Mambo tisa yawasumbuayo wanandoa walio wengi

Bujibuji Simba Nyamaume

JF-Expert Member
Feb 4, 2009
74,864
155,820
MATATIZO katika ndoa ni jambo la kawaida na hakuna mwanandoa anayeweza kushangaa kusikia matatizo ya ndoa ya mwenzake. Wanandoa hupingana na kugombana kuhusiana na mambo mbalimbali, kuanzia katika suala la kupanga familia (mathalani idadi ya watoto) hadi katika masuala madogo madogo ya usafi wa choo.

Huhitaji kuwa na wasiwasi. Kutumia muda mwingi ukiwa katika kampani ya binadamu mwenzako si kitu rahisi, lazima tu zitokee rabsha. Isipokuwa jambo la muhimu ni kwamba usiache matatizo madogo madogo kuumuka na kusababisha ndoa kwenda mrama. Kila linapotokea tatizo kumbuka upendo wako kwa mwenzako pamoja na kule mlikotoka.


Katika kukabiliana na matatizo ya ndoa, hatua ya kwanza ni kutambua kuwa hauko peke yako mwenye matatizo kama hayo katika sayari hii. Hakuna ndoa iliyo kamilifu na pengine ya kwako ina unafuu. Mambo mengi utakayokutana nayo ni ya kawaida (watu wengi wameshakutana nayo na pengine ameyazoea). Lakini la muhimu zaidi ni kwamba unaweza kukabiliana nayo na kuyashinda.

Kama unatarajia kuingia katika ndoa, ni vema kuyafahamu mambo makuu ambayo husababisha ugomvi baina ya wanandoa. Kwa kuanzia, yafahamu haya tisa.

1. UKAME WA TENDO LA NDOA

Pengine hili ndilo tatizo linalofahamika zaidi katika ndoa. Watu waliooana hujikuta mara kwa mara wakishindwa kukutana kimwili (a.k.a. kufanya tendo la ndoa) kwa sababu mbalimbali: hasira, uchovu, fadhaa na kadhalika. Lakini pengine jambo moja linalopuuzwa ni kwamba, kufanya tendo la ndoa ndiyo njia bora zaidi ya kuondoa fadhaa zozote zinazomzuia mtu kufanya tendo la ndoa. Iwapo kutofanya tendo la ndoa kutakuwa chanzo kingine cha shinikizo na msongo wa mawazo, tatizo litazidi kuwa kubwa.

Ili kujiondoa katika mtanziko wa kutoshiriki tendo la ndoa na mwenzi wako wa maisha, jaribu kuondoa vyanzo vyote vya shinikizo katika maisha ya mwenzako. Njia bora zaidi ya kumwondolea mwenzako shinikizo ni kumtendea mema na kumsaidia/kumuunga mkono katika maisha ya kila siku.

2. MGAWANYO USIOFAA WA MAJUKUMU

Katika zama hizi ule mgawanyo wa kazi ambapo mwanamke ndiye hufanya shughuli za nyumbani peke yake na mwanamume kutafuta mkate unaelekea kwisha. Ni kweli kuwa katika nchi zinazoendelea (na hata zilizoendelea) bado kuna shughuli ambazo hufanywa zaidi na wanawake, lakini angalau wanandoa wengi sasa wanajua umuhimu wa kusaidiana.

Ni vema, hususan kwa wanaume, kutumia busara. Usimwache mwenzako kufanya shughuli zote. Jaribu kuangalia jinsi ya kujenga mazingira ya kusaidiana. Iwapo utaonesha moyo wa kusaidiana na mwenzako kazi zitaisha haraka na nyote mtakuwa na furaha. Lakini pia katika kufanya kazi pamoja wenza hujenga hisia za kushikamana zaidi.

3. KUJISAHAU KWA MWANAMKE KIMWILI

Baadhi ya wanawake hujiachia wanapokuwa wameolewa. Wakati wa uchumba hujiweka vizuri kiafya kiasi cha kumvutia mwanamume anayependa wanawake wenye maumbo ya kilimbwende, lakini baada ya kuolewa hujisahau, pengine bila kufahamu kuwa kwa kufanya hivyo wanajiondolea sifa iliyowafanya wapendwe.

Wakati mwingine unaweza kujitetea kuwa umenenepa kutokana na uzazi. Ni kweli kuwa wakati wa ujauzito akina mama hula sana kwa maslahi ya viumbe walivyobeba na wanapojifungua hula sana ili kurejesha damu iliyomwagika huku pia wakiweka akiba ya mtoto, lakini ukiwa mjanja utajitahidi kurejesha mwili wako ukishajifungua. Tatizo ni kwamba unaweza kujiweka katika hali ambayo mwanamume wako hakutamani tena, hapo hutapaswa tena kumlaumu (maana kama hakutamani afanye nini?).

Usijisahau wala kujiona umefika, bali fanya jitihada za kudumisha msisimko wa mwanamume wako kwako. Shughulika, fanya mazoezi – hii pia itakuwa ni kwa afya yako mwenyewe. Mwanamume mjanja naye hakai mahala akamlaumu tu mwanamke, bali huchukua hatua ya kwenda naye mazoezini. Pia, kabla hujafungua kinywa chako kumsema mwenzako kuhusiana na unene wake jiangalie wewe pia. Ondoa kitambi.

4. KUWA AU KUTOKUWA NA WATOTO

Jambo hili halikuwa tatizo siku za nyuma, lakini katika zama hizi – kutokana na utandawazi na umagharibi, tayari kuna ndoa zina mvutano kuhusiana na watoto. Wapo wanawake ambao hawako tayari kuzaa mara tu baada ya kuolewa. Hili ni jambo ambalo kwa hakika linaweza kusababisha matatizo katika ndoa, hususan kama wahusika hawakukubaliana mapema.

Hapa wenza wanapaswa kujadiliana kwa mantiki na kufikia muafaka. Kuna suala la umri – na katika kuzaa ni vema kufanya biashara mapema. Kuna kulea na kusomesha –haipendezi ufikie umri wa kustaafu kabla mtoto wako hajaanza sekondari. Utateseka, mafao yenyewe ya Tanzania yako wapi? Hapa ikitumika hekima mgogoro unaweza kumalizwa kwa amani.

5. UTOFAUTI KATIKA FALSAFA ZA MALEZI

Ndoa inapobarikiwa kuwa na watoto ni vizuri, lakini linaweza kutokea tatizo la kutofautiana kuhusiana na falsafa ya ulezi wa watoto. Katika zama hizi ambapo zimeingia falsafa mbalimbali kuhusiana na kulea watoto, huku elimu za kimagharibi zikizuia kumwadhibu mtoto (hususan kwa kumchapa), wazazi wanaweza kujikuta wakitofautiana.

Watoto ni wazuri, lakini akili yao ni changa na hufanya makosa mengi. Wanahitaji kuelekezwa. Lazima wazazi wakubaliane kuhusu namna njema ya kuwaelekeza kwa kuzingatia maadili ya jamii. La muhimu zaidi ni kuwaonesha upendo watoto, hususan kwa kuwapa mfano wa kupendana kwenu.

6. KUKOSEKANA KWA WATOTO

Mojawapo ya mambo ambayo husababisha fadhaa kubwa katika maisha ya ndoa ni suala la kukosekana kwa uwezo wa kupata watoto. Kukosekana kwa watoto kunaweza kuharibu kabisa dira ya wanandoa na hata kusababisha watengane. Naam, wenza wengi wameachana kwa sababu hii.

Hata hivyo, kukosekana kwa watoto si kosa la yeyote katika ndoa, kwani halitokani na tabia bali maumbile. Watu wanaoingia katika ndoa hupaswa kufahamu tangu mwanzo kuwa upo uwezekano wa kukosekana kwa watoto. Ukishafahamu tangu mwanzo kuwa watoto wanaweza kukosekana (maana kuzaa ni majaliwa) itakuwa rahisi kwako kukabiliana na hali hiyo ikitokea.

7. KUINGILIWA NA NDUGU, JAMAA

Anaweza kuwa ni mama yako (mwanamume) ambaye anafahamika kwa ukorofi wake, au ndugu yako (kaka au dada) – ndugu wanafahamika sana kwa kusababisha matatizo katika ndoa. Kumbuka, ni rahisi kwako kuwakosoa na kuwaponda ndugu za mwenzi wako bila kuona fadhaa wanayomsababishia ndugu zako. Inawezekana kabisa kuwa familia yao wana matatizo na familia yako ni nzuri (angalau kwa jinsi unavyofahamu), lakini inawezekana kabisa kuwa familia yako pia ina matatizo (maana watu husema nyani haoni kundule).

Kabla hujampuuza ndugu wa mwenzi wako kwa sababu yoyote ile, hebu wachunguze ndugu zako. Waheshimu ndugu na jamaa za mwenzi wako naye atawaheshimu wa kwako. Ndiko kuwajibika huko.

8. MATATIZO YA KIFEDHA

Matatizo ya kiuchumi ni mojawapo ya sababu kuu za wanandoa kugombana. Lakini pia, kunapokuwa na mali nyingi pia kuna shinikizo linaloambatana na jinsi ya kuzisimamia mali hizo. Hali huwa mbaya zaidi pale kila mmoja anapokuwa na wasiwasi na mwenzake. Kwa baadhi ya ndoa, pesa ndilo tatizo kubwa lisababishalo ugomvi.

Kama yalivyo matatizo mengine, njia rahisi zaidi ya kumaliza mgogoro unaohusiana na fedha ni kukaa na kuzungumza. Unahitajika uwazi katika masuala ya pesa, mathalani kama una madeni ni busara kumshirikisha mwenzako. Pia, ni busara kuwa muwazi na mkweli katika manunuzi.

9. KUCHOKANA

Kukaa na mtu yuleyule karibu kila wakati huchosha, hata kama mtu mwenyewe ni mwanamke mrembo kuliko wote nchini. Watu wana kawaida ya kupenda likizo kwa kila kitu, maana kitu kile kile wakati wote huchusha. Vivyo hivyo, ni jambo la kawaida kwa wanandoa kuchokana – si kwa nia mbaya, bali kutokana tu na asili yenyewe ya binadamu.

Hata hivyo, wanandoa wajanja hawagombani kwa kuwa wamechokana, bali hufahamu ni wakati gani wa kuingiza uhai katika uhusiano wao. Unaweza kuyafanya mambo kuendelea kuwa motomoto kwa kuanzisha hobi mpya, kusafiri na kwenda katika maeneo mapya pamoja na mwenzako, na zaidi, kujaribu mambo mapya kitandani.

WAWEZA KUPUNGUZA MATATIZO

Hata katika ndoa ya mfano, haiwezekani kabisa kuwa watu wataishi bila mkwaruzano wowote maisha yao yote. Kumbuka, hawa ni watu wawili tofauti na kila mmoja ana matamanio yake na ndoto zake za maisha. Si rahisi kukubaliana katika kila jambo.

Hata hivyo, wenza wenye hekima hujifunza kwamba katika ndoa kuna kuchukuliana na kuvumiliana, huku mara kwa mara wenza wakikubaliana kutokubaliana katika mambo mbalimbali. La muhimu ni kwamba, mikwaruzano isifikie mahala ikaondoa furaha na amani – mambo ambayo ndiyo ya muhimu zaidi katika maisha ya ndoa.

http://vinaora.com/
 
Usisahau na ambitions zisizolingana na kupeana support katika kufikia ambitions za mmoja wa wana ndoa
 
Mkuu kuna swala la kuwepo mtoto wa nje kabla ya wanandoa kuoana. Ni namna gani wanandoa watalihandle hili jambo kwa hekima bila mikwaruzano. Sio lazima mtoa mada ajibu, mwanaJF yeyote anaweza kuchangia kwa faida ya weingine.
 
Mkuu kuna swala la kuwepo mtoto wa nje kabla ya wanandoa kuoana. Ni namna gani wanandoa watalihandle hili jambo kwa hekima bila mikwaruzano. Sio lazima mtoa mada ajibu, mwanaJF yeyote anaweza kuchangia kwa faida ya weingine.


Nadhani suala la mtoto/watoto waliopatikana kabla ya ndoa ni muhimu wajulikane mapema kabla hamjafunga ndoa. Kila upande uwe wazi kwa mwenzake kuwa kuna abiria wengine ambao wamo kwenye gari ili ajue kama atakuwa comfortable kusafiri nao kama sivyo asipande hilo gari (maana abiria hao hawawezi kushuka).
Tatizo kubwa ni kuwa wanandoa huwa hawako wazi kabla ya kuoana. unakuta mmekaa miaka 6 ghafla anakuja jemba anatambulishwa ni mtoto wa mmojawapo wa wanandoa. Hii italeta shida. Ijulikane mapema na kila upande uwe tayari kukubaliana na hali halisi. Maana hii transaction (mtoto wa nje) haina reversing entry. Suala la namna ya kumlea mtoto wa nje litajadiliwa na kukubaliwa na wahusika wakuu (mke na mme)
 
haya mambo ni ya kuzingatia kabla ya kuingia, jamani msifanye mzaha!! manake mnapoambiwa mchunguze mwenzio, nyie mnawaza kama tu mtawezana kitandani. Basi, eti utaingiaje kabla hujajua kma mnawezana? mambo muhimu ya kumchunguza mtarajiwa wako hayapatikani kitandani, yanapatikana kwa ndugu, jamaa, marafiki, na inteligensia iliotulia.
SHAURI YENU.
Mtoto aliepo hai kabla ya ndoa ni vizuri ajulikane kabla na DRAFT ya muafaka ijulikane, mtoto asiekuwapo (abortions) ajulikane tu pale ambapo ameacha kovu litakalokuja kujifichua baade kwa mikiki na stress, kama hakuna haja, basi asizungumziwe.
vivo hivyo na historia zenye makovu, zijulikane mapema, mfano kufungwa, magonjwa, madeni, maugomvi makubwa nk.
 
Back
Top Bottom