Malori yasiruhusiwe kusafirisha wanafunzi

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,112
KATUNI%28172%29.jpg

Maoni ya katuni



Matukio ya ajali za barabarani yameendelea kwa kasi na kusababisha vifo vya watu nchini. Tangu kuanza kwa mwaka huu yameripotiwa matukio mengi ya ajali za barabarani ambazo chanzo chake kinasemekena kuwa ni uzembe wa madereva ambao kwa sababu zisizojulikana wanakiuka sheria za usalama barabarani.
Kila baada ya ajali kutokea, viongozi wa serikali na vyombo vya dola wamekuwa wakitoa kauli za tahadhari kukabiliana na ajali zaidi.
Ziko hatua ambazo serikali iliwahi kuzichukua huko nyuma, zikiwemo za kufunga mabasi vidhibiti mwendo pamoja na kupiga marufuku mabasi yaendayo mikoani kusafiri wakati wa usiku.
Tahadhari hizo hatujaona kama zimesaidia kupunguza kasi ya ajali za barabarani, ambazo zinaendelea kugharimu maisha ya Watanzania.
Hata hivyo wakati hatua hizo zinashindwa kuzaa matunda, baadhi ya wananchi wamekuwa wakitoa kauli za kulalamikia utaratibu wa utoaji wa leseni kwa madereva, wakisema kuwa madereva wengi wanazipata kupitia njia za vichochoroni na kwamba hiyo ndiyo sababu kubwa inayochangia ajali za barabarani nchini.
Katika mwendelezo wa ajali za barabarani, usiku wa kuamkia juzi ilitokea ajali mbaya ambapo wanafunzi 19 wa Shule ya Kiislamu ya Shamsi Maarifa ya jijini Tanga walifariki dunia na wengine 124 kujeruhiwa vibaya, baada ya gari walilokuwa wamepanda kupinduka katika eneo la Mabanda ya Papa.
Wanafunzi hao walikutwa na mkasa huo majira ya saa 4:00 usiku walipokuwa wakitokea katika mhadhara wa Maulid katika Kijiji cha Kibafuta kilichopo katika Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga lilieleza kuwa wanafunzi hao walikuwa wamebebwa na gari aina ya Fusso na kwamba baada ya ajali, dereva wake alikimbilia kusikojulikana.
Taarifa ya polisi ilisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva. Kuna taarifa pia kuwa kabla ya ajali hiyo baadhi ya wanafunzi walikuwa wakining’inia na kushabikia kwa kumtaka dereva kuongeza mwendo na kwamba walipofika kwenye mzunguko wa eneo la Mabanda ya Papa gari lilimzidi nguvu na kupinduka.
Ni jambo la kushangaza kuona gari hilo ambalo sio la kusafirisha binadamu likibeba idadi kubwa ya wanafunzi 140 bila mamlaka husika kuchukua hatua!
Inawezekana kuwa waliokodisha gari hilo kuwasafirisha wanafunzi ni uongozi wa shule hiyo ama waandaaji wa Maulid hayo, lakini bado kuna haja ya Jeshi la Polisi kueleza sababu za kutolizuia gari hilo tangu lilipoanzia safari hadi mahali lilipopinduka na kusababisha vifo hivyo.
Kwa kuwa ni wajibu wa trafiki kuwa barabarani, walitakiwa kulizuia gari hilo kwa makosa ya kubeba binadamu, kubeba idadi kubwa ya wanafunzi na mwendo wa kasi.
Shule nyingi nchini zimekuwa na utaratibu wa kusafirisha wanafunzi kwa kutumia malori pale wanapokuwa wanakwenda kwenye shughuli mbalimbali, zikiwemo za michezo bila kujali kuwa usafiri huo haufai.
Kibaya zaidi ni kwamba wanafunzi hawajui athari za mwendo wa kasi hivyo kujikuta wakiwahamasisha madereva kuendesha kwa mwendo wa kasi na matokeo yake ni ajali kama iliyotokea Tanga.
Sisi tunaamini kuwa moja ya hatua zinazofaa katika kukabiliana na ajali za barabarani ni kudhibiti utoaji leseni kwa madereva ili wanaozipata wawe ni madereva waliokidhi viwango vyote vinavyotakiwa.
Tunachukua fursa hii kuwapa pole wazazi, ndugu na jamaa za wafiwa na kuwaombea majeruhi wapone haraka ili warejee katika masomo yao.
Hata hivyo, pamoja na kauli iliyotolewa na Jeshi la Polisi kwamba linafanya uchunguzi kubaini waliohusika kulitumia Fusso kuwabeba wanafunzi ili wachukuliwe hatua, tunaamini kuwa hatua hiyo imechelewa kuchukuliwa.
Tunalishauri Jeshi pa Polisi kuanzia sasa lipige marufuku malori kusafirisha abiria hususan wanafunzi kwa kuwa ni hatari kwa maisha na ni kinyume cha sheria.




CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom