Mali zilizookolewa na polisi Mbeya 'zayeyuka'

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,470
911,173
Mali zilizookolewa na polisi Mbeya 'zayeyuka'


Na Rashid Mkwinda, Mbeya

WAFANYABIASHARA wa Soko la Uhindini lililoungua moto usiku wa kuamkia jana jijini Mbeya wamelilaumu Jeshi la Polisi kuwa baadhi ya askari wa jeshi hilo wamehusika kupora mali zilizokuwa zinaokolewa wakati linateketea. Mwenyekiti wa Soko hilo, Bw. Emili Mwaituka alisema
kuwa kuna uwezekano mkubwa wa askari polisi kuhusika na uporaji wa mali za wafanyabiashara hao kwa kuwa idadi ya safari za kubeba mali hizo kutoka sokoni haziwiani na mali zilizokuwepo kituo cha polisi.

Bw. Mwaituka alisema kuwa usiku wa kuamkia juzi askari polisi walitumia magari yao kuokoa mali zilikokuwa hatarini kuteketea kwa moto, lakini walipofika katika kituo cha polisi mali walizozikuta hazilingani na zilizookolewa na askari hao.

"Askari tuliwaona ni wasaidizi wetu katika kuokoa mali zetu, tulitarajia kukuta mali zote zilizoporwa kituo cha polisi. Tulichokikuta ni vitenge vichache na khanga," alisema Bw. Mwaituka.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. John Mwakipesile alisema kuwa iwapo zipo tuhuma hizo za uporaji, mtu yoyote mwenye ushahidi autoe ili hatua za kisheria zifuatwe.Jana asubuhi Bw. Mwakipesile alikaa na Kamati ya Ulinzi na Usalama kutathmini tatizo hilo na kuagiza wafanyabiashara wote waliokuwa wakitumia soko hilo kwa kushirikiana na halmashauri ya Jiji la Mbeya kuangalia uwezekano wa kutafuta eneo mbadala kwa ajili ya kujiegesha.

Bw. Mwakipesile alisema kuwa kuungua kwa soko hilo kunatoa mwanya kwa halmashauri ya jiji kujipanga vyema kwa ujenzi wa soko jipya la kisasa, ambalo litakuwa na miundombinu ya kisasa linaloweza kukidhi matukio tofauti ikiwemo kudhibiti majanga ya moto.

Alitolea mfano kuungua kwa soko hilo kuwa ililazimika kuita tingatinga kwa ajili ya kutengeneza njia, ili magari ya zima moto yamudu kufanya kazi hiyo kwa kuwa soko hilo lilikuwa halifikiki.

Bw. Mwakipesile alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa kasoro kadhaa za utendaji wakati wa uzimaji wa moto huo, lakini jitihada zilifanyika ili kuhakikisha moto unazimwa kwa kutumia magari mawili ya zimamoto.

Moto huo ulioanza majira ya saa 2:30 usiku baada ya kuzimika ghafla kwa umeme hali ambayo inadaiwa kuwa inaweza kuwa ni chanzo cha moto huo, ingawa baadhi ya watu wanadai kuwa inawezekana chanzo cha moto huo ni akina mama lishe waliouacha moto katika vibanda vyao usiku huo.

Mara baada ya moto huo kuanza magari mawili ya Kikosi cha Zimamoto yalifika eneo la tukio ambapo gari la kwanza lenye namba za usajili SM 4524 lilifika eneo la tukio likiwa na maji kidogo na gari lenye namba za usajili SM 6043 lilikuwa limekosa nafasi ya kuingia katika eneo soko hadi lilipokuja tingatinga kubomoa baadhi ya vibanda.

Soko hilo lilikuwa likitoa huduma kwa wakazi wa katikati ya Jiji la Mbeya kwa bidhaa mbalimbali ambapo wafanyabiashara wanaokadiriwa 100 vibanda vyao vimeteketea kwa moto.Kuungua kwa soko hilo kumewakumbusha wakazi wa Mbeya mwezi Desemba 2006 Soko la Mwanjelwa lililopoungua moto katika mazingira yanayofanana.
 
Inakuaje huyu bosi wa polisi ndio anazungumzia habari za halmashauri na wafanyabiashara kwenda kutafuta pahala pengina wakati kazi yake ni ulinzi na usalama? wakati hapo analalamikiwa habari ya bidhaa kupotea mikononi mwao? na halmashauri wakwapi kuelezea hatma ya wafanyabiashara hao maana wao ndio wanahusika na mipango miji.
 
Polisi wadaiwa kupora janga la kuungua soko

Moto ukiteketeza Soko la Uhindini lililopo katikati ya Jiji la Mbeya usiku wa kuamkia juzi.
Soko kuu la Uhindini lililopo katikati ya Jiji la Mbeya limeteketea kwa moto, huku Polisi kwa kushirikiana na baadhi ya wananchi wakidaiwa kushiriki kupora mali za wafanyabiashara ambao maduka yao yalikuwa yakiteketea.
Hii ni mara ya pili kwa masoko makubwa kuteketea kwa moto jijini Mbeya ndani ya miaka minne, ambapo Desemba 2006, soko la Mwanjelwa liliteketea na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh. milioni 800 kwa wafanyabiashara.
Moto huo wa juzi uliowasababishia hasara kubwa wafanyabiashara wa soko hilo, ulianza majira ya saa 2:20 usiku na kuendelea kuteketeza maduka huku Kikosi cha Zimamoto cha Halmashauri ya Jiji la Mbeya kikishindwa kuudhibiti.
NIPASHE lilishuhudia baadhi ya wamiliki wa maduka wakihaha kuokoa mali zao huku vibaka nao walitumia fursa hiyo kukwapua bidhaa mbalimbali za wafanyabiashara kwa kuyavunja kutokana na kutokuwepo ulinzi wa kutosha.
Wakati moto huo ukizidi kutanda, gari la kwanza la Kikosi cha Zimamoto namba za usajili SM 6039 liliwasili majira ya saa 2:40 ambapo lilijaribu kuzima moto huo kwa dakika tano tu kisha likaishiwa maji.
Ubovu wa miundombinu hasa njia za kuingia ndani ya soko hilo ilikuwa ni kikwazo kikubwa kwa magari ya zimamoto kufanya kazi yake, hali iliyolazimu kuleta tingatinga ambalo lilitumika kubomoa baadhi ya maduka ili kupata njia ya magari ya zimamoto kuingia ndani ya soko na kuendelea na kazi ya kuzima moto katika maduka yaliyokuwa yakiteketea kwa moto.
Gari jingine la kikosi hicho namba SM 4524 liliwasili saa 2:50 ambalo nalo pia liliishiwa maji hali iliyozua malalamiko kutoka kwa wananchi ambao walianza kuwazomea askari wa kikosi hicho kwa uzembe.
Baadaye polisi wakiwa katika gari namba T 710 APB walifika eneo la tukio na kuanza kuwakamata vibaka ambao walikuwa wanavunja maduka na kupora mali.
Polisi hao walionekana wakizunguka baadhi ya maduka kuwazuia vibaka wasiibe, lakini walizidiwa nguvu na idadi kubwa ya vibaka ambao walifika eneo la tukio wakiwa na zana za kubomolea milango.
Vibaka hao walifanikiwa kubomoa baadhi ya maduka yanayouza simu za mkononi na kuzikusanya kwa kuziweka kwenye mashuka waliyofika nayo eneo la tukio.
Magari ya polisi yenye namba PT 1464 na PT 0796 yalionekana mara kadhaa yakisomba bidhaa za maduka yaliyokuwa yamevunjwa kabla ya kufikiwa na moto huo na kuzipeleka mahali kusipojulikana huku wananchi wakiamini kuwa bidhaa hizo zilikuwa zikipelekwa kituo cha polisi.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na NIPASHE jana asubuhi, wamedai kuwa mizigo iliyokuwa ikisombwa na magari hayo ya Polisi imeyeyuka.
"Usiku ule wakati bidhaa zetu ilikuwa zikipakiwa kwenye magari ya Polisi tulijua wanatusaidia kuokoa, lakini leo (jana) tulipowafuata watukabidhi bidhaa zetu, wanatuonyesha mabegi machache tu, kwa kifupi Polisi nao wameshiriki kuiba mali zetu," alidai Mwenyekiti wa soko hilo, Emily Mwaituka.
Mwaituka alisema baada ya kuona hali hiyo, waliamua kwenda kuonana na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Evance Balama, ambaye aliwashauri kuwa wakamwone Mkurugenzi wa Jiji, Juma Rashid Idd, kwa kuwa soko hilo lipo chini ya Halmashauri ya Jiji hilo.
Mwaituka alisema walipofika kwa Idd, aliwaeleza kuwa kulikuwepo na kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa kuhusiana na suala hilo, ambacho kilikuwa kimeitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile.
Mbali na magari ya Polisi, magari mengine ya kiraia nayo yalionekana katika shughuli za uokoaji wa mali huku yakipakia bidhaa na kuondoka nazo.
Tukio hilo lilisababisha baadhi ya watu wanaodhaniwa kuwa ni vibaka kutaka kujaribu kuingia katika Benki ya NMB tawi la Mbalizi Road iliyopo hatua tano kutoka sokoni hapo, hali iliyowalazimu Polisi kutumia nguvu ya ziada, ikiwemo kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya vijana waliokuwa wameanza kujazana kwenye milango ya benki hiyo.
 
Back
Top Bottom