MAMBO HALISI: Kama ni kuamua, basi hiki ndicho walichokisubiri mawaziri wetu!

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125

KISWAHILI kinao usemi uliozoeleka kwa wengi kwamba, asiyesikia la mkuu huvunjika guu!
Pia, upo mwingine, la kuvunda halina ubani. Semi hizi ndizo zinazofaa kutumika katika zama hizi ili kueleza kile kinachoendelea katika nchi yetu, Tanzania.


Inashangaza kuona kwamba kama nchi tumefika mahali ambako hata viongozi wetu si wasikivu tena.
Tunao viongozi wengi katika nchi hii ambao hawana maadili kabisa wala hawajui tena miiko ya uongozi, ile iliyokuwamo katika Azimio la Arusha la mwaka 1967.


Inawezekana kuwa wengine hata hawakumbuki kuwapo kwa mwongozo wa Tanu wa mwaka 1971, ambao ulieleza wazi kuwa cheo ni dhamana ukaeleza kuwa dhamana ile haitatumika vibaya kwa ajili ya kujinufaisha.

Ni imani yangu kuwa miiko ile ile ipo kwa wengi wetu, watu wa zamani, wakongwe wenzangu ukipenda kina sisi wa mwaka '47', ambao

tulikuzwa na kulelewa katika misingi ile ya maadili, tunaona aibu kuitwa kiongozi. Ninaogopa wakati mwingine hata kuomba uongozi, ambao kwa sasa umekuwa wa kununua au kuuzwa, si utumishi!

Inawezekana kuwa viongozi wetu hasa wa zama hizi, wengi wao wakiwa wale waliozaliwa baada ya Azimio la Arusha na ambalo lilikufa

kibudu kule Zanzibar miaka ya tisini na ambao walikuzwa au kunolewa nje ya vyuo au taasisi kama vile Kivukoni (sasa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere) na matawi yake mbalimbali nchini, ndiyo maana maadili kwao ni bidhaa adimu.

Waulize viongozi hasa wale wa zamani wale waliofunzwa na hata kuujua uadilifu, hasa jinsi ambavyo waliona woga katika kujilimbikizia mali.

Ifahamike wazi kwamba sisemi, Watanzania tuichukie mali kwani mambo yamebadilika mno.
Nakubali kuwa zama za fedha kuwa si msingi wa maendeleo zimepita, zimebadilika sana na kuondoka kabisa, fedha imetukuzwa mno.

Matokeo yake ndiyo maana ni fahari kwa uongozi wetu wa sasa kujivunia au kujitukuza kwa fedha au mali na rasilimali nyingi walizo nazo, hata kama hazilingani na kipato chao.

Ni ajabu ya kipekee kuona kwamba kiongozi wa leo anadiriki kueleza hadharani kuwa anamiliki nyumba ya mamilioni mengi, ambayo hata ukimuuliza ni jinsi gani alizipata, hakika unabaki na shaka.

Huu ni upungufu ambao jamii na Serikali yake haioini tena na ndiyo maana nimesema wazi katika safu hii siku zote kwamba, hata ile

Sheria ya Maadili ya Uongozi wa Umma, iangaliwe upya kwani inawapa uhuru mkubwa viongozi wetu wa kutangaza au kuficha mali zao, kutokana na hiari iliyopo.

Kwani sheria ile inawazima na kuwafunga midomo wanajamii katika kusema au kuhoji jinsi ambavyo viongozi wetu walivyozipata mali.

Mbona ni sheria ileile ambayo inawafunga mikono hata wanahabari kwamba hawapaswi hata kuchapisha mali hizo, hata wameona katika daftari ile ya Serikali!


Matokeo yake, kwa sasa inaelekea tunao viongozi wengi ambao unaweza kusema hawakufundwa vizuri na wengine hawakupelekwa 'jandoni' au kwenye 'unyago' wa uongozi!

Niliwahi kusema siku zilizopita kwamba tulikuwa na vyuo kama Kivukoni, Hombolo na vinginevyo vingi tu, ambavyo ingawa vilikuwa

mahususi kwa mafunzo ya itikadi ya kisiasa, lakini pia vilitumika kuwanoa na kuwafunza maadili wengi wa makada, ambao hatimaye ndiyo wale walioteuliwa kuwa viongozi.

Hata kama nchi yetu imebadili mfumo wake kutoka ule wa chama kimoja kwenda vyama vingi, lakini sioni tatizo liko wapi la kuwa na mahali ambako viongozi wetu wanaandaliwa!

Niliwahi kusema kuwa, hata ndani ya umoja wa vijana wa chama tawala, CCM, umoja huo, yaani UVCCM nao ulikuwa chuo chake kule Ihemi, Iringa.


Huko ni mahali ambako makada wengi vijana walinolewa vizuri na wengine walipohitimu kule ndiyo hao waliokwenda Kivukoni na hata wengine nje ya nchi kama Bulgaria, Yugoslavia na kwingineko, ambako waliandaliwa kuwa viongozi wa siku za usoni.

Haishangazi kuona kwamba wengine waliokuwa wakitumikia vikosi vyetu vya ulinzi na usalama nao walikuwa wamenolewa vyema kule

Monduli na vyuo vingine, wakitokea huko wakawa viongozi hodari na mahiri na ambao nchi inajivunia leo kuwa nao hadi leo, ingawa wapo wachache waliokengeuka.

Sishangai na siogopi kusema kwamba, kwa sasa tuna viongozi ambao kwa kiasi kikubwa si wasikivu, hawaoni tena aibu katika kusema uongo, kuutetea uovu huo ambao ama wametenda wao au wale ambao wapo chini yao, Ihemi imekufa, vijana wa CCM wameparaganyika mno kwani huhitaji kuona kwa darubini yanayotokea ndani yake kwa sasa!

Kwa aina hii ya uongozi, ni ajabu ndiyo maana hata wanaposhauriwa viongozi wetu wajiuzulu, hawalielewi somo hili ambalo linaonekana gumu mno kwao.

Unaweza kueleza kuwa imekuwa kama tabia kwa viongozi wetu kushindwa kuwajibika na ndiyo maana waziri wa leo anaona nongwa

kuwajibika kwa kujiuzulu wadhifa alionao.

Nilidhani kuwa baada ya zile kelele nyingi mno za Dodoma kutoka kwa wabunge karibu wote, wengine wakidiriki kusaini karatasi ya kutokuwa na imani na Serikali au kiongozi mwandamizi kama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, bado mawaziri wetu wangesema kuwa hawayajui makosa yao!

Ninadiriki kusema kwamba hata baada ya Kamati Kuu ya CCM kukutana Ijumaa iliyopita kwa dharura na kumwagiza mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete achukue hatua dhidi ya mawaziri wake, wangeendelea kusubiri huruma ya JK.

Inawezekana kuwa wapo ambao bado hawaoni makosa yao, hata ripoti kama ile ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG),

Ludovick Utouh imeonyesha kwamba ama wao au wizara zao zilikuwa na kasoro lukuki.

Utashangaa kusikia hadi Rais Kikwete atekeleze agizo la Kamati Kuu kwa kuvunja baraza la mawaziri na kuunda jingine jipya, bado mawaziri wanane na pengine wengineo zaidi, wameshindwa kujiuzulu.
Jiulize, uko wapi ugumu wa kufanya hivyo kwa mtu kama waziri katika Tanzania ya leo?

Zipo tafiti kadhaa ambazo zinaonyesha kwamba Waafrika hatuna utamaduni au mazoea ya kuwajibika wenyewe bila kusubiri kusukumwa kwanza na wakati mwingine kuondolewa, tena kwa aibu.

Nilisema wiki jana kwamba mawaziri wetu wanane wenye tuhuma wajipime, kama alivyowahi kueleza aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward

Lowassa (Mbunge wa Monduli) wakati wa kashfa ya Richmond mwaka 2008, kwamba alikuwa amejipima na kisha kuamua kujiuzulu!

Unaweza kusema mfano huu wa Lowassa na wenzake kama, Dk Ibrahim Msabaha (Waziri wa Afrika Mashariki) na Nazir Karamagi wa Nishati na Madini) si sawa au mzuri kwa mawaziri wetu wa sasa.

Lakini, baada kupigiwa kelele hizi na karibu kila mbunge katika mkutano ule wa 7 uliomalizika mjini Dodoma wiki moja iliyopita, wangekuwa makini, tena wasikivu, mawaziri hao wasingesubiri hadi Kamati Kuu iwahukumu.

Ninaamini wao wangetangulia kuandika barua kwa Rais Kikwete, ambaye ndiye mamlaka ya uteuzi, wakamrejeshea uteuzi wake, kisha

wakasonga mbele kivyao, wakiendelea na shughuli zao za uwakilishi katika majimbo yao.

Lakini, kwa kuwa hawakuona haja au sababu, naamini sasa JK amepata nafasi ya kupumua, atawatapika pia kwa kuwaondoa hata wengine wote ambao niliwahi kueleza kuwa hawamsaidii!

Inafaa pia uuamini pia usemi mwingine wa Kiswahili, kuvuja kwa pakacha nafuu kwa mchukuzi na hilo ndilo ambalo JK anaweza kulifanya kwa kuwasukuma nje ya baraza lake wasiofaa wakiwamo wazembe!

MAMBO HALISI: Kama ni kuamua, basi hiki ndicho walichokisubiri mawaziri wetu!
 
Zamani kiongozi alikuwa anawatumikia wananchi, lakini sasa wananchi ndio wanawatumikia viongozi. Siku hizi uongozi ni sehemu ya mtaji wa biashara. Na ndio maana hawataki kujiuzulu kwani watakuwa wameua mtaji. Ama kweli sikio la kufa halisikii dawa!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom