Mama Kilango awabeza wanaonyemelea jimbo lake

Regia Mtema

R I P
Nov 21, 2009
2,970
864
Kilango awabeza wanaonyemelea jimbo lake


na Dixon Busagaga, Moshi


amka2.gif

SIKU chache baada ya baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujitokeza kutoa msaada kwa watu waliopoteza ndugu zao kwenye maafa ya maporomoko yaliyotokea hivi karibuni wilayani Same, Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango, amewabeza watu hao kuwa lengo lao ni kutaka ubunge mwaka 2010.
Kilango ambaye pia ni mjunbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), amewakejeli wanachama hao ambao alidai wako zaidi ya 10 kuwa hawataweza kushindana naye katika kinyang’anyiro cha ubunge.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Jimbo la Vunjo, Kilango alisema baadhi ya wanachama wa CCM wameanza kujipitisha katika jimbo lake wakipiga kampeni za chinichini kwa lengo la kuwashawishi wananchi kuwachagua.
“Kuna watu wameanza kupita huku na huko katika jimbo langu na wengine wametumia maafa yalioua watu 24 kama ndiyo kisingizio cha kujipenyeza kwa wananchi kwa lengo la kujinadi, hadi sasa wako 10 na wote ni wanaume, lakini siwaogopi, nitawagaragaza,” alisema Kilango.
Alisema wanachama walijitokeza katika maafa hayo huku wengine wakitoa fedha taslimu kwa ndugu zao ambazo ziliwasilishwa kwake akiwa mwenyekiti wa kamati ya maafa Same.
Katika mkutano huo uliolenga kuwapongeza wananchi kwa kuipa CCM ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Oktoba mwaka huu, Kilango alisema wanachama hao walichanga zaidi ya sh milioni nne ambazo alidai alizipokea na kutoa risiti kisha akawagawia wananchi waliofikwa na maafa hayo.
Katika hatua nyingine ambayo ilionekana kumshitua Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro, Kilango aliwataka wanawake wenye nia ya kugombea ubunge katika jimbo hilo kujitokeza kugombea naye mwaka 2010.
Alisema upo umuhimu wa wanawake kujitokeza katika kugombea ubunge kutokana na hali ya sasa ya kuwa na bunge ambalo kati ya zaidi ya wabunge 232 wa kuchaguliwa wanawake ni 17.
Kilango alisema suala la mwanachama yeyote kuonyesha nia ya kugombea katika jimbo lolote si makosa, baada ya rais kulivunja Bunge, lakini wale wanaofanya kampeni sasa wanafanya makosa ambayo chama hakitayafumbia macho. “Kila mwanachama anayo haki ya kugombea, lakini ndugu zangu tusubiri muda ukifika wakati rais amelivunja Bunge kila mmoja atakuwa huru kutafuta ridhaa ya chama chake katika kuteuliwa kuwa mgombea,” alisema Kilango. Alisema kero iliyopo sasa kwa wabunge waliopo madarakani ni tabia ya baadhi ya wanachama wa CCM kuanza kujipitisha majimboni, hali inayosababisha wabunge kushindwa kutekeleza majukumu yao na badala yake kuamua kujihami.
 
Back
Top Bottom