Majibu ya BoT yanaishtaki Serikali ya CCM

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,463
39,929
KAMA tungekuwa na nia ya kupigana na ufisadi na hasa ule wa matumizi mabaya ya ofisi, fedha na rasilimali za nchi kama wanavyofanya kule Uchina, basi wale waliopitisha matumizi ya ujenzi wa nyumba mbili za Gavana wa Benki Kuu (BOT) na manaibu wake ya shilingi bilioni 2.5 wangetiwa vitanzini.
Bila hivyo au bila kuharakisha hukumu zao kama tulivyofanya kwa watuhumiwa mauaji ya albino basi hawa watu wataendelea kuthubutu kula mali ya umma huku ofisi zao za mawasiliano zikiandaa taarifa ndefu na zenye tarakimu nyingi kuelezea kwanini wao wamestahili kula!


Nimesoma majibu ya baadhi ya hoja nilizozijenga na watu wengine vile vile wamezijenga dhidi ya matumizi ya Benki yetu Kuu kuwajengea majumba ya kifahari Gavana na Manaibu wake kwa gharama ya dola karibu milioni mbili na theluthi.



Majibu hayo ambayo yalitolewa na Benki hiyo Jumatano iliyopita vimenithibitishia mambo kadhaa ambayo kwa muda mrefu nimeyaelewa kuhusu Benki Kuu ya Tanzania na vile vile juu ya uwezo na nia ya Rais Jakaya Kikwete kupambana na ufisadi nchini. Nitayaangalia yote mawili nikianza na Rais Kikwete.


Ameshindwa kuisafisha Benki Kuu
Matumizi yaliyofanyika Benki Kuu katika kipindi hiki “kigumu” cha uchumi yamethibitisha kwangu kuwa Rais Kikwete ameshindwa kuleta mabadiliko yanayohitajika kwenye taasisi hii nyeti kabisa kwa uchumi wetu.
Ni wazi kuwa Rais Kikwete hakujifunza katika ufisadi wa Benki Kuu chini ya Gavana Daudi Ballali na sasa hivi Serikali yake imehalalisha ufisadi mwingine kwa kuamini kuwa unafanywa kwa nia nzuri.



Kilichonitibua zaidi ni kuwa eti hata Waziri wa Fedha naye anaonyesha kushtushwa na matumizi hayo utadhani yalikuwa yanafanyika uvunguni mwa kitanda! Katika majibu yao Benki Kuu wameeleza kuwa mambo yote yamefanywa “kwa mujibu” wa sheria na kuwa mipango ya matumizi hayo ilifanywa wakati Benki Kuu iko chini ya uongozi wa Gavana Ballali!
Yaani, pamoja na kujua ufisadi mkubwa uliofanyika chini ya gavana huyo, Rais Kikwete hakuona umuhimu na Gavana mpya kuona ulazima wa kupitia kila mipango iliyopitishwa na Gavana Ballali na kuona kama inastahili kuendelezwa? Hili ni kweli kwa sababu badala ya kufanyia mabadiliko ya kiutendaji na kisheria Benki Kuu, Rais Kikwete aliona ni rahisi tu kubadilisha watu!


Ndugu zangu kanuni ya ufisadi inasema hivi: Mfumo wa kifisadi daima huzaa mafisadi. Yaani, tunaweza kubadilisha gavana na manaibu wake lakini bila ya kubadilisha mfumo wa utendaji basi ufisadi utaendelea kutawala Benki Kuu. Serikali hawajaona umuhimu wa kubadili mfumo huo miaka minne tangu ufisadi mkubwa ulipoibuliwa ambao hadi hivi sasa hakuna mtu aliyekutwa na hatia yoyote zaidi ya watu wachache kufikishwa mahakamani.



Benki Kuu na ufisadi
Tunaweza kusema kwa maneno machache kuwa Benki Kuu ndicho kiini cha ufisadi. Ni taasisi ambayo kama ingekuwa ni nchi nyingine viongozi wake wote wangekwisha kutimuliwa. Hadi hivi sasa serikali yetu haijakubali ukweli kuwa Benki Kuu imeshiriki kwenye ufisadi mkubwa zaidi na pamoja nao mlolongo wa viongozi wa juu serikalini.
Naomba niangalie majibu yao kwa hoja zetu ili tuweze kuona kuwa kama kungekuwa na chembe ya uongozi bora imesalia katika taifa letu basi Ndulu na manaibu wake wangetakiwa kuwa wamekwisha jiuzulu tangu majuzi ili wasiwe wanufaika wa maamuzi yao wenyewe.
Majumba yaliyojengwa
Kwa mujibu wa majibu ya Benki Kuu jumba la Gavana na lile la Naibu wake yalitakiwa yawe hivi “Nyumba zote mbili zilipangwa ziwe za ghorofa moja, vyumba vitano vya kulala, wenyeji na wageni, sebule ya wageni, sebule ya familia, mahali pa kulia na vyoo na mabafu yanayoendana na idadi ya vyumba. Majengo ya nje ni pamoja na nyumba ya kuishi watumishi, gereji ya magari, bwawa dogo la kuogelea, ukuta na vyombo vya usalama na kibanda cha walinzi.”



Zaidi ya sifa hizo za majengo, Benki Kuu ikatudokeza kuwa “Huduma zilizogharimiwa katika ujenzi wa nyumba hizi ni pamoja na mashine ya umeme (generator), mashine ya kupoza hewa na matenki ya kuhifadhi maji. Wakati huohuo, shughuli nyingine zilizofanyika ilikuwa ni kutengeneza mahali pa kuegesha magari pamoja na bustani.”



Kwa maneno mengine, ni katika kutekeleza sifa hizo za ujenzi ndiyo shilingi bilioni moja na nusu hivi kwa kila jumba zikatumika. Hapa tuzingatie kuwa tunaangalia taasisi moja tu ambayo imejiamulia (bila kuangaliwa na mtu mwingine) kujijengea wanavyopenda. Hatujaangalia Bima, TANESCO, NSSF, Polisi, Jeshi n.k na jinsi kila taasisi inavyojitahidi kuwaridhisha mabosi wao. Kama Benki Kuu wametumia bilioni mbili na nusu hivi kujenga nyumba za watu wawili tu, tukipanua wigo na kwenda ngazi za Wakurugenzi wa BoT ni kiasi gani kimetumika?



Vigogo kushindwa kukaa kwenye nyumba zao
ndulu_1.jpg


Gavana wa Benki Kuu, Profesa Ndulu
Mojawapo ya vitu vya kushangaza ni kile kinachotajwa kwenye majibu hayo kuwa “Kati ya Oktoba 2007 aliporipoti kazini kama Naibu Gavana hadi Aprili 2008, Profesa Ndulu aliishi kwenye nyumba yake iliyoko Mbezi Beach, na Naibu Gavana Mkila naye pia aliishi nyumbani kwake kabla ya kuhamia kwenye nyumba hizi zilizokodishwa.” Kwa maneno mengine kwa muda wote waliokuwa wakiishi kwenye nyumba zao waliweza kufanya kazi kwenye Benki Kuu na hivyo ulazima wa majumba mapya unajileta sasa.





Na kama wasiofikiria walichoandika Benki Kuu wanajishitaki wenyewe pale wanapotuambia kuwa “Naibu Gavana Dk. Bukuku anaishi kwenye nyumba yake na Benki Kuu inatoa posho ya nyumba kulingana na mkataba.” Kwa maneno mengine Naibu Gavana Bukuku yeye anaishi kwenye nyumba yake na kupewa posho na anafanya kazi yake vizuri tu! Wakati huo huo tunadokezwa kuwa Gavana wa Tanzania analipwa karibu dola 15,000 kwa mwezi na zaidi ya hapo anapewa na jumba la kifahari! Hivi, kwanini na yeye asilipiwe posho na akajitafutia nyumba yake yeye mwenyewe?


Leo hii magavana wa nchi kama Marekani na Uingereza wanalipwa posho ya nyumba na wao wenyewe wamejinunulia majumba yao tena chini ya dola milioni moja! Je ni kipi rahisi? Kutumia dola milioni moja na nusu hivi kwa nyumba ya mtu mmoja au kumlipa mtu posho ya nyumba?



Kama tungeamua kusema Ndulu analipwa posho ya dola 2500 kwa mwezi kwa ajili ya nyumba, kwa miezi kumi nambili itakuwa ni dola elfu thelathini na kwa miaka mitano (kama ataendelea kuwa hapo) ni dola 150,000 (sawa na karibu shilingi milioni 160 hivi. Na hata kama tungesema tumpe posho ya dola 5000 kwa nyumba (kitu ambacho hata Wamarekani na utajiri wao hawampi mtu kirahisi rahisi) bado kwa miaka mitano angetumia dola laki tatu tu!


Sasa mtu mmoja atuambie huko BoT ni mtu gani huyu “genius” aliyeona ni rahisi zaidi kutumia dola milioni moja na nusu kwa kitu ambacho kingeweza kufanywa kwa theluthi moja ya gharama hiyo? Je, kwa kufanya hivyo si kila Gavana hata kama ana nyumba yake mwenyewe anapata posho zaidi ya haki na anakuwa na mahali pa kuishi anapopataka yeye mwenyewe?



Kwa mujibu wa mikataba
Kweli? Sijui tumerogwa na nani kiasi kwamba leo hii tunataka tukubali maneno ya “kwa mujibu wa mikataba” kana kwamba yanabeba umaana fulani. Katika majibu yao mepesi Benki Kuu wanajaribu kuhalalisha matumizi mabaya kabisa ya fedha za umma kwa kudai kuwa “Gavana wa Benki Kuu na manaibu wake kwa mujibu wa mikataba ya kazi zao, wanastahili kupewa nyumba ya kuishi kila mmoja.”



Nilipoanza kusoma kauli hiyo tu nilitamani tungekuwa na uwezo wa aina fulani tungetaka hiyo mikataba iwekwe hadharani ili tuone hawa wenzetu wanastahili vitu gani hasa.


Kwamba, kuna wanasheria wetu ambao wamekaa chini na kusema kuwa basi Gavana na manaibu wake wanastahili kupewa “nyumba” ya kuishi inashangaza! Kwanini mikataba yao isiseme wanastahili kupewa posho na kama ni nyumba ni ile tayari iliyopo na yenye gharama ya kiasi fulani?
Hivi, kwanini leo hii Watanzania tunajaribu kuwalipa watawala na viongozi wa juu kama vile sisi ni nchi ya Magharibi (angalia mawaziri wetu, kocha wa mpira, spika, wakuu wa majeshi, wakuu wa TRA n.k) lakini inapokuja kwenye kuwalipa madaktari na walimu wetu tunadai kuwa hatuwezi kufikia gharama hiyo?


Daktari wa Marekani kwa wastani analipwa dola 11,170 kwa mwezi, je, daktari wa Tanzania analipwa kwa wastani wa kiasi gani?, je, twaweza kumlipa kiasi hicho kama huko Marekani kwa vile tayari tunaweza kumlipa Gavana wetu kwa kiwango kinachokaribiana na wale wakuu wa Benki za Marekani au nchi nyingine zilizoendelea?


Leo hii tunawajengea majumba yenye vikolombwezo na anasa zote za Kimagharibi kwa sababu ya “hadhi” zao hawa watendaji wakati huo huo tukisuasua au kushindwa hata kujenga vyoo vya shule za watoto wetu hadi tulazimishane?



