Mama abambwa ‘eapoti’ amesheheni nyara

smp143

Member
Jun 8, 2009
95
7
JESHI la Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege, Dar es Salaam, linashikilia watu wanne akiwamo mwanamke kwa tuhuma za kukutwa na nyara za Serikali walizokuwa wakitaka kuzisafirisha nje ya nchi. Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Kamishna Msaidizi Mwajuma Kiponza, aliiambia HabariLeo jana kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Julai 7, mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 6.45 mchana.

Kamanda Kiponza alisema mtuhumiwa aliyekamatwa na nyara hizo ni Donatha Kassolo (27) mkazi wa Mikocheni A Dar es Salaam ambaye ni mfanyabiashara. Alisema Donatha alikamatwa katika sehemu ya upekuzi wa mizigo ya abiria, akiwa na sanduku lililokuwa na nyara hizo kinyume cha sheria.

Alizitaja nyara zilizokuwa ndani ya sanduku hilo kuwa ni vipande 91 vya meno ya tembo na vinyago 55 vya binadamu vilivyochongwa kwa meno hayo.Vingine ambavyo vote vimechongwa kwa malighafi hiyo hiyo ni vitatu vyenye sura ya mamba, 18 vya faru, vinne vya tembo, bangili 28 na vinyago vitano vya sura ya ndege.

Vinyago vingine vitano ni vya umbo la simba, vitatu kiboko, 12 vilivyo katika maumbo ya matunda, shanga 44, pete 28, vibanio vya nywele sita, vidani 73, henga moja, stendi mbili za meza, pambo la pembe nne moja na umbo la duara moja. Kwa mujibu wa Kamanda Kiponza, nyara hizo zote zilipimwa uzito na kukutwa vina jumla ya kilo 53 na thamani yake haijajulikana.

Mbali na nyara hizo, vitu vingine vilivyokutwa katika sanduku hilo ni meno ya 11 na kucha 60 za simba, bangili 82 na pete nane zilizotengenezwa kwa magamba ya kasa vyote vikiwa na uzito wa kilo mbili. Mtuhumiwa huyo pia alikuwa na mifuko miwili yenye uzito wa kilo tano ya majongoo bahari na mfuko wa unga ambao hata hivyo haukujulikana ni wa nini na wenye uzito gani.

Kamanda Kiponza aliongeza kuwa sanduku hilo alilokuwa nalo Donatha, lilipitishwa na watuhumiwa Bakari Rashid, Nicholaus Jeremia na Edmund Kabushemela ambao walikuwa wakiangalia mashine ya kuchunguza ya TB II. Wote ni wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Kitengo cha Usalama na walikuwa zamu kwenye mashine hiyo.

Alisema watuhumiwa hao walipaswa kuwataarifu polisi juu ya shaka ya mzigo huo, lakini hawakufanya hivyo kwa kuwa walikuwa wamekula njama na mtuhumiwa na kupitisha sanduku hilo lenye nyara. Askari Polisi waliokuwa kazini katika eneo hilo baada ya kuona nyendo za mtuhumiwa wa kwanza na watuhumiwa wengine, walitilia shaka lile sanduku na kumkamata na kumpeleka katika kituo cha Polisi uwanjani hapo, aliongeza.

Kamanda alisema mtuhumiwa alipofikishwa kituoni pamoja na watuhumiwa wengine, aliamriwa kufungua sanduku hilo na kukutwa nyara hizo na sasa wanashikiliwa na Polisi kwa uchunguzi zaidi na pindi utakapokamilika, watafikishwa mahakamani.

Naye mtuhumiwa huyo alipohojiwa na waandishi kuwa ni vipi alikuwa akisafirisha nyara hizo kinyume cha sheria, alidai kuwa mzigo huo alitumwa kuufikisha uwanjani hapo na raia wa China na kuhakikishiwa kuwa asitie shaka kila kitu kiko sawa.

“Mimi nilipewa sanduku na kuambiwa kuwa taratibu zote zimeshafanyika, hivyo watu wa Usalama hatanisumbua, niliingize ndani kisha niondoke na nilipewa namba za simu za watu wa kuwasiliana nao hapa uwanjani wauvushe mzigo huu,“ Kamanda alimkariri Donatha akisema.

Kiponza alisema mara nyingi kikosi chake kimekuwa kikiwakamata raia wa China wakiwa na nyara hizo lakini si kwa idadi kubwa kama hiyo, na aliongeza kuwa kikosi chake kimejizatiti kulinda mali za Taifa.
 
Back
Top Bottom