Malaki wafaulu darasa la saba

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Jumla ya wanafunzi 456,350 sawa na asilimia 95.3 kati ya 478,912 ya waliofaulu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu, wamechaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka 2011 katika shule za sekondari za serikali.
Taarifa hii ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alipokuwa akitangaza matokeo ya kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2010 kwa waandishi wa habari.
Dk. Kawambwa alifafanua kwamba kati ya wanafunzi hao waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, wasichana ni 211,696 na 244,654 ni wavulana.
Waziri Kawambwa alisema kitakwimu kuna ongezeko la asilimia 2.3 kutoka idadi ya wanafunzi 445,954 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2009.
Dk. Kawambwa alisema kuwa wanafunzi 919,260 waliandikishwa kufanya mtihani huo ambapo wasichana walikuwa 469,846 sawa na asilimia 51.11 na wavulana walikuwa 449,414 sawa na asilimia 48.89.
Alisema wanafunzi waliotahiniwa walikuwa 895,013. Kati yao wasichana walikuwa 459,889 na wavulana walikuwa 435,124 sawa na asilimia 97.36 ya waliofanya mtihani huo.
“Jumla ya wanafunzi 478,912 ambayo ni asilimia 53.51 ya waliofanya mtihani walifaulu. Wasichana 222,094 sawa na asilimia 48.29 ya wasichana waliofanya mtihani na wavulana 256,818 ambayo ni asilimia 59.02 ya wavulana waliofanya mtihani huo,” alisema.
Dk. Kawambwa alifafanua kwamba kulingana na takwimu hizo, ufaulu kwa mwaka huu umepanda kwa asilimia 4.1 toka asilimia 49.41 mwaka 2009 hadi asilimia 53.51 mwaka huu.
Alifafanua pia kuwa kwa mwaka huu wanafunzi 572 wenye ulemavu walifanya mtihani ambapo kati yao, 292 wamefaulu. Wasichana ni 108 na wavulana 184.
“Aidha, watahiniwa 124 kati ya waliofanya mtihani (sawa na asilimia 0.01) wakiwemo wasichana 77 na wavulana 47, matokeo yao yamezuiliwa kutokana na tuhuma za kujihusisha na udanganyifu kwenye mitihani,” alisema Dk. Kawambwa.
Alitoa wito kwa wanafunzi wa ngazi zote za elimu nchini kutojihusisha na masuala ya udanganyifu katika mitihani kwani kufanya hivyo ni kosa lenye madhara makubwa kwao na kwa taifa kwa ujumla. Akizungumzia upande wa matokeo kimasomo, Dk. Kawambwa alisema kwamba ufaulu wa somo la Kiswahili umeongezeka kutoka asilimia 69.08 mwaka 2009 hadi asilimia 71.02 mwaka huu.
Alifafanua kuwa ufaulu wa somo la Maarifa umepanda kutoka asilimia 59.46 mwaka 2009 hadi asilimia 68.01 mwaka huu.
Aidha, alisema kuwa ufaulu wa somo la Sayansi umepanda toka asilimia 53.41 mwaka 2009 hadi asilimia 56.05 mwaka huu.
Kuhusu Kiingereza, Waziri Kawambwa alisema ufaulu umepanda kutoka asilimia 35.44 mwaka jana na kufikia asilimia 36.47 mwaka huu na ufaulu wa somo la Hisabati umepanda kutoka asilimia 20.96 mwaka 2009 hadi asilimia 24.70.
Alifafanua kuwa ili kuwezesha upatikanaji wa nafasi katika elimu ya sekondari, Halmashauri zishirikiane na wadau wote wa elimu katika kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2011.
Aliwahimiza wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushirikiana na uongozi wa shule ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari wanaandikishwa, wanahudhuria ipasavyo na kubakia shuleni hadi wanapohitimu elimu ya sekondari.
 
Back
Top Bottom