BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,005
Majumba ya sinema: kumbukumbu iliyopotea | Send to a friend |
Thursday, 12 January 2012 12:53 |
Na Charles Kayoka Mwananchi Naanza kwa kumshukuru msomaji mmoja aliyenidokeza kuwa kuna mrembo mmoja ambaye bado anaishi jijini Dar es salaam, na alikuwa Miss Chagaland kabla ya uhuru. Na kuwa Wachaga walianza kufanya mashindano hayo mapema kabisa. Ninaahidi wasomaji kuwa panapo majaliwa nitamtafuta mama huyu, atuonjeshe historia kidogo. Leo tunazungumzia sinema. Asubuhi na mapema siku moja wiki iliyopita nilikuwa nawahi miadi eneo la mjini kati hapa Dar-es-Salaam. Nikipita mtaa wa Nkrumah, macho yangu yalielekea juu, kuangalia jengo nililokuwa nikipenda kwenda kupata chai wakati fulani huko nyuma, Continental Hotel. Ghafla macho yangu yakakutana na kitu ambacho kilikuwa kimetoweka katika kumbukumbu yangu. Nacho ni neno NEW CHOX. Kibao kilichofubaa kwa rangi baada ya kutelekezwa miaka dahari kwani umuhimu wa jengo hilo kwa sasa haupo tena, nani anakwenda sinema siku hizi. Watu wa Dar es salaam ukiwaona wakiingia New World Cinema pale Mwenge au majumba ya Mlimani City, wanaweza kudhani kuwa huu ni utamaduni mpya sana. Kabla na baada ya Uhuru kwenda Sinema ilikuwa ni jambo la kawaida na moja kitu kinachoweza kukuletea mapenzi na heshima kubwa kwa familia yako, rafiki au mpenzi wako, kwa wakati ule. New Chox, itakumbukwa kwa filamu zake za kizungu, wakati huo nikiwa bado mdogo, kwenda kuona filamu ilikuwa ni jambo adhimu sana. Na siku mzazi wako akikuambia mnakwenda sinema ni sawa kuwa umahidiwa ufalme. Utaona siku haifiki, na wakati unachelewa. Kwa vijana waliozaliwa miaka ya 1980 hasa 1990 neno Jumba la Sinema, ni kama ruya. Lakini Tanzania yote ilikuwa na majumba ya sinema, ambako kila siku jioni na wikiendi watu walikwenda huko kuburudika. New Chox hapa Dar-es-Salaam ilikuwa ni moja ya majengo ya sinema. Mtaa wa Jamhuri ulikuwa na majengo mawili ya sinema, Odeon, ambako sasa kuna DTV/Channel Ten. Avalon, ambako watu wa GNLD wamekuwa wakifanyia mikutano yao na baadaye watu wa madhehebu ya kilokole kufanyia ibada zao. Jengo hili linaangaliana na uwanja mkubwa yanakoegeshwa magari na ofisi za zamani ya Uhamiaji. Kulikuwa na jengo kubwa zaidi la sinema kule Msasani, likiitwa Drive-IN, ambako sasa pamejengwa jengo la ubalozi wa Marekani. Huko kulikuwa ni kwa watu matajiri zaidi, waliruhusiwa kuingia na magari yao kwenye ukumbi, watu wakikaa ndani ya magari na kuangalia filamu huku wakiburudika na vinywaji. Empress ilikuwa mtaa wa Acacia (Samora au Independence avenues) jirani na ofisi za Maelezo, lakini sasa kunauzwa fenicha. Empire, ambayo ndiko kulikuwa ni kwa watu wenye fedha pia na picha za kifahari zaidi, ilikuwa kwenye jengo ambalo sasa ni makao makuu ya NMB. Nakumbuka nilienda kuona filamu ya Dracula, iliyochezwa na Christopher Lee, na wengi wa watazamaji ambao walikuwa waoga hawakuiangalia filamu hii, ikimwonyesha Dracula akinyonya watu damu na kuambukiza tabia hii kila aliyemdonoa kwa jino lake. Lakini walala hoi tulikuwa na mahali pengine pia pa kwanda, Amana Social Hall. Pale Ilala. Sasa hivi ni kituo cha burudani na taasisi za mafunzo, lakini awali ilikuwa pia ni mahali tukienda kungalia sinema wikiendi na siku za sikukuu. Lakini majumba haya ya jamii- Community Social halls, yalikuwa kila mahali. Pale Kata ya Kingo Morogoro tulikuwa nalo. Na zaidi ya sinema palikuwa ni mahali pa kuchezezea muziki wa dansi na aina nyingine ya shughuli za kijamii. Bado lipo hadi leo. Dar-es-Salaam haukuwa mji pekee wenye majumba ya Sinema. Nakumbuka kule kwetu Morogoro mjini, palikuwa na Shani Cinema na baadaye Sapna. Sapna, njia ya kwendi kituo cha reli, ndipo nilipoiona kwa mara ya kwanza filamu ya Disco Dancer ikimchezesha msanii mkongwe sasa-Mithum Chakrabotty - na pia wanamuziki wa Afrika Kusini Soul Brothers, wakati ule tuliwaita tu kwa jina la Makurukunyi- matamshi potofu ya moja ya wimbo wao. Kila Makao makuu ya mkoa yalikuwa na jengo lake la filamu, na mengi yalikuwa yakiendeshwa na wafanyabiashara wa asili ya India. Kwa hiyo sio jambo geni kuwaona bado wanashika dau kwenye tasnia ya filamu hadi leo. Naambiwa kule Lindi pale kwenye Ukumbi wa unaoitwa Y2K kwa sasa ndipo palikuwa na jengo kubwa la filamu likialika watazamaji kutoka mikoa yote ya kusini, hadi Songea! Ilikuwa ni jambo la kawaida miaka hiyo kabla ya kuanguka tasnia ya sinema ilikuwa ukinunua gazeti, hasa siku za Jumatano, Ijuma, Jumamosi na Jumapili, kufungua kurasa za burudani kutafuta ni sinema ipi inaonyeshwa wapi, na wakati huo Wahindi walikuwa wakichuana sana na wacheza filamu kutoka Marekani na Uingereza. Sasa hivi utamaduni huu umekwisha kwa mikoani. Majengo ya sinema yamekuwa nyumba za ibada, maduka au yamefungwa, au kubomolewa na majengo mengine kusimamishwa badala yake. Lakini cha muhimu zaidi ni kufikiria namna ya kuweka kumbukumbu, kuwa hapo zamani tulikuwa na majengo ya sinema. Tungeteua jambo moja tu ya majengo haya na kuweka kumbukumbu zetu hapo. Kuiona ile nembo ya New Chox kumenikumbusha mengi kuhusiana na burudani hapa nchini! utaliiupdate@gmail.com This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it , 0766959349 |