Manung'uniko ya sarakikya: Taifa lisilo na shukrani

Saint Ivuga

JF-Expert Member
Aug 21, 2008
54,363
58,386
MANUNG'UNIKO YA SARAKIKYA: TAIFA LISILO NA SHUKRANI[/h]




Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela

MWEZI mmoja uliopita, mkuu wa kwanza wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tunavyolijua sasa, Jenerali Sam Hagai Mirisho Sarakikya alizungumza na kutoa manung’uniko ambayo nilitarajia kusikia yamefanyiwa kazi.

Ni manung’uniko ambayo si mageni kwa wazee wetu wengi waliostaafu miaka kama 15 iliyopita. Kwamba, malipo yao ya pensheni yamepangwa bila kuangalia hali halisi, na hayana mantiki yoyote kulinganisha na malipo yanayofanyika katika mishahara leo hii.

Alichozungumzia Sarakikya na kuripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari, ni kuwa yeye ambaye amelitumikia taifa letu kwa karibu miaka 40 anapokea pensheni ya Sh. 50,000! Yaani mkuu wetu mstaafu wa Jeshi la Ulinzi analipwa pensheni yake kwa mwezi kama dola 50 (na hapo nimeipendelea).

Hayuko peke yake; wapo wakuu wa asasi mbalimbali nyeti na hata watumishi wengine tu wa muda mrefu waliostaafu sasa, lakini pensheni zao hazilingani kabisa na utu wao na nafasi walizowahi kuzishikilia.

Wapo maafisa wa Polisi waliolitumikia taifa letu kwa uadilifu mkubwa, lakini sasa hivi wamebaki kubangaiza; huku pensheni zao zikiwa ni kiasi hicho hicho au chini kidogo. Wapo wakurugenzi, mameneja ambao walijitoa mhanga kujenga hili taifa ambalo wengine sasa hivi ‘wanachuma’ bila kutoka jasho. Kinachonishangaza zaidi ni kuwa taifa hili hili limetengeneza mfumo wa ajabu linapokuja suala la pensheni za wanasiasa.

Mwaka 1999 Chama cha Mapinduzi kilipitisha sheria ambayo ingesimamia pensheni ya viongozi wa kisiasa. Katika sheria hiyo, mtu aliyekuwa Rais (kwa sasa hivi Mkapa, Mwinyi na Kikwete akistaafu) anastahili pensheni yake sawa na asilimia 80 ya mshahara wa Rais aliyeko madarakani. Mkono wa asante (posho) ambao utakuwa sawa na asilimia 50 ya jumla ya mishahara yake yote!

Yaani; kama Rais anapokea mshahara wa sawa na dola 12,000 kwa mwezi, basi, kwa muda wa miaka 10 ambayo atakuwa madarakani atakuwa amepokea sawa na Shilingi bilioni 1.44. Hivyo, siku akimaliza madarakani Watanzania wanamlipa nusu ya hiyo kama asante, sawa na Shilingi milioni 720!

Usidhani hiyo imetosha. Pamoja na hilo anapewa posho ya kumaliza kazi ambayo itakuwa sawa na mishahara ya miezi 24 (miaka miwili) ya Rais aliyeko madarakani. Yaani, kama Rais aliyeko madarakani analipwa dola 14,000, basi, yule mstaafu atalipwa kiasi kama hicho kwa mkupuo kikiwa ni jumla ya miezi 24 ambayo ni kama dola 336,000! Halafu watu wanauliza kwa nini wengine wanatumia nguvu kubwa kuingia madarakani!

Hata Spika wa zamani naye ameweka mtindo kidogo kama huo kama ilivyo kwa Waziri Mkuu, mawaziri n.k. Mtu aliyewahi kuwa Spika anapokea pensheni sawa na asilimia 80 ya mshahara wa Spika wa sasa pamoja na posho nyingine nono.

Na inapokuja kwa waliowahi kuwa wabunge, CCM na wabunge wake wakapitisha sheria ambayo ikaweka viwango vifuatavyo. Kwamba, mtu aliyewahi kuwa mbunge, basi, atapewa wakati ambapo siyo mbunge tena (sheria haisemi akifikia umri wa kustaafu!) sawa na asilimia 40 ya mshahara wake kwa kila mwezi aliokuwa mbunge.

Ina maana kama mtu akikaa miaka 5, basi, atalipwa asilimia 40 ya mishahara yake kwa miezi sitini! Na kama mtu alikuwa mbunge miaka 40 ndio tutakoma! Na sheria ilivyo tamu kwao inasema kiasi hicho kitalipwa kwa mkupuo. Kama hiyo haitoshi, huyo mtu aliyewahi kuwa Mbunge atalipwa asilimia 20 ya jumla ya mishahara yote aliyopokea katika miezi 24 (miaka miwili).

Sasa, naomba niweke hili vizuri ili lieleweke kama bado halijazama moyoni kwa msomaji. Kuna sababu nyingi sana za watu kutaka kwenda Bungeni. Mojawapo ni kuwa posho na mfumo wao wa pensheni unamhakikishia mtu mtaji mzuri wa maisha; hata kama akianguka katika kipindi kinachofuatia.

Fikiria kwamba, mshahara wa mbunge kwa sasa ni Shilingi milioni 2.5 kwa mwezi. Asilimia 40 ya fedha hizo ni Shilingi milioni moja. Hivyo atalipwa kwa miezi sitini (miaka mitano) ambayo itakuwa ni sawa na Shilingi milioni 60 kama mkono wa asante.

Kumbuka hapo sijagusia kabisa posho nyingi ambazo atakuwa amezipata kwa miaka yake mitano. Katika hali hiyo, kwa nini watu wasikimbilie bungeni? Na tukiweka zile asilimia 20, kwa nini asiwe tajiri katika nchi yenye masikini wengi?

Hapa ni lazima ujiulize; Hivi hawa wabunge wameitumikia nchi hii kwa uadilifu na umakini mkubwa na kujitolea kuliko Sarakikya? Kweli wametumikia nchi hii kuliko maafisa kadha wa Jeshi la Polisi, Magereza, JKT n.k au wale wazee waliokuwa wafagizi na watunza kumbukumbu kwenye maofisi yetu?

Kweli hawa wanasiasa wanaamini kabisa wanastahili kuliko wale walimu waliotumika kwenye mazingira magumu hivyo? Hapa, ndugu zangu, kuna suala la kikatiba.

Katiba yetu imeweka kipengele kimoja kizito sana ambacho wafanyakazi na wastaafu sidhani kama wamewahi kukitumia kudai haki zao. Ibara ya 23 ya Katiba inasema hivi:

1. Kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na kiasi na sifa za kazi wanayoifanya. (2) Kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya haki.

Sasa naomba nipendekeze kwamba hapa kipengele hiki kinaashiria (bila kusema moja kwa moja) kwamba mtu aliyestaafu baada ya kufanya kazi anastahili pensheni na kifuta jasho kinachoendana na kazi yake.

Kwa maneno mengine, hicho kifuta jasho na pensheni lazima iwe ya haki na naweza kusema pasipo shaka kuwa shilingi elfu 50 kwa mtu aliyetumika kwa miaka karibu 40 si haki hasa ukizingatia kuwa mtu aliyetumika miaka miwili (waziri mkuu mmoja) analipwa asilimia 80 ya waziri wa sasa bila kujali alifanya kazi kwa namna gani!

Mfumo wa pensheni kwa watumishi wa zamani ni wa kinyonyaji, wa kibaguzi na unawadhalilisha watumishi wa zamani.

Bahati mbaya sana Chama cha Mapinduzi ambacho kimetengeneza mfumo huu na mtindo huu, hakiwezi kuubadilisha bila kutafuta visingizio vya kwanini haiwezekani.

Ilani yao ya uchaguzi inasema kitu cha kushangaza kidogo. Ahadi ambayo iliwafanya wazee (wengine wastaafu) kuipigia CCM kura inasema kuwa katika miaka mitano ijayo itakuwa na sera ya “kuendelea kuboresha mafao ya wazee wanaostaafu ili yaendane na hali halisi ya gharama za maisha na matakwa ya soko ili maisha yao tulivu yachangie vema katika amani ya nchi kwa ujumla.”

Sijui kama umesoma vizuri; sera yao inawahusu wazee “wanaostaafu” siyo wale wa “waliostaafu”. Wale waliostaafu kama mzee Sarakikya lwao! Sijui kama hadi hivi sasa wametoa hoja yoyote ya kuonesha wanawajali wastaafu. Labda wiki hii tutasikia, lakini chochote tutakachosikia kuhusu wastaafu kitakuwa hisani; kwani hakiko kwenye ahadi za CCM.

Sasa wazee wetu wafanye nini? Au tuulize sawasawa kabisa ni kitu gani kifanyike ili kuhakikisha kuwa wastaafu wa nchi hii akiwemo Mzee Sarakikya na wazee wengine ambao hawana mpango wa kugombea ubunge au hata udiwani? Naomba kutoa mapendekezo machache.

Kwanza, wazee wastaafu wa sekta mbalimbali wafuate mfano wa Sarakikya wa kuanzisha umoja wao wa kugombania maslahi yao. Umoja ambao utatumika kuwafuatilia na kuwashawishi wabunge kutunga sheria zinazolinda maslahi ya wastaafu na vile vile jumuiya ambazo zitashawishi vyama vya siasa kutunga sera ambazo zitaendana na maslahi ya wazee hao.

Kwenye hilo la jumuiya, naomba kupendekeza kuwa jumuiya hizo zisiwe kwa ajili ya wale waliostaafu tayari; bali ziweke utaratibu kwamba mtu yeyote ambaye amekaribia miaka angalau mitatu ya kustaafu anaweza kuwa mwanachama kamili.

Hii itapanua wigo wa wanachama wake na kuwa kiunganishi kati ya wale walioko kwenye ajira na wale ambao wako kwenye kustaafu. Itawapa mwanga wale wanaokaribia kustaafu kujua nini kinaendelea “uraiani”.
Jambo la pili, wastaafu wasifikirie wanawabembeleza wanasiasa kuwatendea hisani.

Baada ya utumishi wa muda mrefu kama wa mzee Sarakikya, kwa kweli kabisa siyo mtu wa kuomba tena, ni mtu wa kutaka. Miaka yake ya ujana alikuwa anaomba, alipokuwa mtumishi alikuwa anaomba, sasa hivi katika umri wake, na utumishi wake mkubwa amejipa haki ya kutaka.

Hivyo, wastaafu wawatake wawakilishi wao na vyama vyao vya siasa kutekeleza mambo fulani, na wakisita au kurembuarembua, wastaafu wanaenda kwa wengine, hakuna tena kuwabembeleza.

Sielewi kwanini baadhi ya wastaafu wanajisikia kana kwamba CCM ndio chama pekee cha kuinua maisha yao; huku wameyaona madudu yote ya miaka ya karibuni.

Wakati umefika kwa wastaafu kuiambia CCM “basi yatosha”. CCM imeshapoteza vijana wengi, ikianza kupoteza wazee ndio labda inaweza kuchangamka; kwani sasa hivi ngome yake kubwa ni hawa wazee waliochoka. Nyerere alisema CCM siyo mama yake, wakati umefika kwa wazee wengine kufikia hitimisho hilo.
Jambo la Tatu, linahusiana na vijana ambao ni watoto na wajukuu wa wazee hawa.

Vijana wasikae pembeni kuangalia wazee wao wanadhalilika. Vijana ambao wana wazee waliostaafu na wamechoka ni wakati wa kuchukua jukumu la kuwapigania mikononi mwao. Wazee waliotujengea taifa hili wanastahili kutetewa.

Kama vijana, huwa wakiona mzee kwenye basi wanampisha kiti kwa heshima au akianguka wanakimbia kumsaidia na kumpa maji, naamini ni thawabu kubwa zaidi kuwapigani ili maisha yao yainuliwe. Si kwa sababu vijana hawana matatizo yao la hasha, bali ni kutambua wito wa asili wa ulimwengu, vijana wanaenda kwenye uzee na wazee wanaenda kwenye machweo yao; hivyo kupigania maslahi ya wazee sasa hivi, ni kupigania maslahi ya wazee wa baadaye.

Jambo la tatu ni kuwa Tanzania kama inataka kuwa taifa la kisasa kweli ni lazima iwe na sera yake ya kusimamia maisha ya wazee na wastaafu, sera ambayo itazingatia hali halisi ya nchi, na maslahi ya wazee.

Binafsi niko tayari kutoa ushauri wowote kwa jumuiya yoyote ya wazee ambao wanafikiria kufanyia kazi baadhi ya mapendekezo haya bila gharama yoyote kwao. Ni katika kufanya hivyo tunasikia manung’uniko ya Sarakikya, na kuonesha kuwa sisi ni taifa linalojali na zaidi ya kujali.

Sarakikya kanung’unika
Kilio kimesikika,
Nani atahamasika
Jukumu akalishika?

Sipendi kusubiri wazee wetu wakishakufa ndio wanasiasa wajitokeze na vimbelembele vyao vya kutoa kauli za ‘pengo aliloliacha halizibiki’. Kwanini tusubiri wafe ndio tuanze kuwakumbuka na kuwaenzi?
Au sisi kama taifa ni watu wasio na shukrani?

source: Mtwara kumekucha
 
Back
Top Bottom