makala niliyopenda: CHADEMA msirudie kosa la Mrema

kanyagio

JF-Expert Member
Dec 10, 2009
1,021
365
Na mwandishi wetu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kiko katika maandamano ya amani yanyofanyika katika mikoa mbali mbali nchini kwa sasa lengo likiwa ni kuzunguka nchi nzima.
Maandamano haya yamepokewa vema katika kila eneo yanakofanyika, hii ikidhihirisha kukubalika kwa chama hicho na pia jinsi wananchi walivyokatishwa tama na serikali yao.
Hata hivyo ninaanza kupata wasiwasi wa hatma ya maandamano hayo na mustakabali wa chama hicho, hasa jinsi viongozi wa CHADEMA wanavyoyachukulia mapokezi wanayoyapata huko mikoani.
Nimejaribu kuzungumza na watu kadhaa huko mikoani na wakanieleza hali halisi ya mapokezi mazito wanayoyapata, ghafla akili zangu zikanipeleka katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
Naliona kosa wanalolifanya CHADEMAA ndilo alilolifanya Augustin Lyatonga Mrema wa NCCR Mageuzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, ambapo aliangushwa vibaya na Benjamin Mkapa wa CCM.
Mrema aliyetingisha nchi kutokana na maandamano makubwa yaliyofanyika kabla na baada ya kuhutubia mikutano yake ya kampeni, alijipa matumaini makubwa kwamba ataweza kuibuka na suhindi wa kiti cha urais, kuitokana na sapoti kubwa ya kuungwa mkono aliyoipata.
Hata hivyo Mrema ambaye kwa wakati huo nyota yake ilikuwa juu kamka ilivyo ya Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA kwa sasa, hakutambua kitu kimoja, kwamba wapiga kura wengi wapo katika vijiji ambavyo mimi hupenda kuviita vya ujamaa.
Vijiji ambavyo katibu wa kijiji, mwenyekiti, au mwenyekiti wa serikali za mtaa anaogopewa kuliko rais wa nchi, anakamata kuliko polisi na ana mamlaka ya kuhukumu kushinda hata hakimu.
Wanakijiji ambao tangu Tanganyika iipate uhuru mwaka 1961 wao mpaka leo wanaendelea kuwa na ndoto za kunywa maji ya bomba na kuachana na maji ya visima wanayokunywa.
Hivyo Mrema hakujishughulisha nao badala yake akajishughulisha na watu wa mijini ambao kwanza rekodi zinaonyesha kuwa kwa kiasi kikubwa si wapiga kura zaidi ya kupenda kushabikia.
Ni hilo wanalolifanya CHADEMA sasa binafsi naona kama wanacheza ngoma ile ile iliyowabwaga Oktoba 31, kwani shinikizo kwa serikali lingetosha kuzungumziwa katika mkutano mmoja tu kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam.
Nina amini hivyo kwa sababu makombora yaliyorushwa katika mkutano mmoja tu na Dk Slaa, pale Mwembe Yanga mwaka 2007, yalitosha kuitetemesha nchi na hadi leo bado serikali ya CCM inahangaika kujikosha.
Kwa hiyo CHADEMA walikuwa na uwezo wa kuendelea kuishughulisha CCM kwa mkutano mmoja tu, hapa Dar es Salaam, kisha wao wakijiendea zao vijijini badala ya kuzunguka katika miji ya makao makuu ya mikoa na baadhi ya makao ya wilaya nchini.
Ninawahurumia CHADEMA kwa kushindwa kufahamu kwamba miaka minne ni mingi kwa kuitamka lakini ni michache sana kwa maandalizi mazito ya kupita mtaa hadi mtaa na kuwashawishi watu kuiunga mkono.
Ni kampeni za kijiji hadi kijiji zinmazopaswa kufanywa na viongozi wakuu wa kitaifa wa chama hicho ndizo zitakazowapa ushindi na si kutegemea kampeni za majukwaani za miezi miwili kuwaingiza Ikulu.
Inasikitisha kuona kwamba CHADEMA mpaka sasa haijatambua na kufahamu kuwa inapambana na chama tawala ambacho kimefanya madhambi mengi na dhuluma kwa wananchi kwa hiyo hakitakuwa tayari kuachia madaraka kirahisi.
Wakuu wa mikoa na wilaya ndio makatibu wa CCM wa mikoa na wilaya, unategemea nini hapo, watendaji karibu wote wa vijiji ni wanachama watiifu wa CCM, ambao jukumu walilopewa ni kuwahadaa wananchi kila uchaguzi unapokaribia.
Kuna vijiji ambavyo huahidiwa barabara, visima vya maji, zahanati au vituo vya afya kila uchaguzi unapokaribia huku wakiambiwa wanavipata vitu hivyo iwapo tu wataiachagua CCM na kutokana na mateso adha na taabu wanazopata masikini hawa, hulazimika kukubaliana na hadaa hizo na kuipa CCM kura.
Ukiachana na mbinu hiyo ambayo kidogo ni ya kistaarabu, kuna mbinu chafu zinazotumiwa na mara kwa mara na CCM za kutumia vitisho na ukandamizaji kwa wote wanaoonekana kutaka kuhamasisha mageuzi huweza hata kubambikiwa kesi.
Hayo hufanyika katika kuwatisha wananchi na kutokana na kukiukwa kwa kanuni na haki za binadamu kwa kiasi kikubwa huko vijijini, wananchi hulazimika kunywea na kukipigia kura chama hicho kwa kuhofia usalama wao, mali na familia zao.
Kwa hiyo huu ulikuwa wasaa mzuri kwa Dk. Slaa, Naibu wake, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, kufanya ziara za harakati kuwakomboa Watanzania kwa kupita mtaa hadi mtaa, kitongoji hadi kitongoji na kijiji hadi kijiji, kuwafungua macho wananchi.
Wanapaswa waende huko ili kuwaambia wasihadaiwe na CCM ambayo imekuwa na sera za kuwatisha wananchi wengi wa vijijini kwamba wakiwachagua wapinzani nchi itaangukia kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe.
CHADEMA mkiendelea kutumia muda wenu mwingi kuzunguka mijini kuwaeleza uoza wa CCM, watu ambao tayari wanaujua kwa kiasi kikubwa ni kutumia vibaya rasilimali muda, nendeni vijijini mkahubiri sera zenu vinginevyo subirini kuangushwa tena na CCM.
Binafsi sioni dalili za ushindi kwa aina hii ya kampeni za kutumia kilio cha hali ngumu ambacho kwa Watanzania umekuwa kama wimbo wa taifa, ambao unaimbwa na kila mmoja, cha muhimu ni kwenda kuwapa matumaini maelfu ya wananchi waliokatishwa tamaa na matendo ya CCM huko vijijini.
Ninasisitiza kuwa, huu ndio muda muafaka kwa CHADEMA kwenda vijijini kwani maisha yamepanda mara dufu hivyo wana turufu nzuri ya kuiadhiri CCM mbele ya wapiga kura.
Source: Tanzania Daima ya leo


My take: vyama vya siasa vijifunze kwenda vijijini, kwa kweli CCM ina mtandao mkubwa hadi ngazi ya mtaa; vyama vingine vijifunze hilo kama vinataka kuwa na nguvu!!.
 

Similar Discussions

1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom