni wazi, kwa kuzingatia ushahidi huu, kwamba madai ya kuwa na kura ya maoni ya wananchi ili kuamua masuala makubwa yanayohusu Muungano wetu ni ya siku nyingi na yametolewa na watu na taasisi mbali mbali. Madai haya hayajaanzishwa na wana-Uamsho wala CHADEMA. Ni wazi vile vile kwamba kura ya maoni inaruhusiwa kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar.

Kwa sababu hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaungana na wale wote ambao wamedai, na wanaendelea kudai kuitishwa kura ya maoni ya wananchi ili waweze kuamua mustakbala wa nchi yetu. Kuendelea na kiini macho cha Muungano wakati Serikali zote mbili na chama tawala cha CCM wanauvunja kivitendo kutaipelekea nchi yetu kwenye njia ya Ethiopia na Eritrea, au Sudan na Sudan Kusini au Yugoslavia ya zamani.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Watanzania waamue, kwa kura ya maoni, kama bado wanataka kuendelea na Muungano na kama jibu lao ni ndio, ni muundo gani wa Muungano wanautaka. Kama, kwa busara zao, wataamua kwamba nusu karne ya Muungano inatosha basi itakuwa afadhali kwenda njia ya Czechoslovakia ya zamani kuliko kwenda njia ya Yugoslavia ya zamani, au Ethiopia na Eritrea au Sudan na Sudan Kusini.

Mwisho, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwaeleze Watanzania juu ya hatua, kama zipo, ilizozichukua kuzuia ukiukwaji huu wa Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba. Na mwisho, Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu kama - kwa ukiukwaji huu wa Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano – Bunge hili tukufu litakuwa ndani ya mamlaka yake kuchukua hatua za kumshtaki Rais kwa mujibu wa ibara ya 46A ya Katiba kwa kushindwa kuihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Muungano kama kiapo cha kazi yake kinavyomtaka.

HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wajumbe wote wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni chini ya uongozi wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman A. Mbowe kwa ushauri na ushirikiano uliowezesha maandalizi ya maoni haya. Aidha, niwashukuru familia yangu – mke wangu mpenzi Alicia Bosensera na mapacha wetu Agostino Lissu na Edward Bulali – kwa kuendelea kuvumilia upweke unaotokana na 'Daddy' kuwa mbali muda mwingi kwa sababu ya majukumu mazito ya kibunge.

Aidha, niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Singida Mashariki kwa imani na nguvu wanayonipa kila siku kwa kuendeleza msimamo wetu thabiti wa kukataa kunyanyaswa, kunyonywa na kupuuzwa na ‘Ndaa ya Njou'! Mwisho naomba nichukue fursa hii kuwashukuru viongozi, wanachama na wapenzi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wananchi wote wa Tanzania ambao wameendelea kutuunga mkono na kututia nguvu katika kipindi hiki muhimu katika historia ya nchi yetu. Ninawaomba waendelee kutuunga mkono na kututia nguvu katika siku ngumu na za majaribu makubwa zinazokuja!

Mheshimiwa Spika,

Baada ya maelezo haya marefu, naomba kukushukuru na wewe binafsi na naomba kuwasilisha.

---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO)
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
 
Wale wabunge wa Zanzibar wasome hii hotuba kwa makini sana kabla hawaanza kuichangia. Kwa mtizazamo wangu inaendena sana na hisia za wazanzibari wengi including UAMSHO. Kama wabunge hawa toka Zanzibar watarudia kauli za mwaka jana, watajikuta wako kwenye mtihani na wapiga kura wao. Sehemu ya muhimu wanatakia kusoma ni hii hapa:

"...Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaungana na wale wote ambao wamedai, na wanaendelea kudai kuitishwa kura ya maoni ya wananchi ili waweze kuamua mustakbala wa nchi yetu. Kuendelea na kiini macho cha Muungano wakati Serikali zote mbili na chama tawala cha CCM wanauvunja kivitendo kutaipelekea nchi yetu kwenye njia ya Ethiopia na Eritrea, au Sudan na Sudan Kusini au Yugoslavia ya zamani.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Watanzania waamue, kwa kura ya maoni, kama bado wanataka kuendelea na Muungano na kama jibu lao ni ndio, ni muundo gani wa Muungano wanautaka. Kama, kwa busara zao, wataamua kwamba nusu karne ya Muungano inatosha basi itakuwa afadhali kwenda njia ya Czechoslovakia ya zamani kuliko kwenda njia ya Yugoslavia ya zamani, au Ethiopia na Eritrea au Sudan na Sudan Kusini".
 
'Kitu' kiko makini sana hiki. Bila chadema nchi hii itakuwa na 'mbumbumbu' wengi sana!
 
kwa umakini naona kuna move ya kutaka kuwepo kwa Tanganyika yetu.
 
KURUDISHWA KWA SERIKALI YA TANGANYIKA

Katika mazingira ambayo upande mmoja wa Muungano sio tu una Serikali kamili, Bunge kamili, Mahakama kamili, wimbo wa taifa, bendera ya taifa, na sasa una nchi kamili yenye mipaka na eneo la bahari linalojulikana, una majeshi yake na Amiri Jeshi Mkuu wake, huu ni muda mzuri kwa Serikali ya Tanganyika kuzaliwa upya. Katika mazingira kama haya, Mheshimiwa Spika, upande wa pili wa Muungano unatakiwa kuwa na vitu vyote hivyo pia ili uweze kujadiliana na upande wa kwanza katika hali ya usawa.

Huu ni wakati wa kurudishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika kama ilivyopendekezwa na Tume ya Rais ya Chama Kimoja au Vyama vingi mwaka 1991 na Tume ya Kissanga mwaka 1998, na kama ilivyopendekezwa na Kundi la Wabunge 55 wa Bunge hili tukufu na kuungwa mkono na Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi kabla ya hoja hiyo kutunguliwa na Baba wa Taifa mwaka 1993!

Hapo kwenye red: Watakana?
 
Tundu Lissu alikuwa makini sana na amechangia kwa uangalifu mno katika hotuba yake hii kuliko ile ya mwaka jana. Amegusia vipengele muhimu na ambavyo ni kero hasa katika muungano wetu huu. Wabunge kutoka Zanzibar wawe makini katika uchangiaji wao maana wakiendelea na kasumba yao ya kupinga bila kujua maudhui wa mchango wa Tundu Lissu itakula kwao. Nina imani wananchi wa Zanzibar watakuwa wamemuelewa Tundu Lissu kwa mara ya kwanza.

Binafsi naungana na Tundu Lissu kuiomba serikali ifungue milango tuanze kuongelea mstakabali wa huu muungano wazi wazi. Huenda ikaepusha usivunjike bali tukauimarisha zaidi. kama tuliweza kukaa pamoja kwa miaka 50 ukiwa na mapungufu yake, basi tukiuboresha tutaweza kukaa kwa miaka mingine zaidi ya 50.
 
Nimesoma hotuba yote ya Mhe. Lissu na kwa kweli ni nzuri sana. Kitu kilichonivutia zaidi ambacho ndio kiini cha kero na matatizo ya Muungano ni ukweli huu:
Kwa sababu hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaungana na wale wote ambao wamedai, na wanaendelea kudai kuitishwa kura ya maoni ya wananchi ili waweze kuamua mustakbala wa nchi yetu. Kuendelea na kiini macho cha Muungano wakati Serikali zote mbili na chama tawala cha CCM wanauvunja [Muungano] kivitendo
Hapa CCM hawana pa kutokea kwani yote yako wazi. Kama yuko kiongozi wa CCM anayepinga maelezo ya Mhe. Lissu, apinge kwa uthibitisho kuwa hayo sio kweli.

Kwa maoni yangu pamoja na mambo mengine, iko haja kwa serikali ya CCM kusema "USANII BASI TENA" sasa washughulikie kero na maudhi ya Muungano kikweli kweli, vyenginevyo tutaendelea na kuwa na "Silly Union" kama ulivyo sasa.
 
Tundu Lissu alikuwa makini sana na amechangia kwa uangalifu mno katika hotuba yake hii kuliko ile ya mwaka jana. Amegusia vipengele muhimu na ambavyo ni kero hasa katika muungano wetu huu. Wabunge kutoka Zanzibar wawe makini katika uchangiaji wao maana wakiendelea na kasumba yao ya kupinga bila kujua maudhui wa mchango wa Tundu Lissu itakula kwao. Nina imani wananchi wa Zanzibar watakuwa wamemuelewa Tundu Lissu kwa mara ya kwanza.

Binafsi naungana na Tundu Lissu kuiomba serikali ifungue milango tuanze kuongelea mstakabali wa huu muungano wazi wazi. Huenda ikaepusha usivunjike bali tukauimarisha zaidi. kama tuliweza kukaa pamoja kwa miaka 50 ukiwa na mapungufu yake, basi tukiuboresha tutaweza kukaa kwa miaka mingine zaidi ya 50.

Ditto, hii hotuba ni mtihani mkubwa kwa wabunge wa Zanzibar bila kujali wanatoka chama gani. Na hapa ndio wananchi watajua nani mbunge maslahi na nani mtetezi wa wanzanzibari. Watakuwa na ujasiri wa kukata kutumiwa na CCM- bara?
 
Ningetaka sana kusikia maoni ya wale wabunge toka kundi la 55 juu ya hii hotuba ya Lissu. Ningekuwa naongoza kikao cha bunge ningetoa nafasi kwanza kwa wajumbe wa hilo kundi la 55 wakifuatiwa na wabunge wa Zanzibar halafu ndio wengine wafuate.
 
Huu mchango wa CDM umesimama vibaya mno Ngoja tusubiri wakina Mwigulu wakati wa kuchangia tuone Kama wataitupa tena na kusema rubbish
 
cdm hapo wamewapiga chenga ya mwili ccm,inabidi wabunge wa cuf wawe makini sana kuijadili
 
Well said,tusubiri reaction zao maana wengine hawachelewi kuja na maneno ya kwenye kanga .
 
Mbona Zanzibar ina majeshi yake sasa na isiyomtambua Rais wa Tanzania, tena tiifu kwa Rais wa Zanzibar, na Zanzibar ina wizara ya Ulinzi japo kwa jina wanaita wizara ya Vikosi vya SMZ, pia ina wizara ya Fedha, japo hayo yote wameyaunda juzi kwa mwendo wao wa ingiza kidogo kidogo
 
Naunga mkono hutaba hii..amezungumza mambo ambayo wananchi wanataka kwa sasa bravvo
 
Ukisikia Ugali moto na Mboga moto ndio hii.

Lisu kawabana kotekote; Wakiunga mkono hoja, pigo kwa CCM kukubali hadharani muungano kujadiliwa kwa nguvu ya hoja ya chadema. Wakikataa, wataonekana wanapingana na Mabadiriko ya Kumi ya sheria ya Zanzibar..hahahahaa! Kwahiyo Raisi ashitakiwe kwa kutoilinda katiba ya jamhuli ya muungano. Yaani sioni wapi CCM watakapotokea kwa kibano hiki cha Lisu. Hongera Chadema, Hongera Lisu!
 
Mzee wangu alikuwa ni mongoni Mwa wabunge waliokuwa wanaunda kundi la wabunge kutoka bara waliokuwa wanadai Tanganyika yaani kundi la G-55' Balozi Nhigula ambaye aliwahi Kuwa Mbunge wa Kwimba huko Mwanza Naibu Speaker Kabla ya Mzee Msekwa,
hii ilimletea matatizo Makubwa waziri mkuu wa wakati ule mzee Malecela nA Mwalimu Nyerere.

Ni wakati sasa kuondoa utata huu wa muungano kwa dhamira ya dhati na uhalisia wa hali ya nchi, naunga mkono hotuba nA Maoni ya kambi ya upinzani yamejaa facts nA nia njema kwa taifa letu.
Ccm waache mara moja hila za kujifanya watetezi wa muungano mchana wakati behind closed doors nA matendo yao yamekwisha uvunja muungano nA wamevunja katiba ya nchi ambayo wameapa kuinda nA kuitetea.

Wekeni kura ya Maoni tumalize hiki kiini macho
 
Back
Top Bottom