Makatibu CCM mbaroni kwa kugawa kadi holela

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125
kirumbi.jpg
Na Yassin Kayombo
MAKATIBU wa CCM wa matawi mkoani Dar e Salaam, wamekamatwa na polisi kwa tuhuma za kugawa kadi kinyume cha utaratibu. Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kirumbe Ng’enda, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa makatibu hao wawili walikamatwa baada ya maofisa wa maadili wa Chama kubaini upotevu wa kadi katika matawi yao. Kirumbe aliwataja makatibu waliokamatwa ni wa tawi la Balozi Msolomi, lililoko kata ya Mwananyamala, Charles Zyambo ambaye amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na Mohammed Mponda wa tawi la Kivukoni anayeshikiliwa katika kituo cha Polisi cha Pangani, Ilala. Kwa mujibu wa Kirumbe, Zyambo alikamatwa baada ya maofisa wa maadili wa Chama kufanya uchunguzi na kubaini kadi 83 kati ya 120 alizopewa Juni, mwaka jana kuzigawa kwa wananchi walioomba kujiunga na CCM, hazikugawiwa kwa walengwa. Alisema katika uchunguzi huo, Zyambo alishindwa kuwaonyesha stakabadhi zinazoonyesha wanachama waliokabidhiwa kadi hizo na kiasi cha fedha kilichokusanywa, hali iliyomfanya kuingia katika tuhuma. Kirumbe alisema Mponda alikamatwa na polisi juzi baada ya kuwatoroka maofisa wa maadili wa Chama waliokwenda ofisini kwake kufanya ukaguzi wa kadi. Alisema mwishoni mwa wiki iliyopita maofisa hao wakiwa ofisini hapo kukagua kadi, walibaini kadi zaidi ya 160 hazijulikani ziliko, Mponda licha ya kushindwa kutoa maelezo aliwatoroka maofisa hao. Kirumbe alisema maofisa wa maadili wanaendelea kufanya ukaguzi wa kadi kwenye matawi yote 6,408 ya CCM yaliyoko kata 73 katika mkoa wa Dar es Salaam, na kwamba watakaobainika kuzigawa kinyume cha utaratibu watachuliwa hatua kwa mujibu wa katiba, kanuni za Chama na sheria za nchi. Alifafanua kuwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM, mwananchi anayependa kujiunga na Chama analazimika kujaza fomu ya maombi ambayo hujadiliwa na kamati ya siasa ya tawi husika ambayo hutoa ridhaa ya mwombaji apewe au asipewe. Mei 25 mwaka huu, Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, alitangaza kufukuzwa kazi makatibu wa CCM wawili katika wilaya ya Lushoto mkoani Tanga kwa tuhuma za kugawa kadi kinyumbe cha utaratibu. Makamba alisema makatibu hao wanatuhumiwa kugawa kadi kwa viongozi wa Chama ambao wanataka kuzigawa kwa wananchi ili wawapigie kura za maoni watakapoomba kugombea nafasi za ubunge na udiwani. Aikuwa akifungua semina ya siku tatu ya Makatibu wa Siasa na Uenezi wa mikoa mjini Dodoma ambapo alisema wapo makatibu wengine wilayani Kinondoni wanaotuhumiwa kuzihamisha kadi na kuzipeleka katika mikoa ya Singida na Kilimanjaro. Hata hivyo, tuhuma zao zinachunguzwa. Wakati huo huo, David Paul anaripoti kuwa CCM mkoani Mwanza, kimewaonya wanachama wake wanaotarajia kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kuacha kufanya kampeni kabla ya wakati. Pia, kimeonya tabia za baadhi ya viongozi kuwabeba wagombea na kuwapitisha kwa wajumbe na kwamba atayebainika atachukuliwa hatua kali ili kulinda heshima ya Chama. Onyo hilo limetolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Anthony Diallo, wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM wilayani Geita mkoani Mwanza. Katika ziara hiyo, Diallo alikagua uhai wa Chama na kuzungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya wilayani hapa, ambapo alielezwa kuwa kuna wagombea waliotangaza nia wameanza kujipitisha kwa wajumbe huku wakiwakejeli viongozi waliopo madarakani. “Mbaya zaidi kuna baadhi ya viongozi wa Chama ngazi ya wilaya wanawabeba wagombea na kuwafanyia kampeni. Pia wanawatukana na kuwakejeli viongozi waliopo madarakani, hivyo wanachama wanashindwa kuelewa mahali pa kusimama,” alisema mjumbe mmoja akimweleza Diallo. Kufuatia malalamiko hayo, Diallo alionya kuwa muda wa kufanya kampeni haujafika na atayebainika kujihusisha na kampeni ikiwemo kuwachafua viongozi waliopo madarakani, atachukuliwa hatua. Alisema kwa sasa Chama kinafanya utafiti ili kubaini wanachama wanaokwenda kinyume na utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi na kwamba, watakaobanika hawatapewa nafasi. “Msihangaike na wagombea ama viongozi wenye kufanya hujuma hizo, hawa wanajimaliza wenyewe, kwa sababu Chama kinafuatilia mwenendo wao kwa ukaribu na watawajibishwa,” aliongeza.
Makatibu CCM mbaroni kwa kugawa kadi holela
 
Back
Top Bottom