Matumizi haya yanaonesha serikali imepoteza mwelekeo wa maadili. Baba wa Taifa aliwahi kusema kitu kimoja muhimu sana ambacho leo kina Kikwete, CCM na mashabiki wao hawataki kukiangalia.



“Kabla wachache wetu hawajaishi maisha ya anasa, ni lazima wengi wetu wapate kwanza mahitaji yao muhimu”, alinukuliwa kusema wakati mmoja.
Leo hii serikali yetu na chama tawala kimeamua kugeuza kabisa falsafa hiyo; leo hii wanaharakisha wachache wetu waishi kwenye anasa huku wengi wetu bado tukihangaika na mahitaji muhimu na maisha bora yakiendelea kuwa ndoto kwa wengi wetu.



Kinachoniudhi zaidi ni kuwa hakuna mbunge wa CCM mwenye ujasiri wa kuona ubaya wa matumizi haya na wote hawataki kukosoa Serikali yao kwa sababu wanaweza kujiharibia. Na kinachoniudhi zaidi pia ni kuwa wananchi wetu wanafikiria kuwa Gavana anastahili maisha hayo ya anasa ya majumba, watumishi lukuki na vyumba na sebule za wageni utadhani Dar es Salaam imeishiwa hoteli!



Mimi nafikiri wazo la kutafuta dawa ya kudumu kama wafanyavyo China tulifikirie kwa makini labda ndipo wataanza kufikiria mara mbili kabla hawajakaa chini na kuidhinisha matumizi kama haya.
hs3.gif

(Raia Mwema)
 
Mwanakijiji

Hawa watu kama utawafikiria kwa undani zaidi utatamani kulia. Sijui hata walitumia vipimo gani kuhalalalisha hayo malipo. halafu inanishangaza zaidi kuona Gavana anatoa statament ya kipuuzi kama ile. Shame
 
Viongozi wetu wajiulize maisha aliyokuwa akiishi Mwalimu wakati akiwa Rais na baada ya kustaafu. Nyumba kubwa ya Mwalimu pale msasani iwe ndo kipimo kwa viongozi wetu. Kuna nyumba tatu pale za kawaida.

Mwalimu alikopa ili aweze kujenga nyumba yake pale Msasani. Bahati mbaya sana, kutokana na mshahara wake kuwa mdogo, alishindwa kulipa deni lote akalazimika kuirudisha nyumba ile serikalini.
 
Wafanye wafanyalo katika hali halisi mtu unahitaji 1 square meter of space for the rest of his life. Hizo square meters wanazojipendelea sijui zinawanufaishaje?
 
Governor wa BANK KUU YA MAREKANI analipwa U$ 191,300 kwa mwaka sawa na U$ 15,941.67 kwa mwezi....na wa Tanzania naye analipwa up to U$ 15,000?, achilia mbali utofauti wa ukubwa wa uchumi wa nchi hizi lakini linapokuja swala la malipo tunalipana sawa?....du.

Nchi ishauzwa hii, tugawane
 
MMJJ,
Zaidi ya haya majibu ya Prof. Ndulu kuishitaki serikali ya JK, kibaya zaidi ni ubweteka uliouonyeshwa wa kutomchukulia hatua Ndulu ASAP zinazolingana na tatizo lenyewe.

Baada ya uchafu wa Dr. Bilali, inashangaza kuona kuwa Prof. Ndulu bado yuko madarakani eti akisubiri kufanyiwa uchunguzi. Kwa nini asisimamishwe ili uchunguzi uweze kufanyika bila kuingiliwa?

Haya majibu yamesaidia zaidi kuonyesha wazi jinsi watendaji wa serikali ya JK wasivyo na aibu katika kufuja pesa za umma.

Kama JK anaweza kufuja pesa kwa kuzurura na kubembea nchi za wenzetu, kwa nini wateuliwa wake nao waogope kufuja mali ya umma hasa kama wao ndio wanaojua kiasi gani anachotumbua JK?

Kwa kifupi ni kuwa bila ya JK kuondoka madarakani nchi itaendelea kuendeshwa kihuni-kihuni, kama lile baraza la JK pale kariakoo. JK ndio tatizo hawa wengine wanaiga tu afanyayo kiongozi wao.
 
Sasa hivi naanza kutamani rais kama Kabila na mwingine kama Kagame japo wote wawili ni mazao ya Tanzania.. hivi inakuwaje tunaweza kutoa marais wazuri na wenye kuthubutu wa nchi nyingine? Hata Museveni yawezekana ni bora kuliko wa kwetu huyu..
 
Kinachonishangaza mpaka sasa ni hizo Guts walizonazo hawa watumishi wa serikali kutoka hadharani na kujustfy ufisadi, well hawawaogopi wananchi. Lakini what about Mungu? Au ndio uzao wa shehe Yahya!!!!!!!!????????
 
Tiba ya hii nchi ni maandamano na mabango ya amani kuanzia January hadi Disemba labda ndio pamba zilizowekwa masikioni na miwani ya kuchomelea vyuma iliyowekwa machoni mwa viongozi wetu watasikia na kuona vilio vinavyotokana na hali halisi ya kiutawala wa nchi hii. Bila hivyo nadhani wanatuimbia wimbo wa mipasho "Watasema mchana eeeh....usiku watalala wacha wacha waseme".
Ingekuwa vyema hamasa hii ikafika kwa wananchi wa kawaida ambao hata kusoma magazeti ni anasa!
 
"Kinachoniudhi zaidi ni kuwa hakuna mbunge wa CCM mwenye ujasiri wa kuona ubaya wa matumizi haya na wote hawataki kukosoa Serikali yao kwa sababu wanaweza kujiharibia. Na kinachoniudhi zaidi pia ni kuwa wananchi wetu wanafikiria kuwa Gavana anastahili maisha hayo ya anasa ya majumba, watumishi lukuki na vyumba na sebule za wageni utadhani Dar es Salaam imeishiwa hoteli!



Mimi nafikiri wazo la kutafuta dawa ya kudumu kama wafanyavyo China tulifikirie kwa makini labda ndipo wataanza kufikiria mara mbili kabla hawajakaa chini na kuidhinisha matumizi kama haya. "


hs3.gif






Na hapo ndio penye chimbuko la matatizo mengi. Tulio watuma kuhoji serikali hawaiwezi kazi hiyo na sasa wanajiandaa kuiomba tena 2010
 
Leo nikiamka (inshallah) nitaanza kuwapoll wabunge mbalimbali wa CCM wahalalishe matumizi haya!
 
hivi inakuwaje tunaweza kutoa marais wazuri na wenye kuthubutu wa nchi nyingine? Hata Museveni yawezekana ni bora kuliko wa kwetu huyu..

Majirani ambao wanatutegemea kwa bandari, internet (EASSY) n.k., watasonga mbele na kutuacha na mswahili wetu JK ingawa ukweli ni kuwa Kikwete hakuwa chaguo la Watanzania.

JK alinunua uteuzi ndani ya CCM kwa kumpiku Salim A. Salim kwa pesa isiyojulikana ilikotoka hadi leo (tetesi ni Iran, EPA, RA n.k.).

Ukweli ni kuwa ni lazima JK ang'oke ili kuondoa huu uhuni uliopo serikalini. Tunataka mtu mwenye dira na uwezo wa kuongoza nchi yetu.
 
Hii ni aibu sana, hivi hii nchi yetu hatuna kabisa misamiati ya UWAJIBIKAJI NA UZALENDO kwenye uongozi????
je haya JK hayasikii au kuona? mbona anakaa kimya sana, hawa viongozi wanapataje uthubutu? kiburi? dharau?.....

jamani hii ni 2010.....tusifanya makosa
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom